Mungu anapendelea mtu achague mema lakini ni uhuru wa mwanadamu kucgahua kati ya mema na mabaya na kwa maana hiyo mtu yuko huru kuchagua uzima au mauti Mungu anapendelea mtu achague mema lakini ni uhuru wa mwanadamu kucgahua kati ya mema na mabaya na kwa maana hiyo mtu yuko huru kuchagua uzima au mauti 

Amri za Mungu na uhuru wa binadamu!

Kila mtu ana uhuru wa kuchagua kati ya mema na mabaya.Mungu anapendelea mtu achague mema;lakini hamshukurutishi kwani anachagua kwa ufahamu na kwa uhuru kamili.Hivyo kila mtu yuko huru kuchagua kati ya uzima au mauti na hakuna anayelazimishwa.Tumuombe Mungu Baba aliyetuumba atujalie neema na baraka zake tuweze kuutumia vyema uhuru na utashi aliotujalia katika kutimiza mapenzi yake.

Na Padre Paschal Ighondo - Vatican.

Karibu ndugu msikilizaji wa radio Vatican, katika tafakari ya liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 6 ya mwaka A wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Masomo ya leo yanatujuza uhusiano uliopo kati ya Amri za Mungu na uhuru wa mwanadamu.

Yoshua bin Sira katika somo la kwanza anatueleza ukuu wa Mungu kwa kumpatia kila mtu uhuru na utashi. Kila mtu ana uhuru wa kuchagua kati ya mema na mabaya. Mungu anapendelea mtu achague mema; lakini hamshukurutishi kwani anachagua kwa ufahamu na kwa uhuru kamili. Hivyo kila mtu yuko huru kuchagua kati ya uzima au mauti na hakuna anayelazimishwa. Lakini mwisho wa yote kutakuwa na hukumu ya haki kwa yale tunayoyachagua.

Mtume Paulo katika somo la pili la waraka wake wa kwanza kwa Wakorintho anatueleza kuwa Hekima ya Mungu ni mpango wake wa kutukomboa sisi kwa msalaba wa Yesu Kristo. Hekima hii imefunuliwa kwa wanyofu kwa njia ya Roho, maana Roho huchunguza yote, hata mafumbo ya Mungu. Hekima hii, wenye kuitawala dunia hawaijui hata mmoja; maana kama wangaliijua, wasingalimsulibisha Bwana wa utukufu.

Yesu katika Injili ilivyoandikwa na Mathayo, anaweka wazi kuwa Torati na Manabii ni jumla ya mapenzi ya Mungu ambayo aliyafunua katika Agano la Kale. Yesu mwenyewe hajafika kutangua hiyo sheria, bali kuitimiliza kwa kukazia kwamba kila wazo, neno na tendo liwe na lengo moja tu: kutimiza mapenzi ya Mungu. Amri zote zinapaswa kufundishwa na kufuatwa kwa ukamilifu wake. Hakuna amri ambayo ni ndogo ya kupuuzwa na kutofuatwa, zote lazima zifuatwe. Kumbe kuua, kumwonea mwingine hasira au kummfyolea au kuapiza, kuzini au kutamani zote ni dhambi. Ili kuonyesha ubaya wa dhambi Yesu anatumia lugha ngumu kweli kama kung’oa jicho au kuukata mkono na kutupilia mbali. Yesu anasisitiza umuhimu wa kusameheana na kusuluhishana kama kiini cha sisi kusamehewa na sadaka zetu kukubaliwa na Mungu.

Uwezo wetu wa kutambua lipi jema na lipi baya ambao Yoshua Bin Sira anatueleza, umeathiriwa na dhambi ya asili. Tangu Adamu na Eva waliposhindwa kutambua kuwa kula tunda walilokatazwa si jambo jema, kizazi chao chote kimeathirika na kuwekewa amri ambazo lazima tuzifuate. Kumbe amri za Mungu zinamsaidia binadamu awe huru. Uhuru ni uwezo wa kuchagua mema bila kizuio chochote. Jambo ni jema iwapo linaendana na maumbile ya binadamu. Hilo jema linamsaidia mtu kuwa kama alivyokusudiwa kuwa. Mungu ndiye aliyemuumba binadamu. Kwa hiyo, Mungu anaelewa vizuri maumbile ya binadamu na hivyo anaelewa vizuri lipi ni jema kwa mwanadamu litakalomsadia kufikia ukamilifu maana tunakuwa kile tunachochagua. Amri za Mungu zinatuonyesha lipi ni jema kwetu. Hivyo, amri za Mungu zinatusaidia kuwa huru maana zinatusaidia kujua kipi ni kizuri. Mungu akishatuonyesha lipi jema lipi baya anatuacha tuchague wenyewe. Anaheshimu uhuru wetu.

Lakini kwa sababu ya kiburi bado pia hizi amri hatuzifuati tunavyopaswa. Wakati mwingine, tunakataa makusudi kujifunza ili tujue lipi ni jema. Nafasi za kujua zipo lakini hatuweki juhudi. Kwasababu ya kiburi. Wakati mwingine tunajua lililo jema lakini tunakataa kulitenda. Tunafuata hisia zetu ambazo kimsingi zinalegeza uwezo wa utashi wetu kuchagua lilo jema. Kwasababu ya mazoea ya kibinadamu, amri za Mungu zinaonekana kuwa kinyume cha matazamio yetu na mazoea yetu na hivyo kuonekana zinatesa na kudai sana, Injili inaeleza vizuri: mmezoea kufanya hivi, mimi na waambia fanyeni hivi.

Yesu anatukumbusha kila mara kuweka juhudi kufahamu ukweli ni upi. Wimbo wa katikati umetuambia “Bwana nifungue macho niyatazame maajabu ya sheria yako. Ufanye mazoezi ya kutenda mema (Jenga fadhila wakati mwingine tunafahamu jambo fulani ni baya lakini kwasababu tumezoea kulitenda tunashindwa kujizuia kuliacha. Fadhila zinajengwa kwa kutenda mema kwa kurudiarudia mpaka kuyafanya mazoea na hivyo inakuwa ni vyepesi kuchagua lililo jema. Basi tumuombe Mungu Baba aliyetuumba atujalie neema na baraka zake tuweze kuutumia vyema uhuru na utashi aliotujalia katika kutimiza mapenzi yake ili mwisho wa yote tuweze kupokea taji ya utukufu huku mbinguni aliko yeye tuakafurahi na watakatifu wake milele yote.

DOMINIKA YA 6 YA MWAKA
14 February 2020, 09:24