Tafuta

Vatican News
Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili II ya Kipindi cha Majilio: Kiini cha tafakari ni: Haki, amani na uaminifu kama chachu ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu hapa duniani. Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili II ya Kipindi cha Majilio: Kiini cha tafakari ni: Haki, amani na uaminifu kama chachu ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu hapa duniani.  (ANSA)

Tafakari Jumapili 2 ya Majilio: Haki, amani, uaminifu na ustawi!

Ufafanuzi wa Toba: Jambo la kwanza ni toba ya kisakramenti kama maandalizi ya ujio wa pili wa Kristo lakini pia kama maandalizi ya sherehe ya Noeli. Pili ni toba inayotukumbusha kuutwaa wajibu wetu katika kuujenga ufalme wa kimasiha, ufalme tunaoutamani na kuutumainia. Huu ni Ufalme wa kweli na uzima; utakatifu na neema; ufalme wa haki, amani na mapendo, chachu ya maendeleo.

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

Utangulizi: Karibu ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News katika tafakari ya Neno la Mungu. Tunayatafakari leo Masomo ya dominika ya pili ya Majilio, mwaka A. Ujio wa Masiha tunayemgoja unafananishwa na ujio wa ufalme wa Mungu na ni ujio unaotualika kutubu: kusafisha mioyo yetu ili kumlaki masiha ajaye na kujibidiisha kuujenga ufalme wake wa kimasiha katika maisha yetu. Somo la kwanza (Isa. 11:1-10 ) kutoka katika kitabu cha nabii Isaya linatoa matumaini ya ujio wa ufalme wa kimasiha. Tunaanza kwa kusikia “litatoka chipukizi katika shina la Yese”. Yese alikuwa ndio baba wa mfalme Daudi. Shina la Yese ni uzao wake, na kwa vile uzao wa Yese ulihusishwa na ufalme wa Daudi, kumbe shina la Yese lilimaanisha ufalme mzima wa Israeli kuanzia kwa Daudi na wafalme waliofuata baada yake. Shina hili lilikuwa limekatwa kwa maana ufalme wa Israeli uliangushwa na taifa zima likapelekwa utumwani Babiloni. Ni hapa Isaya anautoa unabii wake kuwa shina hili liliokatwa litapata chipukizi.

Kuna kitu kitaanza kuchipua pale katika shina lililobaki: shina litapata mizizi na litatoka tawi litakalozaa matunda. Isaya analifafanua tawi hili kuwa litakaliwa na roho ya Bwana. Huyu ni Roho Mtakatifu ambaye ufunuo wake kamili ulikuja katika Agano Jipya. Hapa anatakwa katika mapaji yake ya hekima, akili, shauri, nguvu, elimu na kumcha Bwana yaani uchaji wa Mungu. Isaya lakini analitambulisha chipukizi hili zaidi katika mapaji ya haki na uaminifu; kuwa ndiye atakayeleta enzi ya haki, uaminifu na amani katika mataifa. Na alama ya ustawi wa haki na amani ni kuwa wanyama wanaowinda watakaa pamoja na wale wanaowindwa halikadhalika hata wale walio hatari watasogelewa bila madhara. Chipukizi hili analoliongelea nabii Isaya, waisraeli walilitambua kuwa ndiye masiha anayatabiriwa kuja na kuanzisha enzi mpya, enzi ya ufalme wa kimasiha ambayo itakuwa na nguvu kuliko enzi ya ufalme wa Daudi na ambayo itawaletea ukombozi wa kweli katika maisha yao. Hii ndiyo majilio ya waisraeli, kumgoja masiha ambayo nasi katika kipindi hiki cha kiliturujia tunaiishi roho yake.

Somo la pili (Rum. 15:4-9) ni kutoka katika waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi. Paulo anawaandikia Warumi akijua kuwa kanisa katika mji wa Roma ni kanisa lililo na watu mchanganyiko kiimani na hata kijamii. Katika aya ya kwanza ya sura hii hii ya 15 anazungumzia utofauti wa imani na hapo anataja kuwa wapo walio na nguvu na wapo walio dhaifu. Mchanganyiko wa kijamii uliokuwapo ulikuwa ni kati ya wakristo Wayahudi na Wakristo wasio Wayahudi (Warumi, Wagiriki nk). Ni katika mazingira haya katika somo la leo anawaasa wajifunze kuchukuliana na wapokeane katika utofauti wao walijenge kanisa moja. Anasema “mkaribishane ninyi kwa ninyi, kama vile Kristo alivyotukaribisha, ili Mungu atukuzwe.” Kanisa linaloutafuta umoja na kuuishi umoja humtukuza Mungu. Paulo kila anapotoa mafundisho ya kijamii hujikita kwa Kristo na kwa mfano wa maisha yake kuwaalika watu kujifunza kutoka kwake.  Hata katika somo hili anawaalika Warumi wajifunze kwa Kristo na kwa mfano wakewajaliwe kunia majoma wao kwa wao na ili kwa moyo mmoja na kwa kinywa kimoja wapate kumtukuza Mungu Baba.

Injili (Mt. 3:1-12) Somo la Injili ni kutoka kwa Mwinjili Mathayo na ni somo hili linatoa mwaliko wa kutubu kwa maana ufalme wa Mungu umekaribia. Mwaliko huu wa kutubu unatajwa pamoja na nafsi ya Yohana Mbatizaji na mazingira ya nyika au jangwa. Katika matumaini ya ujio wa masiha, waisraeli waliamini katika unabii kuwa kabla yake atatangulia kwanza Eliya. Somo la leo linapomtaja Yohane mbatizaji, linataja vazi lake kuwa ni singa za ngamia na mshipi wa ngozi kiunoni. Haya ndiyo yalikuwa mavazi ya Eliya na ndiyo yaliyomtambulisha kama tunavyosoma katika kitabu cha pili cha wafalme 1:8. Kumbe, kumtaja Yohane Mbatizaji katika mavazi ya Eliya ni kumtambulisha kuwa ndiye Eliya mpya, na kwa vile Eliya amekwisharudi kwa nafsi ya Yohane mbatizaji basi Masiha naye amefika.

Pili, Yohane huyu anatokea jangwani. Jangwa linawakumbusha daima waisraeli kipindi cha miaka 40 walipokaa jangwani katika safari yao ya kutoka Misri. Kipindi hicho wakiwa jangwani ni kipindi ambacho walikua katika imani kwa Mungu, kipindi ambacho walionja wema wa Mungu aliyewalisha usiku na mchana, kipindi ambacho Mungu aliwalea na kuwafundisha katika njia zake. Jangwa pia huwakumbusha waisraeli uasi ambao walimfanyia Mungu kwa kumjaribu, kumnung’unikia na kumuasi kwa dhambi zao. Mazingira haya yanayowakumbusha waisraeli mazingira waliyotoka pamoja na kuwaonesha kuwa Eliya amekwishakuja yanawafanya watambue kuwa hawana muda wa kuendelea kupoteza. Ufalme wa mbinguni umekaribia, waupokee kwa kutubu na kwa kubadili maisha yao.

Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, Maandiko Matakatifu katika dominika hii ya pili ya majilio, yanakuza matumaini yetu ya kumgonjea na kumpokea Kristo Masiha anayekuja. Kwa lugha ya kinabii, masomo yameonesha namna ambavyo hali ya ubinadamu ilikuwa kabla ya masiha. Ilikuwa haina matumaini na ni kama ilikuwa imekufa. Masiha anatabiriwa kuchipua kama chipukizi kutoka shina lililokauka. Masomo haya yamemuonesha pia kuwa ni yeye aliye msingi na kiini cha mabadiliko ya kweli katika jamii. Mabadiliko yanayoiunganisha jamii kuwa kitu kimoja bila matabaka. Mabadiliko yanayowaleta watu wote pamoja katika umoja licha ya kuwa na tofauti zao. Lakini hapo hapo masomo yanatuonesha umuhimu wa toba tunapongojea utimilifu wa matumaini hayo. Ujio wa masiha tunayemgoja unafananishwa na ujio wa ufalme wa mbinguni na unabeba mwaliko uleule “tubuni, kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia”.

Mwaliko huu wa toba, ndugu zangu, unatukumbusha mambo mawili. Jambo la kwanza ni toba ya kisakramenti tunayoalikwa kuifanya katika kipindi hiki cha majilio kama maandalizi ya ujio wa pili wa Kristo lakini pia kama maandalizi ya sherehe ya Noeli ili tuweze kumlaki masiha katika moyo safi. Ni kwa sababu hii kanisa limekuwa na desturi ya kuhimiza maungamo katika kipindi hiki cha majilio kama mojawapo ya vipengele muhimu ya kujiandaa kwa sherehe ya Noeli ili sherehe hii isibaki katika shamrashamra za nje tu bali iiguse mioyo ya waamini na kuwaachia wingi wa neema na baraka za Mungu. Jambo la pili ni kwamba mwaliko huu wa toba unatukumbusha kuutwaa wajibu wetu katika kuujenga ufalme wa kimasiha, ufalme tunaoutamani na kuutumainia. Kila jamii inatamani amani na utulivu. Inatamani haki na uaminifu vitawale: inatamani ustawi. Haya yote yametajwa na manabii kuwa ni matunda ya ustawi wa ufalme wa kimasiha.

Ustawi huu lakini unahitaji kuwajibika katika kuujenga. Hili linatukumbusha kuwa neema ya Mungu kufanya kazi ndani yetu inahitaji ushirikiano wetu. Alifundisha Mtakatifu Augustino kuwa “Mungu aliyekuumba wewe pasipo wewe hawezi kukuokoa pasipo wewe”. Tunayatafakari haya leo kwa sababu mara nyingine jamii zetu zinatawaliwa na matumaini ya ustawi, matumaini ya haki na amani, matumaini ya umoja na usawa lakini yanabaki kuwa ni matumaini hewa kwa maana kwamba linapokuja suala ya kuyageuza matumaini haya kuwa uhalisia kwa maana ya kuwajibika kuyajenga, wengi hawako tayari. Tuupokee basi mwaliko huu wa Yohane Mbatizaji, mwaliko wa kutubu kwa maana ya kuisafisha mioyo yetu kumpokea masiha na pia kuutwaa wajibu wetu na wa kujenga ufalme wa kimasiha katika familia na jamii tunamoishi.

Liturujia J2 Majilio
07 December 2019, 10:02