Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili VII ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa: Upendo unaomwilishwa katika msamaha ni chachu ya upatanisho na utakatifu wa maisha! Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili VII ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa: Upendo unaomwilishwa katika msamaha ni chachu ya upatanisho na utakatifu wa maisha! 

Tafakari Jumapili 7 ya Mwaka A wa Kanisa: Upendo, Msamaha na Utakatifu!

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili VII ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa ni mwaliko wa kumwilisha upendo kwa Mungu na jirani ili kukoleza utakatifu wa maisha unaofumbatwa katika msamaha na upatanisho wa kweli! Waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanahasishwa kuwa ni watakatifu kama Baba yao wa mbinguni alivyo mtakatifu! Upendo, Msamaha na Utakatifu!

Na Padre Paschal Ighondo - Vatican.

Karibu ndugu msikilizaji wa Radio Vatican katika tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 7 ya mwaka A wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Somo la kwanza la katika kitabu cha Mambo ya Walawi, Mungu anawataka Waisraeli, taifa lake teule, waishi kitakatifu, wawe watakatifu kama yeye Mungu wao alivyo Mtakatifu, wadumishe uhusiano wao kati yao na Mungu kwa kuishika sheria kuu ya mapendo, wasichukiane wao kwa wao, kila mmoja asimchukie mwenzake kwa dhambi zake, wala asilipize kisasi, wala kuwa na kinyongo juu ya wana wa watu wao, bali kila mmoja ampende jirani yake kama nafsi yake.

Mtume Paulo katika somo la pili la waraka wake wa kwanza kwa Wakorintho bado anaongea juu ya mafarakano ya wakristo wa Korintho. Anawasihi wawe na umoja kwa vile Roho Mtakatifu anakaa ndani yao. Nasi tuone kwamba tukizusha mafarakano kati yetu tunaharibu hekalu la Mungu. Paulo anasema, kama mtu akiliharibu hekalu la Mungu, Mungu atamharibu mtu huyo. Kwa maana hekalu la Mungu ni takatifu, ambalo ndilo sisi tuliobatizwa kwa maji na Roho Mtakatifu. Kama mzaburi anavyotuambia kumjua Mungu ni mwanzo wa hekima ndivyo anavyosisitiza Paulo kuwa tusijione wenye hekima bali tujinyenyekeshe mbele za Mungu tupate kuhekimishwa kwa hekima yake maana hekima ya dunia hii ni upuzi mbele za Mungu.

Katika Injili ilivyoandikwa na Mathayo Yesu anatangua mtazamo wa Wayahudi, kuwa jirani kwao ni yule mtu wa taifa lao tu, watu wengine kama Wasamaria si jirani wala ndugu zao kwani ni najisi. Yesu anakazia kuwa kupendana bila kubaguana kiasi cha kumpenda hata adui yetu ndiyo amri kuu ya mapendo. Hivyo tusishindane na mtu mwovu, tusilipe ovu kwa ovu, bali tuushinde uovu kwa wema. Kwani kwa habari ya jicho kwa jicho sote tutabaki vibofu na habari ya jino kwa jino sote tutabaki vibogoyo. Yesu anasisitiza maisha ya kusaidiana na kusameheana akisema, na mtu atakayekushitaki na kuitwaa kanzu yako, mwachie na joho pia. Na mtu atakayekulazimisha mwendo wa maili moja, nenda naye mbili. Akuombaye, mpe; naye atakayekukopa kwako, usimpe kisogo, waombeeni wanaowaudhi; ili mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye mbinguni; maana yeye huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki.

Maana mkiwapenda wanaowapenda ninyi, mwapata thawabu gani? Hata watoza ushuru; Je! nao hawafanyi yayo hayo? Tena mkiwaamkia ndugu zenu tu, mnatenda tendo gani la ziada? Hata watu wa mataifa, je! nao hawafanyi kama hayo? Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu. Hivi ndivyo sisi tulibatizwa, tukamkataa shetani na fahari zake zote, na tukaahidi kumfuata Yesu Kristo aliyetoa maisha yake ili sisi tukombolewe kutoka utumwa wa dhambi tunavyopaswa kuishi. Maneno haya ya Yesu tunapswa kuyaishi katika ukamilifu wake bila kuongeza wala kupunguza lolote. Tumuombe Mungu Roho mtakatifu atuangazie tuweze kuyaishi haya mafundisho vyema ili siku moja tukayaishi katika ukamilifu wake huko mbinguni aliko Mungu Baba yetu.

Jumapili 7 Mwaka A
21 February 2020, 15:42