Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania: Ujumbe wa Kwaresima Sehemu ya Pili: Neno la Mungu na Ukuaji wa Ufalme wa Mungu Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania: Ujumbe wa Kwaresima Sehemu ya Pili: Neno la Mungu na Ukuaji wa Ufalme wa Mungu 

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania: Neno la Mungu na Ujenzi wa Ufalme wa Mungu

Ujumbe huu unakita mizizi yake katika neema, baraka na mwanga a maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 150 ya Ukristo nchini Tanzania sanjari na maadhimisho ya Mwezi Maalum wa Kimisionari, ulioadhimishwa Oktoba 2019. Sehemu ya kwanza ya kwanza ya Ujumbe huu imegusia kuhusu Ufalme wa Mungu katika Maandiko Matakatifu na umuhimu wa kusali ili Ufalme huu ufike duniani!

Na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, - Da re Salaam.

Ujumbe wa Kwaresima kwa Mwaka 2020 kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania unaongozwa na kauli mbiu “Ufalme wako Ufike”. Ujumbe huu ni matunda ya tafakari ya kina kuhusu tunu msingi za Injili ya familia kama chachu ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Ujumbe huu unakita mizizi yake katika neema, baraka na mwanga a maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 150 ya Ukristo nchini Tanzania sanjari na maadhimisho ya Mwezi Maalum wa Kimisionari, ulioadhimishwa Oktoba 2019.  Sehemu ya kwanza ya kwanza ya Ujumbe huu imegusia kuhusu Ufalme wa Mungu katika Maandiko Matakatifu na umuhimu wa kusali ili Ufalme huu ufike. Leo, Radio Vatican inakuletea sehemu ya Pili ya Ujumbe wa Kwaresima kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kuhusu umuhimu wa Neno la Mungu katika kukuza Ufalme wa Mbinguni.

SURA YA PILI: NENO LA MUNGU LINAKUZA UFALME WA MBINGUNI:

Lengo kuu la mahubiri na utume wa uchungaji katika Kanisa, daima lilikuwa, linabaki, na litabaki kuwa lile ambalo Mtume Paulo analitamka akisema:” Kwa hiyo navumilia yote kwa ajili ya wateule, ili nao wapate wokovu katika Kristo Yesu, ndio utukufu wa milele” (2 Tim 2:10). Kuupokea wokovu na utukufu wa milele, ndiko kuufanya Ufalme wa Mungu ufike. Mtume Paulo anamwandikia Timotheo waraka huu akiwa gerezani jijini Roma wakati ambapo anaonekana ameachwa na wengi wa marafiki zake (rej. 2Tim.1:15-18; 4:9-18) na anakabiliwa na kifo (rej. 2Tim. 3:6-8). Hivyo Mtume Paulo anamtia moyo Timotheo akimwambia “Nami katika hiyo (Injili) nimeteswa hata kufungwa kama mtenda mabaya; Kwa ajili yake (Injili) navumilia mateso, hata nikifungwa minyororo kama mvunja sheria. Neno la Mungu halikufungwa” (2 Tim. 2:9).

Neno la Mungu ni tofauti na neno la mwanadamu. Mungu ndiye muumba wa mbingu na nchi na kila kilichomo; hata mwanadamu aliumbwa na Mungu mwenyewe. Mungu aliumba vitu vyote kwa Neno (rej. Mwa. 1:3-29). Hivyo, ni wazi kwamba Neno lake lina nguvu ajabu kiasi cha kutoweza kuzuiliwa na kitu chochote; ni kwa Neno hilo vyote vilifanyika na pasipo Neno kitu chochote kisingekuwepo ila Mungu mwenyewe (rej. Yn. 1:2-3). Neno linapaswa kutangazwa kadiri ya amri ya Mungu mwenyewe (rej. Mk. 16:15). Hivyo kwa Mkristo aliyepewa jukumu la kuhubiri Injili kwa ujasiri na kuimarishwa na paji la Roho Mtakatifu katika Ubatizo na Kipaimara (rej. Rum. 8:35- 37), ana jukumu la kuona kwamba ufalme wa Mungu unaenezwa bila kukata tamaa, licha ya changamoto anazokutana nazo.

AGANO LA KALE Katika agano la kale kuna mifano ya kutosha ya manabii waliohubiri Neno la Mungu kwa ujasiri bila kujali dhuluma na mateso waliyokutana nayo katika vifungo. Mungu aliponena na Musa na kumwambia aende nchini Misri kuwakomboa watu wake na kuwapeleka Nchi ya Ahadi (rej. Kut 3:10), Musa katika hali ya kibinadamu alijaribu kuweka mnyororo juu ya Neno hilo (rej. Kut 4:10). Pamoja na sababu alizozitoa mwishowe Musa alikwenda nchini Misri kadiri ya Neno la Mungu kwani hakuna kinachoweza kulifunga Neno la Mungu. Huko Musa alikutana na vikwazo vingi vilivyokuwa na lengo la kumkatisha tamaa ili ujumbe wa Mungu aliopeleka usitimie na lengo lisifikiwe. Lakini pamoja na hayo yote, wana wa Israeli walitoka nchini Misri na kuelekea katika Nchi ya Ahadi; na kila aliyejaribu kulizuia Neno la Mungu kutimia alipata mapigo makali (rej. Kut 7:8-11:1-9). 2.1.2 Ingawa hatuambiwi iwapo Nabii Isaya aliwahi kuhubiri akiwa mfungwa lakini mazingira hatarishi ya kisiasa ya wakati wake yalikuwa ni kama kifungo kwake.

Nabii Isaya alihubiri katika kipindi kigumu ambapo yeye pamoja na taifa zima la Israeli lilipitia shida za kisiasa hasa zile zilizosababishwa na uvamizi na ukandamizaji wa Waashuru wakati wa utawala wa Ahazi na Hezekia, wafalme wa Israeli na Yuda (736-700 K.K). Lakini pia Nabii Isaya hakuogopa hata kidogo kuwakemea wafalme na makuhani ambao walikosa uaminifu kwa Mungu, na alitamka waziwazi hukumu ya Mungu juu ya ukaidi wao bila kujali mateso ambayo yangempata mtu yeyote aliyemdhalilisha mtu wa cheo cha juu kama vile mfalme. Aidha Nabii Isaya kwa ujasiri mkubwa alilionya taifa la Israeli kwamba kwa sababu ya kukosa uaminifu kwa Mungu lingeadhibiwa vikali na Mungu mwenyewe (rej. Isa. 6:1-13). 2.1.3 Mfalme Ahazi kwa mfano, alikuwa hana imani ya kutosha kwa Mungu. Hivyo alifanya mikataba ya kivita na mataifa jirani ili kuwashinda maadui wa Israeli. Lakini Nabii Isaya alimwambia mfalme Ahazi asiwaogope Waashuru na kwamba aombe ishara ya Imanueli, mfalme Masiya, ambayo nabii alitabiri kutimia kwake (rej. Isa. 6:6-12) ila mfalme alikaidi na alipata madhara makubwa.

Mfalme Ahazi alikosa imani na uaminifu kwa Mungu, akategemea nguvu za muungano na mapatano ya kijeshi zaidi na matokeo yake alipata madhara makubwa baadaye. Lakini pia taifa lote la Israeli lilikosa imani na uaminifu kwa Mungu na hivyo lilistahili adhabu na toba. Nabii Isaya alisisitiza kuwa Mungu mtukufu ni “Mtakatifu wa Israeli” aliyejiunga na Israeli katika Agano ili amkomboe. Njia ya kukombolewa kwake Israeli ni kumwamini Mungu, Mungu peke yake, katika haki na ukweli. Na kwa sababu Israeli hakumwamini Mungu atahukumiwa na ataangamizwa. Lakini waliobaki watamrudia Mungu na kuokoka (rej. Isa 4:3). Mfalme wao atakuwa Masiya mwana wa Daudi, atakayeweka duniani ufalme wa amani na haki, na “dunia itajawa na kumjua Mungu”, yaani watu wote watampenda na kumtii Mungu. Katika unabii wake, Isaya hakuuma maneno! Alihubiri Neno la Mungu bila kuogopa hatari zilizoonekana kumzonga au kumfunga asihubiri Neno la Mungu kwa ufasaha na uwazi.

Nabii Yeremia alijiona kuwa na umri mdogo hivyo hangeweza kutangaza Neno la Mungu (rej. Yer. 1:6). Pale nabii Yeremia alipojaribu kuweka mnyororo ili asifanye kazi hiyo ya Mungu, Mungu alimthibitishia kuwa umri siyo sababu ya kutotangaza Neno lake (rej. Yer. 1:7). Neno la Mungu halifungwi na chochote hata umri mdogo. Lakini pia nabii Yeremia alikutana na mazingira ya kifungo katika kuhubiri Neno la Mungu (rej. Yer. 32). Uaminifu na imani yake kwa Mungu vilimtia nguvu. “Tazama, mimi ni Bwana, Mungu wa wote wenye mwili; je, kuna neno gumu lolote nisiloliweza?” (rej. Yer. 32:27). Kwa maneno mengine, “Neno la Mungu halifungwi minyororo.”

Katika Mwaka wa kumi wa Zedekia, mfalme wa Yuda, ambao pia ulikuwa mwaka wa kumi na nane wa Nebukadreza, nabii Yeremia alitabiri kuchukuliwa mateka kwa mji wa Yuda na mfalme Nebukadreza. Jambo hili halikumpendeza mfalme Zedekia, hivyo nabii Yeremia alifungwa gerezani ndani ya uwanda wa walinzi uliokuwa katika nyumba ya mfalme wa Yuda. Hata hivyo nabii Yeremia aliendelea kuhubiri Neno la Mungu angali kifungoni; kifungo hakikumzuia kuendelea na kazi yake (rej. Yer. 33). Kama ilivyokuwa kwa Nabii Isaya vivyo hivyo na nabii Yeremia naye alikuwa na ujasiri mkubwa katika kuutangaza ukweli wa Neno la Mungu. Mara kadhaa alilumbana na wafalme Zedekia na Jehoiakimu katika kutetea Ukweli wa Neno la Mungu. Hii inadhihirisha kuwa Neno la Mungu halifungwi minyororo, linavuma katika mazingira yoyote kadiri ya mapenzi ya Mungu na si kwa matakwa dhaifu ya wanadamu.

Nabii mwingine aliyehubiri akiwa kifungoni ni Ezekieli. Nabii Ezekieli anadhaniwa kuwa mhubiri aliyewalenga Waisraeli waliokuwa uhamishoni Babeli (593-571 K.K). Lakini inasemekana pia kuwa kuna ujumbe aliutoa akiwa Palestina (rej. Eze. 2:1-3:9) na mwingine akiwa utumwani Babeli (rej. Eze. 1:4-28, 3:10-15). “Haya! Enenda uwafikie watu hao waliohamishwa, kwa watu wako, ukaseme nao, na kuwaambia, ‘Bwana Mungu asema hivi’; kwamba watasikia, au kwamba hawataki kusikia (rej. Eze. 3:11).” “Enenda ukajifungie nyumbani mwako. Lakini wewe, mwanadamu, tazama, watakutia pingu, nao watakufunga kwazo, wala hutakwenda nje kati yao. Nami nitaufanya ulimi wako ugandamane na kaakaa lako, hata utakuwa bubu, wala hutakuwa mwonyaji kwao, kwa kuwa wao ni nyumba yenye kuasi. Lakini hapo nitakaposema nawe, nitafumbua kinywa chako, nawe utawaambia, ‘Bwana Mungu asema hivi, Yeye asikiaye na asikie, naye akataaye na akatae’; maana wao ni nyumba yenye kuasi (rej. Eze. 3:24-27).” Hivyo, Neno la Mungu linawafikia watu wake hata kama wako kifungoni au latokea kifungoni, lenyewe linapenya tu.

Pia tundu la simba ambamo nabii Danieli alifungiwa jiwe kubwa, utukufu wa Neno la Mungu ulidhihirika kwa Waisraeli. Baada ya kuamka asubuhi mfalme alikwenda nje ya pango alimokuwa Danieli akalia na kuuliza kama Mungu wa Danieli alimwokoa. Ndipo Danieli alipothibitisha kwa kusema kuwa Mungu alimtuma malaika ayafumbe makanwa ya simba wasiweze kumdhuru hata kidogo. Mungu alinena na malaika, akatenda muujiza wa kumwokoa Danieli uliosababisha ongezeko la imani ya Mfalme Dario pamoja na watu wake (rej. Dan. 6). Hivyo Neno la Mungu halizuiliwi na chochote kilichoumbwa naye. 2.1.8 Nabii Amosi alishindana na kuhani Amazia ambaye alimkataza kuhubiri, ya kwamba hakuwa na haki ya kufanya hivyo. Amazia aliyafanya haya kwa sababu Amosi alitabiri kuwa Mfalme Yeroboamu ataangamia kwa upanga na Waisraeli watapelekwa utumwani. Utabiri huu haukumpendeza Amazia hivyo aliamuru nabii Amosi aondoke Betheli na aende kuwatabiria watu wa Israeli (rej. Am. 7:10-17). Lakini Amosi alimthibitishia Amazia kuwa yeye ni nabii halali na kwamba ndiye aliyeteuliwa na Mungu alipokuwa mchungaji na mtunza mikuyu kuwahubiria nyumba ya Israeli. Na papo hapo alimtangazia Neno la Mwenyezi Mungu (rej.Am. 7: 16-17). Maandiko hayo yanaonyesha jinsi gani Neno la Mungu haliwezi kuzuiliwa na yeyote au chochote.

AGANO JIPYA: Yohane Mbatizaji alielewa umuhimu wa kuupata Ufalme wa Mungu alipotoa mwaliko, “Tubuni kwa maana ufalme wa Mungu umekaribia “(Mt. 3: 2)”. Yohane Mbatizaji akiwa gerezani alitafuta faraja ya Neno la Mwenyezi Mungu. Aliamini kuwa Neno hilo litamfikia hata akiwa kifungoni katika mateso na kwalo angepata amani. Hivyo, Yohane Mbatizaji aliwatuma wanafunzi (rej. Mt. 11:2-6) kumwuliza Yesu ili apate kujua iwapo Yeye ndiye yule ajae au wamtarajie mwingine. Jibu lililorudi ni ushuhuda wa Neno la Mungu linavyoendelea kufanya kazi kati ya watu. Hivyo hakuna sababu ya kuwa na mashaka nalo. Neno la Mungu linavunja mipaka ya kifungo na kusafiri kwa urahisi bila ya pingamizi. Neno hilo halifungwi minyororo hata kama wale wanaolipokea wamefungwa minyororo. Aidha kilichompeleka Yohane Mbatizaji kifungoni na kuuawa ni Neno la Mungu ili asiendelee kulitangaza (rej. Mt. 14:1-12). Hata hivyo, akiwa kifungoni Neno la Mungu liliendelea kutangazwa na wengine (rej. Mk. 6:6-29).

Yesu alifungua Hotuba ya Mlimani kwa Heri nane. Heri hizo zinaunganisha tabia anayokuwa nayo mtu muda uliopo sasa na maisha yajayo. Heri ya kwanza na ile ya mwisho (Mt. 5: 3, 10), zote hueleza kuwa ufalme wa Mungu tayari upo hivi sasa miongoni mwetu na kati yetu. Heri sita ambazo zimo (Mt. 5: 4-9) huonyesha Ufalme utafikia ukamilifu wake siku ya mwisho. Heri za mwisho, (Mt. 5: 10-11) ni juu ya ulazima wa kuteseka kwa ajili ya Injili na baraka na utukufu wenye nguvu ya pekee tunavyovipata katika maisha yetu. Hakuna heri ambayo wanadamu wanaweza kuifikia inayokwepa mateso.

Katika Karamu ya Mwisho Yesu alisema, “Sitakunywa tena divai ya zabibu mpaka siku ile nitakapoinywa upya katika ufalme wa Mungu” (Mk. 14: 25). Yesu Kristo mwenyewe akiwa katika praitorio anazungumza ukweli wa Neno la Mungu kwa ujasiri mkubwa (rej. Yn. 18-19:1-15). Kwa mfano, baada ya kuulizwa habari za mafundisho yake, Yesu Kristo anasema waziwazi kwamba hakuficha chochote. Alihubiri Neno la Mungu kwa uwazi hivyo hakuna sababu ya kuendelea kumhoji. Kwa hili Bwana wetu Yesu Kristo anapigwa kofi lakini naye anamjibu aliyempiga kwamba, aliyoyazungumza ni ukweli mtupu na kulikuwa hakuna sababu ya Yeye kupigwa kofi. Alisema haya bila kujali hatari ya kupigwa kofi tena. Neno la Mungu halifungwi kwa kupigwa kofi, au mijeledi, au kutemewa mate. Aidha Neno la Mungu alilolifundisha Bwana wetu Yesu Kristo na ukweli alioutangaza ndio uliomfikisha kwenye mateso makali na kifo cha Msalaba. Hata hivyo, siku ya tatu alifufuka na Neno la Mungu linaendelea kutangazwa (rej. Mt. 28:1-10).

Mitume Petro na Yohane na wengine wengi walianza kulitangaza Neno la Mungu baada ya Pentekoste; lakini walipelekwa gerezani kwa kuwa walilihubiri Neno la Uzima la Bwana wetu Yesu Kristo. Wangali bado gerezani, walipelekwa mbele ya baraza kuhojiwa. Kwamba ni kwa nguvu ya nani wanatenda? Mtume Petro kwa ujasiri mkubwa anazungumza juu ya habari za Yesu ambaye Wayahudi na viongozi wao walimsulubisha kuwa ndiye chanzo cha nguvu na mamlaka yao. Kristo ni jiwe walilolikataa waashi na limekuwa jiwe kuu la pembeni (rej. Mdo. 4:1-22). Neno la Mungu halifungwi minyororo!

Shemasi Stefano, Shahidi naye anapelekwa mbele ya baraza la Wayahudi kwa kuwa alitenda maajabu na ishara kwa jina la Yesu Kristo. Akiwa mbele ya baraza la Wayahudi anaendelea kutoa hotuba inayoshuhudia ukweli wa Neno la Mungu (rej. Mdo. 6:1-7:1-60). Stephano anaonyesha ujasiri wa hali ya juu kabisa. Anaonyesha imani yake kwa Bwana wetu Yesu Kristo bila kuogopa macho ya watesi wake. Anazungumza ukweli bila kuficha lolote. Mwishowe anauawa kwa sababu ya kusema ukweli uliowachoma Wayahudi. Kuuawa kwake hakuzuii Neno la Mungu kuendelea kutangazwa. Neno la Mungu halifungwi na minyororo ya mateso au kifo.

Mtume Paulo naye anafungwa gerezani mara kadhaa kwa sababu ya Neno la Mungu. Alipelekwa mbele ya baraza la Wayahudi na aliwaambia ukweli wa Neno la Mungu wajumbe wa baraza lote la makuhani na Wayahudi (rej. Mdo. 22:30-23:1-11, 24:24-26:32). Neno ambalo Mtume Paulo analihubiri akiwa kifungoni linaonyesha wazi kabisa kwamba Neno la Mungu halifungwi minyororo (rej. 2 Tim. 2:9). Fundisho hili linajirudiarudia sana katika maandishi ya Mtume Paulo katika barua zake (rej. Flm. 1:7-17, 9-13). Lakini zaidi katika Waraka wake kwa Wafilipi (rej. Flp. 1:13-17) na katika waraka kwa Waefeso (rej. Efe. 3:1-13). Neno la Mungu haliwezi kuzuiliwa na kitu chochote kuhubiriwa na kupenya katika mioyo ya watu. Kwa njia ya haya yote, tunajifunza ujumbe mahususi kwamba Neno la Mungu hupenya sehemu yoyote. Mungu katika haya yote anatufunulia asili yake Mwenyewe kuwa ni Roho halisi na ukamilifu wake hauna mipaka. Yeye ni wa mahali pote. Bwana wetu Yesu Kristo anaushuhudia ukweli huu, “…watu hawa wakinyamaza, hata mawe yatasifu” (rej. Lk. 19:40). Hivyo, watu wakizuiwa kutangaza Neno la Mungu hata mawe yatalitangaza. Neno la Mungu halifungwi minyororo. Aidha mambo yote yapita, Neno la Mungu halitapita kamwe (rej. Lk. 21:33). 2.2.7 Neno la Mungu lina nguvu ya ajabu. Tunapaswa kulitafuta Neno la Mwenyezi Mungu siku zote na mahali pote na kwa nguvu zetu zote.

Katika kipindi hiki cha Kwaresima, tunaalikwa kutenga muda maalum wa kulisoma, kulitafakari, na kulitangaza kwa watu wote kwa maneno, matendo yetu mema na ushuhuda wa maisha yetu. Jukumu hili litekelezwe na mtu binafsi, familia, jumuiya, vyama vya kitume na Kanisa lote kwa ujumla (rej. Mk. 16:15-16). Kama asemavyo Mtume Paulo, “Litangaze Neno, sisitiza, hakikisha, onya, himiza kwa uvumilivu wote na elimu” (2Tim. 4:2); na Bwana wetu Yesu Kristo hatatuacha (rej. Mt. 28:20). Matunda ya Neno la Mungu ni haki, amani na furaha kwa mtu binafsi, familia, jumuiya, taifa na ulimwengu wote. Aidha wokovu na uzima wa milele ni matunda ya Neno la Mungu (rej. Yn.14:6, Mt. 22:29, Rum.1:16, Flp. 2:6-11). Neno la Mungu ni uhai wetu. “Mtu hataishi kwa mkate tu ila kwa kila Neno litokalo katika kinywa cha Mungu” (Mt. 4:4). Tunapata uhai katika mateso na vifungo vya kimwili kwa sababu tunajishibisha kwa Neno wake Mungu, Yesu Kristo anayetufundisha na kutulisha. Neno la Mungu ni nuru yetu (rej. Yn. 3:19-20). Tuwapokee wanaotutangazia Neno la Mungu na tulizingatie. (rej. Mt. 10:40-42).

Neno la Mungu linatupatia uthabiti na kutuimarisha katika ukweli kwamba kwa neema ya Mungu, tunao uwezo wa kushinda dhambi na kuufanya Ufalme wa Mungu ufike. Neno la Mungu linasema kuwa yeye alifanywa mdhambi kwa ajili yetu sisi, alichukua dhambi zetu na adhabu katika mwili wake msalabani. Alifanywa kuwa laana kwa ajili yetu, na kwa ajili ya wale wote wanaoweka tumaini lao katika yeye kwao hao hakuna adhabu (rej. 1 Pet. 2: 21-24). Neno la Mungu linaleta matumaini kwamba hitaji la wanadamu kuokolewa limetekelezwa na Mungu tayari. Neno hili ndilo Habari Njema. Lakini Habari Njema hii inaleta pia wajibu kwa upande wa pili, yaani, waamini tunapaswa kumgeukia na kumrudia Mungu, na hiyo ndiyo maana ya kutubu na kuiamini Injili. Kwa namna hiyo Ufalme wa Mungu utakuwa unadhihirishwa maishani mwetu.

Neno la Mungu ni ukweli, na sifa moja ya ukweli ni kwamba hudumu daima bila kubadilika. Kwa vile Neno lake lina pumzi ya Roho wa Mungu, vile ambavyo Roho wa Mungu hafungwi, kadhalika na Neno la Mungu halifungwi na pingu au vizuizi au vikwazo vinavyoweza kumfunga Roho, kama ambavyo usivyoweza kufunga mnyororo upinde wa mvua. Neno lake li hai, tena lenye nguvu (rej. Ebr. 4:12-13); lina nguvu zaidi kuliko kitu chochote hapa duniani. Mambo yote mengine hayana uwezo wowote ukilinganisha na Neno la Mungu. Ilikuwa kwa njia ya Neno la Mungu kwamba mbingu ziliumbwa. Mungu anapotamka kinachotamkwa hufanyika na mambo yote hutii. Neno la Mungu haliwezi kufungwa minyororo kwa sababu ni nguvu isiyoweza kuzuiwa; ni yenye uwezo wa kutaalamisha na kuangaza na kuwafanya watu wengi bila idadi kwa pamoja wafanane zaidi na Kristo. Yesu Kristo ni Neno aliyetwaa mwili, hekima aliyemwilishwa, ukweli uliomwilishwa, na chimbuko lililomwilishwa la kila kitu. Kukosa ukweli, kukosa uwazi na u-ndimi mbili ni kinyume cha uhalisia wa Mungu na Ufalme wa Mungu. Popote ambapo mtu anamkana Kristo, atakuwa daima anaukataa ukweli.

Kupenda lisilo kweli, kutokuwa na msimamo kuhusu ukweli, kuubinafsisha ukweli, kuuweka ukweli na lisilo kweli katika ngazi moja, yote haya hupatikana katika kiini cha dhambi ya Adam na Eva (rej. Mwa. 3:1-24). 2.2.10 Kristo alikuja ili kuubomoa Ufalme wa uwongo na kuusimika Ufalme wake wa ukweli, kwa lengo la kumweka huru binadamu dhidi ya giza la uwongo na udanganyifu: “Kwa sababu hii nalitokea ulimwenguni, ili niushuhudie ukweli. Yeyote yule aliye wa ukweli huisikia sauti yangu” (Yoh. 18: 37). Yesu ndiye ukweli na uzima aliyekuja kuwaweka watu huru dhidi ya utumwa wa utawala wa shetani. Ukweli huu ni nafsi yake mwenyewe anayetualika tumsikie ili tupate kuwa raia wa ufalme wake na ili tupate hatimaye kufika kwa Baba. (rej. Yoh. 14: 6). Kumbe, Neno analotuambia Kristo ni ukweli unaotuonyesha njia ya kufikia uzima wa milele.

HITIMISHO: Kwa kushika Neno lake, tunafanyika warithi wa uzima wa milele na raia wa Ufalme wa Mbinguni. Katika kipindi hiki cha Kwaresima tunao uchaguzi wa kufanya. Tunaalikwa kuliishi Neno la Mungu kwa maneno na matendo yetu; na pia kulishuhudia kwa watu wengine ili ufalme wa Mungu uendelee kujidhihirisha kwetu na watu wengine. Hii ndiyo njia pekee itakayoyafanya maneno haya yatimie, “Ufalme wako Ufike”.

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania: Kwaresima Sehemu II

 

 

27 February 2020, 16:37