Ujumbe kutoka Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Maghariki- RECOWA-CERAO: Chaguzi, ukwapuaji wa ardhi, mabadiliko ya tabianchi na uchimbaji mkubwa wa madini. Ujumbe kutoka Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Maghariki- RECOWA-CERAO: Chaguzi, ukwapuaji wa ardhi, mabadiliko ya tabianchi na uchimbaji mkubwa wa madini. 

Ujumbe wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Afrika Magharibi

Mkutano wa RECOWA_CERAO umejadili kuhusu chaguzi za kisiasa katika nchi za Afrika Magharibi, uporaji wa maeneo makubwa ya ardhi kwa kisingizio cha uwekezaji, athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na madhara ya uchimbaji wa madini. Wameangalia pia jinsi ambavyo Kanisa linapaswa kusimama kidete kwa ajili ya kulinda mafao mapana zaidi ya Bara la Afrika na watu wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Magharibi, RECOWA-CERAO, hivi karibuni, limehitimisha mkutano wake, ambao pamoja na mambo mengine, umejadili kuhusu chaguzi za kisiasa katika nchi za Afrika Magharibi, uporaji wa maeneo makubwa ya ardhi kwa kisingizio cha uwekezaji, athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na madhara ya uchimbaji wa madini. Wameangalia pia jinsi ambavyo Kanisa linapaswa kusimama kidete kwa ajili ya kulinda na kutetea mafao mapana zaidi ya Bara la Afrika na watu wake. Mkutano huu, umeongozwa na kauli mbiu “Tufanye kazi kwa pamoja kwa ajili haki jamii pamoja na utunzaji bora wa mazingira.

Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Magharibi linasema katika kipindi cha mwaka 2020 nchi kadhaa za Afrika Magharibi zitakuwa zinafanya chaguzi kwa ajili ya Rais na Wabunge. Nchi hizi ni pamoja na Burkina Faso, Pwani ya Pembe, Ghana, Guinea, Niger na Togo. Maaskofu wanawasihi watu wa Mungu Afrika Magharibi kuhakikisha kwamba, wanapiga kura kwa busara na uwajibikaji mkubwa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu katika ujumla wake. Viongozi wa kisiasa na wapambe wao, wananchi pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama; vinapaswa kuwajibika kikamilifu katika utekelezaji wa mchakato mzima wa chaguzi hizi, ili ziweze kuwa kweli ni chaguzi huru, haki na amani.

Wahakikishe kwamba, chaguzi hizi zinazingatia misingi ya ukweli na uwazi, ili matokeo yake yaweze kuridhiwa na watu wengi zaidi. Kanuni hizi zitasaidia kutoa ushuhuda wa ukomavu wa kisiasa na kidemokrasia Afrika Magharibi. Hakuna sababu ya kumwaga damu ya watu wasiokuwa na hatia nyakati za chaguzi kwani hizi ni dalili za kusinyaa kwa misingi ya haki na amani. Amani na utulivu ni mambo yanayopaswa pia kuzingatiwa hata baada matokeo ya chaguzi. Umefika wakati kwa wanasiasa kuanza kujenga utamaduni wa kukubali matokeo, ikiwa kama sheria, kanuni na taratibu zimezingatiwa. Kanisa kwa upande wake, litaendelea kufuatilia chaguzi hizi kupitia Tume za Haki na Amani za Mabaraza ya Maaskofu Katoliki katika nchi husika.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake wa Siku ya 52 ya Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2019 anasema “Siasa safi ni huduma ya amani”. Siasa safi ni msingi wa maendeleo endelevu na fungamani; demokrasia shirikishi na uongozi bora unaojikita katika hoja zenye mashiko na huduma kwa wananchi. Siasa safi inafumbatwa katika mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi kwa kuwashirikisha wadau mbali mbali mbali katika jamii; marika pamoja na tamaduni, daima wakijitahidi kujenga imani kati yao kama sehemu ya kukuza na kudumisha amani. Amani ya kweli inalinda na kuheshimu haki msingi; utu na heshima ya binadamu kama unavyofafanuliwa kwenye Tamko la Haki Msingi za Binadamu. Hizi ni haki ya: uhai, elimu, afya, utamaduni, uhuru wa kujieleza na uhuru wa kidini. Mtakatifu Yohane XXIII katika Waraka wake wa Kitume “Pacem in terris” yaani “Amani Duniani” uliochapishwa kunako mwaka 1963 anakazia: Ukweli, haki, upendo na uhuru na kwamba, haki na wajibu ni sawa na chanda na pete ili kujenga na kudumisha jamii inayofumbatwa katika msingi wa amani inayodumishwa katika upendo na msamaha.

Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Magharibi katika mkutano wake limebainisha kwamba, Bara la Afrika limebarikiwa kuwa na rasilimali na utajiri mkubwa kama ungetumika barabara, ungeweza kusaidia mchakato wa mapambano dhidi ya umaskini, ujinga na magonjwa yanayoipekenya familia ya Mungu Barani Afrika. Utunzaji bora wa mazingira ni changamoto inayojikita katika misingi ya haki, amani na maendeleo fungamani ya binadamu kwa sababu mazingira ni sehemu muhimu sana ya maisha ya mwanadamu. Hiki ndicho kiini cha Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko, “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”. Papa anakazia umuhimu wa kutunza mazingira, kama sehemu ya mchakato wa utekelezaji wa haki. Kwa bahati mbaya, Bara la Afrika limekuwa kama kichwa cha mwendawazi, mashirika na makampuni makubwa kimataifa yanaendelea kufaidika kwa utajiri wa madini na rasilimali za Bara la Afrika, wakati watu wa Mungu Barani Afrika wakiendelea kuteseka kwa baa la njaa, ujinga, magonjwa na umaskini

Uharibifu wa mazingira unalinganishwa na umaskini; anaihimiza jamii pamoja na kuendelea kutunza furaha, amani na utulivu wa ndani; mambo ambayo ni sawa na chanda na pete na kamwe hayawezi kutenganishwa. Sifa na utukufu kwa Mwenyezi Mungu ni matunda ya tafakari ya kina kuhusu kazi ya uumbaji inayomwajibisha mwanadamu kuilinda, kuitunza na kuiendeleza kama njia inayofaa kwa ajili ya kuheshimu kazi ya uumbaji na Mwenyezi Mungu ambaye ndiye Muumba mwenyewe! Baba Mtakatifu anawataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuwa na mwelekeo wa Kiekaristi katika mchakato wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote kwa kutambua kwamba, kazi ya uumbaji ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu ambayo mwanadamu amekabidhiwa kuitunza na kuiendeleza. Kumbe, anawajibu wa kushirikishana zawadi hii na jirani zake, ili watu wengi zaidi waweze kupata furaha kwa kushiriki matendo makuu ya Mungu katika maisha ya mwanadamu! Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Magharibi linawataka wanasiasa, wachumi na watunga sheria kuhakikisha kwamba, wanasaidia kulinda ardhi kwa wananchi wa kawaida kwani ardhi ni mtaji na rasilimali inayoweza kuwasaidia kuondokana na umaskini.

Maaskofu RECOWA
28 February 2020, 15:50