Jubilei ya Miaka 50 ya Seminari ya Mtakatifu Petro Morogoro! Kumekucha!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Hivi karibuni, Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri limechapisha mwongozo wa malezi ya Kipadre unaojulikana kama “Ratio Fundamentalisi Institutionis Sacerdotalis” yaani “Zawadi ya wito wa Kipadre”. Utangulizi wa mwongozo huu unabainisha changamoto iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kama sehemu ya mchakato wa kulinda, kukuza na kudumisha wito na maisha ya Daraja Takatifu ya Upadre. Huu ni wito wenye thamani kubwa katika maisha na utume wa Kanisa unaopaswa kuhudumiwa kwa umakini mkubwa kwa kuheshimu dhamiri nyofu, wajibu unaotekelezwa kwa unyenyekevu na uvumilivu mkubwa, ili kweli Wakleri waweze kung’ara kati ya watu wa Mungu wanaowahudumia!
Mwongozo huu ni matunda ya ushirikiano mkubwa kutoka katika Sektretarieti kuu ya Vatican, kazi iliyoanza kutimua vumbi kunako mwaka 2014. Mwongozo unatoa kwa muhtasari sheria, kanuni na mambo msingi ambayo yanapaswa kuzingatiwa kwa ajili ya malezi na makuzi ya wito wa Daraja Takatifu ya Upadre. Unabainisha wajibu wa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki; Waratibu wa Seminari kitaifa na kimataifa pamoja na mwongozo wa malezi ya Seminari moja moja. Mwongozo huu unapembua kwa kina na mapana kanuni msingi za maisha na wito wa Daraja Takatifu ya Upadre: Yaani wanapaswa kuunganika na Kristo ili kuwaongoza, kuwachunga na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Wanapaswa kuungana na Kristo Yesu katika maisha, upendo na ukweli kwa ajili ya wokovu wa watu na kuendelea kuwa ni mwanga wa mataifa na chumvi ya dunia. Dhamana ya Kanisa ni kulea, kusindikiza na kupalilia miito mitakatifu, lakini kwa namna ya pekee wito wa Daraja Takatifu.
Seminari ndogo na nyumba za malezi ni mahali pa kulea na kuwasindikiza vijana katika maisha na wito wa Daraja Takatifu ya Upadre. Hapa waseminari wadogo wanapaswa kupewa malezi ya tunu msingi za maisha ya Kikristo kwa kukazia majiundo ya kiakili, kiroho, kiutu na kimaadili. Ni mahali pa kukuza ukomavu, umoja na mshikamano na Kristo Yesu kwa njia ya Sala, Neno la Mungu na Mashauri ya Kiinjili. Walezi wawe kweli ni mashuhuda wa Injili ya Kristo! Mwongozo pia unaangalia wito kwa Daraja takatifu wa watu wenye umri mkubwa, wasaidiwe na kupatiwa malezi makini katika nyumba maalum, ili waweze hatimaye, kufanya maamuzi muhimu katika maisha yao! Waseminari ni matumaini ya Kanisa katika ujumla wake. Ni katika muktadha huu, Seminari Ndogo ya Mtakatifu Petro, Jimbo Katoliki la Morogoro, Ijumaa tarehe 21 Februari 2020 inazindua maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwake; kwa Ibada ya Misa Takatifu inayotarajiwa kuongozwa na Askofu Agapiti Ndorobo wa Jimbo Katoliki la Mahenge ambaye pia tunda la Seminari Ndogo ya Mtakatifu Petro, Jimbo Katoliki la Morogoro.
Mgeni rasmi katika maadhimisho haya ni Jaji Mstaafu Bernard Luanda ambaye pia ni tunda la Mama “SPS” kama anavyojulikana kwa wale wote waliochota hekima, ujuzi na maarifa kutoka kwake! Kati ya mambo msingi yanayofanyika katika uzinduzi wa Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Seminari Ndogo ya Mtakatifu Petro Morogoro ni harambee ya kuchangia ukarabati mkubwa wa miundo mbinu, ili kukabiliana na changamoto mamboleo pamoja na kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia, ili kweli Kanisa na jamii iweze kupata viongozi makini, watakatifu na wachapakazi. Jimbo la Morogoro lina seminari ndogo moja ambayo inamilikiwa na Majimbo ya Morogoro, Jimbo kuu la Dodoma, Tanga, Same, Zanzibar na Jimbo kuu la Dar es Salaam. Kuunda seminari moja ya majimbo ni uamuzi uliotokana na Kikao cha Maaskofu Katoliki Tanzania cha mwaka 1967. Seminari ya Mtakatifu Petro, Morogoro ilijengwa ili kutekeleza azimio hilo. Seminari ya Mtakatifu Petro ambayo historia yake inaanza huko Ilonga katika mwaka wa 1937, na kuhamia baadaye Bagamoyo mwaka 1939 ina vidato I hadi VI. Seminari inaongozwa na Bodi ya Magavana ambayo ni Maskofu wa majimbo yanayohusika. Kwa maswala madogo madogo Maaskofu huwakilishwa na wakurugenzi wa miito wa majimbo yanayohusika.
Ingawaje mpango wa kuwa na seminari ya jumla pia ilikuwa na manufaa yake, lakini majimbo yaliyotajwa hapo juu sasa kila moja ina seminari yake ya jimbo isipokuwa jimbo la Zanzibar. Mpaka Mei, 1992 kumekuwa na waseminari 258 ambao kati yao 213 wako katika vidato I – VI na 45 wapo vidato V – VI. Wanafunzi hao wanatoka majimbo mbalimbali na Mashirika ya kitawa na kazi za kitume kutoka sehemu mbali mbali za Tanzania. Majimbo hayo ni: Singida (1); Morogoro (107); Mahenge (3); Jimbo kuu la Dodoma (37); Zanzibar (16); Jimbo kuu la Mbeya (1); Lindi (2); Moshi (5); Tanga (5); Rulenge (1); pamoja na Majimbo Makuu ya Dar es Salaam (59); Songea (2) na Mwanza (1). Mashirika yenye waseminaristi ni Wakarmeliti (14); Wastigmatine (1). Seminari Ndogo ya Mtakatifu Petro Morogoro ilifunguliwa rasmi mwezi Agosti 1969 na Mwadhama Kardinali Laurean Rugambwa. Magambera kadhaa wameshaiongoza seminari ya Mtakatifu Petro.
Seminari hii kwa namna ya pekee inamkumbuka kwa masikitiko Gambera wa kwanza hayati Padri Nicas Kipengele ambaye baadaye alikuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Mahenge (1970 – 1971). Wengine ni Mapadri Emmanuel Makala wa Morogoro; Martin Maganga wa Tanga; Damas Mpunta wa Dodoma (1974 – 1979), Octavian Linuma wa Mahenge (1980 – Agosti 1987) Wengine ni Padre Bunus Kizee wa Mahenge; Padre Patrick Kung’aro, Jimbo Katoliki la Morogoro, Padre M. Chikila, Padre Joseph Mluge, Jimbo Katoliki la Morogoro, Padre Karoli Mloka, Jimbo Katoliki Morogoro, Padre Valentini Chilega, Jimbo Katoliki Morogoro na kwa sasa Padre Aloyce Mwenyasi wa Jimbo Katoliki Morogoro.
Seminari ya Mtakatifu Petro Morogoro imewahi kushika nafasi ya kwanza katika kufaulu mtihani wa kidato cha nne wa mwaka 1990 kitaifa. Seminari ndogo ya Mtakatifu Petro iliyopo Jimboni Morogoro ni shule inayomilikiwa na Kanisa Katoliki inayotoa elimu ya sekondari kufikia kidato cha sita. Pia shule hii, inafundisha malezi maalumu ya Kikristo na maadili kwa vijana wanaoandaliwa kuwa mapadre wa Kanisa Katoliki. Shule hii inamilikiwa kwa pamoja na majimbo saba ya Kanisa Katoliki, yaani Dar es Salaam, Zanzibar, Morogoro, Tanga, Same, Mahenge, Kwa ruhusa maalumu ya Mwenyekiti wa Bodi ya Maaskofu, Seminari hiyo ina wanafunzi wanaojulikana kama waseminaristi kutoka jimbo kuu la Songea, mashirika ya Wasalvatori, Wabenediktine na Wakarmeli.
Kihistoria Seminari hii ilianzia Ilonga,Wilayani Kilosa, Mkoani Morogoro mwaka 1936, Kisha ikahamia Bagamoyo na 1969 ikahamishiwa Morogoro ilipo hadi sasa. Utume wa seminari hiyo maarufu kwa jina la “Saint Peter’s Seminary” tangu iasisiwe ni kutoa elimu bora na malezi bora kwa vijana wenye mwelekeo wa kuwa mapadre kwa gharama nafuu ambayo hata familia zenye kipato kidogo wanaweza kuimudu. Gambera Msaidizi wa seminari hiyo, Padre Joseph Torondo anasema seminari hiyo ni moja ya shule zenye kiwango kidogo cha ada miongoni mwa shule za bweni za kulipia nchini Tanzania Seminari hii imekuwa na mafanikio makubwa katika nyanja mbalimbali hususani katika kutoa wahitimu wengi wakiwamo mapadre, maaskofu na viongozi wengine wa serikali na taasisi binafsi. Historia inaonesha kuwa Seminari Ndogo ya Mtakatifu Petro, ni moja kati ya shule bora Tanzania kwa wanafunzi kufanya vizuri katika mitihani yao ya Taifa.Pamoja na ukweli kuwa kuna nyakati inashuka, lakini daima kiwango cha taaluma ni kizuri. Padre Torondo anasema wale ambao hawakufikia lengo la kuwa mapadre wamekuwa hazina njema kwa jamii ndani na nje ya Tanzania.
Baadhi ya Maskofu waliosoma katika Seminari Ndogo ya Mtakatifu Petro Morogoro ni: Askofu Agapiti Ndorobo wa Jimbo Katoliki la Mahenge, Askofu mstaafu Jacob Koda wa Jimbo Katoliki la Same, Askofu Msaidizi Eusebius Nzigilwa Jimbo kuu la Dar es Salaam, Askofu Titus Mdoe wa Jimbo Katoliki la Mtwara pamoja na Askofu Bernardine Mfumbusa wa Jimbo Katoliki la Kondoa. Mbali na viongozi hao wa dini, pia kuna viongozi wa Serikali waliosoma katika shule hii akiwamo Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Bernard Luanda, aliyekuwa Katibu wa Rais mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete, Prosper Mbena ambaye kwa sasa ni Mbunge, aliyekuwa Mkurugenzi wa Mpango wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF),Crescentius Magori. “Kwa ujumla ni kwamba Seminari yetu imetoa wataalamu katika medani mbalimbali wakiwamo walimu, wanahabari, wanadiplomasia, wanasheria, waandishi na wanauchumi” Anasema Padre Torondo. Kuna Mapadre waliohitimu Seminarini hapo na wanaendelea kutoa mchango mkubwa katika maisha na utume wa Kanisa la Kiulimwengu. Monsinyo Romanus Mbena, Mshauri mkuu wa Ubalozi wa Vatican nchini Albania. Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S, Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu, anatekeleza utume wake Radio Vatican, huko mjini Vatican. Kuna wengine wengi ambao wanaendelea kuchakarika sehemu mbali mbali za dunia kama wamisionari, matunda ya Seminari Ndogo ya Mtakatifu Petro.
Kung’ara: Miaka ya 1990 seminari hii ilikuwa miongoni mwa shule bora nchini Tanzania kutokana na kushika nafasi za juu kitaifa kidato cha nne, ambapo mwaka huo, Seminari ndogo ya Mtakatifu Petro Morogoro ilishika nafasi ya kwanza kitaifa kati ya shule 305, na mwaka 1992 ikashika tena nafasi ya kwanza kitaifa. Mwaka 1996 ilishika nafasi ya 13 kati ya shule 506 kitaifa na 1998, ikashika nafasi 13 kati ya shule 611 kitaifa. Mwaka 2000 ilikuwa ya nane kati ya shule 611 za sekondari kitaifa kidato cha nne. Mwaka 2001, ilishika nafasi ya saba kati ya shule 619 kitaifa. Baada ya kiwango cha ufaulu katika shule hii kilianza kuporomoka kwani mwaka 2003 ilishika nafasi ya 23 kati ya shule 754 kitaifa hali ambayo haikuwapendeza viongozi wa shule. Kwa mwaka 2012 idadi ya watahiniwa ilikuwa 60 waliopata daraja la kwanza walikuwa watatu, daraja la pili 15, daraja la tatu 19, daraja la nne 23, shule ikashika nafasi 67 kati ya 3,392 kitaifa.
Mwaka 2013 idadi ya watahiniwa ilikuwa ni 30 waliopata daraja la kwanza walikuwa ni watatu, daraja la pili tisa, daraja la tatu 17 na mwanafunzi mmoja alipata daraja la nne shule ilishika nafasi ya 48 kati ya 1,099 kitaifa. 2015 idadi ya wahitimu ilikuwa ni 45 waliopata daraja la kwanza walikuwa 21, daraja la pili walikuwa wanafunzi 33, daraja la tatu mmoja ambapo shule hii ilionekana kufanya vibaya zaidi kwani ilishika nafasi ya 77 kati ya shule 3,452 kitaifa. Kwa kidato cha sita, mwaka 1988 idadi ya watahiniwa ilikuwa ni 13, waliopata daraja la kwanza walikuwa ni wanafunzi tisa, daraja la pili wane. Shule hiyo ikashika nafasi ya kwanza kitaifa kati ya shule 75. Aidha, mwaka 1989 idadi ya wanafunzi ilikuwa 38 waliopata daraja la kwanza walikuwa wananfunzi 10, daraja la pili 14, daraja la tatu 12, daraja la nne mmoja na sifuri mmoja. Mwaka huo shule ilishika nafasi ya 18 kati ya shule 70 kitaifa. Mwaka 1990 ilikuwa na watahiniwa 21, waliopata daraja la kwanza walikuwa saba, daraja la pili 10, daraja la tatu wane. Shule hiyo ikashika namba 9 kati ya shule 75 kitaifa.
Mwaka 2010 ilikuwa na wanafunzi 25 waliopata daraja la kwanza walikuwa wanne, daraja la pili 15, daraja la tatu 16. Shule ikashika nafasi ya nane kati ya shule 81 kitaifa. Aidha, 2011 kulikuwa na watahiniwa 51. Waliopata daraja la kwanza walikuwa 10, daraja la pili 23, daraja la tatu 17 na mmoja alipata daraja la nne, hivyo shule ikashika nafasi ya 29 kati ya shule 334 kitaifa. Mwaka 2012 watahiniwa walikuwa 37. Wahitimu saba wakapata daraja la kwanza, darja la pili walikuwa 17, 10 daraja la tatu, watatu wakapata daraja la nne, shule ikashika namba 36 kati ya shule 326 kitaifa. Mwaka uliofuata kulikuwa na watahiniwa 17, wanafunzi 9 wakapata daraja la pili, daraja la tatu walikuwa nane, shule ikashika nafasi ya 9 kati ya shule 121 kitaifa na ya kwanza kimkoa kati ya shule 7 kwa shule zenye wanafunzi chini ya 30. Aidha, mwaka 2014 idadi ya wanafunzi ilikuwa 31. Waliopata daraja la kwanza mmoja, la pili 12, la tatu 18 Seminari hiyo ikawa namba 119 kati ya shule 268 kitaifa. Mwaka 2019 watahiniwa walikuwa 31, mmoja alipata daraja la kwanza, la pili 20 na daraja la tatu 10, shule ikashika nafasi ya 137 kati ya shule 423 kitaifa.
Changamoto: Pamoja na nia nzuri ya seminari hiyo ambayo kwa sasa ina wanafunzi 290, ni kutoa elimu na malezi bora kwa gharama nafuu, shule imejikuta katika wakati mgumu kiuchumi. Bajeti ya shule inakuwa ndogo na hivyo kuathiri mambo mengi. Na kwamba kupungua kasi ya ufaulu tofauti na miaka ya nyuma kumechangiwa na changamoto kadhaa zilizopo shuleni hapo ambazo baadhi yake zimesababishwa na uhaba wa fedha. Baadhi ya changamoto hizo kuwa ni uchakavu wa miundo mbinu, uhaba wa vitabu vya kiada na rejea kwa matumizi ya wanafunzi, uhaba mkubwa wa vifaa vya maabara ikiwa ni pamoja na shule kutokuwa na uzio.
Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu ambalo kwa miaka mingi lilikuwa linatoa ruzuku kwa ajili ya kusaidia kupunguza makali ya uendeshaji wa Seminari, imesitisha ruzuku. Mwamko kwa wakati huu ni waamini kuanza kuyategemeza Makanisa mahalia kwa rasilimali watu na vitu. Inakatisha tamaa kuona kwamba, waseminari wengi wanaishia njiani bila ya kuendelea na wito wa Upadre, tofauti na miaka ya nyuma, ambapo takribani robo tatu ya wahitimu walikuwa wanafikia Daraja Takatifu ya Upadre. “Kati ya wahitimu 30 wanaoendelea na masomo ya juu ngazi ya seminari huwa mmoja au wawili, kimsingi hali hii inasikitisha ndio maana wafadhili wakachukua uamuzi wa kusitisha utoaji msaada,” anasema Padre Torondo ambaye pia amesoma seminarini hapo!
Mpango mkakati: Kwa sasa Seminari imekamilisha ujenzi wa madarasa mapya mawili kwa ajili ya wanafunzi wa kidato cha tano na sita mchepuo wa sayansi na tayari yameanza kutumika na wanafunzi wake wako kidato cha sita kwa mwaka 2020. Pia uongozi umedhamiria kujenga maabara mpya na kuongeza vitatu kwenye maktaba hatua ambayo itasaidia kurejesha ufaulu mzuri kwa wanafunzi. “Tumedhamiria kuboresha mradi wa mifugo hususani nguruwe, ng’ombe wa maziwa pamoja na kuku ili kuongeza kipato na kuboresha lishe ya majandokasisi. “Tunaamini tukiwa na uchumi imara seminari yetu itakuwa katika nafasi ya kuendelea na utume wake wa kutoa elimu bora ya sekondari na malezi bora kwa vijana wenye muelekeo wa kuwa mapadre kwa gharama nafuu inayoweza kulipwa hata na familia zenye kipato cha chini,” anasema Padre Torondo. Mwito wake kwa wahitimu waliosoma shuleni hapo ni kujitokeza kuisaidia kwa namna yoyote ile.
“Wakati uongozi wa seminari unabuni na kutekeleza miradi ya kiuchumi, ni muhimu pia kuomba wahisani ndani na nje, mashirika, vikundi na mtu mmoja mmoja ambao wanaamini katika utume wa seminari hii ili waungane nasi katika kuchangia maendeleo ya utume huu,” anasema. “Tunawashukuru sana wanafunzi waliosoma hapa zamani (St. Peter’s Seminary Alumni) ambao kwa namna ya pekee hivi karibuni wameamua kusaidia maendeleo ya seminari hii, naomba wasichoke waendelee kuisaidia.” Mabweni matano yaliyopo shuleni hapo yamepewa majina ya mashahidi wafia dini wa Uganda. Mabweni hayo ni pamoja na bweni la Kagwa, Tuzinde, Mukasa, Mulumba na Kizito.