Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya kwanza ya Kipindi cha Kwaresima: Usikubali hata siku moja kufanya majadiliano na Shetani, Ibilisi, atakubwaga chini! Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya kwanza ya Kipindi cha Kwaresima: Usikubali hata siku moja kufanya majadiliano na Shetani, Ibilisi, atakubwaga chini! 

Tafakari Neno la Mungu: Jumapili ya Kwanza ya Kwaresima: Mapambano dhidi ya vishawishi!

Injili ya leo inatueleza bayana kwamba shetani alimwendea Yesu bila kuogopa na kumjaribu. Hapa tunatahadharishwa kuwa endapo shetani hakumwogopa Yesu, basi wafuasi wake Kristo tutaweza kujaribiwa kirahisi zaidi. Kwa hiyo mwinjili anataka kututahadharisha tusilogwe kumsikiliza shetani. Lugha ya shetani ni nzuri sana, lakini inadanganya na kutuponza. Hapo utashikishwa adabu!

Na Padre Alcuin Maurus Nyirenda, O.S.B., - Roma.

Binadamu aliumbwa kwa mfano na sura ya Mungu. Kufanana huko maana yake kuwa na roho au (spirit) ya Mungu, anayeitwa Roho Mtakatifu wa Mungu (the Holy Spirit) na kwa lugha nyepesi Roho huyo tungeweza pia kumwita kuwa ni DNA ya Mungu yaani “vinasaba vya Mwenyezi Mungu”. Kutokana na dhambi ya asili binadamu amempoteza DNA ya Mungu, Yaani huyo Roho Mtakatifu na mapaji yake yote. Yesu kwa kujifanya binadamu, alijimwilisha huyo Roho wa Mungu (DNA) katika ukamilifu wake wote pale alipobatizwa. "Ikawa Watu wote walipokwisha kubatizwa, na Yesu anaye amebatizwa, naye anaomba, mbingu zitakufunika, Roho Mtakatifu akashuka juu yake ka mfano wa kiwiliwili, kama hua;" (Lk 3:21), na "Sauti ikatoka mbinguni, 'Mwanangu, mpendwa wangu; nimependezwa nawe." (Lk 3:22). Roho huyo wa Baba na maweza yake yote saba ndiye aliyemsukumiza kwa nguvu Yesu kwenda jangwani. "Kisha Yesu alipandishwa na Roho nyikani, ili ajaribiwe na shetani" (Mt 4:1). Huko jangwani Yesu alisali, alifunga kwa siku arobaini na kujaribiwa na shetani. Mapaji ya Roho ya Mungu aliyempandisha Yesu jangwani yalimpa nguvu ya kushinda majaribu yote.

Nguvu ya Roho wa Mungu katika Kristo ni hazina iliyomo ndani ya kila binadamu. Mapaji au nguvu hiyo ya Roho wa Mungu ni silaha tunayoweza kuitumia katika maisha yetu ya kila siku hususani wakati huu wa Kwaresima. Ndugu zangu Injili ya leo inatueleza bayana kwamba shetani alimwendea Yesu bila kuogopa na kumjaribu. Hapa tunatahadharishwa kuwa endapo shetani hakumwogopa Yesu, basi wafuasi wake Kristo tutaweza kujaribiwa kirahisi zaidi. Kwa hiyo mwinjili anataka kututahadharisha tusilogwe kumsikiliza shetani. Lugha ya shetani ni nzuri sana, lakini inadanganya na kutuponza. Ukimfuata utafungwa naye na hautaweza kuwa huru na kumpendeza Mungu bali utakuwa mtumwa wa dhambi na kufuata mambo ya ulimwengu. Mawazo ya shetani kuhusu mtu aliyefanikiwa na mwenye furaha hapa ulimwenguni ni yule anayeishi vyema, mwenye chakula cha kumwaga, mwenye nyumba, mwenye afya na aliye maarufu. Mawazo hayo ndiyo yanayotufanya tudhani kuwa maisha hayo ndiyo yenyewe. Hebu tuone shetani anavyoshawishi, na jinsi Yesu anavyotumia mapaji ya Roho Mtakatifu aliye ndani mwake anavyopangua hoja.

Mathalani, Katika kishawishi cha kwanza, Yesu anaambiwa kugeuza mawe kuwa mikate. Mkate unawakilisha kila kitu tunachohitaji kwa ajili ya maisha hapa duniani. Kwa vyovyote shetani hawezi kutoa mkate kwa uzima wa milele. Yaani mali ya duniani hayawezi kumtosheleza binadamu. Ni dhahiri kwamba binadamu tunahitaji kula chakula. Mungu ameshatuandalia meza kwa ajili ya maisha haya. Kwa hiyo binadamu ni mkuu zaidi kuliko mali ya duniani. Ukitaka kuwa mkuu basi utumie mali ya maisha haya kwa ajili yake. Kumbe shetani anachomtakia binadamu ajilimbikizie mali haya kama vile yangekuwa Ngingamtima au kinga pekee ya maisha haya. HapaYesu anatumia paji la roho mtakatifu la hekima, akili na elimu kumjibu mshawishi: "Siyo kwa mkate pekee bali kwa kila Neno litokalo kinywani mwa Mungu."

Katika kishawishi cha pili, Shetani alimshawishi Yesu ajirushe kutoka juu hadi chini na malaika wangemdaka juu kwa juu. Hapa shetani anataka kumwingizia Yesu roho ya wasiwasi juu ya uwezo wa Mungu wa kulinda. Alimtaka Yesu amhoji Mungu kama anaweza kweli kumlinda au endapo kuna mmoja yuko juu yake zaidi au yuko peke yake. Shetani ndiye anaweza kutuingiza wasiwasi na kujihoji endapo Mungu anaweza kutulinda, au endapo kuna mmoja yuko tena juu yangu au la. Kama hayuko mtu zaidi, basi "ninashika sheria mkononi". Yaani, nitategemea mali ya ulimwengu huu. Kumbe binadamu tunaye Baba juu yetu. Katika yeye tunaweza kupata furaha. Kumbe binadamu tunapotegemea kufanyiwa miujiza katika imani yetu, hapo ujue dini hiyo ni ushirikina au uko kwa mganga wa kienyeji. Waamini wakatoliki hatuhitaji Mungu atende mambo ya pekee ili uweze kumwamini. Imani ina nguvu kwa yenyewe haihitaji kutendewa muujiza. Yesu akatumia paji la Roho Mtakatifu la Ushauri na nguvu kumjibu mshawishi kimkato: "Usimjaribu Bwana Mungu wako."

Katika kishawishi cha tatu, shetani anataka kummilikisha Yesu dola ya ulimwengu huu; anataka amezwe na malimwengu yaani balaa tu!. Hii inadhihirisha wazi kwamba shetani ndiye aliyeshika dola hadi sasa. Kwa vyovyote mantiki ya ulimwengu huu ni ile ya kila mmoja kufanya anavyotaka yeye, kwa sababu hadi sasa ulimwengu unafuata katiba ya chama tawala cha shetani. Katiba ya shetani ni ile ya kutafuta kiki, ya kutoangalia uso wa mtu unapotaka kuinuka kiuchumi. Yaani, unapotaka kufaulu inakubidi uangalie maslahi yako tu na kujiweka juu ya wengine. Hali hii ya kufuata mantiki ya utawala na ya ushindani hutaweza kujikubali na kuwa mtumishi na kuwajali wengine. Yesu anatumia paji la Roho mtakatifu la ibada na la kumwogopa Mungu na kumjibu shetani kwa ukali: "Nenda zako shetani, kwani utamwabudu Bwana Mungu wako peke yake."

Ndugu zangu, sisi waamini tumempata Roho Mtakatifu atokaye kwa Baba na kwa Mwana kwa hiyo tunaweza kumwita Mungu Baba Abba, yaani Baba Yetu! Kwa maneno mengine,  tunaweza kusali na kumwabudu Mungu kama waana wanaozungumza na baba yao. Ndiyo maana ya sala ya "Baba yetu..." Roho huyo ndiye aliyemsukumizia Yesu jangwani. Na ni roho huyo huyo ndiye aliye pamoja nasi hapa duniani na hasa sasa wakati huu wa kwaresima. Wakati huu ni mwafaka kutafakari mapaji ya roho mtakatifu na kuyatumia tunapopambana na vishawishi katika sala zetu, katika kufunga na katika kutenda matendo ya upendo. Tumwige Bwana wetu Yesu Kristo aliyejaa mapaji hayo ya Roho Mtakatifu kwa ukamilifu wake wote jinsi alivyoshinda vishawishi vya shetani. Nakutakia Kwaresima njema. Kumbuka daima hata siku moja usithubutu kujadiliana na Shetani, Ibilisi, utapata kipigo cha Mbwa koko!

28 February 2020, 17:00