Tafuta

Familia ya Mungu nchini Tanzania inahamasishwa kupyaisha maisha na utume wa Kanisa kwa kujikita katika toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha. Familia ya Mungu nchini Tanzania inahamasishwa kupyaisha maisha na utume wa Kanisa kwa kujikita katika toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha. 

Familia ya Mungu nchini Tanzania boresheni maisha na utume wa Kanisa

Kiwango cha: Ujuzi, Elimu, Maarifa na mang’amuzi tunayoyapata hapa Roma lazima yasaidie kuwatumikia watanzania wenzetu hasa wanyonge kwa ari, moyo mkuu na unyenyekevu. Lazima tuhusike moja kwa moja katika kulijenga Kanisa la Bara la Afrika ambao linazidi kukua na kuonesha matumaini makubwa. Baada ya miongo si mingi Afrika litakuwa ndilo Bara lenye Wakristo wengi.

Na Padre Walter Milandu, C.PP.S. – Roma.

Jumamosi tarehe 16/11/2019 siku ya kuwakaribisha mjini Roma Watanzania wanaokuja kuanza masomo katika kipindi cha mwaka 2019-2020 na kuwaaga wale waliohitimu masomo yao tayari kurudi nchini Tanzania kuendeleza gurudumu la maendeleo fungamani ya binadamu. Siku hii ni ya furaha kubwa kwani kwanza kabisa tunakusanyika kama ndugu wamoja ili kusali pamoja. Inapendeza kuona pia kwamba wapo pia ndugu wengine ambao si Watanzania lakini ni majirani zetu wachache toka Rwanda na Zambia  ambao wameungana pamoja nasi kusali pamoja. Hii itukumbushe kuwa undugu wetu unavuka mipaka kwani ni Kristo mwenyewe anayetuunganisha. Nilipokuwa natafakari juu ya nini niseme kama ujumbe kwa ndugu zetu waliofika kuanza masomo na kwa wale waliohitimu sikuwa na sehemu ya kupata ujumbe huo zaidi ya kurejea Neno la Mungu ambalo Mama Kanisa ametutayarishia leo. Ujumbe huu lakini unatuhusu sote, wale walofika kuanza masomo, wale waliomaliza, wale wanaoendelea na masomo lakini pia wale ambao wako hapa Roma na Italia kwa ajili ya utume.

Sote tunataka tuuanze kwaka huu wa 2019 pamoja na Mungu na yeye mwenyewe ndiye akamilishe yote aliyoyaanzisha ndani yetu. Katika Injili tumesikia juu ya mama mjane ambaye hakukata tamaa kuomba haki yake kwa hakimu ambaye alikuwa dhalimu. Pamoja na udhalimu wake, hatimaye hakimu alimpa mama mjane haki yake. Kama fundisho la kwanza Bwana wetu Yesu Kristu katika Injili hii anatufundisha kuwa watu wa imani na wenye kudumu katika sala. Hakuna hata sala moja ambayo Mungu haisikilizi. Sisi ambao tumeitwa kuwa viongozi lazima tuwe watu wa imani ili tuweze kuwasaidia ndugu zetu nao wawe na imani na matumaini katika sala bila kukata tamaa. Injili ya leo pia inatualika kutafakari juu ya tabia ya Mungu ya kuwa karibu na wale walio wanyonge na wanaoonewa. Mungu daima anasikiliza kilio cha wanyonge na wanaodhulumiwa na mara zote anakuwa mtetezi wao. Biblia imejaa mifano mingi mbalimbali ambayo Mungu anajibu kilio cha wanyonge na wanaodhulumiwa haki yao.

Katika historia nzima ya taifa la Israeli Mungu amekuwa akijibu vilio vya wanyonge vya mtu mmoja mmoja au jumuiya. Sehemu ya kwanza kabisa ambayo tunamsikia Mungu akijibu kilio cha mnyonge ni wakati ambapo Kaini alipomwaga damu ya ndugu yake Abeli. Mwenyezi Mungu anamuuliza Kaini akisema, yuko wapi ndugu yako Abeli? Pamoja na kwamba yeye ndiye aliyemuua, Kaini anakataa kuwajibika na anasema hajui alipo ndugu yake kwani yeye si mlinzi wake. Mungu anajua kila kitu alichofanya Kaini na anamwambia ukweli akisema kuwa sauti ya damu ya ndugu yako inanililia toka ardhini. Mfano mwingine wa jinsi Mungu anavyojibu kilio cha wanyonge tunaupata katika somo la kwanza tulilolisikia. Mfalme Sulemani anatafakari juu ya wema na upendo wa Mungu aliouonyesha usiku ule alipowakomboa Waisraeli  toka utumwani Misri. Mungu alipotaka kuitimiza azma yake ya kuwakomboa Waisraeli alimwita Musa akamwambia, “Hakika nimeyaona mateso ya watu wangu walioko Misri, nami nimekisikia kilio chao.”

Mungu alimwita Musa ili atimize mpango wake wa kuwakomboa watu wake toka utumwani. Hata kwa kupitia manabii mbalimbali Mungu ameendelea kusikia kilio cha wanyonge. Nabii Amos ni maarufu kwa jinsi alivyotetea haki ya wanyonge na masikini dhidi ya matajiri. Kwa namna ya pekee, Mungu amejibu kilio cha wanadamu kwa kumtuma Mwanae wa pekee ili awakomboe kwa. Ili kutimiza azma hii ya Mungu, Yesu alikubali kujishusha, akaachilia yote, akatwaa mwili na damu yetu ya kibinadamu, akawa sawa na sisi isipokuwa hakutenda dhambi. Maisha na utume wake Yesu ulikuwa ni sadaka kubwa na aliwapa upendelea wa pekee wale ambao walikuwa ni wanyonge, masikini na waliokuwa wakidharauliwa na kuwekwa pembeni na jamii. Ndugu yangu wewe na mimi tumeitwa ili kupitia sisi Mungu aweze kujibu kilio cha wanyonge wengi hasa katika kujibu mahitaji mbalimbali ya Kanisa letu la Bara la Afrika. Kwa hiyo hata kuja kwetu hapa si kwa sababu ya faida yetu binafsi.

Sitegemei kuwa mtu alipigania kwa ubani na uvumba ili aweze kufika hapa. Kinyume chake Mungu kwa kupitia wakuu wa mashirika yetu au Maaskofu, ametuteua ili aweze kujibu kilio fulani. Hatuna budi kuepuka yele mawazo ya kidunia ambayo yanaweza kututoa katika lengo na mpango huo wa Mungu. Hatuko huko kwa ajili ya kujipatia utajiri au kujipatia madaraka kutokana na kiwango cha elimu tuliyoipata. Elimu na mang’amuzi tunayoyapata hapa lazima vitusaidie kuwatumikia wenzetu hasa wanyonge vizuri zaidi. Lazima tuhusike moja kwa moja katika kulijenga Kanisa letu la Afrika ambao linazidi kukua na kuonesha matumaini makubwa. Baada ya miongo si mingi Afrika litakuwa ndilo Bara lenye Wakristo wengi. Hata hivyo hatuwezi kuridhika na idadi kubwa ya waamini katika Bara letu bali changamoto tuliyo nayo ni kuhakikisha kuwa Kristo ajisikie nyumbani katika bara letu. Kati ya vilio vinavyosikika katika Kanisa letu ni kwamba watu hawaijui vema dini yetu na wengi wana kiu ya kujua Neno la Mungu.

Lazima tujibidishe kuwashirikisha yale tunayojifunza. Ndani ya Kanisa lenyewe kuna jumuiya za waamini ambazo ziko pembezoni kabisa na zinasahauliwa. Kumbe tuwe daima tayari kuwa karibu nao. Elimu yetu isitupeleke mbali na wanyonge bali itusaidie kuwa nao karibu zaidi maana ni kwa ajili yao Mungu ametuita na kututeua. Mwisho wa siku lazima wewe na mimi tujiulize, Je, uwepo wangu hapa na elimu niliyoipata, vimenisaidia kumjua  na kumpenda Mungu zaidi, kuupenda Msalaba zaidi na zaidi na kuwa tayari kuwatumia wanyonge? Mungu atusaidie tuweze kutimiza mpango wake katika maisha yetu.

18 November 2019, 09:24