Tafuta

Vatican News
Maadhimisho ya Jubilei na Siku kuu ya Mwaka ya Jimbo Kuu la Asmara nchini Eritrea. Maadhimisho ya Jubilei na Siku kuu ya Mwaka ya Jimbo Kuu la Asmara nchini Eritrea. 

Eritrea:Maaskofu waomba maelezo kwa Serikali ya nchi!

Maaskofu wa Eritrea wanaomba maelezo kwa serikali kufuatia na tukio la kuwakatalia wawakilishi wa Kanisa la Ethiopia kuweza kuingia nchini Eritrea mara baada ya kutua uwanja wa ndege, katika fursa ya maadhimisho ya Jubilei ya dhahabu na siku kuu ya mwaka ya Kanisa Kuu la Asmara.

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican

Kanisa Katoliki nchini Eritrea limeonesha kusononeka kwake dhidi ya Serikali ya Asmara kufuatia na kutoruhusu kuingia kwa uwakilishi wa kanisa kutoka nchini Ethiopia tarehe 22 Februari 2020. Kardinali Berhaneyesus Demerew Souraphiel, Askofu Mkuu wa Addis Abeba, Askofu  Abune Mussiè Ghebreghiorghis Uqbu, wa Emdeber na Padre  Teshome Fiqre Weldetensae, Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu nchini Ethiopia walikuwa washiriki katika maadhimisho ya Jubilei ya dhahabu  na sikukuu ya Kanisa la Kidane Mehert, ambayo ni Makao makuu ya Askofu  Mkuu wa Asmara, Menghesteab Tesfamariam, lakini walizuiwa katika uwanja wa Mji mkuu wa Eritrea na kulazimishwa kurudi nchini kwao Ethiopia siku iliyofuata baada ya mjadala mkubwa ambao haukuleta muafaka.

Wawakilishi walikuwa na vitambulisho halali

Katika barua iliyoelekezwa kwenye Ofisi ya mambo ya  kidini, Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu nchini Eritrea Padre Tesfaghiroghis Kiflom, anaandika kuwa wageni wa ethiopia walikuwa na vitambulisho halali vya kuingia nchini Eritrea na kupigwa muhuri katika pasport zao kwa muda wa mwezi mmoja na kwa maana  hiyo anaomba sababu zilizosababisha waziweze kuruhusiwa kukaa nchini humo.

Lengo la Kanisa nchini Eritrea ni kwa ajili ya huduma na zaidi wenye kuhitaji

Siku chache zilizopita Askofu Mkuu Ivan Jurkovič, mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Ofisi za Umoja wa Mataifa na mashirika mengine ya Kimataifa huko Geneva, katika Kikao cha 43 cha Baraza kwa ajili ya haki za binadamu, alikuwa ametoa hotuba yake kuhusiana na hali halisi ya Kanisa Katoliki nchini Eritrea na kuelezea kwamba shughuli zake  za kihisani, upendo na kijamii ni kwa ajili ya watu wote, kwa kuwa na umakini kwa namna ya pekee wale wenye kuhitaji zaidi bila kubagua na kwamba lengo la kundelezwa ni la kibinadamu na siyo la kisiasa na ili hatimaye kuweza  kuhamasisha haki, amani, mapatano na majadiliano.

Kuanzisha majadiliano yenye tija na heshima

Mwakilishi wa kudumu aidha alikuwa amewatia moyo serikali ya Eritrea ili kuanzisha majadiliano yenye tija na heshima na Vatican kwa mtazamo wa ujenzi wa wakati mwema ujao na  matarajio ya amani ambamo haki ya uhuru na kidini au imani yoyote viweze kuheshimiwa. Vile vile Papa Francisko alipokutana na Taasisi ya Kipapa ya Kiethiopia kunako tarehe 11 Januari 2020, matarajio yake mema yalikuwa ni kwamba Kanisa Katoliki la Ethiopia na Eritrea liweze kuhakikishiwa uhuru na kuweza kuhudumia kwa ajili ya ustawi wa pamoja wa watu na taifa kwa ujumla.

04 March 2020, 11:36