Baba Mtakatifu alitembelea makatakombe ya Priscilla tarehe 2 Novemba 2019. Ndani humo kuna baadhi ya michoro ya wakristo inayoonesha ishara mbalimbali za Agano la Kale na Jipya Baba Mtakatifu alitembelea makatakombe ya Priscilla tarehe 2 Novemba 2019. Ndani humo kuna baadhi ya michoro ya wakristo inayoonesha ishara mbalimbali za Agano la Kale na Jipya 

Imani thabiti ya wakristo wa kwanza katika michoro ndani ya makatakombe!

Katika makatakombe ya Kirumi picha ya zamani sana ya Bikira Maria imehifadhiwa,kwenye mchoro.Na michoro mingine mingi inaonesha uthabiti wa imani kubwa ya wakristo wa kwanza.Katika makala hii utaona ishara tofauti zilizo tumika kwenye michoro kama vile ya Agano la Kale na Agano Jipya.Upo uthibitisho wa mababa wa Kanisa kutembelea makatakombe.

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican

Kila tarehe 2 Novemba ya kila mwaka ni siku ya kumbu kumbu ya marehemu wote, ambapo Mama Kanisa aliweka mwezi wa Novemba, kwa ajili ya kuwakumbuka kwa karibu watu ambao wametutangulia katika raha ya milele. Katika siku hiyo kwa ajili ya kuwaombea marehemu wote, Baba Mtakatifu Francisko Jumamosi  jioni alikwenda kuadhimisha Misa Takatifu katika moja ya Makatakombe yaliyoko Roma (Catacombs of Rome). Katika sehemu yetu ya kwanza ya historia  ya Makatakombe tuliona asili ya makatakombe, tabia za makatakombe, makatakombe nchini Italia, sanaa zilizopo kwenye makatakombe, hasa katika michoro inayowakilisha Agano la Kale na Agano Jipya. Katika makala hii, tuendelee kuona ishara mbalimbali na ibada maalum zinazowakilishwa ndani ya makatakombe hayo kwa ujumla.

Makatakombe na Mama wa Mungu

Katika makatakombe ya Kirumi picha ya zamani sana ya  Bikira Maria  imehifadhiwa, inayowakilishwa katika mchoro kwenye makaburi ya Priscilla njia ya  Salaria, Roma. Mchoro huo unawakilisha katika nusu ya kwanza ya karne ya II ikimwonesha Bikira Maria na mtoto  wake katika magoti  na mbele ya nabii (labda Balaamu, au labda Isaya haijulikani vizuri) huku akiashiria nyota kwa maana ya kuelezea unabii wa masiha. Aidha katika Makatakombe hayo sehemu nyingine zinawakilishwa na matukio ya Mama Maria, kama vile ibada ya mamajusi kuabudu na  picha ya kuzaliwa, japokuwa  inaaminika kwamba, kabla ya Mtaguso wa Efeso, uwasilishaji huu wa michoro ulikuwa bado una maana ya elimu ya Kristo (Christology) na siyo elimu ya Maria mama (Mariology).

Elimu ya Mama Maria di baada ya Mtaguso wa Trento

Je ni kwa sababu gani? Tunajua wazi ya kwamba elimu ya Maria ni tawi la Taalimungu ya kikristo ambayo inafundisha juu ya Maria Mama wa Mungu. Kwa namna ya pekee  katika umbu la Kanisa Katoliki, elimu ya Maria ina nafasi kubwa sana kwa sababu hata katika madhehebu mengine, nafasi ya Mama Maria kwa namna moja au nyingine inatambulika. Hii kwa mfano hata katika dini ya Kiislam, Mama Maria anajulikana na kuheshimiwa sana inatosha kufikiria Sura ya tatu katika  Quran Tukufu, inaelezea Miriam! Katika mantiki ya kikatoliki ibada ya Mama Maria imezidi kuendelezwa sana kadiri ya miaka ilivyoendelea mbele hadi kufikia ngazi kuu ya utafiti na mafunzo kuhusu Mama Maria, Nyaraka  mbali mbali za kipapa kuhusiana na Mama Maria na ibada kwa ajili ya heshima yake. Kwa maana hiyo elimu juu ya  Mama Maria ni baada ya Mtaguso wa Trento, ndipo ilianza kujikita zaidi Elimu ya Maria hasa ikiwa katika mantiki kuu ya kutetea umama wake, kulinda na kuthibitisha ukweli wa Mama wa Mkombozi. Lakini basi ndugu wasomaji na wasikilizaji, bado tunaendelea kuona michoro muhimu inayowakilishwa katika makatakombe ya wakristo.

Mchungaji mwema katika makatakombe

Mojawapo ya picha zilizowakilishwa zaidi katika sanaa ya makatakombe ni ile ya “mchungaji mwema” ingawa inajionesha katika muundo kutoka tamaduni ya kipagani, lakini ni mara moja ilianza kuchukua maana halisi ya Kikristo, ikiongozwa na mfano wa kondoo aliyepotea. Na kwa maana ya Kristo aliwakilishwa kama mchungaji, mnyenyekevu akiwa na  kondoo juu ya mabega yake na wakati anachunga kundi ndogo. Kadhalika, wakati mwingine alichorwa wakioneshwa na  kondoo wawili tu waliowekwa kandoni mwake.

Wafiadini katika makatakombe

Jambo jingine muhimu katika makatakombe ukiyatembelea utakuta historia ya wafiadini kwa maana katika makatakombe walikuwa wakizikwa hata wafiadini waliouawa wakati wa mateso na umwagaji damu  wa wakristo wakati wa utawala Decius, Valerian na Diocletian. Karibu na kaburi la wafia dini ilikuwa  imezuka imani kubwa na ibada ya  wahujaji wengi ambao waliweza kuacha mchoro fulani au kuandikia sala zao kwenye kuta za makaburi haya ya kipekee. Na wakati huo huo wakristo wengi walipenda  kuzika marehemu wao  kwa karibu sana na makaburi hayo ya wafiadini  kwa sababu iliaminika kuwa hata mbinguni ukaribu huo wa ibada ya ajabu itakuwapo! Na ndiyo maana ukitembelea makatakombe, ukifikia mahali ambapo alikuwa amezikwa mfiadini, kuna mlundikano sana wa makaburi.

Makatakombe na Mababa wa Kanisa

Kuhusiana na suala hili la makatakombe kuna hata uthibitisho wa mababa wa Kanisa kwenye maandiko yao kufuatia na uzoefu walio ufanya wakati wa maisha yao. Kwa mfano, kati  ya mwisho wa karne ya IV na mwanzoni mwa karne ya V,  Mababa wa Kanisa walielezea juu ya Makatakombe. Wa kwanza ni Mtakatifu Jerome ambaye anasimulia historia hii na uzoefu wake binafsi kwamba, alipokuwa mwanafunzi alikuwa anakwenda kila Jumapili kutembelea makaburi ya mitume na wafiadini akiwa pamoja na wanafunzi wenzake ambapo walikuwa wakiingia humo  kwenye njia ndefu na nyembamba zilizochimbwa katika tumbo la dunia… anaandika. Aidha anasema “Taa zisizo za kawaida (kwa maana hiyo ni vibatali vya kutumia mafuta katika enzi hizo) ziliwaka na kupunguza  angalau kidogo lile giza nene... Waliendelea polepole, hatua moja baada ya nyingine na wakati  mwengine njia nyingi zilikuwa zimenikwa gizani kabisa! Anathibitisha katika maandiko yake Mtakatifu Jerome. Vile vile hata Mshairi wa Iberian aitwaye Prudentius pia anakumbuka kwamba, mwanzoni mwa karne ya V, mahujaji wengi walitoka nje ya mji wa Roma, pia kutoka katika mikoa  ya jirani ili kutoa heshima na kuomba katika kaburi la mfiadini Ippolito, ambaye alizikwa kwenye Makatakombe yaliyopo katika  njia ya Tiburtina, Roma.

Kuanzishwa kwa ukarabati wa Makatakombe kwa mijibu wa Papa

Katika nusu ya pili ya karne ya IV, Papa Damas alijikita kutafuta makaburi ya wafiadini  waliokuwa wamezikwa katika makatakombe kadhaa  ya  Roma. Mara tu baada ya kupata makaburi hayo walianza kuyakarabati kufanya kila njia ya kuweza kuandika zile sifa zao  nzuri kwa heshima ya mabingwa wa kwanza wa imani. Katika karne ya VI hata  mapapa kama vile Vigilio, Yohane  III walikarabati makatakombe mengine baada ya uvamizi kwa sababu ya vita vya Ugiriki na Gothic. Hata baadaye, kati ya karne ya VIII na IX, Papa Adrian I na Leo III waliweza kurudisha madhabahu ya wafiadini katika makatakombe ya Roma. Baada ya kutengwa kwa muda mrefu sana, katika karne ya XVI, tendo la  kupatikana kwa mara nyingine tena maeneo haya chini ya ardhi, iliwezesha kutoa uthibitisho muhimu wa  ushuhuda wa imani ya kweli ya Wakristo wa kwanza na ambao walitumiwa na harakati za mabadiliko na  matengenezo ya makatakombe hayo. Na hatimaye katika karne ya XIX Papa Pius IX alianzisha Tume ya wataalam wa maarifa ya mambo ya kale na matakatifu ili kuweza  kuhifadhi vyema na kutafiti  maeneo ya Ukristo wa zamani.

Usikose kutembelea makatakombe upatapo fursa ya kuja Roma

Hadi leo hii, makatakombe yana urithi mkubwa wa historia na imani kuu ya wakristo wa kwanza, na ambayo ni vigumu kuelezea yote. Kila yeyote anayepata /atakayepata fursa ya kufika hija mjini Roma hasikose kabisa  kutembelea makatakombe haya, na ili kuchota ukweli wa imani na misingi mikuu ya ukristo. Ukristo ni kioo cha Kanisa, na Ukristo ni historia hai ambayo ina mwanzilishi wake na anayedumu Milele. Ninaaandika haya kwa maana nimejionea kwa macho yangu katika makatakombe haya, ambayo ni uthibitisho hai wa imani ya wakristo wa kwanza na ambao wameturithisha na itaendelea kizazi hadi kizazi.

MAKATAKOMBE II
09 November 2019, 10:55