Tafakari ya neno la Mungu, Jumapili II ya Kipindi cha Majilio: Wazo Kuu ni kutubu na kumwongokea Mungu katika maisha. Tafakari ya neno la Mungu, Jumapili II ya Kipindi cha Majilio: Wazo Kuu ni kutubu na kumwongokea Mungu katika maisha. 

Tafakari Jumapili ya 2 ya Majilio: Tubuni na Kuiamini Injili!

Yohane Mbatizaji ni kielelezo cha jinsi ya kujiandaa kwa ujio wa Yesu Kristo. Ni mwaliko wa kuishi kwa tahadhari kuu na kuishi maisha ya kiasi. Kutoka katika maisha ya anasa na starehe ili tuweze kwenda jangwani kuweza kuisikia sauti ya Mungu. Ujumbe wa Yohane Mbatizaji katika Dominika hii ya leo unafupishwa kwa ujumbe wa kutubu na kubatizwa kwa kuwa ufalme wa mbinguni ukaribu.

Na Padre Gaston George Mkude. – Roma.

Amani na Salama! Sehemu ya Injili ya leo tunakutana na Yohane Mbatizaji, ambaye habari zake tunazipata si tu katika Maandiko bali hata kutoka kwa mwanahistoria Giuseppe Flavio anayetuambia kuwa alikuwa ni mtu mwema na mwenye hofu kubwa ya Mungu. Ni Yohana Mbatizaji aliyekuwa anawahubiria na kuwaalika waebrania kubadili maisha yao kwa maana ya kuyanyoosha ndio kuenenda kadiri ya mapenzi ya Mungu. Aliwabatiza kwa kuwaalika kufanya mabadiliko ya maisha yao. Hata mwinjili Mathayo leo anatuonesha jinsi Yohane Mbatizaji alivyokuwa mtu wa nidhamu kali katika maisha yake binafsi. Aliishi na kuhubiri jangwani. Hivyo chakula chake kilikuwa ni kile cha kawaida kinachoweza kupatikana jangwani, na hata mavazi yale ni yale waliyovaa wachungaji waliokuwa wanabaki jangwani ili kuhimili mazingira magumu ya baridi na hata wanyama wakali wa nyikani. Kifupi Yohane Mbatizaji ni kielelezo cha jinsi tunavyopaswa kujiandaa kwa ujio wa Bwana wetu Yesu Kristo.

Huu ni mwaliko wa kuishi kwa tahadhari kuu na hasa kutualika nasi kuishi maisha ya kiasi. Kutoka katika maisha ya anasa na starehe ili tuweze kwenda jangwani kuweza kuisikia sauti ya Mungu. Ujumbe wa Yohane Mbatizaji katika Dominika hii ya leo unafupishwa kwa ujumbe wa kutubu na kubatizwa kwa kuwa ufalme wa mbinguni ukaribu. Ni shime kubwa kwa waliomsikiliza Yohana Mbatizaji kiasi cha kuwafanya kutoka katika nchi ile ya ahadi na kurejea tena jangwani, maisha waliyopitia baba zao. Jangwani ni sehemu ya ukiwa na kimya kikuu ili kila mmoja aweze kufikiwa na ile sauti ya Mungu. Ni mahali pakuweza kila mmoja wetu kuingia ndani mwake na kubaki na Mungu pekee. Leo tunaishi katika ulimwengu wenye kelele za kila aina, ila kwa kipindi hiki cha majilio ni fursa tena nyingine ya kwenda jangwani. Wana Waisraeli walisafiri jangwani kwa muda wa miaka 40, ndio kusema muda mrefu, ni lengo na shabaha ya Mungu kutumia muda huo mrefu ili awaunde na kutengeza kuwa wana na Taifa lake teule.

Kwa njia yao, watu wa mataifa mengine yote waweze kumjua Mungu. Jangwani ni mahali ambapo huwezi kuweka makazi au makao ya kudumu, ni sehemu ya mpito, hivyo kubaki na mambo ya msingi tu tunayoyahitaji kwa maisha yetu. Leo tunaishi katika ulimwengu wa kumiliki na kukumbatia kila aina ya mali na utajiri wa ulimwengu huu. Sisi rafiki zake Kristo tunaalikwa kurejea jangwani, kuishi kwa yale ya msingi na kutojilimbikizia mali na utajiri bali kutumia yote tunayojaliwa kwa upendo kwa wengine wanaosafiri pamoja nasi. Jangwani ni mahali ambapo tunaalikwa kuungana ili kusafiri kwa pamoja. Ni mahali ambapo kila mmoja wetu anamjali mwingine na kuona fahari kubaki katika muungano na mshikamano wa upendo na mwingine. Ni katika muktadha huo wa kurejea tena jangwani pembeni mwa mto ule wa Yordan tunaona Yohane Mbatizaji anawaalika wasikilizaji wake kutubu na kubatizwa. Ni mwaliko wa kubadili maisha yao, na ndio kubadili vichwa, namna na jinsi zao za kufikiri. Wanatoka Yerusalemu na miji yote ya Yuda, ndio kusema wanatoka katika ardhi ile waliodhani wapo huru, ili warudi tena nyikani kuweza kupata uhuru wa kweli. Uhuru wa kweli ni katika kupokea toba na kubatizwa, ni katika kubadili vichwa na kukubali kuongozwa na sauti ya Mungu, yaani ni Neno lake.

Yohane Mbatizaji anawatambua Mafarisayo na Masadukayo kama uzao wa nyoka, kwa mafundisho na namna zao za maisha kuwa ni kinyume na mapenzi ya Mungu na Sura ya Mungu. Nao waliofika pale nyikani wanaalikwa kuzaa matunda yapasayo toba. Haitoshi kuwa wazaliwa wa Ibrahimu bali tunaalikwa sote kushiriki kuwa wana wa Mungu ndio kushiriki ufalme wa Mungu, kuwa wana wa ufalme huo. Lugha ya kiapokaliptiki inayotumika katika somo la Injili ya leo naomba ieleweke kuwa sio lengo na shabaha ya Mungu kumwangamiza mwanadamu. Naomba tuepuke kila mara tafsiri potofu za Neno la Mungu ambazo zinatupotosha kuuona Sura ya Mungu wa kweli. Ilikuwa ni lugha ya kawaida kwa nyakati zile za Yesu na wasikilizaji walielewa aina ile ya uandishi na lugha, hivyo nasi leo ili kupata ujumbe kusudiwa hatuna budi kusaidiwa na wataalamu wa Maandiko Matakatifu, hivyo nawasihi tuepuke kila mara kutoa au kupokea tafsiri zinazokinzana na Sura ya Mungu.

Yohane Mbatizaji anawatahadharisha wasikilizaji wake juu ya ujio wa yule atakayebatiza si kwa maji bali kwa moto. Moto ni ishara inayotumika kuleta mwanzo mpya kwa kutekeza ulimwengu ule wa kale na mabaya yote, ni mwaliko wa mwanzo mpya katika ukamilifu wake. Ubatizo wa moto ndio unaotufanya sasa sisi kuwa viumbe vipya, kuweza kuondolewa dhambi zetu na kufanyika kweli wana wa Mungu. Si tu ishara ya nje bali ni ubatizo unaotuwezesha kuwa wapya kwa maana halisi. Kama ambavyo wanawaisraeli walivyoalikwa kutoka katika nchi yao, hivyo nasi leo kila mmoja wetu anaalikwa kutoka katika hali na mtindo ule wa maisha tunaojisikia kuwa tupo huru na nyumbani ili tuweze kwenda jangwani na kuanza maisha mapya, maisha ya kuishi katika kumsikiliza Mungu, kubaki kuishi kwa yale ya msingi tu na si kujilimbikizia. Kuishi tukijua tupo njiani, tupo katika malezi na majiundo ili tuweze kuingia sasa nchi ile ya ahadi, nchi ya maziwa na asali, ndio katika ufalme wa Mungu tunaoalikwa kuuishi kila siku za maisha yetu.

Yohane anatuambia kuwa ufalme wa Mungu umekaribia, sio kwa maana kuwa upo mbali nasi bali tayari ukatikati yetu ndio kusema kumpokea Masiha na kukubali kila ovu na ubaya uondoke na kutosikika katikakati yetu. Nawatakia tafakari njema na Dominika njema.

07 December 2019, 09:12