Tafuta

Vatican News
Tamko la Viongozi wa Kidini baada ya Mkutano wa Kumi huko Lindau, Ujerumani 2019. Tamko la Viongozi wa Kidini baada ya Mkutano wa Kumi huko Lindau, Ujerumani 2019. 

Tamko la Viongozi wa Kidini: Mchakato wa Amani Duniani 2019

Leo hii dunia imekuwa ni uwanja wa fujo, vurugu na ghasia. Watu wanateseka kutokana na misimamo mikali ya kidini na kiimani. Matamanio ya wengi ni kiu ya amani na matumaini; kwa kusimama kidete: kulinda, utu wa binadamu, kutafuta na kudumisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; kwa kuoneshana huruma na upendo pamoja na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mkutano wa Dini kwa Ajili ya Amani Duniani, “Religions for Peace” ambao kwa mwaka 2019 umeingia katika awamu yake ya kumi, ni tukio la maisha ya kiroho linalowaunganisha viongozi wa kidini na waamini wenye mapenzi mema zaidi ya 900 kutoka katika nchi 125 duniani. Mkutano huu umezinduliwa hapo tarehe 20 Agosti na kukamilika tarehe 23 Agosti 2019 huko mjini Lindau nchini Ujerumani. Ni mkutano ambao umehudhuriwa pia na viongozi wakuu wa serikali, mashirika ya kitaifa na kimataifa pamoja na makundi mbali mbali ya kiraia yanayojipambanua kwa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha: utu, heshima na haki msingi za binadamu; ustawi, maendeleo na mafao ya wengi sehemu mbali mbali za dunia! Ni watu wanaoguswa kwa namna ya pekee kabisa na tabia ya: kuwajali wengine, kuwahurumia na kuwapenda, ili kweli dini ziweze kuwa ni vyombo vya huduma ya haki, amani na upatanisho. Mkutano wa Dini kwa Ajili ya Amani Duniani kwa mwaka 2019 katika tamko lake mara tu baada ya mkutano wake, wajumbe wanasikitika kusema kwamba, leo hii dunia imekuwa ni uwanja wa fujo, vurugu na ghasia.

Watu wanateseka kutokana na misimamo mikali ya kidini na kiimani, kinyume kabisa cha matamanio ya wengi, ambacho ni kiu na kilio cha amani na matumaini; kwa kuwajibikiana, kwa kusimama kidete: kutafuta, kulinda na kudumisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; kwa kuoneshana huruma na upendo pamoja na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Wajumbe wanasema kwamba, mambo yote haya yanategemeana na kukamilishana katika mtandao wa maisha ya binadamu. Leo hii familia ya binadamu inakabiliwa kwa kiasi kikubwa na madhara ya vita ambacho kimekuwa ni chanzo kikuu cha majanga yanayomsibu mwanadamu katika ulimwengu mamboleo. Kuna mamilioni ya watu ambao wamepoteza maisha na mali zao; kuna watu wanaoendelea kutumbukizwa katika baa la umaskini na magonjwa. Zaidi ya watu milioni 70 wamegeuka kuwa ni wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum hata katika nchi zao wenyewe.

Licha ya matatizo na changamoto zote hizi mintarafu madhara ya vita duniani, lakini bado kuna nchi ambazo zinaendelea kushindana kutengeneza, kujaribu na kulimbikiza silaha za kinyklia, bila kusahau silaha za kisasa zinazotumia “inteligensia” ya hali ya juu kabisa. Matokeo ya majaribio ya silaha duniani ni pamoja na ongezeko la kiwango cha joto kinachotishia usalama wa maisha ya viumbe hai. Misitu inaendelea kuteketea kwa moto na kuna uchafuzi mkubwa wa mazingira na maji ya bahari; mambo yanayohatarisha mtandao wa maisha ya binadamu. Wajumbe wanasikitika kuona kwamba, Umoja wa Mataifa hauna tena nguvu ya kimaadili na kisheria kuweza kusimamia kwa ukamilifu: haki msingi za binadamu, utu na heshima yake mintarafu: Tamko la Haki Msingi za Binadamu, Itifaki, Sheria, Kanuni na Taratibu mbali mbali zilizowekwa na Jumuiya ya Kimataifa katika medani mbali mbali za maisha. Sheria ya biashara na viwanda imetupwa “kapuni”, na kinachotawala kwa wakati huu ni “mwenye nguvu mpishe, vinginevyo utakiona cha mtema kuni”.

Masuala ya uhuru, haki, amani na usawa si tena vipaumbele vya familia ya Mungu Kimataifa. Leo hii kuna dhana ya utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya watu wengine na matokeo yake ni ubinafsi na uchoyo, kiasi kwamba, rasilimali, amana na utajiri wa dunia hii, unahodhiwa na watu wachache sana katika jamii, wakati kuna mamilioni ya watu wanaoteseka na kutopea katika umaskini, ujinga na maradhi sehemu mbali mbali za dunia. Wajumbe wanasema, siasa imegeuka kuwa ni “kichaka cha uchu wa mali na madaraka na wala sio tena wito unaofumbatwa katika huduma makini kwa wananchi.” Maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano ya jamii, yameibua changamoto changamani kuhusu ukweli wa mambo kutokana na kusambaa kwa kasi ya ajabu kwa habari za kughushi ambazo mara nyingi zinafumbatwa katika masilahi ya uchumi na biashara pamoja na kutaka kuwachafulia watu wengine sifa, utu na heshima yao kwa masilahi ya kisiasa!

Siasa imegeuka kuwa mchezo mchafu kwa dhana kwamba, “Niguse, kinuke”. Umefika wakati wa kutafuta, kusimamia na kulinda ukweli kama ulivyo! Habari za kughushi, “fake news” zina madhara makubwa katika mchakato mzima wa utu, heshima na haki msingi za binadamu. Wajumbe katika tamko hili wanakazia umuhimu wa kusimama kidete: kulinda, kutetea na kudumisha mazingira nyumba ya wote, kwa kutambua kwamba, mazingira ni kazi ya uumbaji ambao Mwenyezi Mungu amemdhaminisha mwanadamu na kamwe mwanadamu si mmiliki wa kazi ya uumbaji, kiasi cha kuitumia kama anavyotaka! Mwanadamu amejaliwa akili na utashi wa kuweza kuamua mema na mabaya katika maisha yake. Binadamu wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, wanahimizwa kupendana, kusaidiana na kuheshimiana kama ndugu. Katika Jamii ya binadamu kuna tofauti msingi kadiri ya mpango wa Mungu kwa mwanadamu. Tofauti hizi msingi zinategemeana na kukamilishana kadiri ya mpango wa Mungu.

Wajumbe wanatambua na kukiri umuhimu wa uhuru katika maisha ya binadamu, lakini wanakaza kusema kwamba, uhuru una mipaka yake na uwawajibisha binadamu katika kufikiri na kutenda, ili waweze kutenda kwa busara zaidi. Uhuru ni jambo takatifu sana katika maisha ya mwanadamu, lakini pale uhuru unapotumika vibaya, mambo yanakwenda mrama! Matokeo yake ni unafsia na utupu wa mawazo katika maisha ya watu. Katika muktadha huu, utu, heshima na haki msingi za binadamu zinapokwa na wajanja wachache kwa ajili ya mafao yao binafsi. Wajumbe wanawahimiza watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia, kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha: utu, heshima na haki msingi za binadamu. Watu wawe ni vyombo na mashuhuda wa: huruma, rehema na mapendo, ili kujenga umoja na mshikamano. Iwe ni fursa ya kuondokana na ujinga, ubinafsi na uchoyo wa makundi, ili kujenga Jumuiya inayosimikwa katika ukweli na haki.

Rasilimali, utajiri na amana za dunia ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wote. Watu wana haki ya kupata ardhi kwa ajili ya maendeleo yao, kuvuta hewa safi ili kudumisha afya na maisha bora zaidi na kwamba, maji safi na salama ni sehemu ya haki msingi za binadamu. Hii ni changamoto kwa familia ya Mungu kuhakikisha kwamba, inajenga jamii inayowajibikiana na kusimamia haki. Lengo ni kuzuia vita, kinzani na mipasuko ya kidini na kijamii inayoweza kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao sanjari na kutunza kazi ya uumbaji. Wajumbe wa Mkutano wa Dini kwa Ajili ya Amani Duniani wanasema, wanataka kujizatiti katika kutoa elimu ya amani inayomwilishwa katika maisha ya watu, kuanzia kwa watoto wadogo, kwa kukazia: ukweli, haki, upendo na uhuru unaowajibisha. Wajumbe wanataka kuona vita huko: Myanmar, Sudan ya Kusini, DRC, Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati, Mashariki ya Kati na Korea ya Kaskazini vinakoma na amani inatawala tena.

Wajumbe wanaunga mkono Mkataba wa Kimataifa wa Kuzuia: Utengenezaji, Uenezaji na Matumizi ya Silaha za Kinyuklia Duniani ili, hatimaye, kuuwezesha ulimwengu kuwa huru dhidi ya silaha za maangamizi ya halaiki za kinyuklia. Katika mlolongo huu zimo pia silaha za: kemikali, nyuklia, kibaiyolojia na zile zinazoibukia na kutamba kwa wakati huu. Wajumbe wataendelea kuwa mstari wa mbele katika kuragibisha mkakati wa amani unaofumbatwa katika msamaha na upatanisho. Watasimama kidete kuwalinda na kuwatetea: wanawake, watoto na wagonjwa dhidi ya utamaduni wa kifo. Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kupambana na vitendo vya rushwa na ufisadi wa mali ya umma; kwa kukuza na kudumisha utawala bora unaozingatia : katiba, sheria na kanuni za nchi husika. Uhuru wa kuabudu na kidini ni nguzo ya haki msingi za binadamu na ni sehemu ya vinasaba vya maisha ya binadamu. Uhuru wa kuabudu na kidini unaweza kusaidia kukuza na kudumisha umoja, mshikamano na udugu wa kibinadamu.

Hii ni chachu ya haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa na kwamba, ukweli na uwazi ni kanuni msingi katika majadiliano ya kidini na kiekumene. Kumbe, hapa kuna haja ya kusimama kidete, kulinda, kutetea na kudumisha uhuru wa kuabudu na uhuru wa kidini sehemu mbali mbali za dunia. Wajumbe wanasema, Malengo ya Maendeleo Endelevu na Fungamani ya Binadamu kufikia mwaka 2030 ni mchakato wa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inajizatiti katika kutokomeza umaskini, baa la njaa na magonjwa duniani. Watu wanapaswa kupatiwa elimu bora, kwa kuhakikisha usawa wa kijinsia pamoja na uwezeshaji wa wanawake na wasichana wote. Jumuiya ya Kimataifa inataka kuhakikisha kwamba, kunakuwepo na upatikanaji wa maji safi na salama; nishati mbadala kwa gharama nafuu pamoja na uwepo wa mipango bora ya miji na makazi ya watu, ili kudumisha usalama na upatikanaji wa maendeleo fungamani ya binadamu.

Jumuiya ya Kimataifa haina budi kujifunga kibwebwe kulinda mazingira pamoja na kudumisha amani duniani kwa kujikita katika teknolojia rafiki kwa maendeleo ya binadamu. Wajumbe wanaendelea kufafanua kwamba, watajitahidi kuhakikisha kwamba, wanawahamasisha waamini wao kuendeleza elimu bora na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote pamoja na Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inashikamana kwa dhati ili kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi kwa kutekeleza kwa vitendo makubaliano ya Mkutano wa 21 wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi, Cop21 uliofanyika mjini Paris, nchini Ufaransa, kuanzia tarehe 30 Novemba hadi 12 Desemba 2015. Jumuiya ya Kimataifa ilipitisha mkataba mpya wa Paris ambao umeweka historia mpya kwa nchi 195 kukubali kushirikiana katika kushughulikia athari na changamoto za mabadiliko ya tabianchi kwa kupitisha mkataba mpya wa kisheria unaozijumuisha nchi zote katika kupunguza gesi joto duniani.

Makubaliano haya yanatoa taswira, mwelekeo, na malengo ambayo nchi zote duniani zitashiriki katika kupunguza gesi joto ili kufikia lengo la dunia la kutokuongezeka kwa wastani wa joto la dunia kwa zaidi ya nyuzi 20C au 1.50C. Hatua hii ni muhimu katika kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi ambazo zimeendelea kuathiri nchi changa duniani hasa katika sekta muhimu zinazochangia ukuaji wa uchumi, ustawi na maendeleo ya wengi kama vile: kilimo, mifugo, uvuvi na utalii. Kimsingi Mkutano wa Dini kwa Ajili ya Amani Duniani kwa mwaka 2019 umekazia umuhimu wa kumwilisha tunu msingi katika maisha ya watu, waamini kwa kuhakikisha kwamba, wanazifahamu vyema dini zao, ili kuishi kadiri ya maongozi ya Mwenyezi Mungu. Jamii iendeleze mchakato wa kuelimisha watu kuwa na mwelekeo chanya kuhusu amani duniani, ili kuondokana na vita, kinzani na misigano mbali mbali inayoweza kuhatarisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Huu ni wakati wa kujenga na kudumisha fadhila ya msamaha na upatanisho; kwa kuwahurumia na kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji sehemu mbali mbali za dunia. Dini ziendelee kuwekeza katika utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu na Fungamani ya Binadamu kufikia mwaka 2030 pamoja na kusimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha mazingira nyumba ya wote pamoja na kushikamana katika utekelezaji wa Mkataba wa Kimataifa wa Kuzuia: Utengenezaji, Uenezaji na Matumizi ya Silaha za Kinyuklia Duniani.

Tamko la Dini: Amani
12 November 2019, 16:18