Tafuta

Vatican News
Parokia ya Mama Yetu wa Matumaini Mema, Jimbo kuu la Mombasa iliyoko eneo la Bura imekuwa ni chemchemi ya : Imani Katoliki na Miito mbali mbali nchini Kenya. Parokia ya Mama Yetu wa Matumaini Mema, Jimbo kuu la Mombasa iliyoko eneo la Bura imekuwa ni chemchemi ya : Imani Katoliki na Miito mbali mbali nchini Kenya.  (Vatican Media)

Jimbo kuu la Mombasa, Kenya: Wahudumu wa Mafumbo ya Kanisa! Bura kitovu cha imani

Askofu mkuu Martin Kivuva Musonde wa Jimbo kuu la Mombasa, Kenya ametoa Daraja Takatifu ya Upadre kwa Mashemasi watano na Daraja Takatifu ya Ushemasi kwa Majandokasisi watano, wanao ongeza nguvu ari na mwamko mpya katika mchakato mzima wa uinjilishaji wa kina Jimbo Kuu Katoliki la Mombasa. Bura imekuwa ni chemchemi ya imani na kitovu cha matumaini.

Na Sr. Bridgita S. Mwawasi, - Mombasa; Na Padre Richard Mjigwa, - Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika tafakari yake kuhusu wito na maisha ya Daraja takatifu ya Upadre anapenda kukazia sana umuhimu wa huruma ya Mungu katika maisha ya mwanadamu; Fumbo la Ekaristi Takatifu kuwa ni kiini cha maisha na utume wa Kanisa kwa sababu Kristo Yesu ndiye chemchemu ya upendo kwa waja wake. Wakleri wanakumbushwa kwamba, kabla hata ya kuwekewa mikono na kuwa ni: Mashemasi, Mapadre na Maaskofu,  wao kimsingi ni: waamini waliobatizwa kwa maji na Roho Mtakatifu na kwamba, utambulisho wao wa kwanza ni waamini na wafuasi wa Kristo Yesu. Kwa kuwekwa wakfu katika Sakramenti ya Daraja Takatifu wanakuwa ni mashuhuda, vyombo na wahudumu wa Mafumbo ya Kanisa.

Kwa namna ya pekee,  ni wahudumu wa Sakramenti za huruma ya Mungu, yaani: Ekaristi Takatifu inayowajalia waamini chakula cha njiani katika hija ya maisha yao hapa bondeni kwenye machozi pamoja na Sakramenti ya Upatanisho, inayowaonjesha waamini, huruma, upendo na msamaha wa Mungu katika maisha yao, tayari hata wao kuwa ni mashuhuda wa huruma ya Mungu, inayomwilishwa katika vipaumbele vya maisha yao! Huu ndio urithi unaojikita katika Mafundisho tanzu ya Mama Kanisa. Ni ukweli ambao wakleri wanapaswa kuumwilisha katika maisha na utume wao kwa njia ya Roho Mtakatifu. Padre daima anapaswa kuwa ni chombo na shuhuda wa huruma ya Mungu kwa waja wake na kwamba, Ibada kwa Bikira Maria inawawezesha wakleri kujifunza kutoka katika shule ya Bikira Maria, ili kweli waweze kuwa wafuasi na mitume hodari wa Kristo Yesu kwa kusikiliza na kutenda kama alivyokuwa Bikira Maria. Daima amekumbusha kwamba, maskini ni amana na utajiri wa Kanisa, ni watu wanaopaswa kupewa kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wa Kanisa.

Hivi karibuni Askofu mkuu Martin Kivuva Musonde wa Jimbo kuu la Mombasa, Kenya ametoa Daraja Takatifu ya Upadre kwa Mashemasi watano na Daraja Takatifu ya Ushemasi kwa Majandokasisi watano, wanao ongeza nguvu ari na mwamko mpya katika mchakato mzima wa uinjilishaji wa kina Jimbo Kuu Katoliki la Mombasa. Makleri wapya wamekumbushwa kwamba, Kristo Yesu amewaita, akawapaka Mafuta na kuwatuma kwenda kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Wamepewa dhamana na wajibu wa kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu, utume wanaopaswa kuutekeleza kwa ari, moyo mkuu na unyenyekevu wa hali ya juu. Wasaidie kuwafafanuliwa watu wa Mungu Mafumbo ya Kanisa kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Askofu mkuu Martin Kivuva Musonde amewataka watu wa Mungu Jimbo kuu la Mombasa, lakini zaidi Wakleri kuwa wasikivu kwa Neno la Mungu kwa kulisoma, kulitafakari na kulimwilisha katika vipaumbele vya maisha na utume wao.

Makleri wawe wepesi kusoma alama za nyakati, tayari kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yao. Watu wa Mungu, Jimbo kuu la Mombasa, waendelee kufurahia uwepo endelevu wa Makleri katika maisha na utume wao kwa kuwa mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Amewataka Mapadre wa Jimbo kuu la Mombasa kuwapokea Makleri vijana na kuwaingiza katika urika wao. Sherehe hii imehudhuria na umati mkubwa wa watu wa Mungu kutoka Jimbo kuu la Mombasa ambao walitumia fursa hii kufanya hija ya kiroho. Mwanadamu ni hujaji katika maisha na kwamba, hata huruma ya Mungu ni lengo ambalo waamini wanapaswa kulipatia kipaumbele cha pekee katika safari ya maisha yao ya kiroho hapa duniani. Mama Kanisa anawahimiza waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kutambua umuhimu wa kufanya hija katika maeneo mbali mbali ya kihistoria, maisha na utume wa Kanisa.

Hija ni kielelezo cha ujasiri na sadaka ya kutaka kuzima kiu ya hamu ya kukutana na mashuhuda wa imani, ili kujenga na kuimarisha imani, matumaini na huruma na mapendo. Ni changamoto ya kukuza ukarimu unaomwilishwa kwa namna ya pekee, katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili! Kwa upande wake, Askofu mkuu Hubertus Matheus Maria Van Megen, Balozi wa Vatican nchini Kenya aliyeshiriki katika Ibada hii, aliwataka watu wa Mungu kushikamana na makleri wao kwa sala na sadaka ya maisha, huku wakiendelea kuombea miito, ili Bwana wa mavuno aweze kupeleka watenda kazi: wema, watakatifu na wachapakazi katika shamba lake. Familia ya Mungu Jimbo Kuu la Mombasa imefanya hija hii ya kiroho kwa kutembelea Parokia ya Mama Yetu wa Matumaini mema, iliyoanzishwa na Wamisionari wa Shirika la Roho Mtakatifu “Spiritans” kunako mwaka 1896, eneo la Bura. Tangu wakati huo, Bura imekuwa ni chemchemi ya imani Katoliki nchini Kenya.

Bura kimekua ni kitovu cha huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu kwani hapa, watumwa wengi waliweza kukukombolea na hivyo kurejeshewa tena utu, heshima na haki zao msingi. Kunako mwaka 1929, Shirika la Masista wa Mtakatifu Yosefu, Jimbo Kuu la Mombasa likaanzishwa hapa.Leo hii, Parokia ya Mama Yetu wa Matumaini mema imekuwa ni mlango wa imani na matumaini kwa waamini wa kizazi kipya. Waamini walipata nafasi ya kusali na kutafakari Mafumbo ya Kanisa, hasa katika Kipindi hiki cha Kwaresima. Huu ni mwaliko wa kuona fahari juu ya Msalaba, kielelezo cha huruma, upendo, msamaha na hekima ya Mungu. Tume ya Haki na Amani Jimbo kuu la Mombasa, imetumia fursa hii kuzindua Kampeni ya Kipindi cha Kwaresima nchini Kenya. Bura, Kituo cha Hija Jimbo Kuu la Mombasa kinaendelea kukua na kupanuka kwa kuwa ni kivutio cha pekee katika maisha na utume wa Kanisa Jimbo Kuu la Mombasa.

Jimbo kuu la Mombasa

 

 

10 March 2020, 10:06