Kwaresima ni hija ya maisha ya kiroho inayompatia mwamini fursa ya kutubu na kumwongokea Mungu kwa kusali, kufunga, kutafakari Neno la Mungu na matendo ya huruma. Kwaresima ni hija ya maisha ya kiroho inayompatia mwamini fursa ya kutubu na kumwongokea Mungu kwa kusali, kufunga, kutafakari Neno la Mungu na matendo ya huruma. 

Kwaresima ni kipindi cha toba, kufunga, kusali, kutafakari na matendo ya huruma

Mama Kanisa anakianza kipindi cha Kwaresima kwa Jumatano ya Majivu, mwaliko wa kutubu na kumwongokea Mungu. Hii ni hija ya maisha ya kiroho inayofumbatwa kwa namna ya pekee katika toba na wongofu wa ndani ili kufanana zaidi na Mwenyezi Mungu; Kwa kusali na kufunga; kusoma, kutafakari na kumwilisha tunu za Injili katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili!

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.

Amani na Salama! Jumatano ya majivu ndio mwanzo wa kipindi cha neema cha Kwaresima. Tunaalikwa kufunga siku hii ambapo kila mmoja anapakwa majivu kwenye paji la uso na kukumbushwa kufanya toba, pia kuwa tu mavumbi na mavumbini tutarudi, ni kukumbushwa juu ya kifo chetu na hivyo mwaliko wa kufanya toba ya kweli na kubadili maisha yetu kwa dhati. Ni kuanza kujaribu kufanana na Mungu mwenyewe katika utakatifu. Kutenda na kufanya yote kadiri ya Mungu. Hilo ndio lengo kuu la Kwaresima kufanya mageuzi au “metanoia” ya maisha yetu kwa kufanana na Mungu. Furaha ya kweli haipo katika mateso tunayoweza kujipatia katika kipindi hiki maana sio lengo la maisha ya mkristo bali ni katika kuishi furaha ya kweli na kuwashirikisha wengine furaha hiyo. Tutaona hapo chini lengo na shabaha ya kutenda matendo ya huruma, kusali na kufunga ni ili tufanane na Mungu aliye furaha yetu ya kweli na si kinyume chake.

Katika maisha yetu kuna kishawishi kikubwa cha kufanya mema ili tuonekane na hata kusifiwa na wengine. Ni kishawishi cha hatari kwani kinatupelekea kuanza kujiabudu sisi wenyewe. Ni kujiweka katika nafasi ya Mungu mwenyewe. Ni kuwaalika wengine watuangalie sisi badala ya kumkazia macho Mungu mwenyewe kuwa ndio kielelezo cha maisha ya kila mfuasi wa Yesu Kristo. Na ndio maneno ya leo katika Injili tunapoanza kipindi cha neema za Kwaresma yanatuonya na kishawishi cha kutenda mema ili kuonekana na watu. Thawabu yetu yapaswa kuwa mbinguni na kamwe sio ya kujionesha kwa wengine ili tusifiwe au kuonekana tunafanya jambo jema. Labda yafaa kutafakari zaidi juu ya thawabu anazozizungumzia Yesu katika Injili ya leo.

Thawabu tunaona ni ‘’motif ‘’au wazo linalojirudiarudia mara 7 katika Injili ya leo. Wazo la thawabu lilikuwa ni wazo la msingi kabisa katika imani ya kifarisayo. Mtu mchamungu aliyeenenda kadiri ya amri na maagizo ya Mungu, basi huyo alijiwekea thawabu zake mbele ya Mungu na hivyo kubarikiwa na kinyume chake basi alipokea laana na kila aina ya ubaya iwe hapa duniani na maisha ya baadaye. Hata katika Agano Jipya wazo la kupata thawabu au adhabu tunakutana nalo mara nyingi. Ndipo mwana wa Adamu atakapokuja katika utukufu wake pamoja na malaika wake na kumpa kila mmoja kadiri ya matendo yake. Rejea Matayo 16:27 na hata kujiwekea hazina yetu mbinguni. Matayo 6:20

Hivyo kwa haraka haraka tunaweza kusema kuwa kwa thawabu basi Yesu anamaanisha kama tunavyoweza kutafsiri hizi aya jinsi zinavyosomeka. Lakini yafaa tukumbuke na kuzingatia kuwa mwaliko wa Yesu ni kufanana naye na ndio kutoa maisha yetu bila kujibakiza wala kungojea faida au thawabu fulani. Ni mwaliko wa kujitoa kamili bila kujibakiza kama alivyofanya yeye pale msalabani. Ni kuutoa uhai kwa ajili ya mwingine, na ndio furaha ya kweli inapatikana na si kwa kuangalia masilahi yangu binafsi. Thawabu anayotuambia Yesu leo katika Injili sio sehemu ya heshima mbinguni ila ni kuwa na uwezo wa kupenda bila kujibakiza kama Yeye, na ndiko kufanana na Mungu kwa hali ya ndani kabisa, kuwa watu tunaopenda kweli kwa namna na jinsi ile ya Mungu mwenyewe. Hivyo zawadi yetu ni furaha katika kupenda kama Mungu anavyotupenda, kushiriki katika hali yake ya Kimungu na ndio kushirika au kuujenga ufalme wa Mungu hapa duniani.

Ili KUKUA KATIKA KUFANANA NA MUNGU tunaona katika kipindi hiki cha Kwaresima tunaalikwa kufanya mambo makuu matatu lakini katika muono tofauti na ule wa kifarisayo yaani: Kusaidia maskini/matendo ya huruma, kusali na kufunga. Nyakati za Yesu  kulikuwa na utaratibu kwa kila kijiji kusaidia maskini na wasiojiweza kwa matoleo yaliyokusanywa siku ya Sabato katika masinagogi yao. Hivi siku ya Sabato walitoa matoleo hayo yaliyojulikana pia kama ‘’tzedakàh’’ yaani sadaka kwa namna ya kujionesha. Hivyo aliyetoa kiasi kikubwa aliweza kuitwa mbele na Rabbi ili aonekane na wote na kukaa karibu na marabi wa kiyahudi waliowajibika katika kuongoza ibada za Neno la Mungu siku za Sabato.

Ni katika muktadha huu tunaona Yesu anatuonya wanafunzi wake kutokufanya wema ili kujionesha au kuonekana kuwa tumefanya wema kwani kwa kufanya hivyo tunakuwa mbali na ile thawabu ya kufanana na Mungu anayetufanyia wema wake kila siku na wakati mwingine anabaki amejificha hivi hata wengine kutokiri wema na uwepo wake. Kusaidia maskini hakuna budi kusukumwa na upendo wa kweli ndani mwetu na sio kujitafuta na kumdhalilisha au kumshusha muhitaji anayefika kwetu au tunaokutana nao siku kwa siku. Na ndio sadaka ya kweli kama tunavyoona katika lugha ya kiyunani ‘’tzedakàh’’ ambayo maana yake sisisi ni haki. Na ndio hata Mtakatifu Ambrosi anaelezea sadaka kwa muhitaji ni kumpa iliyo haki yake. Vyote tulivyo navyo katika ziada hatuna budi kutambua kuwa ni kuwadhulumu wengine wasiokuwa na kitu kabisa. Ni ziada iliyotokana na kujilimbikizia kwetu katika maisha.

Kama nina mashati mawili anatukumbusha kuwa moja sio langu bali ni la ndugu yangu asiyekuwa na nguo.  Na ndio mwaliko wa kuachana na ubinafsi kwa kujilimbikizia katika maisha, ni kuwa na maisha ya kuwa na kiasi na kuwakumbuka wahitaji. Vyote tulivyonavyo navyo si mali yetu bali ni mali ya Bwana. Zaburi 24 Hivyo tunaalikwa kutenda haki na ndio kuwapa wengine mastahili yao. Hivyo katika kusaidia wahitaji sio kwamba nawafanyia upendeleo bali ni kuwashirikisha yale mema ya Mungu tuliyokabidhiwa kuwa watunzaji tu. Yafaa kufanya matendo ya huruma kwa unyenyekevu mkubwa maana ni kuwashirikisha wengine mema ya Mungu na kamwe si mema yetu! Kwaresima pia tunaalikwa kuwa ni kipindi cha sala. Ulimwengu wa leo yafaa tukiri kuwa wengi wetu hatujui tena maana ya sala na jinsi ya kusali vizuri.  Yesu anatuonya kutopayukapayuka maneno kama wafanyavyo wapagani. Lakini pia tunajiuliza kwa nini tusali wakati Mungu anajua kabla hali yetu na hata mahitaji yetu ya ndani? Matayo 6:8

Katika nyakati za Yesu kama leo kulikuwa na aina kuu mbili za sala nazo ni sala za jumuiya na zile za binafsi. Sala za jumuiya ndizo zilifanyika hekaluni, katika masinagogi na hata sehemu za wazi na zilifanyika mara mbili kwa siku, yaani saa 3 asubuhi na saa 9 alasiri na mara moja kwa mwaka walitolea sadaka hekaluni kule Yerusalemu kwa kila myahudi mchamungu. Yesu hapingi taratibu hizi za kusali maana hata naye alisali na alienda Hekaluni ila anawaonya juu ya namna wanavyosali mintarafu thawabu.  Wasifanye kwa ajili ya kujionesha au kusifiwa bali ni kujaribu kufanana na Mungu tunayeongea naye katika sala zetu. Nasi lazima kuwa makini na namna yetu na sababu ya kusali, je ni ili nionekane na kusifiwa kuwa mimi ni mtu wa sala au ni muda wa kuwa na Mungu ili niweze kufanana naye zaidi siku kwa siku?

Na upande wa sala binafsi Yesu anatualika kuingia chumbani kwa maana katika hali ya kubaki mimi na Mungu wangu tu. Ni kuingia katika mdahalo na huyu anayenijua mimi undani wangu, ni kubaki naye katika mdahalo si tu wa mimi kuzungumza bali zaidi kumsikiliza. Ni mazungumzo ya masikilizano kwa pande zote mbili yaani Mungu na sisi tulio wanae, ni mdahalo wa upendo na kirafiki ni moyo unaoongea na moyo mwingine kama Baba Mtakatifu Francisko anavyotuambia katika ujumbe wake wa Kwaresima mwaka 2020. Ni kuliweka kati fumbo la Pasaka katika maisha yetu ya kila siku. Ni mdahalo na Mungu sio ili kumshawishi ili afanye kadiri ya matakwa yangu mimi na matamanio yangu bali kukubali mipango ya Mungu katika maisha yangu.  Ni kujikabidhi ili neema yake itutie nguvu ya kuenenda kadiri ya mpango wake katika maisha yetu. Ni kujinyenyekeza kwake mzima mzima bila kujibakiza na hapo inakuwa ni sala ya kweli na sio kutaka yafanyike kadiri yetu na matamanio yetu katika maisha.

Ni kukubali kushiriki fumbo la ukombozi yaani mateso, kifo na ufufuko. Na daima tunapokuwa katika safari ya kipindi cha Kwaresma hatuna budi kukumbuka ni kuadhimisha fumbo la Pasaka, ni kubaki na tumaini na faraja ile ya kipasaka. Hivyo sala ni kujiweka wazi mbele ya Mungu, ni kumsikiliza Mungu ili kuweza kujua ni nini mpango wa Mungu katika maisha yangu. Na ndio tunaalikwa kuangalia pia mahali ambapo tunaweza kujikusanya kweli na kuweza kuingia katika mazungumzo ya kina na Muumba wetu. Yesu alijua jinsi ya kusali na hata kuchagua mahali ambapo alijitenga na ulimwengu ili aweze kubaki na Baba yake wa Mbinguni. Marko 1:35; 6:46; Luka 5:16; 6:12. Sala ya kweli thawabu yake ni kutuunganisha na Mungu ili nasi tuweze kuenenda kadiri ya mpango wake kwetu.

Kwaresima pia ni kipindi cha kufunga.  Kufunga katika dini nyingi inachukuliwa kama aina ya kujitesa na kujinyima na hata wengine kipindi hiki utasikia wakisema wanalala chini bila godoro au wanazima simu zao au mitandao ya kijamii au wanajikatalia kula nyama au kunywa bia au mvinyo au hata soda, na mambo mengi mengine watu wanajikatalia katika kipindi cha Kwaresma. Wakati wa Yesu kama tulivyoona katika historia fupi ya Kwaresma wengine walijipaka majivu na kuvaa magunia kama ishara ya toba kwa kujitesa na kujikatalia. Kufunga chakula kati ya Wayahudi ilikuwa ni kitu cha kawaida na hivyo wachamungu walifunga mara mbili kwa wiki bila kula wala kunywa kuanzia waawio ya jua mpaka machweo yake, ilikuwa ni kila Jumatatu na Alhamisi. Na hata Marabi waliwasisitiza wanafunzi wao kushika amri hii ya kufunga kila wiki. Luka 18:12. Na ndio katika himaya ya Kirumi kukawa na msemo mashuhuri mpaka leo kati ya Warumi kuwa unafunga kama Myahudi.

Katika Agano Jipya mkazo juu ya umuhimu wa kufunga tunaona ni kidogo sana maana Mtume Paolo katika nyaraka zake hataji hata mara moja na Yesu anazungumzia mara mbili tu juu ya kufunga, yaani pale alipoulizwa kwa nini wanafunzi wake hawafungi na katika Injili ya leo. Ni katika Injili ya leo anatuonesha lengo na shabaha ya kufunga sio kujitesa au kubaki na njaa bali kuwashirikisha wengine furaha na tumaini lile lililopo ndani mwetu. Baba Mtakatifu katika upande huo wa kufunga anatusisitiza kwa maneno yafuatayo nakuu ‘’Charitable giving makes us more human, whereas hoarding risks making us less human’’. Hakika ni katika kutoa kwa upendo ndipo ubinadamu wetu unapata kuonekana na si kinyume chake.

Jumuiya ya Wakristo tunajua kuwa tupo siku zote na Bwana harusi yaani Kristo mwenyewe mpaka mwisho wa nyakati na hivyo mfungo hauna maana kwetu.  Mathayo 28:20 Hivyo tusifunge kama wafanyavyo wanafiki kwa kukunja sura zao bali kuosha uso na kuupaka mafuta. Ni kuwa na uso wa matumaini na furaha na kuwashirikisha wengine furaha na matumaini yetu. Mfungo ni mwaliko wa kufurahi kwani tunaalikwa kuwa na furaha kwa kujikatalia kwetu ili ndugu yetu muhitaji abaki na furaha kwa kushirikishwa mema aliyotujalia Mwenyezi Mungu. Furaha ya kweli hupatikana katika kupenda! Mfungo wetu hauna budi kukubaliwa na Mungu kwa kumuiga Mungu mwenyewe kufungua mioyo yetu kwa upendo na kumwelekea kila muhitaji anayetuzunguka katika nyumba zetu, makazini, na popote pale wanapokuwepo wahitaji. Sio kujinyima kwa sababu tunataka kufanya tu diet au malengo na makusudio kama hayo yenye nia za kujipenda sisi wenyewe. Naomba kusisitiza hili kila ninachojinyima naalikwa kumshirikisha mwingine aliyemuhitaji zaidi.

Nawaalika pia kusoma tupatapo nafasi Isaya 58:6-7 na Zakaria 7:5-10 na kwa wale wanaoweza kupata kitabu cha “Pastor of Erma” kilichosomwa sana na waamini wakristo wa karne ya pili. Ni mwaliko wa kuelewa funga ya kweli ni ipi. Baba Mtakatifu Francisko katika mojawapo ya mahubiri yake anatualika pia kufunga ndimi zetu kwa kuzing’ata ili zivimbe ili kuepuka kusengenya na kuwasema vibaya wengine. Labda ni mfano wa kichekesho ila tukumbuke Kwaresima inakuwa na maana tu kama tunajaribu kufanana zaidi na Mungu kwa kuwapenda wengine na hivyo wakati mwingine tunaweza kusali au kutoa sadaka na kufunga ila kama hatuna upendo kwa mwingine ni kazi bure. Tumuombe Mungu mfungo wetu wa Kwaresima utusaidie kufanana zaidi na Mungu. Nawatakieni nyote kila lililo jema katika safari hii ya siku 40 za kutenda matendo ya huruma, kusali na kufunga vyote vikilenga kutusaidia kufanana zaidi na Mungu.

26 February 2020, 06:59