Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya kwanza ya Kipindi cha Majilio inakita ujumbe wake katika kukesha ili kuweza kumngojea Masiha ajaye! Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya kwanza ya Kipindi cha Majilio inakita ujumbe wake katika kukesha ili kuweza kumngojea Masiha ajaye! 

Tafakari Jumapili 1 ya Majilio: Kesheni, jiandaeni kikamilifu!

Wafuasi wanamwalika Yesu kuangalia uzuri wa Hekalu lile la Yerusalemu. Ni katika muktadha huo Yesu badala ya kushiriki nao katika kujivunia uzuri wa hekalu lile, anatumia fursa hii kuwapa ujumbe wa kinabii. Yerusalemu haitabaki salama kama hawatakubali kubadilika na kumpokea huyu aliye Masiha na Mkombozi. Kutompokea Masiha ni kujitakia angamizo na mwisho wetu. Kesheni basi!

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma

Amani na Salama! Lugha inayotumika katika somo la Injili ya leo ni ngumu na hivyo huweza kupelekea hata kutoa tafsiri ya Neno la Mungu zinazopotosha na hasa kuogofya msikilizaji, na hivyo Neno la Mungu kukosa kuwa Habari Njema ya Wokovu. Aina ya lugha ya kiapokaliptiko ilikuwa inatumika sana katika nyakati zile za Yesu Kristo. Daima tuongozwe na kanuni ya msingi kuwa Neno la Mungu ni Habari Njema ya wokovu, ni tangazo au habari ya furaha na matumaini. Hivyo sio lengo wala kusudi wa Neno la Mungu kutujaza hofu na woga na mahangahiko katika maisha yetu. Ni mwaliko wa kushiriki maisha ya kila siku kadiri ya mapenzi na mpango wa Mungu kwetu wanadamu. Ni kweli kuwa lugha ya sehemu ya Injili ya Dominika hii ya kwanza ya majilio tunaona inatumia lugha ya kuogofya. Yesu anatumia aina hii ya lugha kutuonesha hatari ya kupoteza fursa hii adhimu na adimu yaani wokovu wetu. Ni mwaliko wa kubadili vichwa vyetu katika maisha yetu na hivyo kuishi si kana kwamba hakuna tena maisha baada ya maisha ya hapa duniani, ni kuishi kwa matumaini na hasa kwa kuongozwa na Neno la Mungu na si kwa namna za dunia hii. Ni kukesha!

Wafuasi wanamwalika Yesu kuangalia uzuri wa Hekalu lile la Yerusalemu. Ni katika muktadha huo Yesu badala ya kushiriki nao katika kujivunia uzuri wa hekalu lile, anatumia fursa hii kuwapa ujumbe wa kinabii. Yerusalemu haitabaki salama kama hawatakubali kubadilika na kumpokea huyu aliye Masiha na Mkombozi.  Kutompokea Masiha ni kujitakia angamizo na mwisho wetu. Ni hapo wanafunzi wanahoji zaidi ni lini maangamizi hayo yatakapojiri. Maswali yao yanampelekea Yesu kutumia fursa hii kuwapa mafundisho yanayotugusa hata nasi leo.  Yesu ananukuu mifano mitatu, yote ikiwa na shabaha ya kutualika kukesha, kuwa macho, kubadili vichwa na hasa aina zatu za maisha. Nukuu ya kwanza anaitumia kutoka Kitabu cha Mwanzo sura zile za 6-9. Nyakati za Nuhu kulikuwa na makundi mawili ya watu. Kundi la kwanza ni la wale waliokuwa wanaishi kwa ajili ya kula na kunywa, hivyo hawakuwa wanasoma alama za nyakati na kubaki kutenda na kufikiri ya kiulimwengu huu. Na kundi la pili ni la wale waliosoma alama za nyakati na hivyo kujiandaa kwa ile hatari ya gharika kuu. Kama ambavyo ilivyokuwa ghafla tukio la gharika ndivyo Yesu leo anatuonya juu ya ujio wa Masiha. Ni mwaliko wa kukesha na kubaki daima katika matarajio ya ujio wa Masiha.

Mfano wa pili Yesu anaoutumia ni shughuli za kila siku za mwanadamu. Hatuna budi kuwa macho ndio kusema kutenda yote tukiongozwa sio na mantiki ya dunia hii bali daima tukiongozwa na mantiki ya Neno la Mungu, tuishi na kutenda sio kwa namna za kiulimwengu bali kimungu. Ni kubadili vichwa vyetu na hapo kuishi maisha ya kila siku kwa mantiki ya Neno la Mungu. Yesu kama Masiha na Mkombozi wetu anakuja kila siku katika maisha yetu, na ndio mwaliko wa tafakari wa kipindi cha majilio. Yesu anakuja na kutualika kuishi na kutenda yote tukiongozwa naye, tukiongozwa na Neno lake. Mfano wa tatu anaotumia Yesu leo ndio ule wa ujio wa mwizi, kama vile hatoi taarifa ya ujio wake, hivyo anatualika nasi kukesha. Ni wazi inatafakarisha kama Mungu ni Baba yetu Mwema na anayetupenda upeo iweje atujilie kama mwivi?! Kwa kweli lugha hii kama nilivyotangulia mwanzoni kuwa lengo na shabaha yake sio kutufanya tuogope bali tuone thamani na ukubwa wa wokovu wetu. Hivyo ni alarm ya kutuamsha na kutufanya tubadili namna zetu za maisha. Neno la Mungu na hasa tunapoanza kipindi hiki cha neema za Majilio linatualika kuwa na mtazamo mpya.

Hatuna budi kuwa na mtazamo mpya unaoongozwa na Neno la Mungu kwani hatujui siku wala saa atakapokuja Mwana wa Adamu! Majilio ni kipindi kizuri kwetu kwani kinatualika kutafakari sio tu ule ujio wa kwanza wa Bwana wetu Yesu Kristo bali pia siku ile atakapokuja tena katika utukufu kuwahukumu wazima na wafu. Lakini zaidi sana hatuna budi kuishi kila siku ya maisha yetu kama vile ni siku yetu ya mwisho kwa kuongozwa na Neno la Mungu. Nawatakia tafakari na Dominika na majilio mema.

01 December 2019, 09:43