Kipindi cha Kwaresima ni muda muafaka wa kuimarisha kinga za maisha ya kiroho ili kupambana na vishawishi pamoja na malimwengu! Kipindi cha Kwaresima ni muda muafaka wa kuimarisha kinga za maisha ya kiroho ili kupambana na vishawishi pamoja na malimwengu! 

Kipindi cha Kwaresima: Imarisheni kinga ya maisha ya kiroho!

Kadiri ya mapokeo ya zamani, kanisa hili la Mtakatifu Sabina lilikuwa ni moja ya vituo walivyoita “Stational churches”. Vituo hivyo vilichaguliwa ili kufanya ibada za pekee za asubuhi na jioni wakati wa Kwaresima, wakati wa Pasaka na hata siku nyingine maarufu za Kipindi cha mwaka wa Liturujia. Mapokeo haya ya Kirumi yalilenga kuimarisha roho ya kijumuiya katika kanisa.

Na Padre Alcuin Maurus Nyirenda, O.S.B., - Roma.

Kila mwaka Jumatano ya Majivu, Baba Mtakatifu anaadhimisha Ibada ya Misa Takatifu na kuwapaka Majivu waamini katika Kanisa la mtakatifu Sabina lililoko juu ya kilima cha Aventino-Roma. Pamoja na Baba Mtakatifu, waamini wote ulimwenguni tunaanza safari refu ya siku arobaini ya Kwaresima kwa kupakwa majivu na maaskofu na mapadre katika makanisa yetu. Kadiri ya mapokeo ya zamani, kanisa hili la Mtakatifu Sabina lilikuwa ni moja ya vituo walivyoita “Stational churches”. Vituo hivyo vilichaguliwa ili kufanya ibada za pekee za asubuhi na jioni wakati wa Kwaresima, wakati wa Pasaka na hata siku nyingine maarufu za Kipindi cha mwaka wa Liturujia. Mapokeo haya ya Kirumi yalilenga kuimarisha roho ya kijumuiya katika kanisa.

Kwa hiyo daima Baba Mtakatifu alivitembelea vituo hivyo ili kuadhimisha Misa pamoja na waamini wa hapo. Kila kituo kilitambulika kwa jina la mtakatifu fulani aliyekuwa mlinzi wake. Waamini waliamini kuwa mtakatifu huyo alikuwa kati yao, akiongea nao na kuabudu pamoja nao. Mathalani, katika misale tunasoma, “Statio ad Sanctum Paulum” - Kigango (kituo) cha Mt. Paulo. Ikimaanisha kwamba, katika liturjia hiyo Paulo alikuwa kati yao akishiriki kama kiongozi na kipeo cha waabudio hapo. Kwa hiyo waamini waliungana tikitiki na fumbo la umoja na mtakatifu wao kwa kushiriki utukufu wake na kwamba katika mtakatifu huyo walikuwa pia na Bwana wetu Yesu Kristu katika Misa Takatifu. Kituo cha mtakatifu Sabina (sasa Basilika la Mt. Sabina) kilijengwa karne ya tano, kipindi ulipoanzia utamaduni huu wa vituo. Hivi kikaitwa “Titulus Sabinae”, yaani kituo cha nyumbani kwa mt. Sabina. Mtakatifu huyo aliuawa shahidi mwaka 114. Jinsi miaka ilivyozidi kupita, vituo hivyo (tituli) vikaja kuwa maparokia ya kwanza ya Roma na hatimaye yamekuwa mabasilika.

Dominika ya kwanza ya kwaresima tutasikia kuwa Roho Mtakatifu anamsukumiza Yesu Jangwani kwenda kujaribiwa na shetani. Kwa wakristu pia, wakati wa Kwaresima Kanisa linawasukumiza wakristu wote kwenda jangwani na kusafiri pamoja na Kristu kwa siku arobaini. Katika kipindi hiki wakristu wanapambana na majaribu mengi. Kwaresima ya mwaka huu inaambatana na jaribio kuu lililoikumba dunia nzima la Virusi vya Corona. Lakini kwetu yabidi tukumbuke kwamba kabla ya safari yoyote ile refu, au kabla ya kwenda vitani, au kuwinda wanyama wakali Wahenga wetu wakifanya maandalizi ya kutosha ikiwa ni pamoja na kujinyima ndoa, kutokunywa pombe, nk. Walitolea sadaka na kusali kwa mahoka ili walindwe. Waliandaa pia pamba au chakula cha njiani ili kula pamoja na wenzie. Walikunywa pia dawa ya kinga kama ilivyokuwa kwa vita ya Majimaji.

Maandalizi hayo yaliitwa Kinga ya roho au kwa lugha ya “Kingoni Ngingamtima”. Leo waamini tunapata "Ngingamtima", itakayotukinga kipindi chote cha Kwaresima.  Aidha Ngingamtima hii inaweza pia kutukinga na Corona virus. Kwanza tunapakwa majivu (kujipaka dawa). Lakini Ngingamtima itayotukinga na kutusaidia sana na virus hii na hasa itasaidia kuponya roho zetu dhidi ya shetani ni Sala, Kufunga, na Matendo ya huruma. (Mat. 6:1-6, 16-18). Kingamtima hii imegunduliwa na wahenga wetu kwa hekima kubwa sana. Ugunduzi wao ulitokana na mang’amuzi ya muda mrefu ya watakatifu waliofanikiwa kuwa karibu sana na Mungu wakati huu wa Kwaresima kwa kutumia Kingamtima ya sala, kufunga na kufanya matendo ya huruma. Aidha, Kingamtima hiyo inatokana na hekima ya mafundisho ya Yesu. Kama tulivyoishasikia katika Injili, kwamba Yesu alifundisha juu ya faida ya sala, ya kufunga na ya kufanya matendo ya huruma. Yesu aliyetutangulia kusafiri Jangwani ni mfano wetu pia katika kipindi hiki cha Kwaresima. Mapendo yetu kwa Yesu yanatuvuta kuwa naye karibu na kutuimarisha katika safari yetu. Hivyo tutaweza tu kusafiri salama siku hizi arobaini kwa kushika masherti ya ngingamtima hii ya kusali, kufunga na kufanya matendo ya huruma.

Ngingamtima hii aliitumia Yesu kumkemea Shetani, Ibilisi Jangwani (Lk 4:1-13). Mathalani, Ngingamtima ya Sala, Yesu alimkemea shetani aliposema: "utamwabudu Bwana Mungu wako, na utamtumikia Yeye tu" (Lk 4:8, na Walawi (Kumb, la Torati 6:13). Yaani, mafundisho ya Yesu yalilenga kumpa Mungu kipao mbele katika sala na katika kumwabudu. Hivi Yesu anataka kutufundisha kumweka Mungu kwanza katika sala na katika kuabudu. Mbele ya magonjwa yawayo yote, tumtolee Mungu maisha yetu kwa kusali na kumwabudu. Halafu Ngingamtima ya Kufunga: Yesu alimwambia shetani bayana kabisa kwamba "Mtu haishi kwa mkate tu" (Lk 4:4, na Kumb 8:3). Yesu anatukumbusha kwamba kufunga kunadhihirisha ukuu na ubora wa Mungu zaidi kuliko kuwania (kutaka) mali ya malimwengu.

Kwa vile kipindi hiki kinatudai zaidi kuacha dhambi, hivi mfungo unatupatia nguvu za kutotenda dhambi. Aidha, mbele ya gonjwa hili Mungu ametaka kutushtua ili tumtambue kwani amegusa uhai anaojivunia binadamu kiasi cha kumsahau aliyempa uhai huo. Na nchi iliyogubikwa n giza la kutomjua Mungu kabisa ndiko huko amerusha jiwe na ulimwengu mzima unalia hivi yaonekana jiwe limetutua pahala pake. Hivi Virusi Corona hii pamoja na mfungo vitukumbushe kuacha dhambi na kutong'ang'ana na mali yanayoweza kutufikisha pabaya. Kisha Kingamtima ya Matendo ya huruma: Yesu alimtolea uvivu shetani na kumwambia: "Usimjaribu Bwana Mungu wako" (Lk 4:12 na Kumb 6:16). Hapa Yesu anatukumbusha kutokumjaribu Mungu na kumtaka eti aingilie kati hata kuwashughulikia wahitaji na maskini badala ya kusaidiana sisi wenyewe kwa wenyewe. Tutumie wakati huu tunapokumbukwa na majanga ya mateso na vifo kusaidiana na kutahadharishana. Tusisahau kumpa Mungu kipaombele kwa sala na kuabudu, tuache dhambi na kutokumbatia mali kwa kufunga na tusimjaribu Mungu kwa kutokusaidiana sisi wenyewe. Nakutakia safari njema ya Kipindi cha Kwaresima.

26 February 2020, 17:03