Shirikisho la Vyama Vya Wanawake Wakatoliki Duniani, WUCWO linaungana na wanawake wote duniani kupinga nyanyaso na dhuluma dhidi ya wanawake na wasichana! Shirikisho la Vyama Vya Wanawake Wakatoliki Duniani, WUCWO linaungana na wanawake wote duniani kupinga nyanyaso na dhuluma dhidi ya wanawake na wasichana! 

Shirikisho la Vyama vya Wanawake Wakatoliki Duniani: Mapambano dhidi ya nyanyaso za kijinsia

Takwimu zinaonesha kwamba, sehemu kubwa ya nyanyaso za kijinsia inatendeka ndani ya familia. Kuna wasichana zaidi ya milioni 750 ambao wametumbukizwa kwenye ndoa za utotoni, wanawake na wasichana milioni 18, 200 kutoka sehemu mbali mbali za dunia wamekeketwa. Asilimia 70% ya wahanga wa mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo ni wanawake, wasichana na watoto.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Shirikisho la Vyama vya Wanawake Wakatoliki Duniani, WUCWO, UMOFC, katika mkutano wake mkuu uliofanyika mjini Dakar, Senegal kuanzia tarehe 15-22 Oktoba 2018, uliazimia kutekeleza mambo makuu manne katika kipindi cha mwaka 2018 hadi mwaka 2022. Utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, kadiri ya mafundisho ya Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kitume: “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”. Wanawake Wakatoliki wanahamasishwa kujali na kuzisaidia familia zinazoishi katika mazingira na hatarishi, kwa kulinda na kudumisha utu na heshima yao kama binadamu! Wanawake Wakatoliki wanahimizwa kujifunga kibwebwe ili kutokomeza ubaguzi, nyanyaso na ukatili wanaofanyiwa wanawake majumbani kwa kuwa na maandalizi bora kwa wanandoa watarajiwa, ili kukuza na kushirikishana upendo wa dhati, ili kuwaimarisha wanandoa na hatimaye, waweze kutakatifuzana.

Wanawake Wakatoliki wanahimizwa kujielimisha zaidi ili hatimaye, waweze kutikia wito wa utakatifu wa maisha kwa kuendelea kuyatakatifuza mazingira kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto! Jumuiya ya Kimataifa, tarehe 25 Novemba 2019 imeadhimisha Siku ya Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Wasichana Duniani. Umoja wa Mataifa unakiri kwamba, unyanyasaji wa kijinsia na masuala ya rushwa ya ngono maeneo ya kazi dhidi ya wanawake na wasichana ni matokeo ya kukomaa kwa mfumo dume unaopelekea ukosefu wa usawa wa kijinsia na hivyo kuchochea kushamiri kwa tabia chafu ya ubakaji inayodhalilisha utu, heshima na haki msingi za wanawake na wasichana. Kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete kupinga tabia ya unyanyapaa, dhana na tamaduni potofu kuhusu wanawake, pamoja na kuhakikisha kwamba, nyanyaso na dhuluma dhidi ya wanawake zinatolewa taarifa ili wahusika waweze kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria, ili haki iweze kushika mkondo wake.

Bi María Lía Zervino, Servidora, Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wanawake Wakatoliki Duniani, WUCWO, UMOFC, katika ujumbe wake kwenye maadhimisho haya, amewataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuunganisha juhudi zao dhidi ya nyanyaso na dhuluma kwa wanawake na wasichana na kwamba, huu ni muda wa kufanya mageuzi. Takwimu zinaonesha kwamba, sehemu kubwa ya nyanyaso za kijinsia inatendeka ndani ya familia. Kuna wasichana zaidi ya milioni 750 ambao wametumbukizwa kwenye ndoa za utotoni, wanawake na wasichana milioni 18, 200 kutoka sehemu mbali mbali za dunia wamekeketwa na hivyo kuhatarisha usalama wa maisha yao. Hizi ni mila ambazo zimepitwa na wakati kwani zinakwenda kinyume cha utu na heshima ya wanawake. Takwimu zinaonesha kwamba, asilimia 70% ya wahanga wa mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo ni wanawake, wasichana na watoto.

Bi María Lía Zervino, Servidora, anasema huu ni wakati wa kufanya mageuzi ya kweli kwa kutambua na kuheshimu: utu, heshima na haki msingi za wanawake. Jamii zinapaswa kuachana na mila pamoja na desturi ambazo zimepitwa na wakati, zinazowageuza wanawake kuwa kama bidhaa za kuuzwa na kununuliwa sokoni! Ikumbukwe kwamba, hawa ni watu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, wana utu, historia na haki zao msingi. Kuna haja yakupitia sheria na kurekebisha zile sheria zinazoendelea kuwakandamiza wanawake.  Zaidi ya wanawake milioni 8 kutoka katika Shirikisho la Vyama vya Wanawake Wakatoliki Duniani, WUCWO, UMOFC wanaungana na wanawake wenzao kutoka katika dini, makanisa na madhehebu mbali mbali ya Kikristo kuhimiza mchakato wa wongofu wa ekolojia ya binadamu, kwa kukazia utu, heshima, haki na usawa kama nyenzo msingi za ujenzi wa udugu wa kibinadamu, amani na utulivu duniani!

Wanawake: Nyanyaso
26 November 2019, 16:40