Sherehe ya Yesu Kristo Mfalme wa Ulimwengu: Huu ni Ufalme wa: Haki na Uzima; Utakatifu na Neema; Mapendo na Amani. Sherehe ya Yesu Kristo Mfalme wa Ulimwengu: Huu ni Ufalme wa: Haki na Uzima; Utakatifu na Neema; Mapendo na Amani. 

Sherehe ya Yesu Kristo Mfalme wa Ulimwengu: Utakatifu na Neema

Ufalme wa Kristo ni wa haki na uzima, utakatitifu na neema, ufalme wa mapendo na amani. Kama Wafuasi wa Yesu katika ufalme wake, tumwombe leo aendelee kubadili sura ya dunia, nchi, kanisa, familia zetu na hata nafsi ya kila mmoja wetu ili zidumu na kuendelea kadiri ya malengo ya ufalme huo. Tujaliwe roho ya kumpenda huyo Mfalme kisha hapo tuweze kupendana na kusameheana.

Na Padre Paschal Ighondo - Vatican.

Karibu ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, katika tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 34 ya mwaka C wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Leo ni Dominika ya mwisho ya mwaka “C” katika mzunguko wake kadiri ya mpangilio wa kiliturjia. Kadiri ya utaratibu wa Mama Kanisa, Jumapili hii tunaadhimisha Sherehe ya Yesu Kristo Mfalme. Katika Kanisa kuna baadhi ya sherehe, kadiri ya utaratibu wake zilipaswa ziadhimishwe ndani ya juma kuu. Lakini kutokana na mazingira ya kuadhimisha sherehe hizo kutokuwa mazuri, sherehe hizo zimehamishiwa katika kipindi mara baada ya Pasaka au katika kipindi cha mwaka. Kati ya sherehe hizo ni Moyo Mtakatifu wa Yesu, Ekaristi Takatifu na Yesu Kristo Mfalme. Sherehe ya Yesu Kristo Mfalme ilipaswa iadhimishwe siku ya Jumapili ya Matawi. Liturujia ya siku ya Jumapili ya Matawi ilivyo imegawanyika katika sehemu tatu: Sehemu ya kwanza ni sehemu ya maandamano ambayo humwonesha Yesu Kristo anaingia Yerusalemu kwa shangwe kama Mfalme, umati mkubwa wa watu unamshangilia na kumlaki, wakishika matawi mikononi na kumshangilia Kristo kama walivyofanya nyakati zile kule Yerusalemu.

Sehemu ya Pili ya historia ya mateso ya Bwana wetu Yesu Kristo inayoonesha jinsi Bwana wetu Yesu Kristo alivyokamatwa na kutiwa nguvuni, mchakato mzima wa kesi yake ulivyoendeshwa hadi kuhukumiwa na kuteswa mpaka kufa kifo cha aibu msalabani. Sehemu ya tatu ni sehemu ya Liturujia ya kawaida kama Jumapili ya Kwaresma. Kutokana na mwingiliano wa furaha na huzuni katika siku ya Jumapili ya Matawi, Kanisa limeihamishia sherehe hii kutoka Jumapili ya Matawi na kuiweka katika Jumapili ya 34 ya mwaka ili kupata wasaa mzuri wa kumtafakari Kristo kama Mfalme wetu wa kweli, Mfalme asiyeeleweka kwa watu wake, kutokueleweka kwake kunapelekea kuhukumiwa na kusulubiwa kwake na mwishowe kuuawa kifo cha aibu msalabani. Lakini kwa kifo chake kilivyokuwa cha ajabu umati wa watu walioshuhudia, wanakiri Ufalme wake na kusema hakika huyu alikuwa mwana wa Mungu.

Somo la kwanza la Kitabu cha Pili cha Samweli (2 Sam. 5:1 – 3) ambalo ni sehemu ya simulizi la ufalme wa mfalme Daudi aliyeteuliwa na Mungu kuwa mfalme wa Israeli, jinsi alivyofaulu kuyaunganisha makabila kumi na mbili ya Israeli yaliyotengana ni msingi wa tafakari ya ufalme wa Yesu Kristo. Mnamo mwaka 1250 – 1000 K.K, Waisraeli waliingia nchi ya Kanaani na kukaa huko. Kazi ya kuitwaa nchi hii haikuwa rahisi. Waisraeli walipaswa kupigana vita na wananchi wa Kanaani, ili waweze kuimiliki na kuikalia nchi ya Kaanani. Waisraeli waliamini kuwa ushindi waliojipatia ulitokana na uwezo wa Mungu aliyetaka kuwapa wao nchi hiyo. Joshua aliyekuwa kiongozi wa Waisraeli kipindi hicho, aliamua kuligawia kila kabila eneo lake la kukaa, hata hivyo mapambano na majirani zao yaliibuka mara kwa mara. Kutokana na vita vya mara kwa mara, Waisraeli walitamani muungano wa makabila yote chini ya Mfalme mmoja kama mataifa mengine. Mwamuzi wa mwisho aliyewaongoza waisraeli alikuwa ni Samweli.

Mnamo mwaka 1000 K.K makabila kumi na mbili ya Israeli yalijiunga na kuingia mfumo wa taifa moja chini ya mfalme wao wa kwanza Sauli ambaye alitawala muda mfupi, akafuatiwa na Mfalme Daudi ambaye alifanikiwa kuweka muunganiko imara wa taifa la Israeli, akafanikiwa kuyashinda mataifa jirani yaliyowasumbua waisraeli. Daudi aliweka makao makuu ya taifa lake mjini Yerusalemu, akajenga hema na kuweka humo sanduku la Agano. Kumbe, kuna uhusiano kati ya ufalme wa Daudi na utimilifu wake kwatika ufalme na umasiha wa Yesu Kristo. Daudi ni ishara ya ufalme na umasiya wa Yesu Kristo. Historia inaonesha kwamba Mfalme Daudi alizaliwa katika mji wa Bethlehemu. Naye Yesu alizaliwa Bethlehemu (Lk 2:4). Daudi alikuwa mchungaji wa kondoo, mwenye nguvu, hata akaweza kumwua Goliati kwa kombeo. Yesu Kristo ni mchungaji mwema na kwa msalaba wake akaweza kumshinda shetani. Daudi alipotenda dhambi, alitoka katika mji wa Yerusalemu na kwenda kufanya toba akipitia bonde la mto Kedroni huku akilia na kuhuzunika kwa dhambi alizotenda.

Yesu Kristo ambaye hakutenda dhambi lakini alizichukua dhambi zetu sisi wanadamu badala yetu na kutoka katika mji wa Yerusalemu na kuuawa katika mlima Golgota naye pia baada ya karamu ya mwisho, alitelemka na kupita katika bonde la mto Kedroni katika kuikabili ile saa yake ya mateso. Mfalme Daudi alipanda mlima wa Mizeituni. Yesu Kristo alipanda mlima wa Mizeituni kabla ya mateso yake. Daudi anaporudi kutoka vitani, alikuwa na furaha kubwa na hivyo alipokewa na watu wake kwa heshima kubwa. Yesu Kristo alitoka kaburini mwenye utukufu mkubwa na ulimwengu wote ulimsifu. Uhusiano huu uliopo kati ya Mfalme Daudi na Yesu Kristo unaonesha kuwa ufalme wa Agano la kale, utimilifu wake ni katika Yesu Kristo katika Agano Jipya. Kumbe Yesu ni Mfalme wa kweli kwa kuwa alikuwepo kabla ya kuumbwa ulimwengu, na katika yeye vitu vyote vilifanyika, (Yoh 1:3). Yesu Kristo ni uzima na uhai wetu hivyo ni Mfalme kweli.

Picha ya falme zetu ni tofauti na hii ya Yesu Kristo, kwani zinasisitiza mambo ya kimwili na si kiroho. Wafalme wetu wamejikita katika ufisadi, uonevu, ukandamizaji na unyanyasaji; ufalme wa Kristo ni wa huruma, mapendo, msamaha, uadilifu. Yesu ni Mfalme anayewajali vilema, viwete, wagonjwa, wajane, yatima, maskini na wazee.  Yesu Kristo ni Mfalme milele kwa mfano wa Melkisedeki. Ufalme wa Bwana wetu Yesu Kristo ni tofauti na falme nyingine zote zilizowahi kutokea na zitakazotokea katika ulimwengu huu. Mamlaka ya Kristo ni ya milele na hivyo kumtenganisha na falme za leo na sasa. Ufalme wake ni ufalme usioangamizwa. “Naye akapewa mamlaka, na utukufu, na ufalme, ili watu wa kabila zote, na taifa zote, na lugha zote, wamtumikie; mamlaka yake ni mamlaka ya milele, ambayo hayatapita kamwe, na ufalme wake ni ufalme usioweza kuangamizwa,” Dan 7:14. Ufalme wa Kristo ni ufalme wa haki na uzima, ufalme wa utakatitifu na neema, ufalme wa mapendo na amani.

Kama Wafuasi wa Yesu katika ufalme wake, tumwombe leo aendelee kubadili sura ya dunia, nchi, kanisa, familia zetu na hata nafsi ya kila mmoja wetu ili zidumu na kuendelea kadiri ya malengo ya ufalme huo. Tujaliwe roho ya kumpenda huyo Mfalme kisha hapo tuweze kupendana, kusameheana, kusaidiana na kuombeana sisi kwa sisi. Katika ufalme au taifa, watu wa ufalme huo wanayo sheria au katiba inayoongoza mahusiano na maisha ndani ya ufalme huo. Watu wa ufalme au taifa hilo wanatambulika kwa kufuata katiba na sheria hiyo. Watu wa ufalme fulani wanafuata amri ya Mfalme wao. Kwa hiyo, ufalme wa Mungu ni pale amri ya Mungu inapofuatwa na watu wanatumikia. Na amri hii ni amri ya Mapendo “Pendaneni kama mimi nilivyowapenda ninyi”. Nira yangu ni laini na mzingo wangu ni mwepesi

Tofauti kati ya Ufalme wa Mungu na falme nyingine: Kristo amesema ufalme wangu sio wa ulimwengu huu kwa sababu; Ufalme wake si wa mahali. Ufalme wa Kristo hauna mipaka kama falme za dunia. Ufalme wake haupatikani kwa kampeini au kwa vita; ni ufalme wa Amani. Unapatikana kwa Amani na unaleta Amani “Na kwa yeye kuvipatanisha vitu vyote na nafsi yake, akiisha kufanya amani”. Unapatikana kwa msalaba. Anawapata watu si kwa shuruti bali kwa kuwaonyesha upendo msalabani. Ni juu ya msalaba alitangazwa kuwa ni Mfalme: Huyu ndiye Mfalme wa Wayahudi. Kanisa ni ishara ya ufalme wa Mungu, Kanisa ni wakala wa ufalme wa Mungu. Kristo ni Mfalme wa Nyakati. Yeye ni Alfa na Omega. Yesu ni mwanzo na mwisho wa mwaka. Hivyo, ni wakati mzuri kumshukuru Kristo aliyetulinda na kutuongoza katika kipindi cha mwaka mzima na hivyo, tumtangaze kuwa ndiye Mfalme wetu nyakati zote. Tumsifu Yesu Kristo. 

Sherehe

 

23 November 2019, 15:13