Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya Nne ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa: Emmanueli, yaani Mungu pamoja nasi! Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya Nne ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa: Emmanueli, yaani Mungu pamoja nasi! 

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya Nne ya Majilio: Emmanueli!

Mwinjili Mathayo katika Injili anaonyesha jinsi utabiri wa Nabii Isaya usemao, Tazama, bikira atachukua mimba, naye atazaa mwana; nao watamwita jinalake Emanueli; yaani, Mungu pamoja nasi, unavyotimia katika kuzaliwa kwake Yesu. Huyu ni Emanueli halisi. Dokezo kwa kazi yake, mtoto ataitwa “Yesu” yaani “Mungu mkombozi wetu”. Waamini jiandaeni vyema kumpokea Kristo Yesu nyoyoni mwenu.

Na Padre Paschal Ighondo - Vatican.

Karibu ndugu msikilizaji wa Radio Vatican katika tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya nne ya Kipindi cha Majilio mwaka A wa Kanisa. Dominika ya leo ni ya mwisho katika kipindi cha majilio. Siku chache zijazo tutasherehekea sherehe ya kuzaliwa kwa Bwana wetu Yesu Kristo yaani Krismasi, Noeli, kuzaliwa kwa Emanuel, Mungu pamoja nasi. Kuzaliwa kwake ni zao la utii na heshima kwa mpango wa Mungu wa kutukomboa sisi wanadamu. Maria na Yosefu kila mmoja kwa nafasi yake wanaridhia nia ya Mungu kwa viumbe wake. Nabii Isaya katika somo la kwanza anatoa utabiri kwa Mfalme wa Yerusalemu Ahaz, wa ukoo wa Daudi, aliyeshambuliwa na maadui, Mungu anamwahidia msaada iwapo atakuwa na imani na matumaini juu yake. Ingawa mfalme anakosa imani, Mungu anampa alama ya mtoto ambaye ataitwa Imanueli yaani “Mungu pamoja nasi”. Mwanamke anayetajwa na nabii Isaya ni Bikira Maria na mtoto mwanaume atakayezaliwa ni Yesu Kristo (Mt 1:22-25) anayetajwa katika somo la pili kuwa ni mwana wa Mungu.

Mtume Paulo katika somo la pili la Waraka wake kwa Warumi anatueleza kuwa Kristo ni Mwana wa Mungu na wa Daudi. Kwa uwezo wa kimungu alifufuka kutoka wafu na anaongoza historia ya wokovu wetu kutoka mbinguni. Mwinjili Mathayo katika Injili anaonyesha jinsi utabiri wa Nabii Isaya usemao, Tazama, bikira atachukua mimba, naye atazaa mwana; nao watamwita jinalake Emanueli; yaani, Mungu pamoja nasi, unavyotimia katika kuzaliwa kwake Yesu. Huyu ni Emanueli halisi. Dokezo kwa kazi yake, mtoto ataitwa “Yesu” yaani “Mungu mkombozi wetu”. Injili pia inamtaja Yosefu kwa namna ya pekee kuwa ni mtu mwenye haki. Maana yake mtu aliyeshika Torati vizuri, alifuata mafundisho na kanuni za Kiyahudi vizuri, tena alikuwa mcha Mungu. Katika mila na desturi za Kiyahudi taratibu za kuoa na kuolewa zilifuata hatua kuu tatu. Maria na Yosefu walikuwa wamefikia hatua ya pili ambayo wachumba walitambulika kisheria, tena katika hatua hiyo sheria na taratibu zilizowabana watu wa ndoa zilianza kutumika kwa wachumba hao ingawa hawakuruhusiwa kukutana kimwili.

Kwa hiyo katika hali hiyo, kama mchumba wa kiume angefariki, basi mchumba wa kike alihesabiwa kama mjane na ilimpasa kufuata taratibu zote za wajane kabla ya kuolewa kwa mme mwingine. Mchumba wa kike akipata mimba kabla ya ndoa, sheria iliamuru mwanamke huyo apelekwe mahakamani ili akapewe talaka na adhabu ya kupigwa kwa mawe hadi kufa. Tena mme hakuruhusiwa kuendelea kuishi na mwanamke mzinzi. Hivyo basi, jambo mojawapo kati ya hayo mawili lingempata Bikira Maria. Mtakatifu Yosefu kwa kuwa mtu wa haki hakupenda kumuaibisha Bikira Maria kwa kumtangaza au kumpeleka mahakamani na kumuacha apigwe kwa mawe hadi kufa. Yeye alitaka kumuacha kwa siri. Mtakatifu Yosefu anakuwa kielelezo na mfano bora wa kuiga kwetu Sisi tusio mcha Mungu, tusio wasamehe wenzetu, na tunaopenda kuwaaibisha watu walio na mkosa, mwenyezi Mungu anataka tusameheane na kuheshimiana. Tuchukie dhambi siyo mdhambi. Tukumbuke kila mmoja ameumbwa kwa sura na mfano wa Mwenyezi Mungu.

Ujauzito ambao ameelezwa kuwa nao Bikira Maria katika Injili ya leo ni zao la ukubali wake kwa ujumbe aliopewa na malaika Gabriel mjumbe wa Mungu wa kutaka kwa njia yake azaliwe Mwana wa Mungu atakayeikomboa dunia kutoka katika utawala wa Shetani (Lk 1:28-35). Kutokana na utii, heshima na ukubali wa Bikira Maria pamoja na utayari wa Yosefu kukubali kumtwaa Maria kama mke wake ndio kunamfanya Mungu kuzaliwa kwetu na kuwa kama mwanadamu ili auinue ubinadamu wetu ulioharibika na kuchakaa kwa dhambi na sasa tusitahili tena kuitwa wana wapenzi wa Mungu. Kama Bikira Maria tuwe na utii na kuitikia wito wa Mungu na kusema, mimi ni mjakazi wa Bwana na iwe kwangu kama ulivyosema hasa pale Mungu anapotutaka tumtumikie kwa namna ya pekee jinsi ile Bikira Maria alivyoridhia. Moja kati ya maandalizi tunayoalikwa kuyafanya kwa ajili ya Sherehe ya Noeli, ni Kitubio. Hivyo basi nawaalika tutafakari juu ya faida za Sakramenti ya Kitubio.

Tangu domenika ya kwanza tulipewa mwaliko wa kuitengeneza njia ya Bwana, kuyanyoosha mapito yake. Kumbe, mwaliko huo sio wa siku moja bali ni katika maisha yetu ya kila siku. Tujiandae vyema ili kweli Kristo aweze kuzaliwa katika maisha yetu, katika nafsi zetu, katika familia zetu na jumuiya zetu. Kitubio kinanirudishia urafiki wangu na wengine. Kitubio kinanisaidia kutunza dhamiri yangu. Ninapotenda dhambi na kutoiugama kwa muda mrefu, dhamiri yangu inaanza kuizoea hiyo dhambi. Matokeo yake hainionyi tena kuwa hiyo ni dhambi. Ninaacha kuogopa dhambi na ninaweza kufanya dhambi yoyote, wakati wowote na mbele ya yeyote. Ninapoungama, ninaifundisha dhamiri kuwa jambo hilo ni baya. Hivyo, itakuwa macho kila mara na kunionya ninapokaribia kutenda jambo hilo na nikiitenda itanisuta kuwa nimefanya vibaya. Mzaburi anasema, “Dhambi huongea na mtu mwovu ndani kabisa moyoni mwake; wala jambo la kumcha Mungu halimo kabisa kwake.

Kwa vile anajiona kuwa maarufu hufikiri kuwa uovu wake hautagunduliwa na kulaaniwa. Kila asemacho ni uovu na uongo; ameacha kutumia hekima na kutenda mema. Alalapo huwaza kutenda maovu, wala haepukani na lolote lililo baya.” (Zab.36:1-4). Tunapokuwa katika hali ya dhambi tunakuwa kama vipofu. Tunahitaji kitubio ili kuondoa huu upofu unaoletwa na dhambi ili tuweze kurudisha hali ya kuwa na haya kuhusu dhambi. Kutokuionea haya dhambi ni kukosa mizani ya maadili, ni kushindwa kufa kuhusu dhambi. Kitubio kinatusaidia kurudisha urafiki wetu na Mungu. Kwa kutenda dhambi tunamkataa Mungu na kwenda mbali naye; tunaharibu urafiki wetu na Mungu. Kitubio kinatusaidia kumwomba msamaha Mungu, kuondolewa dhambi na kurudisha urafiki wetu na Mungu, Kristo, Emanueli Mungu pamoja nasi anakuwa ndani mwetu. Kitubio kinaniondolea adhabu ya milele. Hii adhabu ingenipeleka katika moto wa milele. Nikiungama ninaepuka hii adhabu.

Tutambue kuwa lazima kuungama kwa Padre kwa kuwa ni agizo la Kristo, “Wowote mtakaowaondolea dhambi wameondolewa; na wowote mtakaowafungia dhambi wamefungiwa.” (Yoh. 20:23).  Neno nenda kwa amani umesamehewa dhambi zako haliwezi kusemwa na yeyote ila Padre anayefanya hivyo katika nafsi ya Kristo mwenyewe. Basi ndugu tujiandae vyema kumpokea Mungu katika Sherehe ya Noeli. Tumsifu Yesu Kristo.

Jumapili 4 Majilio
17 December 2019, 15:53