Tafuta

Vatican News
Nyanyaso, dhuluma na mauaji dhidi ya Wakristo nchini Burkina Faso yanatisha sana. Kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete kulinda na kutetea uhuru wa kuabudu. Nyanyaso, dhuluma na mauaji dhidi ya Wakristo nchini Burkina Faso yanatisha sana. Kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete kulinda na kutetea uhuru wa kuabudu.  (AFP or licensors)

Burkina Faso: Nyanyaso na mauaji ya Wakristo yanatisha sana!

Uhuru wa kidini unafumbatwa katika mambo yafuatayo: Umuhimu wa kujenga na kudumisha umoja na mshikamano miongoni mwa waamini wa dini mbali mbali; Pili, ni kudumisha amani na utulivu kama chachu muhimu ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Tatu, ni majadiliano ya kidini katika ukweli na uwazi, mbinu mkakati inayoweza kuleta suluhu ya migogoro mingi duniani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Madhulumu na nyanyaso za kidini dhidi ya Wakristo sehemu mbali mbali za dunia ni dhana inayotishia misingi ya haki, amani, mshikamano na mfungamano wa kimataifa. Jumuiya ya Kimataifa, haiwezi kuendelea kukaa kimya na kufumbia macho mauaji ya kinyama, mateso na nyanyaso dhidi ya Wakristo. Baba Mtakatifu Francisko anasema kuna idadi kubwa ya mashuhuda wa imani wanaoendelea kuwawa kila mwaka kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake katika Karne hii, pengine kuliko ilivyowahi kutokea kwenye Karne zilizopita. Uhuru wa kidini na uhuru wa kuabudu ni kati ya haki msingi za binadamu zinazopaswa kulindwa na kuendelezwa, kwa kuheshimu na kuthamini dhamiri ya mtu binafsi na Jamii katika ujumla wake. Hii ni haki inayojikita katika masuala ya kidini na uhuru wa kuabudu.

Uhuru wa kidini unafumbatwa katika mambo makuu matatu: Umuhimu wa kujenga na kudumisha umoja na mshikamano miongoni mwa waamini wa dini mbali mbali; Pili, ni kulinda na kudumisha amani na utulivu kama chachu muhimu ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Tatu, ni majadiliano ya kidini katika ukweli na uwazi, mbinu mkakati inayoweza kuleta suluhu ya migogoro mingi duniani! Mauaji ya kikatili yaliyofanyika nchini Burkina Faso, Jumapili tarehe 1 Desemba 2019 ni kielelezo cha kushamiri kwa biashara haramu ya silaha duniani inayoendelea kushamirisha vitendo vya kigaidi dhidi ya watu wasiokuwa na hatia. Hali hii inahatarisha sana umoja na mafungamano ya kijamii. Jumapili iliyopita Wakristo 14 katika eneo la N’Gourma, mpakani na Niger, waliuwawa kikatili wakati wakiwa wanahudhuria Ibada ya Jumapili. Katika miaka ya hivi karibuni, kumeibuka waamini wenye misimamo mikali ya kidini na kiimani, ambao wamekuwa wakiendesha mashambulizi ya kushtukiza dhidi ya Wakristo wanapokuwa kwenye Ibada mbali mbali.

Burkina Faso
02 December 2019, 16:12