Tafuta

Vatican News
Kardinali Giuseppe Petrocchi anawaalika waamini kujiandaa kikamilifu kumpokea Mtoto Yesu anayezaliwa tena katika hali, mazingira na historia ya maisha yao. Kardinali Giuseppe Petrocchi anawaalika waamini kujiandaa kikamilifu kumpokea Mtoto Yesu anayezaliwa tena katika hali, mazingira na historia ya maisha yao.  

Sherehe ya Noeli 2019: Jiandaeni kumpokea Mtoto Yesu kati yenu!

Kardinali Giuseppe Petrocchi, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Aquila katika ujumbe wake wa Noeli anasema, Mtoto Yesu anazaliwa tena katika hali, mazingira na maisha yao yaliyoathiriwa na tetemeko la ardhi. Mtoto Yesu, kielelezo cha Mungu pamoja na watu wake ndicho kiini cha Fumbo la Umwilisho, ambalo waamini wanaliadhimisha wakati wa Sherehe ya Noeli. Mshikamano!

Na Padre Richard A. Mjigwa, - Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “ADMIRABILE SIGNUM” yaani “Ishara ya Kushangaza”: Maana na Umuhimu wa Pango la Noeli” anasema, Malaika wa Bwana na nyota angavu ni mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kwenda kumwabudu Mwana wa Mungu. Wachungaji wakawa ni watu wa kwanza kuona zawadi ya ukombozi. Maskini na wanyenyekevu wa moyo wakashuhudia Fumbo la Umwilisho. Kwa njia ya Kristo Yesu, Mwenyezi Mungu akapata tena nafasi ya kukutana na watoto wake katika mazingira ya Pango la Noeli. Mazingira ya Pango la Noeli kwa kawaida yanapaswa kuonesha uwepo wa maskini wanaothamini zaidi ufukara wa maisha ya kiroho. Hawa pia wanayo haki ya kuwa karibu na Mtoto Yesu na wala asiwepo mtu anayetaka kuwafukuzia mbali!

Katika muktadha huu, nyumba inakuwa ni mahali pa ukarimu kwa maskini, kwa sababu hawa ndio watu wa kwanza kabisa kutambua uwepo wa Mungu kati ya waja wake na hawa kimsingi ndio walengwa wa Habari Njema ya Wokovu. Pango la Noeli ni ukumbusho kwamba, utajiri na raha za dunia ni mambo mpito. Kardinali Giuseppe Petrocchi, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Aquila katika ujumbe wake wa Noeli anasema, Mtoto Yesu anazaliwa tena katika hali, mazingira na maisha yao yaliyoathiriwa na tetemeko la ardhi. Mtoto Yesu, kielelezo cha Mungu pamoja na watu wake ndicho kiini cha Fumbo la Umwilisho, ambalo waamini wanaliadhimisha wakati wa Sherehe ya Noeli.

Huu ni wajibu wa kusimama kidete kulinda, utu, heshima na haki msingi za binadamu. Watu waoneshe umoja, upendo na mshikamano wa dhati, bila kuwageuzia maskini kisogo. Noeli ni muda wa maalum wa upatanisho na Mungu pamoja na jirani; kwa kujikita katika upendo wa dhati. Waamini wawe na ujasiri wa kuchunguza undani wa maisha yao na kuona wapi wanapaswa kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani zao, ili kumpatia nafasi Kristo Yesu, aweze kuzaliwa tena katika maisha, historia na mazingira yao. Waamini waoneshe ujasiri wa kuwaendelea na kuwamegea Injili ya imani, matumaini na mapendo, watu wote waliosukumizwa pembezoni mwa jamii: kutokana na udhaifu wa maisha ya kiroho; kisiasa, kijamii na kiuchumi, ili wote hawa waweze kuonja huruma na upendo wa Mungu wakati huu wa Sherehe ya Noeli.

Kardinali Petrocchi
17 December 2019, 11:24