Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya Kwanza Kipindi cha Majilio: Kukesha na kusali! Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya Kwanza Kipindi cha Majilio: Kukesha na kusali! 

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya Kwanza ya Majilio: Kesheni

Kipindi cha Majilio kimegawanywa katika sehemu kuu mbili: Dominika ya kwanza ya Majilio na huishia tarehe 16 Desemba. Hapa Kanisa linatualika kutafakari juu ya ujio wa pili wa Kristo katika utukufu wake. Sehemu ya pili huanza tarehe 17 hadi 24 Desemba. Tunaongozwa kutafakari juu ya ujio wa kwanza wa Yesu Kristo. Ni wakati wa matayarisho ya sikukuu ya kuzaliwa kwake Kristo.

Na Padre Paschal Ighondo - Vatican.

Karibu ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, katika tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya kwanza ya majilio mwaka A wa Kanisa. Leo tunaanza kipindi cha majilio. Tumemaliza mwaka C katika liturjia ya kanisa na tunaanza mwaka mpya A wa Kanisa. Katika Kalenda ya liturujia, Kanisa limetenga kipindi hiki kwa ajili ya maandalizi ya kumpokea Mungu anayekuja kwetu katika hali ya kibinadamu yaani Yesu Kristo, Mkombozi wetu. Kipindi hiki kinaitwa majilio. Kipindi cha Majilio kimegawanywa katika sehemu kuu mbili. Sehemu ya kwanza huanza Dominika ya kwanza ya Majilio na huishia tarehe 16 Desemba. Katika sehemu hii Kanisa linatualika kutafakari juu ya ujio wa pili wa Kristo katika utukufu wake. Sehemu ya pili huanza tarehe 17 hadi 24 Desemba. Masomo ya sehemu hii yanatuongoza kutafakari juu ya ujio wa kwanza wa Yesu Kristo. Ni wakati wa matayarisho ya sikukuu ya kuzaliwa kwake Kristo.

Nabii Isaya mwana wa Amozi katika somo la kwanza anatabiri kwamba wakati wa Masiya mataifa yote watamwelekea Mungu; naye atawapa amani, heri na baraka. Ukweli, kadiri ya utabiri huu, utadhihirika katika ujio wa pili wa Masiya, Yesu Kristo. Katika somo la pili la waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi, tunaambiwa kuwa Mwanga uliotabiriwa na nabii Isaya umefika. Mwanga huu ni Yesu Kristo. Katika ubatizo tumeupata mwanga huo mara ya kwanza kwa imani yetu. Tunakutana tena na mwanga huu yaani Yesu Kristo katika maisha ya uzima wa milele baaada ya kifo. Paulo anatuasa tuyavue matendo ya giza, na kuzivaa silaha za nuru, tuenende kwa adabu, si kwa ulafi na ulevi, si kwa ufisadi na uasherati, si kwa ugomvi na wivu. Bali tumvae Yesu Kristo, wala tusiuangalie mwili, hata kuwasha tamaa zake.

Katika Injili Mathayo anatukumbusha kuwa, Kristo atafika tena kutimiliza nyakati zote na kutuhukumu. Tutambue kuwa hapa duniani tu wasafiri, safari yetu ni ya kuelekea mbinguni. Kwa kuwa hatujui lini tutakapoiacha dunia hii na mambo yake yote wala siku wala saa hakuna aijuaye, basi tuwe tayari wakati wote. Yesu anatuambia tuweni macho na tukeshe kwa kutoa mifano mitatu: mfano wa kwanza ni wa nyakati za Nuhu. Nyakati hizo kulikuwa na makundi mawili ya watu; kundi la kwanza ni la wale waliokuwa wamezama katika kujishughulisha na mambo ya dunia: kula, kunywa, kuoa na kuolewa wakamsahau Mungu na amri zake, hatimaye wakaangamizwa na gharika kuu. Kundi la pili ni la watu waliokesha na kumsikiliza Mungu, hao ndio waliookoka na gharika. Mfano wa pili unahusu shughuli za kila siku za binadamu: kazi za shambani, na kazi ya kusaga nafaka. Nao pia katika shughuli hizo za kila siku hawana budi kukesha. Mfano wa tatu ni mfano wa mwizi ambaye hatangazi muda aendapo kufanya uhalifu. Mifano hiyo mitatu aliyoitoa Yesu inatualika tuwe tayari mda wote kwani hatujui saa ya kifo chetu.

Mtu hawezi kukesha akimsubiri Bwana wake huku akiwa katika hali ya huzuni, hali ya majonzi, hali ya vita. Mazingira ya wale wakeshao ni lazima yawe mazingira ya amani na utulivu. Hali hiyo ya amani itajengwa na watu wanaomtafuta Mungu, wanaomwendea ili awafundishe njia zake ili wapate kutembea katika mapito yake Mungu mwenyewe. Watu hao wanaofundishwa njia zake, wanaopokea neno lake na sheria zake watakuwa na uwezo wa kutofautisha kati ya jambo zuri na jambo baya. Wakishatambua ubaya uletwao na mambo maovu, watu hao watazibadili zana za vita kuwa zana za uzalishaji mali, panga zitafuliwa na kuwa majembe, na mikuki iliyotumika katika vita itageuzwa kuwa miundu. Hivyo, hakutakuwa na vita kati ya mtu na mtu au kati ya taifa na taifa hili ni dokezo juu ya ulimwengu mpya. Amani hiyo ya dunia, amani kwa wote ni tunda la haki litokanalo na kuliishi Neno la Mungu. Ni amani ambayo haiji kama mvua kutoka mbinguni na kukaa duniani bila ushiriki wa binadamu.

Katika somo la kwanza Isaya anatabiri ambayo yangetokea katika Israeli kwa kuja kwake Kristo, anasema, “Mlima wa Nyumba ya Bwana utawekwa imara. Na mataifa mengi wakwenda na kusema, Njoni twende juu mlimani kwa Bwana, nyumbani kwa Mungu wa Yakobo, naye atatufundisha njia zake.” Kristo amekwisha kuja na ameuweka imara mlima wa nyumba ya Bwana yaani Kanisa na akatuingiza sisi katika mlima wa Bwana. Kwa sababu hiyo Mwandishi wa barua kwa Waebrania anasema “Lakini ninyi mmefika katika mlima Siyoni, kwenye mji wa Mungu” (Waebr.12:22). Ni kweli hakuna ajuaye atakufa lini. Kila mtu akifa anahukumiwa peke yake pale pale kulingana na Bwana alivyomkuta wakati huo. Kwa hiyo, tusitwaliwe na mkumbo, tukisema kila mtu ndivyo anavyofanya, watu wengi tuko hivyo. Kifo cha wengi ni harusi. Unahukumiwa peke yako. Kristo amesema “Mmoja atatwaliwa mwingine ataachwa”. Hivyo, kuna umuhimu wa kila mara kuwa tayari.

Tusilale usingizi. “Usiku umekwisha na mchana umekaribia”. Tusiahirishe maandalizi na kujiridhisha kuwa tutajipatanisha na Mungu wakati ukikaribia. Hujui utakufa lini. Kama una ugomvi na ndugu yako au jirani yako afadhali kuumaliza mapema, kama hupokei Sakramenti kwasababu ya vizuizi vitoe mapema, usiseme baadaye kidogo maana hiyo baadae haijui siku ya kifo. Kama kuna kitu umeiba afadhali kukirudisha mapema. Kama una tabia fulani isiyo nzuri afadhali kuiacha mapema. Kama hupokei kitubio afadhali uanze leo. Usiseme mimi ni kijana nikifikia uzeeni nitajipatanisha na kanisa na kushughulikia mambo ya imani maana huna kibali cha kufika uzeeni. Usisubiri wamwite Padre ukiwa kufani wakati katika uzima wako hukujali sakramenti kwani hakuna mkataba wa kuwa utaugua na hautakufa kwa ajali. Angalieni, Kesheni, Ombeni maana hamjui Bwana atakuja lini. Na hilo niwaambialo ninyi, nawaambia wote, kesheni. Tumsifu Yesu Kristo.

Jumapili 1 Majilio
29 November 2019, 14:59