Tafuta

Vatican News
Jumuiya ya watu wa Mungu kutoka DRC inamshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kusimama kidete kulinda na kutetea utu, heshima na haki msingi za wakimbizi na wahamiaji. Jumuiya ya watu wa Mungu kutoka DRC inamshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kusimama kidete kulinda na kutetea utu, heshima na haki msingi za wakimbizi na wahamiaji. 

Familia ya watu wa Mungu kutoka DRC: Kiu ya amani na utulivu!

Ibada hii ya Misa Takatifu ni kumbu kumbu ya Jubilei ya Miaka 25 tangu Jimbo Kuu la Roma lilipowakabidhi watu wa Mungu kutoka DRC, Kanisa la “Natività” ili kuweza kukutanika ili kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa: Kumbu kumbu ya Mwenyeheri Sr. Marie Clemente Anwarite alipouwawa kikatili tarehe 1 Desemba 1964 na kumbukumbu ya Miaka 25 ya Mwenyeheri Isidori Bakanja! AMANI!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko kwa kuguswa na mateso pamoja na mahangaiko ya watu wa Mungu nchini Jahuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Congo, DRC, Jumapili ya kwanza ya Kipindi cha Majilio, yaani tarehe 1 Desemba 2019, majira ya saa 4: 00 kwa saa za Ulaya ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya watu wa Mungu nchini DRC, kama sehemu ya hija ya faraja na matumaini kwa Mungu nchini DRC ambao kwa miaka ya hivi karibuni wamepitia vipindi vigumu vya vita, kinzani, migogoro, majanga pamoja na milipuko ya mbali mbali ya magonjwa. Baba Mtakatifu anapenda kusali ili kuwatia shime watu wa Mungu kutokukata tamaa, bali waendelee kujiaminisha chini ya ulinzi na tunza ya Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo! Ibada hii ya Misa Takatifu ni kumbu kumbu ya Jubilei ya Miaka 25 tangu Jimbo Kuu la Roma lilipowakabidhi watu wa Mungu kutoka DRC, Kanisa la “Natività” ili kuweza kukutanika ili kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa.

Hii ilikuwa ni mwaka 1994 Kardinali Frèdèric Etsou, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Kinshasa, DRC alipoonesha busara na hekima ya kichungaji kwa kuomba Kanisa ambalo lingewakutanisha watu wa Mungu kutoka DRC. Ibada zao zinaongozwa na “Misale ya Kirumi kwa ajili ya Majimbo ya DRC” iliyoidhinishwa kunako tarehe 30 Aprili 1988 kama sehemu ya uinjilishaji wa tamaduni na utamadunisho wa Injili kwa watu wa Mungu nchini DRC. Utamadunisho nchini DRC ulihamasishwa kwa namna ya pekee na Mtakatifu Paulo VI kama sehemu ya utekelezaji wa Mafundisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican na hatimaye, Mtakatifu Yohane Paulo II akawatia shime kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu. Mwenyeheri Sr. Marie- Clementine Anwarite Nengapeta maana yake “utajiri si mali kitu” aliyezaliwa kunako tarehe 29 Desemba 1939 huko Wamba, nchini DRC.

Kunako mwaka 1959 akajiunga na Shirika la Watawa wa Familia Takatifu. Na kunako mwaka 1964 kutokana na chuki dhidi ya imani akauwawa kikatili tarehe 1 Desemba 1964. Huyu alikiwa ni mtawa wa shoka aliyesadaka maisha yake kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini DRC kiasi kwamba, akawa ni chemchemi ya furaha na matumaini ya maisha mapya! Wakati akiwa kufani anasema Baba Mtakatifu Francisko akawasamehe watesi na wauaji wake kwani walikuwa wanatenda yote haya bila kufahamu. Kunako mwaka 1985 akatangazwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kuwa Mwenyeheri wakati wa hija yake ya kitume nchini DRC. Kanisa limeadhimisha pia Jubilei ya Miaka 25 tangu Mwenyeheri Isidori Bakanja alipotangazwa kuwa Mwenyeheri na Mtakatifu Yohane Paulo II kunako tarehe 24 Aprili 1994. Itakumbukwa kwamba, Mwenyeheri Isidori Bakanja alizaliwa mwaka 1887 huko Bokendela nchini DRC.

Kanisa linathamini sana ushuhuda wake kama chombo cha upatanisho miongoni mwa watu wa Mataifa. Familia ya Mungu kutoka DRC kwa kinywa cha Sr. Rita Mboshu Kongo, wamemshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kusimama kidete kulinda na kutetea utu, heshima na haki msingi za wakimbizi na wahamiaji kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Wamempongeza kwa kuendelea kukazia kuhusu umuhimu wa kukuza na kudumisha dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa ili kukabiliana na changamoto za tunu msingi za maisha ya ndoa na familia; utunzaji wa mazingira nyumba ya wote sanjari na kuwajengea vijana wa kizazi kipya matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi kwa kutambua kwamba, hata wao wanachangia katika kufaniskisha leo la Mungu katika maisha yao.

Sr. Rita Mboshu Kongo amesema, katika kipindi cha Miaka 20 watu wa Mungu nchini DRC wamekumbana na vita pamoja na majanga mbali mbali ya maisha. Takwimu zinaonesha kwamba, kuna watu zaidi milioni sita wameuwawa kutokana na vita nchini DRC. Mauaji yote haya ni kielelezo cha uchu wa mali, madaraka na utajiri wa haraka haraka; mambo yanayotekelezwa na viongozi ambao wamekengeuka na kumezwa na malimwengu, kwao utu, heshima na haki msingi za binadamu si mali kitu! Ni viongozi ambao wanamezea mate raslimali na utajiri wa DRC kwa ajili ya mafao yao binafsi, jambo ambalo si sawa hata kidogo! Familia ya Mungu nchini DRC inataka amani na utulivu kama chachu ya maendeleo fungamani ya binadamu. Vita imekuwa chanzo cha nyanyaso wa utu wa binadamu kiasi kwamba, ubakaji unatumika pia kama silaha ya vita nchini DRC.

Ibada hii ya Misa Takatifu imehudhuriwa na watu wa familia ya Mungu DRC kutoka sehemu mbali mbali za Bara la Ulaya.  Kwa hakika ulikuwa ni moto wa kuotea mbali kutoka kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Wachunguzi wa mambo wanakumbukia tukio kama hili lilifanyika kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican wakati wa kuzindua maadhimisho ya Sinodi ya kwanza ya Maaskofu wa Afrika kunako mwaka 1994. Yaani hadi raha, Achana na "Batu ba Congo" kwa kutamadunisha Ibada, kiasi cha waamini kujisikia kwamba, wanaguswa hadi undani wa maisha yao!

Waamini wa DRC
01 December 2019, 16:13