Tafuta

Vatican News
Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya IV ya Kipindi cha Majilio: Emmanueli yaani Mungu pamoja nasi! Mungu anachukua jukumu la kuwakomboa watu wake! Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya IV ya Kipindi cha Majilio: Emmanueli yaani Mungu pamoja nasi! Mungu anachukua jukumu la kuwakomboa watu wake! 

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili 4 Majilio: Mungu pamoja nasi!

Yosefu amekuwa na mchango mkubwa katika kufanikisha mpango wa Mungu wa kumleta duniani mwanae Yesu Kristo kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu. Yosefu alimpokea Maria kama mke wake na hivi kumuandalia Maria mazingira mazuri ya kuwa Mama wa Mungu na pia kumwandalia Mtoto Yesu mazingira mazuri ya kuzaliwa na kukua katika familia. Yosefu amemlea Mtoto Yesu.

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

UTANGULIZI: Karibu ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News katika tafakari ya Neno la Mungu. Tunayatafakari leo Masomo ya dominika ya nne ya Majilio, mwaka A. Hii ni dominika inayotusogeza karibu kabisa na sikukuu ya Noeli na hivi hata masomo yanatualika kuyatafakari mazingira ya kuzaliwa kwake masiha mkombozi wetu. Somo la kwanza (Isa. 7:10-14 ) ni kutoka katika kitabu cha nabii Isaya. Ni somo linalofahamika kama somo la unabii wa Imanueli, Mungu pamoja nasi. Katika somo hili Ahaz mfalme wa Yuda anatishiwa kushambuliwa na ufalme wa Siria na wa Efraemu. Katika tishio hili, yeye anaamua kutafuta wa ufalme uliokuwa na nguvu zaidi, ufalme wa Ashuru. Nabii Isaya anamfata anamwambia asifanye ushirika na ufalme wa Ashuru, akabili tishio hilo mwenyewe na kwa uwezo wa Mungu atashinda. Ahazi anakataa. Ndipo Isaya anamwambia aombe ishara yoyote kutoka kwa Mungu kumthibitishia kuwa Mungu atakuwa naye na atashinda. Ahazi bado anakataa kwa kisingizio kuwa hataki kumjaribu Mungu.

Ndipo Isaya anamwambia kuwa Mungu mwenyewe atatoa ishara, na ishara hiyo ni kuwa bikira atatwaa mimba na atamzaa mwana na huyo mwana ataitwa Imanueli yaani Mungu pamoja nasi. Tunapoendelea mbele tunaona kuwa Ahazi alikataa kumtegemea Mungu akaungana na ufalme wa Ashuru. Vita walishinda lakini Ashuru akamfanya Ahazi kuwa mateka na kumuingiza utumwani. Somo hili linatuonesha kuwa masiha tunayemngoja ni Mungu mwenyewe anayechukua jukumu la kuja kwa watu wake awaokoe. Na watu wake hawa ni watu ambao wamejaa katika nafsi zao kiasi kwamba hawaoni ukubwa wa tatizo walilomo na mbaya zaidi wanajiona hawahitaji msaada wa Mungu katika kuokoka. Masiha tunayemgoja ni Mungu anayekuja kutusaidia kuamini. Somo la pili (Rum 1:1-7) ni kutoka katika Waraka wa mtume Paulo kwa Warumi. Mtume Paulo, mwanzoni kabisa mwa waraka wake huu anachukua jukumu la kumtambulisha Kristo kwa warumi.Kwanza kabisa anawaonesha kuwa Kristo ndiye injili ya Mungu ambayo yeye Paulo amewekwa kuwa mtume na mhubiri wake. Na Kristo huyu kimwili alizaliwa katika ukoo wa Daudi na kiroho amedhihirishwa kwa ufufuko wake kuwa mwana wa Mungu. Ni yeye ambaye kwa njia yake na kwa jina lake watu wamepokea neema ya kuwa mitume na wahubiri. Kristo ndiye asili ya utume injili na yeye mwenyewe ndiye injili inayohubiriwa. Kumbe hili ni somo linalomtambulisha Kristo, masiha tunayemgoja.

Injili (Mt. 1:18-24) Somo la injili ni kutoka kwa Mwinjili Mathayo. Linaonesha mazingira yaliyotangulia kuzaliwa kwa Yesu. Kwa namna ya pekee, somo linamtambulisha Yosefu, baba mlishi wa Yesu na kuonesha namna alivyoshiriki na namna alivyoupokea mpango wa Mungu. Yosefu akiwa amemposa Maria, kabla hata hawakaribiana anagundua kuwa ni mjamzito. Kwa kufuata sheria ya Musa, Yosefu angeweza kumshitaki Maria ambaye angeadhibiwa kwa kupondwa mawe hadi kufa. Yeye lakini somo linatuambia, kwa kuwa alikuwa ni mtu mwenye haki hakutaka kumwaibisha bali alikusudia kumwacha kwa siri.  Katika mahangaiko haya yote, Yosefu hakujua ni nini kinaendelea hadi hapo katika ndoto malaika alipomtokea na kumwambia kuwa Maria amepata mimba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. Malaika anamjulisha juu ya mtoto atakayezaliwa kuwa atampa jina Yesu. Yosefu anafanya kama alivyofunuliwa na malaika. Anamtwaa Maria kuwa mkewe na anakubali kutwaa majukumu ya kuwa baba mlishi. Ni yeye pia wa kumpa mtoto jina Yesu. Kwa kumpa jina anampokea katika ukoo wake wa Daudi na kadiri ya mwinjili Mathayo hii inatimiza unabii kuwa masiha ajaye atakuwa mwana wa Daudi na atakirithi kiti cha enzi cha Daudi baba yake. Jina Yesu kwa Kiyahudi ni Yoshua na maana yake ni “Mungu anayeokoa”. Jina hili linawakumbusha Wayahudi Yoshua mwana wa Nuni aliyemrithi Musa kama kiongozi aliyewaingiza wayahudi katika nchi ya ahadi. Ni jina linalomtambulisha Yesu kama mwokozi anayekuja kwa mamlaka kama ya Musa. Na ndicho tunachokiona kuwa kama Musa alivyowapa waisraeli Torati (Sheria), Yesu anasema “nimekuja si kuitangua Torati bali kuikamilisha” na anatoa Torati mpya au amri mpya ya mapendo.

Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, masomo ya Liturujia ya leo yanatuingiza katika kuyatafakari mazingira ya kuzaliwa kwa Yesu ili kuliingia kwa ukaribu zaidi fumbo la Noeli. Kwa namna ya pekee, Injili imetupatia mfano wa Yosefu, mume wa Bikira Maria kama kichocheo katika tafakari yetu. Yosefu amekuwa na mchango mkubwa katika kufanikisha mpango wa Mungu wa kumleta duniani mwanae Yesu Kristo kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu. Yosefu alimpokea Maria kama mke wake na hivi kumuandalia Maria mazingira mazuri ya kuwa mama wa Mungu na pia kumwandalia mtoto Yesu mazingira mazuri ya kuzaliwa na kukua katika familia. Yosefu amemlea mtoto Yesu kama walivyolelewa watoto wengine wa Kiyahudi wa wakati huo. Na familia yake hii, Yosefu ameihudumia, ameilinda na ameitunza kama baba, akijibidiisha na kufanya kazi yake ya useremala.  Ni kwa sababu hii Kanisa limemweka kama msimamizi wa wafanyakazi na wa baba wote wa familia. Tena amewekwa kuwa Mtakatifu msimamizi na mlinzi wa Kanisa ili aendeleze kwa familia ya kanisa zima tunza ile ile aliyoipa familia yake takatifu.

Mtakatifu Yosefu anatajwa kuwa mwenye haki na mkimya. Katika sehemu zote za Maandiko Matakatifu Yosefu hazungumzi neno. Haki ya Yosefu sio haki ya kisheria ya kufuata sheria kwa nukta bali haki yake ni haki ya uadilifu, wema, uungwana na kwa maneno mengine ni kuwa na ubinadamu katika kuhusiana na watu. Hali kadhalika ukimya wake sio ukimya wa kunyamazia mambo magumu na kuumia kwa ndani. Ni ukimya wa kujiachia mikononi mwa Mungu na kuacha Yeye Mungu achukue nafasi ya kwanza. Ni ukimya wa kutolea sadaka utashi binafsi na kuukabidhi katika utashi mpana wa mapenzi ya Mungu. Ukimya wake ni ukimya wa kuonesha kuwa japokuwa kwa wakati huo haelewi kinagaubaga ni nini, ni lini na ni kwa namna gani Mungu atatenda anakaa kwa matumaini kuwa Mungu atatenda tu. Ni kwa sababu hii Yosefu amewekwa kuwa msimamizi wa wote wanaoishi fadhila ya utii na ya usafi wa moyo kama zawadi ya mtu kujikatalia na kujikabidhi katika mapenzi mapana ya Mungu.

Yosefu aliyekufa mikononi mwa Yesu na Maria ni mwombezi wa kifo chema na wote walio kufani. Kutokana na ukuu na utakatifu wake, wakristo na kanisa zima limechochea ibada nyingi na majitoleo kwake. Mojawapo ya ibada inayohusika kwa ukaribu na injili ya leo ni ile ibada kwa Mtakatifu Yosefu anayelala. Ibada hii ina msingi katika injili ya leo ambapo Yosefu alipokuwa anajiandaa kufanya maamuzi kuhusu suala zito lililokuwa mbele yake alilala, na katika ndoto malaika akamfafanulia anavyopaswa kufanya. Wale wanaojikuta katika hali ya mkangayiko na wasijue cha kufanya au wanaohitaji mwangaza juu ya jambo zito wamefanya ibada kwa mtakatifu Yosefu kwa kusali na kwa kuweka chini ya sanamu ya Yosefu anayelala maombi yao. Mojawapo ya mashuhuda wa ibada hii katika nyakati zetu ni Papa Francisko ambaye amekuwa akifanya majitoleo na ibada kwa mtakatifu Yosefu tangu utoto wake huko Argentina. Mtakatifu Yosefu awe ni kichocheo kwetu cha maisha ya fadhila na uwajibikaji na kutoka kwake tujifunze kuyapokea mapenzi ya Mungu katika maisha yetu. Tujenge ibada kwake, naye atuombee tumpokee Yesu masiha na mkombozi wetu kama alivyofanya yeye.

Liturujia J4 Majilio
20 December 2019, 13:48