Jumatano ya Majivu ni mwanzo wa Kipindi cha Kwaresima kinachosimikwa katika: toba na wongofu wa ndani; sala, tafakari ya Neno la Mungu; kufunga pamoja na matendo ya huruma. Jumatano ya Majivu ni mwanzo wa Kipindi cha Kwaresima kinachosimikwa katika: toba na wongofu wa ndani; sala, tafakari ya Neno la Mungu; kufunga pamoja na matendo ya huruma. 

Jumatano ya Majivu: Mwanzo wa Kipindi cha Kwaresima: Toba!

Siku hii huitwa Jumatano ya Majivu kutokana na tendo la kupakwa majivu katika paji la uso na wakati huo mhudumu wa tendo hili takatifu la kiroho anasema maneno Mwanadamu kumbuka, u mavumbi wewe na mavumbini utarudi. Jina hili la Jumatano ya Majivu, lilianza kutumika rasmi mwaka 1099 na Papa Urbani II, mwanzoni iliitwa “Mwanzo wa Mfungo”. wa Kwaresima!

Na Padre Paschal Ighondo - Vatican.

Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, karibu katika tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, katika Siku ya jumatano ya majivu tunapoanza kipidi cha kwaresma. Leo ni Jumatano ya Majivu, Siku rasmi na ya kwanza katika kipindi cha Kwaresima, kipindi cha toba, kipindi cha kujipatanisha na Mungu. Siku hii huitwa Jumatano ya Majivu kutokana na tendo la kupakwa majivu katika paji la uso na wakati huo mhudumu wa tendo hili takatifu la kiroho anasema maneno Mwanadamu kumbuka, u mavumbi wewe na mavumbini utarudi. Jina hili la Jumatano ya Majivu, lilianza kutumika rasmi mwaka 1099 na Papa Urbani II, mwanzoni iliitwa “Mwanzo wa Mfungo”. Majivu ni nini? Majivu ni mabaki ya vitu vilivyochomwa moto. Majivu yanayotumika siku hii ya Jumatano ya Majivu ni mabaki ya matawi ya mitende yaliyochomwa moto. Matawi haya ni yale yaliyotumika Jumapili ya Matawi ya mwaka uliopita ambayo yanaashiria ushindi na amani dhidi ya kifo na mauti kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo.

Majivu ni alama au ishara tu ya nje inayoashiria toba tunayoifanya ndani ya mioyo yetu na manufaa yake. Kwanza kabisa ni arngi yake. Majivu yana rangi ya kijivu. Hii ni rangi ya toba na matumaini. Kupakwa majibu ni ishara ya toba yetu ya ndani ya nafsi zetu tunayoifanya ambayo inatutakasa na kutusafisha na uovu wote, kama Majivu yanavyotumika kusafisha vyombo. Kumbe, kupakwa majivu kwa maana nyingine ni kusema kuwa tu wachafu, tu wadhambi tunahitaji kutakaswa katika Sakramenti ya Upatanisho. Majivu ni mbolea na mbolea hutumika kukuza mimea na kuifanya izae matunda mema, mengi na bora. Toba ya kweli hutusaidia kukua na kuzaa matunda mema ya kiroho. Majivu yanapakwa kwenye paji la uso, kama vile siku ile ya Ubatizo tulipakwa mafuta ya Krisma takatifu, tukaondolewa dhambi ya asili na adhabu zake zote, kwa ishara ya msalaba alama ya ushindi tuliyokombolewa nayo. Kumbe, majivu yanatukumbusha kufanya toba na kuungama dhambi tulizotenda baada ya ubatizo.

Kwaresima ni kipindi cha siku arobaini za kufunga, kusali, kutafakari Neno la Mungu na kufanya matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Ni kipindi kinachotualika kumwilisha ndani mwetu utamaduni wa upendo, kwa kufunga na kutenda matendo ya huruma, kama vile kuwasaidia wahitaji hasa maskini, kuwatembelea wagonjwa na hata wafungwa. Kipindi hiki cha Kwaresima ni safari ambayo kilele chake ni adhimisho la fumbo la ukombozi wetu yaani : mateso, kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo tunaloliadhimisha katika juma kuu, kuanzia alhamisi kuu, ijumaa kuu na jumamosi kuu, kilele chake ni dominika ya Pasaka. Kusali, kujitoa sadaka kwa ukarimu kwa wahitaji na kufunga, ndizo nguzo kuu tatu za kipindi cha Kwaresima, kipindi cha toba.

Kupakwa majivu katika paji la uso ni kukiri hadharani bila kujificha kuwa ni mdhambi na unahitaji huruma ya Mungu Baba, unahitaji msamaha, unahitaji kutakaswa na kufanywa upya mtoto wa Mungu na wa kanisa.Tendo hili la kiroho la kupakwa majivu katika paji la uso ni ishara ya toba ya kweli, ishara ambayo imekuwa ikitumika kwa maelfu ya miaka iliyopita hata kabla ya kuja Kristo. Katika ulimwengu wa wayahudi majivu yalikuwa ni alama ya huzuni, masumbuko, uchungu au uduni (Ayubu 2:8, 30:19; Zab 102:10). Baadaye utamaduni huu wa kupakwa majivu ulitumiwa na wakristo wa kwanza kama alama ya toba. Mwaka 600 hivi, Gregory Mkuu aliifanya Siku ya Jumatano ya majivu kuwa siku ya kwanza ya Kwaresma na akaongeza urefu wa kipindi hiki cha toba hadi siku arobaini. Miaka ya 800 hivi, baadhi ya makanisa yaliadhimisha ibada ya Jumatano ya majivu kwaajili ya wadhambi waliokubuhu katika dhambi na waliojulikana. Sasa pale walipoamua kufanya toba ndio walipakwa majivu. Hivi wakati huu si wote walipakwa majivu ila tu wale waliokuwa wadhambi waliojulikana wazi, kama vile makahaba, wauaji na waasi. Kuanzia karne ya 11, Kanisa lilipanua ibada hii na kuwahusisha waamini wake wote kwani mbele za Mungu hakuna asiye na dhambi. Tendo hili liliambatana na kufunga, kusali, kutoa sadaka, na kufanya matendo ya huruma.

Kama ilivyokuwa nyakati za Nabii Yoeli leo hii Mwenyezi Mungu nasi anatuita tumrudie kwa mioyo yetu yote, kwa kufunga na kwa kulia na kwa kuomboleza. Tunalikwa tuirarue mioyo yetu, na siyo mavazi yetu. Mwaliko huu si wa mtu mmoja mmoja, bali ni mwito wa watu wote, kama anavyosema Nabii Yoeli, kusanyikeni kusanyiko kuu; kusanyikeni watu, litakaseni kusanyiko, kusanyikeni wazee, kusanyeni watoto na hao wanyonyao maziwa (Yoe 2:15). Naye Mtume Paulo, katika somo la pili la Waraka wake wa pili kwa Wakorintho, anatusihi tukubali kupatanishwa na Mungu kwa njia ya Kristo yeye asiyejua dhambi alifanywa kuwa dhambi kwa ajili yetu, ili sisi tupate kuwa haki ya Mungu katika Yeye (2Kor 5:21).

Katika Injili Yesu anatuonya tusiwe wanafiki, tusifanye matendo mema ili tuonekane machoni pa watu wengine, kwani kwa kufanya hivyo tunakuwa tumepokea thawabu yatu kwa njia ya watu wanaotutazama, kutustaajabia, na kutusifia. Kumbe, matendo yetu mema yasiwe yale yanayolenga kujionesha kwa watu wengine, bali yawe ni mawasiliano binafsi kati yetu na Mungu yaani kujenga muungano na Mungu wetu aliyemtakatifu mtakatifu kwa sala, sadaka na kufunga. Tutembee wakati wote na Kristo katika maisha yetu, kuanzia asubuhi tunapoamka hadi tunapoelekea kulala, wakati wa usiku. Matumaini ya mfungo wetu hayana budi kujengeka katika njaa na kiu ya muungano na Mungu wetu mtakatifu. Muungano huu unawezekana tukiwafungulia mlango wenzetu hasa wahitaji na kuwapatia yale tutakayojinyima. Ni katika mfungo ndipo tunaweza kuiga mfano wa Msamaria mwema, anayejitolea kumsaidia mhitaji bila kuangalia tofauti zao. Mfungo unaoambatana na huduma kwa wahitaji ni njia ya kushinda tofauti zetu na vishawishi vinavyoambatana na tofauti hizo. Kwa hiyo, tunaalikwa katika kila hali tuliyonayo tushiriki mfungo huu wa Kwaresima kwa malengo zaidi ya maisha yetu ya kiroho.

Hatua za kuchukua ili tuweze kufanya vema mapinduzi ya kiroho, toba na kubadilika. Tukubali kwamba sisi ni wadhambi. Tusipokubali kuwa sisi ni wadhambi hatutaona hitaji la kufanya toba na kubadilika. Hivi kila atakayepakwa majivu leo anakubaliana na ukweli huu. Sala, kufunga na matendo ya huruma ni mambo matatu ambayo tunahimizwa kuyafanya katika kipindi hiki cha Kwaresma. Yesu anatuangalisha kuwa, ili tuweze kufaidika kutokana na sala, matendo yetu ya huruma, na kufunga kwetu, tuondokane na unafiki. Tusianze kipindi hiki cha Kwaresima kwa mazoea. Kila mmoja wetu akiingie kipindi hiki kama vile ni cha kwanza na cha mwisho katika maisha yake. Tuitumie kwaresma hii kana kwamba hakuna tena Kwaresima nyingine. Kwa hakika hakuna hata mmoja mwenye uhakika wa kuiona Kwaresma nyingine. Mtume Paulo anatukumbusha kwamba kipindi cha Kwaresima ndio wakati ulikubalika, siku ya wokovu ndiyo sasa. Tusisubiri wakati mwingine. Tukitumie vema kipindi hiki. Nawatakieni nyote mwanzo mwema wa kipindi cha Kwaresima.

Jumatano ya Majivu Kwaresima 2020
25 February 2020, 17:50