Askofu Ludovick Joseph Minde wa Jimbo Katoliki la Moshi, Tanzania, tarehe 19 Machi 2020 anasimikwa rasmi tayari kuanza utume wake kama kiongozi mkuu wa Jimbo Katoliki la Moshi Askofu Ludovick Joseph Minde wa Jimbo Katoliki la Moshi, Tanzania, tarehe 19 Machi 2020 anasimikwa rasmi tayari kuanza utume wake kama kiongozi mkuu wa Jimbo Katoliki la Moshi 

Askofu Ludovick Joseph Minde: Jimbo Katoliki la Moshi! Utume!

Askofu Flaviani Matindi Kassala, Makamu wa Rais, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania anawaalika waamini na watu wote wa Mungu kumpokea kwa moyo wa ukarimu na shukrani Askofu Ludovick Joseph Minde, ALCP/OSS anayesimikwa rasmi kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Moshi, tarehe 19 Machi 2020, Mama Kanisa anapoadhimisha Sherehe ya Mtakatifu Yosefu Mume wake Bikira Maria.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, Kristo Yesu, Mwana wa Mungu aliye hai, alikuja ili kuwakomboa watu wake kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Alitaka watu wote watakatifuzwe, kama alivyotumwa na Baba yake wa mbinguni, hata naye akawachagua Mitume, aliowatakatifuza kwa kuwajalia Roho Mtakatifu, kusudi wao nao wamtukuze Mwenyezi Mungu hapa duniani, na kuwaokoa watu, ili kujenga Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani, Kanisa. Viongozi wa Kanisa wamepewa dhamana na mamlaka ya kuwafundisha mataifa yote, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu katika ukweli, wote wakiwa wamoja katika urika wao kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa zima.

Askofu anayo dhamana ya kusali kwa ajili ya kuwaombea watu wote, kwa kutambua kwamba, kimsingi yeye ni mtu wa Mungu, aliyeteuliwa kati ya watu kwa ajili ya huduma, ili kuhakikisha kwamba, anakuza na kudumisha Ibada na Uchaji wa Mungu, mambo msingi katika kulinda na kudumisha utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Utume huu, umwezeshe Askofu kuwa kiongozi mkarimu, akitambua kwamba, Kristo Yesu ndiye anayewaita waja wake na kuwaweka wakfu ili kuendeleza kazi ya ukombozi! Ni katika muktadha huu, Askofu Flaviani Matindi Kassala, Makamu wa Rais, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania anawaalika waamini na watu wote wa Mungu kumpokea kwa moyo wa ukarimu na shukrani Askofu Ludovick Joseph Minde, ALCP/OSS anayesimikwa rasmi kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Moshi, tarehe 19 Machi 2020, Mama Kanisa anapoadhimisha Sherehe ya Mtakatifu Yosefu Mume wake Bikira Maria.

Sherehe za kusimikwa kwa Askofu Minde, zimetanguliwa na tukio la kukabidhiwa funguo za Kanisa kuu la Kristo Mfalme, Jimbo Katoliki la Moshi, Jumatano tarehe 18 Machi 2020. Askofu Flaviani Matindi Kassala, katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema, tukio hili limekuja wakati ambapo kuna hofu ya mlipuko wa Virusi vya Corona, COVID-19 nchini Tanzania. Kanisa kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania linaendelea kuchukua hatua za tahadhari ikiwa ni pamoja na kufuata itifaki ya mapambano dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19. Huu ndio muujiza mkuu unaotekelezwa na Mwenyezi Mungu kupitia kwa wataalam wa sekta ya afya pamoja na uwajibikaji wa wananchi wenyewe. Hiki si kipindi cha kufanya mzaha kwa ugonjwa huu kwani ni hatari sana kwa mustakabali wa taifa.

Ili Askofu aweze kutekeleza vyema dhamana na utume wake wa kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu, hana budi kujenga na kudumisha mahusiano ya karibu sana na Kristo Yesu kwa njia ya: Sala, tafakari ya kina ya Fumbo la Msalaba na Neno la Mungu linalopaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha; kwa kuongozwa na hekima na busara katika maamuzi na utekelezaji wake. Kwa kuwa na mawasiliano mazuri na Kristo Yesu, Askofu ataweza kujenga na kudumisha uhusiano mwema na wasaidizi wake wa karibu ambao kimsingi ni wakleri wanaopaswa kutambua uwepo wake wa kibaba! Askofu Flaviani Matindi Kassala anawaalika watu wa Mungu Jimbo Katoliki la Moshi kumpokea Askofu Ludovick Joseph Minde kama zawadi kutoka kwa Mungu, kama jibu la sala zao kwa ajili ya kumpata kiongozi mkuu wa Jimbo. Ni wajibu na dhamana ya watu wa Mungu kuonesha umoja, upendo na ushirikiano wa dhati, ili Askofu Minde aweze kuwaongoza, kuwatakatifuza na kuwafundisha, huku akiwapeleka katika malisho ya kijani kibichi! Ushirikiano na mshikamano huu ni muhimu ili kuhakikisha kwamba, Kanisa la Tanzania linasonga mbele katika sera na mikakati yake ya shughuli za kichungaji zinazopania: ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Tanzania.

Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko tarehe 2 Desemba 2019 alimteuwa Askofu Ludovick Joseph Minde, ALCP/OSS kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki Moshi, nchini Tanzania. Kabla ya uteuzi huu Askofu Ludovick Joseph Minde alikuwa ni Askofu wa Jimbo Katoliki Kahama. Itakumbukwa kwamba, Askofu Minde alizaliwa tarehe 9 Desemba 1952 kwenye Parokia ya Kibosho, Jimbo Katoliki la Moshi. Ni mtoto wa mzee Joseph Ndasika Minde na Mama Maria Joseph Mukure. Baada ya masomo yake Seminari Ndogo ya Mtakatifu James, Jimbo Katoliki la Moshi kunako mwaka 1979 alijiunga na Shirika la Mapadre wa Maisha ya Kitume na Kazi ya Roho Mtakatifu ALCP/OSS. Akaendelea na masomo yake ya falsafa Seminari kuu ya Kibosho na kuhitimisha masomo ya taalimungu kwenye Seminari kuu ya Segerea, Jimbo kuu la Dar es Salaam.

Tarehe 26 Juni 1986 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Mtakatifu Yohane Paulo II kunako tarehe 24 Aprili 2001 akamteuwa kuwa ni Askofu wa Jimbo Katoliki la Kahama na kuwekwa wakfu kuwa Askofu tarehe 5 Agosti 2001 na Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, akisaidiana na Askofu Mathew Shija, Muasisi wa Jimbo Katoliki la Kahama pamoja na Hayati Askofu Mstaafu Amedeus Msarikie wa Jimbo Katoliki la Moshi. Itakumbukwa kwamba, Askofu Ludovick Joseph Minde, ALCP/OSS ni kati ya Mapadre watano walioteuliwa kwenda Roma kwa masomo zaidi baada ya hija ya kitume ya Mtakatifu Yohane Paulo II nchini Tanzania kunako mwaka 1990. Mtakatifu Yohane Paulo II alitaka kuimarisha malezi na makuzi ya majandokasisi kutoka Tanzania.

Tangu mwaka 1990 hadi mwaka 1995 alikuwa mjini Roma akijifunza Maandiko Matakatifu na hatimaye, akajipatia Shahada ya Uzamivu kutoka Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana, kilichoko mjini Roma. Ni kati ya wanafunzi waliofanya vizuri sana katika masomo yao kwa mwaka huo. Katika maisha na utume wake, amewahi kuwa Jaalimu wa Maandiko Matakatifu, Mlezi na Baba wa maisha ya kiroho, Seminari kuu ya Segerea, Jimbo kuu la Dar es Salaam. Itakumbukwa kwamba, Jimbo katoliki la Moshi limekuwa wazi baada ya Baba Mtakatifu Francisko tarehe 27 Desemba 2017 kumteua Askofu Isaac Amani Massawe wa Jimbo Katoliki Moshi, kuwa Askofu mkuu mpya wa Jimbo Kuu la Arusha, nchini Tanzania.

Jimbo Katoliki Moshi

 

18 March 2020, 16:54