Tafuta

Vatican News
Baraza la Maaskofu Katoliki Japan linampongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kuwatembelea na kuwatia shime katika mchakato wa kulinda maisha yote! Baraza la Maaskofu Katoliki Japan linampongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kuwatembelea na kuwatia shime katika mchakato wa kulinda maisha yote!  (AFP or licensors)

Baraza la Maaskofu Katoliki Japan linamshukuru Papa Francisko!

Amani na utulivu wa kimataifa vinaweza kujengeka katika msingi wa mshikamano na ushirikiano wa haki na kwa ajili ya ustawi wa familia nzima ya binadamu. Nagasaki ni mji ambao umeshuhudia maafa makubwa na uharibifu wa mazingira; kielelezo cha mashindano ya utengenezaji wa silaha za maangamizi; upotevu mkubwa wa rasilimali fedha ambayo ingeweza kutumika kuchochea ustawi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, - Vatican.

Kauli mbiu iliyochaguliwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Japan kwa ajili ya hija ya 32 ya Baba Mtakatifu Francisko nchini humo kuanzia tarehe 23 hadi 26 Novemba 2019, ilikuwa ni “Linda Maisha Yote”. Huu ni ujumbe mzito unaotikisa “sakafu ya nyoyo za watu” ili kusimama kidete kulinda tunu msingi, utu na heshima ya binadamu dhidi ya vitisho vinavyohatarisha misingi ya amani na utulivu na hasa zaidi mapambano ya silaha. Baba Mtakatifu katika ujumbe wake kwa watu wa Mungu nchini Japan alisema, kwamba, Japan inatambua fika madhara ya vita. Baba Mtakatifu alipenda kuungana na Japan ili kudhibiti nguvu ya uharibifu kutoka kwenye silaha za kinyuklia, isirejee tena na kusababisha madhara makubwa katika historia ya maisha ya binadamu. Matumizi ya silaha za kinyuklia ni kinyume kabisa cha kanuni maadili. Familia ya Mungu nchini Japan inatambua fika umuhimu wa utamaduni wa majadiliano na udugu miongoni mwa waamini wa dini mbali mbali; ili kujenga umoja na mshikamano sanjari na kulinda utu, heshima na haki msingi za binadamu, tayari kujielekeza zaidi katika mchakato wa maendeleo fungamani kwa ajili ya watu wote.

Askofu mkuu Joseph Mitsuaki Takami, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Japan, amemwandikia Baba Mtakatifu Francisko barua ya shukrani kwa kutembelea Japan, Novemba 2019. Anawashukuru wale wote waliojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuhakikisha kwamba, hija hii ya kitume inapata mafanikio makubwa. Kwa namna ya pekee kabisa anawashukuru watu wa Mungu nchini Japan walioonesha moyo wa ukarimu na upendo kwa Baba Mtakatifu. Anapenda kuchukua fursa hii kuomba msamaha kwa mapungufu yaliyoyojitokeza wakati wa hija hii. Jambo la msingi ni kwamba, kwa hakika, Baba Mtakatifu amegusa na kukonga nyoyo za watu wa Mungu nchini Japan. Amani inatishiwa sana na mashindano ya silaha; utengenezaji na biashara ya silaha pamoja na mchakato wa ulimbikizaji wa silaha duniani! Ni wajibu wa Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha amani ambalo ni jina jipya la maendeleo fungamani ya binadamu.

Baba Mtakatifu, Jumapili, tarehe 24 Novemba 2019 alizungumzia kuhusu mateso na maafa makubwa yaliyosababishwa na mashambulizi ya mabomu ya atomiki, changamoto na mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete kulinda na kudumisha misingi ya: usalama, amani na utulivu kwa kuondokana na wasi wasi pamoja na hofu inayotawala akilini na mioyoni mwa watu kiasi cha kushindwa kuaminiana na hivyo kudhohofisha mafungamano ya watu pamoja na mchakato wa majadiliano. Amani na utulivu wa kimataifa vinaweza kujengeka katika msingi wa mshikamano na ushirikiano wa haki kwa ajili ya huduma kwa kutambua kwamba, watu wanategemeana na wanapaswa kuwajibika kama wamoja kwa ajili ya ustawi wa familia nzima ya binadamu. Baba Mtakatifu anasema, Nagasaki ni mji ambao umeshuhudia maafa makubwa kwa binadamu sanjari na uharibifu wa mazingira; kielelezo cha mashindano ya utengenezaji wa silaha za maangamizi; upotevu mkubwa wa rasilimali fedha ambayo ingeweza kutumika kuchochea maendeleo fungamani ya binadamu pamoja na utunzaji bora wa mazingira.

Ili kulinda maisha, kuna haja ya kusimama kidete kuyapenda, kuyatetea na kuyalinda. Baba Mtakatifu aliguswa sana na ushuhuda wa watakatifu na wafiadini kutoka nchini Japan. Alikutana na kuzungumza na vijana wa kizazi kipya. Akawasikiliza na kujibu maswali yao msingi na kuwataka kuondokana na ukatili na nyanyaso za kimtandao, daima wakijitahidi kushuhudia huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao. Baba Mtakatifu aliwataka vijana wawe ni mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu kwa jirani zao; kwa kujenga na kudumisha mahusiano mema kwa njia ya sala na huduma kwa jirani zao. Amekipongeza Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Sophia nchini Japan kwa huduma na mchango wake kwa watu wa Mungu kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Baba Mtakatifu alikutana na kuzungumza na viongozi wa Serikali ya Japan pamoja na wanadiplomasia wanaowakilisha nchi zao hapo Japan Alitumia fursa hii kuwahimiza kujenga na kudumisha utamaduni wa watu kukutana na kujadiliana, sanjari na kuendeleza tunu msingi za maisha ya kiroho na kimaadili, daima wakiwa tayari kupokea ujumbe wa Injili, ili Japan iweze kuwa kweli ni nchi ambayo inasimikwa katika misingi ya haki, amani, maridhiano pamoja na  utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.

Papa: Japana 2019
21 December 2019, 10:03