Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu; Jumapili ya kwanza ya Kwaresima: Shindeni vishawishi kwa sala, kufunga, tafakari ya Neno la Mungu inayomwilishwa katika matendo ya huruma Tafakari ya Neno la Mungu; Jumapili ya kwanza ya Kwaresima: Shindeni vishawishi kwa sala, kufunga, tafakari ya Neno la Mungu inayomwilishwa katika matendo ya huruma 

Jumapili ya kwanza Kwaresima: Shindeni vishawishi kwa: Sala, Kufunga na Matendo ya huruma

Kwaresima ni kipindi cha kukuza fadhila hasa fadhila za haki, kiasi, huruma na kujiimarisha zaidi kiimani na kujenga muunganiko na Mwenyezi Mungu katika kuwatumikia ndugu zetu waliodhaifu na wahitaji ili tuweze kumwilisha ndani mwetu utamaduni wa upendo. Kipindi hiki cha Kwaresima ni safari ambayo kilele chake ni adhimisho la Fumbo la Pasaka: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu.

Na Padre Paschal Ighondo - Vatican.

Karibu ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, katika tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, domenika ya kwanza ya Kwaresima mwaka A wa Kanisa. Leo ni siku ya 5 tangu tumeanza kipindi hiki cha siku arobaini cha majiundo ya kiroho kwa kufunga, kusali, kutafakari Neno la Mungu na kufanya matendo ya huruma. Ni kipindi cha kukuza fadhila mbalimbali hasa fadhila za haki, kiasi, huruma na kujiimarisha zaidi kiimani na kujenga muunganiko na Mungu wetu Mtakatifu katika kuwatumikia ndugu zetu waliodhaifu na wahitaji ili tuweze kumwilisha ndani mwetu utamaduni wa upendo. Kipindi hiki cha Kwaresima ni safari ambayo kilele chake ni adhimisho la mateso, kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu kutoka utumwa wa dhambi. Kipindi hiki tulikianza siku ya Jumatano ya Majivu tulipopakwa majivu katika paji la uso. Tendo hili takatifu la kiroho ni ishara ya toba ya kweli. Tendo hili linatufanya tutambue ya kuwa sisi ni jumuiya ya wakosaji tunaohitaji kufanya toba ya kweli, kutakaswa na kufanywa upya watoto wa Mungu ndani ya Kanisa.

Somo la kwanza, kutoka Kitabu cha Mwanzo, linatupa mwanga na ufahamu wa chanzo na asili ya magonjwa, mateso na kifo kuwa ni dhambi ya asili, dhambi ya kutotii amri na maagizo ya Mungu iliyofanywa na wazazi wetu wa kwanza Adam una Eva. Mungu alimuumba mtu mzima, mwili na roho, akampa maisha ya heri na amani bila kufa. Hali hii ingedumu tu iwapo mtu angejinyenyekea chini ya mapenzi ya Mungu. Walakini mtu alimwasi Mungu. Kilichotokea kwa Adamu na Eva baada ya kumwasi Mungu kwa kukosa utii ndicho kilichotokea kwetu kwani asili yetu ilikuwa ndani mwao; biblia inasema; baada ya kutenda dhambi Adamu na Eva walitambua kuwa walikuwa uchi Mw. 3:7. Uchi unawakilisha hali ya udhaifu, hali ya kutojiweza, hali ya kupoteza neema na kuwa mbali na Mungu. Katika somo la pili kutoka barua ya Mtume Paulo kwa Warumi, Paulo anatuambia jinsi Mungu katika hekima yake na upendo wake alivyogeuza ubaya wa mwanadamu kuwa wema na alivyobadili laana ya mwanadamu kuwa baraka ya thamani kwa njia ya mateso na kifo cha mwanae Yesu kristu. Kumbe, Adamu wa kwanza aliingiza hali ya dhambi na mauti katika dunia hii na Adamu wa pili, yaani Yesu Kristo, alileta neema inayoshinda dhambi na mauti.

Kwa kila jumapili ya kwanza ya Kwaresma, Injili kwa mwaka A, B, C husimulia majaribu ya Yesu. Hii ni kutuambia kwamba kwaresma ni kipindi cha kupambana na majaribu na vishawishi vya shetani katika maisha yetu ya kikristo. Kishawishi ni nini? Kishawishi ni mvuto au msukumo kutoka ndani au nje ya mtu, unaomvuta au kumsukuma kutenda jambo zuri au baya. Vishawishi, mara nyingi hutujia katika namna mbili: Kwanza, tunasukumwa na vionjo vya miili yetu. Miili yetu inawaka tamaa mbalimbali kama vile kula au kunywa, kupenda au kupendwa, au kufanya chochote kile ambacho mwili unadai ufanye na kukusukuma kutoa uamuzi. Pili, tunashawishiwa na kuvutwa na watu wengine kutenda jambo fulani. Ushauri huo unaweza kuwa mzuri au mbaya. Yesu baada ya Ubatizo wake, anaongozwa na roho mtakatifu mpaka jangwani, kama waisraeli walipotolewa katika utumwa wa Misri walivyopita jangwani kuelekea nchi ya ahadi, anafunga kwa siku 40, kuwakumbusha Waisraeli walivyokaa jangwani miaka 40, Musa alivyokaa mlimani siku 40, gharika ilivyochukua siku 40, waninawi walivyofunga siku 40 ikimaanisha kipindi cha kutosha cha kufanya maandalizi kwa ajili ya jambo zito litakalotukia na kupokelewa.

Huko jangwani Yesu anafunga na kusali ili kujipatia nguvu ya kuwakomboa wanadamu kutoka katika utumwa wa dhambi. Katika mazingira hayo ya upweke shetani anamjaribu na kumshawishi Yesu avunje uhusiano wake na Mungu katika mpango mzima wa ukombozi. Kishawishi cha kwanza ni kutafuta heshima au sifa, Yesu anaambiwa jitupe chini toka hapa hutaumia maana imeandikwa atakutumia malaika zake wakulinde usijejikwaa, cha pili ni cha kutafuta ukuu au utawala, shetani anamwambia nitakupa mali hii kama ukiniabudu, na cha tatu ni kutafuta mamlaka na uwezo, shetani anamwambia amuru jiwe hili liwe mkate. Yesu alivishinda vishawishi hivi na majaribu hayo akasonga mbele na kazi ya kumkomboa mwanadamu kutoka utumwa wa dhambi kwa njia ya mateso nasi tunafurahia ushindi huo.

Katika jaribu la kubadili jiwe kuwa mkate, shetani anamshawishi Yesu abadili mwelekeo wa kazi yake ya kumkomboa mwandamu kutoka utumwa wa dhambi, kuelekea zaidi katika utumwa wa mahitaji ya kimwili kwa kumwambia afanye muujiza wa kubadili jiwe kuwa mkate ambao ndio mahitaji ya kila siku. Ndivyo alivyomjaribu Eva na kumwambia, Ati!  Hivi ndivyo alivyosema Mungu, Msile matunda ya miti yote ya bustani? Ni wazi hakuna maisha bila chakula cha kimwili. Lakini Yesu anatufahamisha kuwa binadamu sio mwili tu ana roho ndani mwake na roho ndiyo itiayo uzima, hivyo hatuishi kwa mkate tu, yaani mahitaji yetu ya kimwili peke yake bali tunahitaji pia chakula cha kiroho tunachokipata kwa kufanya mapenzi ya Mungu, ndiyo maana Yesu anasema; “chakula changu ni kuyafanya mapezi ya Mungu”. Jaribu hili la miujiza limetushika kwelikweli wakristo wa sasa, kizazi chetu cha sasa kinalilia miujiza, ya uponyaji wa magonjwa, miujuiza ya kuondokana na balaa na mikosi, kupata mume au mke, miujiza ya kupata kazi na mafanikio, miujiza ya kupanda vyeo miujiza kwa kila kitu tunachofanya. Kwaresima hii tufanye mabadiliko, tumrudie Mungu, tufanye toba ya kweli, tutapata Baraka na kibali machoni pa Bwana Mungu na tutafanikiwa katika maisha yetu.

Jaribu la kutafuta mamlaka, kupenda vitu kuliko kumpenda Mungu. Adamu na Eva wanaamua kutokumtii Mungu kwa kula tunda la mti waliokatazwa na Mungu ili wawe sawa na Mungu, wawe na mamlaka juu yao wenyewe. Yesu hakudhubutu kumjaribu Mungu, yeye hakufikiri kule kuwa sawa na Mungu ni kitu cha kung’ang’ania, hakutaka mamlaka za kisiasa au utajiri na mali alizoahidiwa na shetani. Yeye alibaki mwaminifu kwa Mungu Baba, akiwa mpole, mnyenyekevu, mvumilivu na mtiifu kwa Mungu, rafiki wa watoto, maskini na wanyonge, na sasa anafurahi milele yote mbinguni. Je kizazi chetu sasa kikoje. Kinatafuta mamlaka, ufahari, na nguvu kwa kila namna hata kwa nguvu za giza na mauaji ya watu wasio na hatia. Kwaresima hii tufanye mabadiliko, tumrudie Mungu, tufanye toba ya kweli, tutapata Baraka na kibali machoni pa Bwana Mungu na tutafanikiwa katika maisha yetu.

Kwaresima hii tusali na tufunge kwa ajili ya dhambi za mauaji ya kinyama kwa binadamu hasa wasio na hatia kwa ajili ya kulindi maslahi na mamlaka yao, tusali na kufunga kwa ajili ya wanaojitenga na Kanisa kwa kudai wanakarama hasa za kunena kwa lugha na uponyaji, tusali na kufunga kwa ajili ya wanaotafuta mali kwa njia zisizo halali, wanaojikusanyia mali ambazo wao wenyewe hawawezi kuzimaliza, tulie na kuomboleza, tumrudie Mungu kwa mioyo yetu yote. Hii ndiyo kwaresma yenyewe ambayo Jumatano ya majivu nabii Yoeli alituasa tuifanye toba ya kweli kwa kurarua mioyo yetu wala si mavazi yetu kwa kufunga na kuomboleza.

Majaribu ya Yesu ni kielelezo cha majaribu yote tunayokutana nayo kila siku katika safari yetu ya kuelekea mbinguni. Hakuna hata mmoja atakayemaliza maisha ya hapa duniani bila magumu au majaribu yoyote. Udhaifu wetu wa kimwili kama njaa, kiu, uchovu, wivu au tamaa ni majaribu ambayo yanatupatia mahangaiko, huzuni na ugomvi wa kila aina. Vipawa tulivyo navyo kama elimu, uwezo wa kuongea, cheo, au kuponya hutufanya tuwe na majivuno na kusababisha masengenyo, utengano na mauaji makubwa. Hivi kutokana na uwezo au nafasi tulizonazo katika maisha wengine tunajiona ni wa maana sana kuliko wengine na hivyo tutananyanyasa na kuwakatilia mbali kabisa. Hayo yote hutokana na vishawishi vya mali, heshima na mamlaka.

Hivyo tutambue kuwa tunakabiliwa na vishawishi vingi vya kila aina. Tunaalikwa leo kuvitambua vishawishi hivyo na tuwe tayari kukabiliana navyo. Kiongozi wetu Kristo aliyashinda majaribu yote. Nasi tukimtegemea Mungu tutashinda hayo yote pia. Tunaweza kuepuka vishawishi endapo tunasali daima, tunafunga, tunatenda matendo ya huruma, tunatenga muda wa kuongea na Mungu, tunashiriki Misa Takatifu na kupokea sakramenti hasa kitubio na Ekaristi pasipo unafiki na kufuru. Basi tuendelee kujiweka chini ya maongozi ya Mungu tukiomba neema na msaada wake ili tudumu katika imani yetu ili Kristo atakapofufuka tufufuke naye tutoke katika makaburi ya dhambi zetu tuuridhi ufalme wa mbinguni tuliotayarishiwa tangu kuumbwa kwa ulimwengu.

Tumsifu Yesu Kristo.

Jumapili ya Kwanza ya Kwaresima
28 February 2020, 16:33