Tafuta

Vatican News
Tarehe 28 Desemba, kila mwaka Kanisa linawakumbuka watoto mashahidi waliouwawa kikatili kama mashuhuda wa Mtoto Yesu! Tarehe 28 Desemba, kila mwaka Kanisa linawakumbuka watoto mashahidi waliouwawa kikatili kama mashuhuda wa Mtoto Yesu! 

Siku kuu ya Watoto Mashahidi: Utoto Mtakatifu Jimbo Kuu la Dar!

Shirika la Kimissionari la Kipapa la Utoto Mtakatifu, Jimbo kuu la Dar es Salaam, kila mwaka linaadhimisha kumbu kumbu ya Watoto Mashahidi kwa kuwakusanya watoto kutoka katika Parokia zote ili kumzunguka Askofu mkuu na kwa mwaka huu wanamzunguka Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwaichi, ili aweze kuwatia shime na ari ya kuwa ni mitume wamissionari kati ya watoto wenzao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mama Kanisa tarehe 28 Desemba ya kila Mwaka anaadhimisha Siku kuu ya Watoto Mashahidi waliomshuhudia Kristo Yesu si kwa maneno bali kwa kuyamimina maisha yao kutokana na ukatili wa Mfalme Herode. Watoto hawa wanalikumbusha Kanisa kwamba, kifo dini ni zawadi kubwa kutoka kwa Kristo Yesu kwa ajili ya Kanisa lake. Hawa ni watoto waliouwawa kikatili kwa upanga wa Mfalme Herode aliposikia kwamba, kuna Mfalme amezaliwa mjini Bethlehemu. Siku kuu hii ilianza kuadhimishwa na Kanisa kunako karne ya VI kadiri ya taarifa za Kitabu cha Orodha ya Majina na Habari za Wafia dini cha Yerome! Hata katika ulimwengu mamboleo bado kuna watoto wanaoendelea kufutiliwa mbali na upanga wa Herode kutokana na vita, baa la njaa, magonjwa, ukatili, nyanyaso na majanga asilia; pamoja na ubinafsi unaofanywa na watu wazima. Hii ni changamoto ya kuhakikisha kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inajizatiti ili kulinda utakatifu wa maisha, utu, heshima na haki msingi za watoto.

Lengo ni kuwawezesha watoto kufurahia malezi, makuzi na utoto wao pasi na kubebeshwa mtutu wa bunduki kwenda mstari wa mbele badala ya kucheza na kufurahia maisha na watoto wenzao au kutumbukizwa katika biashara haramu ya dawa za kulevya, viungo vya binadamu na mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo. Vitendo vyote hivi vinasigina utu, heshima na haki msingi za binadamu Shirika la Kimissionari la Kipapa la Utoto Mtakatifu, Jimbo kuu la Dar es Salaam, kila mwaka linaadhimisha kumbu kumbu ya Watoto Mashahidi kama siku yao maalum, inayowakusanya watoto kutoka katika Parokia zote za Jimbo kuu la Dar es Salaam, ili kumzunguka Askofu mkuu na kwa mwaka huu wanamzunguka Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwaichi, ili aweze kuwatia shime na ari ya kuwa ni mitume wamissionari kati ya watoto wenzao wanaoteseka na kusumbuka kutokana na sababu mbali mbali. Ibada ya Misa Takatifu ni kwa ajili ya kumshukuru Mungu na kuomba heri na baraka kwa mwaka mpya wa 2020.

Watoto watatoa taarifa ya matendo ya huruma waliyotenda katika kipindi cha mwaka 2019 pamoja na kuzindua mpango mkakati wa kuunga mkono juhudi za Baba Mtakatifu Francisko katika kuwasaidia watoto wanaoishi katika umaskini, mazingira tete na hatarishi, ili hata katika umaskini wao, waweze kushirikishana neema na baraka za Mungu na watoto wengine. Shirika la Kimissionari la Kipapa la Utoto Mtakatifu, Jimbo kuu la Dar es Salaam litatumia fursa hii kuzindua mpango kazi kwa Mwaka 2020! Dar es Salaam, moto wa kuotea mbali kwa utume wa watoto hadi raha!

Utoto Mtakatifu Jimbo kuu la Dar Es Salaam
27 December 2019, 16:07