-Siku ya III ya Maskini Duniani 2019: Sala ya Wafungwa kwa Baba Mtakatifu Francisko -Siku ya III ya Maskini Duniani 2019: Sala ya Wafungwa kwa Baba Mtakatifu Francisko 

Siku ya Maskini Duniani 2019: Sala ya Wafungwa kwa Papa Francisko

Wafungwa watasali kwa ajili ya kumkumbuka na kumwombea Papa Francisko katika maisha na utume wake. Hii ni Siku ya Sala kwa Maskini Magerezani kama kielelezo cha umoja na mshikamano na Khalifa wa Mtakifu Petro kwa njia ya sala. Papa daima amekuwa mstari wa mbele kuwasihi waamini kumkumbuka na kumsindikiza katika maisha na utume wake kwa njia ya sala na sadaka zao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Siku ya III ya Maskini Duniani tarehe 17 Novemba, 2019 yanaongozwa na kauli mbiu "Matumaini ya wanyonge hayatapotea milele” itakuwa pia ni siku ya umoja na mshikamano na wafungwa wanaoendelea kutumikia adhabu zao magerezani sehemu mbali mbali za dunia, lakini kwa namna ya wafungwa walioko nchini Italia. Wafungwa watasali kwa ajili ya kumkumbuka na kumwombea Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake. Hii ni Siku ya Sala Ya Maskini Magerezani kama kielelezo cha umoja na mshikamano na Khalifa wa Mtakifu Petro kwa njia ya sala. Baba Mtakatifu daima amekuwa mstari wa mbele kuwasihi waamini kumkumbuka na kumsindikiza katika maisha na utume wake kwa njia ya sala na sadaka zao. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu pia anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuwa kweli ni mashuhuda wa Injili ya huduma ya upendo na mshikamano na maskini, kwa kusimama kidete kupambana na vyanzo vya umaskini wa hali na kipato; kwa kukuza na kudumisha haki jamii, amani na maridhiano kati ya watu.

Ukosefu wa haki msingi ni chanzo kikuu cha umaskini duniani. Baba Mtakatifu anawakumbusha waamini kwamba, ndani ya magereza wamo pia maskini na watu wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; watu ambao hawana tena sauti, lakini wanahitaji watu wa kuwasikiliza na kujibu kilio chao cha ndani kabisa katika maisha. Nia ya sala kutoka kwa wafungwa wanaotumikia adhabu zao kwenye magereza nchini Italia, hivi karibuni imewasilishwa kwa Baba Mtakatifu Francisko alipokutana na kuzungumza na wahudumu wa maisha ya kiroho magerezani kutoka sehemu mbali mbali za dunia, ili kuwajengea uwezo wa kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini kwa wafungwa na familia zao. Sala ya wafungwa kutoka magereza ya Italia ni alama ya sala ya watu wa Mungu waliokuwa wanamwombea Mtakatifu Petro wakati alipokuwa amefungwa gerezani na hatimaye, akafunguliwa na kuwekwa huru. Hata leo hii, Baba Mtakatifu Francisko anakabiliwa na changamoto nyingi hasa kutokana na vipaumbele katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, yaani: Maskini, Utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote; haki na amani duniani.

Wafungwa hawa maskini, wanataka kusali ili Mwenyezi Mungu aweze kumlinda na kumtia nguvu Baba Mtakatifu Francisko, ili aweze kusonga mbele kwa imani, matumaini na mapendo ya dhati kabisa. Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni alisema, taswira inayotolewa na magereza sehemu mbali mbali za dunia inaonesha ukweli wa jamii ambamo uchoyo, ubinafsi na utandawazi wa kutoguswa na mahangaiko ya jirani vinatawala. Kuna maamuzi ambayo yamefanywa kisheria lakini yanakiuka utu, heshima na haki msingi za binadamu; kwa kujidai kukuza na kutaka kudumisha ulinzi na usalama wa raia na mali zao. Matokeo yake ni watu kutengwa na kutupwa magerezani kama suluhu ya matatizo mbali mbali yanayoisonga jamii. Lakini ikumbukwe kwamba, kuna kiasi kikubwa cha rasilimali na utajiri wa nchi unaotumika kwa ajili ya kuwahudumia wafungwa magerezani, ikilinganishwa na kiasi cha fedha zinazotengwa kwa ajili ya kuchochea kasi ya maendeleo fungamani ya binadamu, ambayo yangewezesha idadi kubwa ya wafungwa kupata kazi na kipato halali badala ya kujiingiza kwenye vitendo vya uvunjaji wa sheria.

Wafungwa waonjeshwe matumaini na kupewa tena fursa ya kufanya kazi, ili kujipatia mahitaji yao msingi. Pale ambapo wafungwa baada ya kumaliza adhabu yao wanashindwa kutambuliwa utu na heshima yao, wanajikuta wakiwa kwenye majaribu makubwa kati ya kutafuta fursa za kazi, kutenda uhalifu pamoja na kujenga mazingira yasiokuwa salama. Baba Mtakatifu anaitaka Jumuiya ya waamini kuwaonjesha wafungwa huruma na mapendo, dhamana na utume unaopaswa kutekelezwa na Makanisa mahalia. Kila mwamini awe ni shuhuda na chombo cha huruma ya Mungu kwa wafungwa, ili kuiwezesha jamii kukita mizizi yake katika misingi ya haki na amani. Matendo ya huruma: kiroho na kimwili ni nyenzo thabiti katika mchakato wa huduma kwa wafungwa magerezani.

Sala ya Wafungwa

 

12 November 2019, 15:35