Tafuta

Vatican News
Askofu mkuu Renatus Leonard Nkwande, tarehe 7 Desemba 2019 amevikwa Pallio Takatifu alama ya Kristo Mchungaji Mwema na Umoja na Mshikamano na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Askofu mkuu Renatus Leonard Nkwande, tarehe 7 Desemba 2019 amevikwa Pallio Takatifu alama ya Kristo Mchungaji Mwema na Umoja na Mshikamano na Khalifa wa Mtakatifu Petro.  (ANSA)

Askofu mkuu Renatus Nkwande avishwa Pallio Takatifu Mwanza!

Askofu mkuu Marek Solczyński, Balozi Vatican nchini Tanzania, Jumamosi tarehe 7 Desemba 2019 katika Ibada ya Misa Takatifu katika Madhabahu ya Bikira Maria wa Kawekamo Jimbo kuu la Mwanza amemvika Askofu mkuu Nkwande, Pallio Takatifu kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko. Pallio Takatifu ni alama ya Kristo mchungaji mwema; umoja na mshikamano na Baba Mtakatifu.

Na Padre Celestine Richard Nyanda, -Jimbo kuu la Mwanza.

Askofu mkuu Renatus Leonard Nkwande ni jembe la uhakika na ni chuma ambacho Mwenyezi Mungu kajitwalia ili: Kufundisha, Kuongoza na Kuwatakatifuza watu wa Mungu kwa: kukemea maovu, kufundisha imani thabiti na maadili sanjari na kutetea wanyonge na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Hayo yamesemwa na Askofu Severine Niwemugizi wa Jimbo Katoliki la Rulenge-Ngara wakati wa mahubiri katika adhimisho la kumvika Pallio Takatifu, Askofu mkuu Renatus Nkwande wa Jimbo kuu la Mwanza. Pallio Takatifu ni kitambaa cha sufi safi kinachovaliwa na Baba Mtakatifu pamoja na Maaskofu wakuu wa majimbo ya Kanisa Katoliki. Hii ni alama ya Kristo mchungaji mwema; Kristo Yesu aliyesadaka maisha yake kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Ni alama ya umoja na mshikamano kati ya Maaskofu wakuu pamoja na Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Baada ya mabadiliko yaliyotangazwa na Baba Mtakatifu Francisko kunako mwaka 2015, Maaskofu wakuu wapya wanavishwa Pallio Takatifu na Mabalozi wa Vatican majimboni mwao, ili kuwashirikisha watu wa Mungu kutoka katika majimbo yanayounda Jimbo kuu husika tukio hili adhimu katika maisha na utume wa Kanisa mahalia! Ni katika muktadha huu, Askofu mkuu Marek Solczyński,  Balozi Vatican nchini Tanzania, Jumamosi tarehe 7 Desemba 2019 katika Ibada ya Misa Takatifu katika Madhabahu ya Bikira Maria wa Kawekamo Jimbo kuu la Mwanza amemvika Askofu mkuu Nkwande, Pallio Takatifu kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko. Askofu Niwemugizi katika mahubiri yake amewaalika waamini kumwombea Askofu mkuu Nkwande ili adumu katika moyo huo wa ushujaa na ushupavu wa kiimani. Katika adhimisho hilo, Jimbo Kuu la Mwanza limehitimisha kilele cha Mpango Mkakati wa Mwezi Oktoba 2019 uliotengwa maalum na Mama Kanisa kwa ajili ya kuhamasisha ari na mwamko wa kimisionari sehemu mbali mbali za dunia, kwa kuongozwa na kauli mbiu “Mmebatizwa na kutumwa. Kanisa la Kristo katika utume”.

Itakumbukwa kwamba, Novemba 2019, Kanisa limeadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu Papa Benedikto XV alipochapisha Waraka wa Kitume "Maximum Illud" yaani “Kuhusu Shughuli za Kimisionari” akafungua rasmi ukurasa mpya wa maisha na utume wa Kanisa mintarafu shughuli za kimisionari, kwa kulitaka Kanisa kuanzisha mchakato wa majiundo na malezi kwa ajili ya kuyategemeza Makanisa mahalia kwa rasilimali watu, yaani mihimili ya uinjilishaji. Hiki kimekuwa ni kipindi cha kupyaisha ari na mwamko wa kimisionari. Imekuwa ni fursa muhimu kwa Kanisa kujikita zaidi katika utekelezaji wa mambo makuu manne: Mosi, waamini wamejitahidi kukutana na Kristo Yesu kwa njia ya Ekaristi Takatifu, Tafakari ya Neno la Mungu na Maisha ya Sala. Pili, ni ushuhuda wa wamisionari watakatifu, wafiadini na waungama imani, kielelezo makini cha uwepo endelevu wa Kanisa sehemu mbali mbali za dunia. Tatu, ni majiundo makini, endelevu na fungamani ya kimisionari kwa kujikita katika: Biblia, Katekesi, Tasaufi na Taalimungu. Nne, ni huduma ya upendo kama kielelezo cha Injili ya upendo inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu, kama kielelezo makini cha imani tendaji!

Huu umekuwa ni muda muafaka wa Injili kutangazwa, Sakramenti za Kanisa kuadhimishwa na Wakristo kutoa ushuhuda wa imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake pamoja na kuendelea kujikita katika Tafakari ya Neno la Mungu. Haya ni mambo yanayopaswa kuendelezwa katika sera, mikakati, maisha na utume kwa Makanisa mahalia. Ni katika muktadha huu madekano wa dekania saba zinazounda Jimbo kuu la Mwanza wamekabidhiwa Misalaba na Biblia, ishara ya kutangaza fumbo la imani, mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu;  kuliishi na kulitangaza Neno la Mungu. Waamini Jimbo kuu la Mwanza wameadhimisha pia kilele kijimbo cha Jubilei ya miaka 50 ya utume wa Halmashauri Walei Tanzania. Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 ya Utume wa Walei nchini Tanzania, yaliongozwa na kauli mbiu “Kuyatakatifuza Malimwengu”. Itakumbukwa kwamba, utume wa waamini walei ndani ya Kanisa ni matunda ya maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, unaowataka waamini walei kutambua kwamba, wanashiriki kikamilifu huduma za Kristo za kikuhani, kinabii na kifalme na kwamba, wanapaswa kutimiza wajibu wao kadiri ya hali yao katika Kanisa, na Ulimwengu katika ujumla wake. Waamini walei wanamahasishwa kushiriki kwa dhati kabisa, maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa na hasa Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa.

Jambo la msingi kwa walei ni kujibidiisha kushikamana na viongozi wao wa Kanisa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu. Walei wajitahidi kutumia kikamilifu karama na matunda ya Roho Mtakatifu waliyokirimiwa katika maisha! Karama na mapaji haya yawaongoze katika utakatifu na ushuhuda wa kazi njema zinazofumbatwa katika huduma, ili kujenga na kudumisha Ufalme wa Mungu na kwamba, kila mwamini anayo nafasi ya pekee katika ujenzi wa Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Kupitia Mwenyekiti wao, walei 12 wamekabidhiwa na Askofu mkuu Nkwande, Hati za Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, Katekisimu ya Kanisa Katoliki, Maazimio, Sera na Matamko ya Sinodi ya Jimbo Kuu la Mwanza, Mwongozo wa Kichungaji, pamoja na Mwongozo wa Jumuiya ndogo ndogo Kijimbo, vitendea kazi vyao katika kuyatakatifuza malimwengu. Wamekabidhiwa pia mishumaa inayowaka, ishara ya kuwa mwanga kwa mataifa, ili watu wapate kuona na kuchota mfano bora kupitia maisha yao. Zaidi sana katika adhimisho hilo, waamini wamezindua maadhimisho ya Jubilei ya miaka 25 ya Upadrisho wa Askofu mkuu Nkwande, ambapo amewasha mishumaa 25 ishara ya utumishi uliotukuka katika shamba la Bwana.

Hata hivyo, Askofu mkuu Nkwande amesema kuwa, anatambua kwamba naye ni mdhambi na anahitaji kuendelea kuomba huruma ya Mungu ili azidi kuuchuchumilia utakatifu. Baada ya kuwashwa mishumaa hiyo 25, wamesali sala maalumu ya kuombea utumishi wake, sala ambayo itasaliwa mwaka mzima katika maadhimisho na makusanyiko mbali mbali kijimbo, kiparokia, katika jumuiya na taaisisi za Jimbo kuu la Mwanza. Wakati huo huo, Askofu Mkuu Marek Balozi wa Vatican nchini Tanzania, mbali ya kumvika Pallio Takatifu Askofu mkuu Nkwande, alipata nafasi tarehe 6 Desemba 2019 kutembelea Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agostino Tanzania (St. Augustine University of Tanzania (SAUT) ambapo amewahimiza wanafunzi kuwa na bidii katika masomo yao na kutumia elimu hiyo kujikomboa wenyewe na kulikomboa taifa la Tanzania, wakisaidiana bega kwa bega na juhudi za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu.

Askofu Mkuu Nkwande: Pallio Takatifu
09 December 2019, 16:12