Tafuta

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika ujumbe wake wa Kwaresima kwa mwaka 2020, Sehemu ya III inazungumzia: Ufalme wa Mungu na Mamlaka ya watu! Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika ujumbe wake wa Kwaresima kwa mwaka 2020, Sehemu ya III inazungumzia: Ufalme wa Mungu na Mamlaka ya watu! 

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania: Ufalme wa Mungu na Mamlaka za watu!

Sehemu ya kwanza ya Ujumbe huu imegusia kuhusu Ufalme wa Mungu katika Maandiko Matakatifu na umuhimu wa kusali ili Ufalme huu ufike. Sehemu ya Pili ya Ujumbe wa Kwaresima kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania unafafanua kuhusu umuhimu wa Neno la Mungu katika kukuza Ufalme wa Mbinguni. Katika sehemu ya tatu: Ufalme wa Mungu na Mamlaka ya watu!

Na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, - Dar Es Salaam.

Ujumbe wa Kwaresima kwa Mwaka 2020 kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania unaongozwa na kauli mbiu “Ufalme wako Ufike”. Ujumbe huu ni matunda ya tafakari ya kina kuhusu tunu msingi za Injili ya familia kama chachu ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Ujumbe huu unakita mizizi yake katika neema, baraka na mwanga a maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 150 ya Ukristo nchini Tanzania sanjari na maadhimisho ya Mwezi Maalum wa Kimisionari, ulioadhimishwa Oktoba 2019.  Sehemu ya kwanza ya Ujumbe huu imegusia kuhusu Ufalme wa Mungu katika Maandiko Matakatifu na umuhimu wa kusali ili Ufalme huu ufike. Sehemu ya Pili ya Ujumbe wa Kwaresima kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania unafafanua kuhusu umuhimu wa Neno la Mungu katika kukuza Ufalme wa Mbinguni. Katika sehemu ya tatu, Radio Vatican inapenda kukushirikisha kuhusu Ufalme wa Mungu na Mamlaka ya watu!

SURA YA TATU UFALME WA MUNGU NA MAMLAKA YA WATU: Katika Barua yake kwa Warumi, Mtume Paulo anachagua sura ya 13:1-7 kueleza uhusiano uliopo kati ya mamlaka au tawala za watu na ufalme wa Mungu. Mtume Paulo anatambua kuwa tawala zote za dunia zilizo halali zimewekwa na Mungu mwenyewe aliyeumba ulimwengu kwa upendo wake mkubwa. Hivyo kila mtu inabidi atii mamlaka hizo ili kuweza kuendana na mpango wa mwenyezi Mungu aliyeweka mamlaka hizo. Mungu anaendelea kuvileta viumbe vyote pamoja ili vibaki katika mpango wake wa uumbaji: kumjua, kumpenda, kumtumikia na hatimaye kuurithi uzima wa milele. Katika sura hii tunawaalika kutafakari uhusiano uliopo kati ya ufalme wa Mungu na mamlaka ya watu, tukiongozwa na Maandiko Matakatifu na Mafundisho ya Kanisa Katoliki.

AGANO LA KALE: Mwanzoni Taifa la Israeli lilikuwa tofauti na mataifa mengine kwani hawakuwa na mfalme bali walitambua utawala wa Yahweh pekee. Ni Mungu aliyeingilia kati kwa niaba ya Waisraeli kwa kupitia watu wenye karama kama ilivyoandikwa katika Kitabu cha Waamuzi. Watu wanamwendea aliyekuwa wa mwisho wa hao, Samweli, nabii na mwamuzi, wakimwomba awateulie mfalme (rej.1Sam. 8:5; 10: 18-19). Samweli anawaonya Waisraeli kuhusiana na athari za utawala dhalimu (rej.1Sam. 8:11-18). Hata hivyo, mamlaka ya Mfalme yanaweza kuonekana kama zawadi ya Mungu anayekuja kuwasaidia watu wake (rej. 1 Sam. 9:16). Mwishowe, Sauli anapakwa mafuta na kuwa mfalme (rej. 1 Sam. 10: 1-2). Matukio haya yanadhihirisha fadhaa iliyowafanya Waisraeli kuelewa ufalme kwa namna tofauti na vile ulivyokuwa ukieleweka kwa jirani zao. Mfalme, aliyeteuliwa na Mungu (rej. Kum. 17: 15; 1 Sam. 9:16) na aliyewekwa wakfu naye (rej.1 Sam. 16:12-14), anaonekana kama mtoto wa Mungu (rej. Zab. 72).

Mfalme, kwa hivyo, anakuwa mlinzi wa walio dhaifu na mdhamini wa haki kwa watu wake. Shutuma za manabii zinalenga haswa katika wafalme kushindwa kutekeleza wajibu hizo (rej. 1 Fal. 21; Isa 10:14; Amo. 2:6 – 8:48, Mik. 3:1-4). 3.1.2 Katika Agano la kale, kwa nyakati tofauti, Mungu anajionyesha kuwa ndiye anayewaongoza watu wake kwa mkono wa wale aliowachagua yeye mwenyewe kutenda kwa niaba yake. Anaeleza wazi kuwa, katika yeye, watawala na mamlaka yao hutekeleza kile kilicho ndani ya mpango wake mwenyewe (rej. Mith. 8:15). Mungu aliye mtawala pekee katika wateule wake, anazidi sana kuwajalia hekima na busara ya kutenda kwa niaba yake (rej. 1Fal. 3:4-15). Watawala wanakuwa vyombo anavyotumia Mungu kutekeleza kazi alizokusudia yeye mwenyewe kwa watu wake (rej. Isa. 11:2-5; Yer. 23:5; Sir. 10:4). Watawala nao kwa upande wao walijifungamanisha na upendo wa Mungu ili kuimarisha uhusiano mwema na Mungu wao. Aidha watawala wa Agano la Kale walitekeleza majukumu yao kadiri ya mapenzi ya Mungu. Hivyo waliheshimiwa kwa kazi zao hizo zilizowastahilisha wao wokovu na wale waliowaongoza (rej. Hek. 6:12, YbS.1:16). 3.1.3 Mungu mwenyewe aliwaweka watawala, akiwatarajia kuwaongoza watu na kuyafanya mawazo na matendo yao kuwa ya hekima, kwani Mungu alikusudia kutengeneza Taifa lenye heshima na mwenendo mwema (rej. Hek. 6:3; Zab. 2:10; Mith. 8: 15-16).

Watawala hao wa Agano la Kale pia walipaswa kuwa waamuzi kati ya watu. Kwa hiyo, iliwabidi kujaa hekima itokayo kwa Mungu ili wahukumu kwa upendo na haki maana walitenda mahala pa Mungu mwenyewe mwenye upendo na haki (rej. Hek. 6:4-7; Ayu. 34:17-19; YbS. 35:12). Mungu aliyekusudia hayo yote yafanyike, pia aliwasaidia watu kutii kanuni, taratibu, na sheria za mamlaka halali za watu. Sio tu wanadamu peke yao walipaswa kutii mamlaka hiyo bali kila kitu kilichoumbwa na Mungu (rej. Yer. 27:7-10; Jdt11:7). Kwa jinsi hiyo, watu walimtii Mungu na Watawala pia (rej. Yer. 27:5-7), ambao wanamwakilisha Mungu aliye chanzo cha mamlaka zote duniani.

AGANO JIPYA: Mtume Paulo katika waraka wake kwa Warumi anaongea juu ya kuheshimu serikali, yaani “kujisalimisha” kwa serikali, “kuwa chini” ya serikali au “kutii” serikali; kwani mamlaka zilizopo duniani zimetoka kwa Mungu (rej. Rum. 13:1). Mungu kwa huruma na upendo wake anawashirikisha baadhi ya wanadamu zawadi ya kuwa na mamlaka juu ya wanadamu wenzao. Ingawa Mungu ameamua kuwashirikisha baadhi ya wanadamu zawadi ya kuwa na mamlaka juu ya wanadamu wenzao, lakini namna ya kuchagua viongozi hao na jinsi wanavyoongoza ni jukumu la kibinadamu. Hii inafanya suala la kuongoza kuwa taasisi ya kibinadamu iliyowekwa na Mungu mwenyewe, hivyo watu wanahimizwa kuzitii mamlaka hizo (rej. Rum. 13:1-7).

Kwa kusema: “Hakuna mamlaka yasiyotoka kwa Mungu, na kila yaliyoko yamewekwa na Mungu” (Rum. 13:1), Mtume Paulo analinganisha utii kwa serikali na utii kwa Mungu. Utii huu wote ni wa lazima. Wakristo ambao hawatii kanuni, taratibu na sheria halali za serikali hawamtii Mungu. Hata Bwana wetu Yesu Kristo akiwa hapa duniani alitii mamlaka za kibinadamu zilizokuwa zikiongoza Taifa lake la Israeli wakati wake (rej. Lk. 2:51-52, Mt. 17:24-17). Hata hivyo, ni vema ijulikane wazi kuwa hatutakiwi kutii tu mamlaka halali zilizowekwa na Mungu bila kuzingatia dhamiri yetu njema (rej. Rum. 13:5) yenye kutambua wajibu na nafasi yetu katika jamii.

Tena tutii tukijua kuwa yatupasa kuzitii mamlaka zilizo halali ili tuweze kuuona ufalme wa Mungu. Tunahimizwa kutimiza wajibu wetu kwa Mungu, kwa mamlaka za kidunia na kwa jamii (rej. Mt. 22:21) ili kuwepo haki, amani, furaha, maelewano, na kuchangia maendeleo ya jamii zetu; kwa mfano, kwa kulipa kodi (rej. Rum. 13:7, Mt. 22:21). Mtume Paulo aliamini kuwa Wakristo na raia wote kwa ujumla lazima walipe kodi kwa serikali, ili Serikali nayo kwa upande wake, itoe huduma nzuri za kijamii ikitumia mali ya raia wake kwa ukweli na uaminifu. Raia kwa upande mmoja, na serikali kwa upande mwingine, tunapaswa kufanya vivyo hivyo, tukizingatia kanuni, taratibu na sheria zetu.

Watawala kwa upande wao, wanaowaongoza watu, wanatakiwa wawaelekeze namna ya kuenenda kadiri ya mpango wa Mungu, wakiwakumbusha kanuni, taratibu, na sheria za msingi za kufuata. Iwapo raia watakosea, basi namna inayofaa kadiri ya mpango wa Mungu, itumike kuwakosoa. Kumbe, watawala wameshirikishwa hadhi ya Baba mwenye upendo na huruma ambaye anahukumu kwa haki na ambaye anakemea na kukaripia ikiwa ni kwa uvumilivu na mafundisho (rej. 2Tim. 4:2). 3.2.4 Hata hivyo, Watawala wanalo jukumu la kuwaadhibu watu waovu kwa mujibu wa sheria halali za nchi. Raia wema hawana sababu ya kuwaogopa watawala. Watu ambao hufanya vitendo vibaya lazima watarajie kuadhibiwa na watawala wao. Kwa hiyo, watu waovu wana sababu ya kuogopa watawala wao (rej. Rum. 13:3-4). Kile kinachoweza kuonekana kuwa ni uasi wa raia, kinaweza kuhesabiwa haki ikiwa tu sheria ya serikali inapingana waziwazi na sheria ya Mungu.

Mtakatifu Petro anawasihi Wakristo asemapo, “Tiini kila kiamriwacho na watu kwa ajili ya Bwana” (1 Pet. 2:13). Mfalme na watawala wake wana wajibu “wa kuwaadhibu watenda mabaya na kuwasifu watenda mema” (1 Pet. 2:14). Mamlaka yao hayo sharti “yaheshimiwe”, yaani, yatambuliwe kwa sababu Mungu anadai mwenendo sahihi” (1 Pet. 2:17). Uhuru usitumike kwa kusisitiza ubaya, bali kumtumikia Mungu (rej. 1 Pet. 2:16). Msisitizo ni juu ya utii ulio huru wa kuwajibika kwa mamlaka iwezeshayo haki kuheshimika, ikihakikisha manufaa kwa wote.

Kwa upande mwingine, Kanisa linatufundisha kwamba hatuna ruhusa ya kuwatii viongozi wetu pale wanapotuamuru kutenda kinyume na Amri za Mungu. Ni muhimu kuzingatia kuwa kujiweka chini ya mamlaka haya hakumaanishi kwamba ni lazima tutii kama vipofu amri inayotolewa na dola ambayo ni mbaya au inakwenda kinyume na Amri ya Kristo ya kuwapenda jirani zetu. Hoja ni kwamba raia wanapotii mamlaka iliyoko, mamlaka hiyo nayo lazima imtii Mungu. Hivyo, mamlaka inapoacha kutunuku matendo mema au tabia njema, au inapoacha kuadhibu maovu, na badala yake ikaamrisha mambo yaliyo kinyume; mamlaka hiyo inapoteza nguvu au uwezo wake wa kimaadili wa kuongoza watu. Mamlaka ya kiraia yamewekwa ili kudumisha utulivu katika jamii. Hivyo basi, raia ni lazima wafanye kile ambacho ni sahihi ikiwa wanataka kuepukana na hukumu au adhabu. Tuitii mamlaka kwa sababu ya dhamiri zetu sahihi. Kwa maneno mengine, dhamiri zetu zituelekeze kwamba Mungu, ambaye ndiye mwenye mamlaka kuu kupita zote, ameweka ngazi mbalimbali na kuweka sheria ili kuhakikisha kuwa kuna utulivu na utaratibu.

Aidha, kupingana na ngazi hizo ni kupingana na mpango wa Mungu wenye lengo la kuwa na jamii yenye utulivu. (rej. Mdo. 4:18-20). Kwa kuwa Mungu ametuumba ili tumjue, tumpende, tumtumikie na mwisho tufike kwake mbinguni, ni wajibu wa kila mmoja wetu kwa nafasi yake, awe mtawala au mtawaliwa, kuutafuta kwanza ufalme wa Mungu (rej. Lk 12:31). Ufalme wa Mungu tutaupata kwa kutenda kadiri ya mapenzi ya Mungu na kutimiza wajibu wetu itupasavyo katika nafasi zetu. Kila mmoja wetu ni kiongozi wa nafsi yake mwenyewe, hivyo tujifunze kuzitii dhamiri zetu njema zinazotuongoza kutenda mema na kutuzuia kutenda mabaya. Kwa kufanya hivyo tutaweza kueneza utawala wa Mungu maishani mwetu, utawala wa haki, amani na furaha. Basi, utawala wa watu au mamlaka ya watu iwe na lengo la kuuleta ufalme wa Mungu karibu zaidi katika maisha ya kila siku ya watu.

TEC: Kwaresima Sehemu ya Tatu:

 

29 February 2020, 18:44