Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Mwenge, MWECAU, kimeanzisha mapambano dhidi ya ukatili na unyanyasaji kwa watoto ili kulinda na kudumisha haki msingi za watoto. Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Mwenge, MWECAU, kimeanzisha mapambano dhidi ya ukatili na unyanyasaji kwa watoto ili kulinda na kudumisha haki msingi za watoto. 

Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge: Haki Msingi za Watoto dhidi ya ukatili na nyanyaso ndani ya jamii!

MWECAU wameanza kuwaandaa walimu wao wote kuwa wakufunzi wa masuala ya utetezi wa haki za watoto, lakini pia wanafunzi wote hawataruhusiwa kumaliza masoma bila kupitia mafunzo haya ya utetezi wa haki za watoto. Ambao baadaye watapaswa kwenda kufundisha jamii katika makundi mbalimbali ili elimu hii isambae maeneo yote yenye viashiria vya unyanyasaji wa watoto.

Na Athanas Singambi, Moshi na Padre Richard Mjigwa, C.PP.S. - Vatican.

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kunako mwaka 1989 lilipitisha makubaliano ya haki msingi za watoto duniani. Haki hizo ni pamoja na kutobaguliwa, haki ya kuzaliwa na kuishi, haki ya kukua, na haki ya kusikilizwa. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kubainisha: sera na mikakati itakayotumika kuwalinda, kuwatetea na kuwaendeleza watoto, ili kupunguza vifo vya watoto wadogo pamoja na kuwakinga dhidi ya nyanyaso mbali mbali wanazokabiliana nazo katika maisha, malezi na makuzi yao! Ili kufikia lengo hili kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuendelea kuwekeza zaidi katika lishe bora, maji safi na salama pamoja na uhakika wa elimu bora na wala si bora elimu pamoja na kuwaandalia mazingira bora yatakayosaidia malezi na makuzi yao endelevu na fungamani! Jumuiya ya Kimataifa iendelee kusimama kidete kulinda, kutetea na kuendeleza haki msingi za watoto; utu na heshima yao kama binadamu. Watoto wajengewe mazingira mazuri ya maisha, kwa ajili ya ustawi na maendeleo yao kiroho na kimwili.

Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake kwa viongozi wa Serikali na wanadiplomasia wakati wa hija yake ya kitume nchini Thailand alisema kwamba, Jumuiya ya Kimataifa kwa Mwaka 2019 inaadhimisha Kumbu kumbu ya Miaka 30 ya Tamko la Haki ya Mtoto Duniani, changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete kulinda, kutetea na kuendeleza haki msingi za watoto; utu na heshima yao kama binadamu. Watoto wajengewe mazingira mazuri ya maisha, kwa ajili ya ustawi na maendeleo yao kiroho, kimwili, kisaikolojia na kiakili. Matumaini ya kesho iliyo bora zaidi yanafumbatwa kwa namna ya pekee, katika huduma kwa watoto. Baba Mtakatifu anakaza kusema, leo hii jamii inawahitaji wajenzi wa ukarimu, watu wanaoweza kujisadaka kwa ajili ya kukoleza mchakato wa maendeleo fungamani katika familia ya binadamu kwa kuzama zaidi katika misingi ya haki, mshikamano, udugu wa kibinadamu na utulivu. Kila mmoja anapaswa kuchangia katika mchakato wa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Kutokana na ongezeko la vitendo vya unyanyasaji kwa watoto katika jamii, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge nchini Tanzania kimeamua kujitosa ili kusaidia kupunguza nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo. Kumekuwa na taarifa mbalimbali zinazoripotiwa katika vyombo vya habari zinazoelezea matukio mbalimbali ya unyanyasaji kwa watoto. Akizungumza wakati wa kufunga warsha ya siku tatu iliyowahusisha wahadhiri wote Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge hivi karibuni, Makamu Mkuu wa Chuo, Pd. Prof. Philbert Vumilia alisema kwamba, juhudi za kuhakikisha jamii inakuwa salama lazima zianze kwa kuwatengenezea watoto mazingira yenye uhakika wa usalama kwa malezi na makuzi yao. Padre Vumilia alisema kwamba, kwa kuanzia “MWECAU” wameamua kuanza kuwaandaa walimu wao wote kuwa wakufunzi wa masuala ya utetezi wa haki za watoto, lakini pia wafanyakazi na wanafunzi wote hawataruhusiwa kumaliza masoma bila kupitia mafunzo haya ya utetezi wa haki za watoto. Ambao baadaye watapaswa kwenda kufundisha jamii katika makundi mbalimbali ili elimu hii isambae maeneo yote yenye viashiria vya unyanyasaji wa watoto.

Kwa upande wake msimamizi wa warsha hii Padre Daktari Peter Siamoo alisema mafunzo yaliyotolewa yalilenga kuandaa wataalamu takribani 112 wa kufundisha wataalamu wengine (trainer of trainers) watakaoweza kufundisha mahali pengine watakapohitajika. Alikazia kwa kusema mafunzo yameandaliwa kwa lugha zote mbili yaani Kingereza na Kiswahili ili kuwafikia watu wengi zaidi katika nchi za Afrika Mashariki. Kwa sasa Chuo Kinajiaandaa kwa ajili ya kuandaa warsha nyingine itakayojumuisha wanafunzi zaidi ya 4,500 ili waweze kuwa mabalozi wazuri wa kutetea haki za watoto. Kwa upande wao baadhi ya washiriki walikiri wazi kwamba, mafunzo haya yamekuwa yenye manufaa na tija kubwa kwao na kwamba watayatumia mafunzo hayo kuiwezesha jamii kutambua haki za watoto na kuboresha malezi ya watoto katika jamii.  Washiriki hao wamehitimisha kwa kusema kwamba, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge bado wadau wengine wanaoweza kushirikiana na Chuo ili kuwezesha adhma hii ya kuisaidia jamii kutambua na kusimamia haki za watoto katika jamii.

MWECAU: Haki za Watoto
19 December 2019, 11:37