Siku kuu ya kutolewa Bwana wetu Yesu Kristo Hekaluni, ni siku 40 baada ya kuzaliwa kwake kama ilivyokuwa desturi ya Musa. Siku kuu ya kutolewa Bwana wetu Yesu Kristo Hekaluni, ni siku 40 baada ya kuzaliwa kwake kama ilivyokuwa desturi ya Musa.  

Yesu ni mwanga daima utusaidie kuona njia ya uzima wa milele!

Yesu Kristo ni sababu ya kusimama kwetu,ni Mwanga wa daima,tuuchukue Mwanga huu ili utusaidie tuione njia ya uzima wa milele,tuwaangaze na watu wengine ili nao pia waione njia ile iongozayo katika uzima wa milele.

Na Padre Pascal Ighondo – Vatican

Karibu ndugu msikilizaji wa radio Vatican, katika tafakari ya Neno la Mungu, katika sikukuu ya kutolewa Bwana wetu Yesu Kristo Hekaluni, siku 40 baada ya kuzaliwa kwake kama ilivyokuwa desturi ya Musa. Sherehe hii ilianza kusherehekewa Yerusalemu miaka 400 baada ya kuzaliwa Kristo. Katika sherehe hii waamini walifanya maandamano ya kuingia kanisani wakiwa wambeba mishumaa kama ishara ya Kristo kuwa mwanga kwa mataifa.

Katika somo la kwanza la kitabu cha “Malaki”, Mjumbe wa Mungu, Malaki, analalamika kwa kuwa Makuhani na watu wao waliishi maisha ya dhambi. Ibada zao zilikuwa ni kama mlio wa madebe mbele ya Mungu, hazikuwa na uchaji wowote mbele ya Mungu kwani Makuhani waliendesha ibada Hekaluni kwa namna isiyo ya heshima, bila kufuata taratibu na sheria za Musa na Watu nao sababu ya uchoyo hawakuwa tayari kutegemeza Hekalu na wahudumu wake kwa zaka na sadaka. Hivyo Mungu kupitia mtumishi wake Malaki anatangaza kwamba: atamtuma Mjumbe wake kumwandalia njia, kwani Mungu mwenyewe ameamua kuja Hekaluni mwake. Atafanya hivyo katika nafsi ya Masiha ajaye. Atawatakasa makuhani na watu wa Israeli kutoka dhambi za ona kuwafundisha kutolea dhabihu zenye mastahili machoni pa Mungu. Ibada na matoleo hayo ya dhabihu hayatafanyika tu Yerusalemu bali katika ulimwengu wote kama tunavyosali katika sala ya Ekaristi ya III tukisema; “Maana, kwa njia ya Mwanao, Bwana wetu Yesu Kristo, na kwa uwezo tendaji wa Roho Mtakatifu, unavitia uzima vitu vyote na kuvitakatifuza, wala huachi kuwakusanya watu kwako, ili, toka maawio ya jua hata machweo yake, dhabihu safi itolewe kwa jina lako” Mal 1:11.

Ujumbe wa malaki unakamilishwa kwa kutolewa Yesu hekaluni. Mwinjili Luka anasimulia jinsi mpango huo wa Mungu ulivyokamilika. Siku ya 40 baada ya kuzaliwa Kristo, Maria na Yosefu walienda Hekaluni kadiri ya Sheria ya Musa ilivyowadai. Kadiri ya Sheria ya Musa, mwanamke aliyejifungua hakuruhusiwa kuingia Hekaluni kwa ibada wala kutoa sadaka kwa siku 40 ikiwa mtoto ni wa kiume na siku 80 ikiwa mtoto ni wa kike. Baada ya siku 40 mwanamke ikiwa alizaa mtoto wa kiume alilazimika kujionesha na kujitambulisha Hekaluni kutolea dhabihu ya mwanakondoo au njiwa ili apate kutakaswa na kuruhusiwa sasa kuingia hekaluni kusali na kutolea sadaka mbele za Mungu Walawi12:1-8. Wanawake maskini ambao hawakuweza kununua mwanakondoo ilibidi watafute njiwa kama sadaka mbadala. Luka anatuambia kwamba Yosefu na Maria walitolea njiwa wawili. Hapa tuna uhakika kwamba Familia Takatifu ilikuwa ni familia “Maskini na Fukara”. Sheria ya pili ilikuwa ni ya kuwafanya Waisraeli kukumbuka kwamba walikuwa watumwa Misri na walikombolewa kutoka utumwani kwa malipo ya kifo cha wazaliwa wa Kwanza wa Wamisri, hivyo kila mzaliwa wa kwanza wa kiume atakuwa mali ya Mungu Kut 13:12-14. Kwa kuwa Yesu ni mzaliwa wa kwanza hivyo alistahili kuwa ni Mali ya Mungu. Ili kumkomboa mtoto asiwe mali ya Mungu walipaswa kumtolea Mungu shekeli 5 ambazo ni sawa na mshahara wa siku 15 wa mfanyakazi wa kawaida. Hes 18:16. Kumbe Maria na Yosefu walienda Hekaluni Yerusalemu kutimiza sheria hizi mbili.

Hili lilikuwa tukio la kawaida la kila mwisraeli. Kumbe machoni pa watu, hakuna cha ajabu ambacho kingeweza kuwatofautisha Yesu, Maria na Yosefu kati ya familia nyingi zilizofika kwa lengo lile lile la kuwatolea watoto wao kwa Bwana. Lakini kadiri ya mpango wa Mungu, fumbo kubwa lilijidhihirisha na kupata ukamilifu wake Maria na Yosefu walipomtolea mtoto wao. Tofauti ni kuwa Yesu anajitoa mwenyewe Hekaluni kwa Mungu na anajiachilia au kujiweka kikamilifu chini ya mamlaka ya Mungu ili kukamilisha mpango wa Mungu ambao kwa huo alichukuliwa mimba tumboni mwa mama Bikira Maria yaani ukombozi wa Mwanadamu kama tunavyosoma katika waraka kwa waebrania; dhabihu na matoleo hukupendezwanazo, kafara na sadaka za dhambi hakuzitaka, ndipo nikasema, tazama nimekuja, niyafanye mapenzi yako Ee Mungu. Waebr 10: 5-7. Kumbe, katika tukio hili Mwenyezi Mungu anakamilisha kile alichoahidi kwa kinywa cha Nabii Malaki kwamba kuwa atakuja mwenyewe Hekaluni, katika nafsi ya Mwanae na huko atatolea dhabihu iliyo hai na Takatifu, na inayopendeza. Ni katika ujio wake atawatakasa makuhani na watu wote, tena atawafundisha namna iliyobora ya kuadhimisha ibada katika Hekalu la Mungu. Kitendo cha Yesu kujitoa kwa Mungu ni Ibada iliyo na mastahili na heshima kubwa kwa Mungu.

Ni Roho wa Mungu pekee anayeweza kuwaongoza watu kumtambua na kumpokea Yesu kama Bwana na Mwokozi. Ndivyo alivyofanya kwa Simeoni na Anna. Simeoni hakuwa kuhani, bali mzee, mlei Mcha Mungu aliyesali daima juu ya ujio wa Masiha kuwakomboa Waisraeli. Siku ile Simeoni alienda Hekaluni kusali. Kulikuwa na watu wengi hekaluni waliowaleta watoto wao kuwatolea kwa Bwana. Katika umati wa watu wengi na watoto wengi waliokuja kutolewa Hekaluni, Simeoni aliweza kumtambua Mtoto Yesu kuwa ndiye Masiha aliyesubiriwa. Roho wa Mungu alimfunulia akamtambua yule aliyekuwa akimsubiri kwa hamu. Moyo wake ukawakwa kwa furaha kubwa, akaimba wimbo wa kumsifu Mungu: “Sasa Bwana waweza kumruhusu mtumishi wako aende kwa amani, kwani kwa macho yangu nimeuona wokovu wako, uliouweka machoni pa watu wote, nuru ya kuwa mwangaza kwa mataifa, na kuwa utukufu kwa watu wako Israeli [Lk 2:29-32]. Luka anasema: “Babaye na Mamaye walikuwa wakiyastaajabia yaliyonenwa juu yake” Lk 2:33. Mzee Simeoni anaendelea kusema; “Tazama, huyu amewekwa kwa kuanguka na kuinuka kwa wengi walio katika Israeli, na kuwa ishara itakayonenewa. Kisha akamwambia Bikira Maria; Nawe mwenyewe upanga utakuingia moyoni mwako, ili ukafunuliwe mawazo ya mioyo mingi.” Lk 2:33-35. Maria licha ya kutambua kwamba atateseka kuhusiana na mtoto wake, aliendelea kujiachia mikononi mwa Mungu kama alivyojiachia kwake alipopewa ujumbe na Malaika na kusema; “Tazama Mimi ni mjakazi wa Bwana na nitendewe kama ulivyonena.” Lk1:38

Katika masimulizi haya ni kana kwamba Yosefu hakuna linalomhusu. Tukumbuke kuwa katika maisha yake yote, Yosefu alishirikiana na Maria katika mateso, mashaka, wasiwasi na huzuni itokanayo na mtoto Yesu. Siku chache baadaye itawapasa kukimbilia uhamishoni Misri kuokoa maisha ya mtoto Yesu dhidi ya Herodi. Tena waliporudi Nazarethi, Yosefu na Maria walivumilia pamoja taabu itokanayo na umaskini wao. Kumbe tunajifunza kutoka familia hii takatifu utayari wao wa kujiachilia kwa Mungu ingawa walijua wakifanya hivyo itawabidi kuteseka kuwa; Mungu hawezi kuruhusu mateso na mahangaiko yatupate kama hakuna jema tutakalovuna katika mateso yale. Kristo Yesu ni Nuru yetu, ni mwanga kwa kila mmoja wetu [Yn 1:9]. Imani yetu kwake ni kama taa ituongozayo katika ile njia ya Uzima. Sherehe hii inatufundisha tujitoa na kujiachilia kwa Mungu hata kama tutateseka. Majitoleo yetu yawe kamili, sadaka iliyo hai, takatifu na inayopendeza machoni mwa Mungu [Rum 12:1-2]. Yesu Kristo ni sababu ya kusimama kwetu, ni Mwanga wa daima, tuuchukue Mwanga huu ili utusaidie tuione njia ya uzima wa milele, tuwaangaze na watu wengine ili nao pia waione njia ile iongozayo katika uzima wa milele.

31 January 2020, 15:29