Tafuta

Sherehe ya Yesu Kristo Mfalme wa Ulimwengu: Utukufu na ukuu wa Kristo Yesu Mfalme wa Ulimwengu umetundikwa juu ya Msalaba! Sherehe ya Yesu Kristo Mfalme wa Ulimwengu: Utukufu na ukuu wa Kristo Yesu Mfalme wa Ulimwengu umetundikwa juu ya Msalaba! 

Sherehe ya Yesu Kristo Mfalme wa Ulimwengu: Unyenyekevu!

Katika Sherehe ya Yesu Kristo Mfaome wa Ulimwengu, Mama Kanisa anatafakari juu ya ufalme wa Yesu ambao ni: wa ukweli, maisha, utakatifu, neema, haki, upendo na amani. Huu ni mwaliko kwa Wakristo kushuhudia tunu hizi kama kikolezo cha uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Yote yanaanza na kupata utimilifu wake katika Fumbo la Msalaba!

Na Gaston George Mkude, - Roma.

Amani na Salama! Wayahudi au wanawaisraeli walimsubiri kwa hamu na shauku kubwa ujio wa Mfalme mkuu. Mfalme mwenye kila aina ya nguvu, utajiri, mavazi ya thamani kubwa, na hata aketiye juu ya kiti cha kifalme cha dhahabu au madini ya kito ya thamani kubwa. Mfalme anayetawala kwa mabavu na nguvu kubwa kiasi cha kuwanyenyekesha hata maadui wake kuweza kulamba vumbi la miguu yake. Rejea Zaburi 72:9-11. Hivyo ufalme wake ni kwa watu wote na wa milele. Katika Injili ya leo ya Sherehe ya Kristo Mfalme ndio tunapata jibu la hamu na shauku ile ya wanawaisraeli.  Injili ya leo inatupeleka pale mlimani Kalvari, ambapo Yesu ametundikwa na kuwambwa misumali na pembeni yake wakiwepo wale wezi wawili, na juu ya msalaba wake kukiwa imewekwa anwani iliyoandikwa: Huyu ni Mfalme wa Wayahudi! Ni huyu ambaye wayahudi walimsubiri kwa hamu na shauku kubwa kama mfalme wao? Hakika haiwezekani kwani machoni mwa watesi na watu wengine alionekana kushindwa, hivyo hatuoni ishara wazi za ufalme na ukuu wake.

Akiwa juu Msalabani haonekani kutawala akiwa ameketi katika kiti za enzi na fahari kuu, ila amewambwa pale juu Msalabani, hajazungukwa na watumishi wanaomtumikia na kumwangukia na kumsujudia miguuni mwake, hatuoni maaskari wanaomlinda na kumlaki Bwana Mkuu. Yesu pale juu Msalabani chini ya Msalaba wapo watesi wake wanaomtusi, na kumkejeli na kumdhihaki,  hajavaa mavazi ya thamani na badala yake alivuliwa vazi lake na kubaki karibu uchi bila nguo. Yesu akiwa juu Msalabani sio tishio la mtu yeyote, bali anatamka maneno ya upendo na msamaha kwa wote, halazimishi maadui zake kulamba vumbi la miguu yake kama mfalme, ila kinyume chake ni Yeye ndiye anayekunywa siki anayonyweshwa na maadui zake.  Pembeni yake hatuoni watumishi wanaomtumikia na badala yake ni wale waarifu wawili. Yesu kabla ya mateso yake pale juu Msalabani aliwajibu ombi la wana wale wawili wa Zebedayo kwa kuwataadharisha ni aina gani ya utawala na ufalme wake. Marko 10:37.

Ufalme wa Yesu ni tofauti kabisa na ule wa ulimwengu huu au labda na ule ambao wengi wetu bado tunao vichwani mwetu. Kwa bahati mbaya hata nasi leo bado tunashawishika kufikiri kuwa ufalme wa Yesu ni ule wa ushindi na hata wakati mwingine kutaka nasi kupewa heshima kubwa na watawala na wafalme wa dunia hii. Anwani ile iliyowekwa juu ya msalaba wake inamtambulisha  Yesu kama Mfalme wa Wayahudi kwa kejeli na dhihaka kwani alionekana kushindwa, mnyonge na dhaifu asiyeweza hata kujitetea yeye mwenyewe kwa kutenda muujiza ili ashuke kutoka pale juu msalabani. Mfalme wa namna akiwa hana jinsi ya kujitetea wala kujihami pale juu Msalabani, ndio kusema mipango na miradi yetu yote nayo inakwama. Kuna mkwamo pale msalabani kila mara tunapoangalia kwa jicho letu la kibinadamu! Ni katika mazingira ya namna hii linarudi swali inawezekanaje mtu huyu kuwa ndiye yule Masiha, Kristo au Mpakwa Mafuta wa Mungu?

Katika sehemu ya kwanza ya Injili ya leo tunakutana na makundi matatu ya watu wanaoonekana wakiwa chini ya Msalaba wake Yesu, chini ya miguu ya mfalme.  Kulikuwa na makutano. Hawa ni wale wanaobaki pale chini ya msalaba bila kufanya lolote, si kwa ubaya wala wema. Wanabaki na mshangao ila bila kuelewa maana ya yale yanayojiri pale. Hawaelewi yawezekanaje mtu aliye mfalme kuteseka na hata kufa kifo cha aibu kubwa bila kujitetea kwa namna yeyote ile si kwa upande wake na hata waliokuwa marafiki zake wa karibu. Ni fedheha kubwa kwao! Ni Mtu mwenye haki lakini kwa nini Mungu hafanyi kitu na kuruhusu mtu huyu kuteseka na hata kufa!? Wakati tunasoma kwa kipindi chote cha Mwaka huu wa Kiliturjia tunaweza kukiri kuwa Mwinjili Luka daima ameonesha jinsi Mungu anavyojali maskini, walisetwa na watu wanaonekana kuwa ni mwisho katika dunia yetu. Mwinjili Luka leo anawaonesha pia watu wale au makutano wanaobaki pale kimya wakisongwa na mshangao mkuu, ndio kusema hawakuhusika kwa kifo cha Yesu.

Hivyo walirejea makwao wakijipigapiga kifua. Luka 23:48. Kundi hili la makutano linawakilishwa wale wote ambao bado kuelewa mpango wa Mungu katika maisha yao. Ni watu wanaobaki katika upofu, hivyo wenye uhitaji wa mwanga wa kuweza kuuona uso na mpango wa Mungu katika maisha yao. Chini ya msalaba pia walikuwepo wakuu wa makuhani. Ni hawa sasa wahusika wa mateso na kifo chake Yesu. Ni kama wale wazee wa Kiyahudi waliokutana ili kumpaka mafuta Daudi ili awe mfalme wao, hivyo wakuu wa makuhani walipaswa kumtambua Yesu kama Mfalme wa Wayahudi. Na badala yake hawakumtambua na kubaki wakimdhihaki na kumkejeli, siyo mfalme kadiri ya matarajio yao, asiyeweza kujiokoa wala kujipigania yeye mwenyewe na kujikomboa, asiyeweza kushuka Msalabani. Kwa nini Yesu ajidhihirishi kadiri ya matarajio na matamanio yao? Kwa nini atendi muujiza akiwa pale juu Msalabani?

Kama angetenda muujiza basi kwa hakika wote wangemwamini na kumfuasa na hata kukwepa kukinywa kikombe kile. Hivyo watu wangemwamini mfalme mwenye nguvu na mabavu, Mungu anayewanyenyekesha maadui zake, anayejibu kila pigo kwa pigo lingine, anayetisha na kuogofya kwa nguvu na mabavu yake, asiyekuwa na mchezo wala utani, kwa kutumia msemo wa mtaani, angekuwa ni Mungu jiwe kweli kweli! Lakini huyo sio Mungu wa Yesu! Kama angelishuka pale msalabani basi angekuwa amesaliti misheni yake., angeonesha sura isiyo ya Mungu wa kweli, picha waliyokuwa naye wale wakuu wa watu. Ndio kusema angekuwa mungu wa herufi ‘’m’’ ndogo kwani sawa na mungu wa dunia hii, mwenye mabavu, maguvu, mbabe, mwenye kisasi na kulipiza kila ubaya na uovu, na mwenye kila aina ya ulinzi. Hivyo Mungu anayefunuliwa pale juu msalabani ni tofauti na yule wa ulimwengu huu. Mungu anayependa wote hata wale wanaompinga na kumkataa waziwazi, anayesamehe wote na daima, anayeokoa n asio kuangamiza, anayependa bila mipaka. Ni Mungu anayependa hivi kama asemavyo Mtakatifu Katarina wa Siena, ‘’Pazzo d’amore’’ He is crazy in love!

Mungu sio mwenye enzi na uwezo kwa kuwa anaweza kutenda kila anachotaka kufanya na badala enzi na ukuu wake tunauonja katika upendo wake usio na kipimo kwa mwanadamu! Ni Mungu anayebaki kuwa mtumishi kwa mwanadamu kwa namna isiyoelezeka wala kueleweka kwa akili zetu za kibinadamu.  Uwezo wake sio ule wa kutawala kwa mabavu bali kutumikia kwa upendo. Tunamuona Yesu anayejivika na kujifunga kiuno chake na kuwaosha miguu wanafunzi wake. Hiyo ndio sura halisi ya Mungu! Kundi la tatu chini ya msalaba ndio maaskari wa kirumi. Ni kundi linabaki kutekeleza sio matakwa yao bali ya wakuu na watawala wao. Wanachojua ni kutii tu amri na maagizo kutoka kwa watawala na wakuu. Ni watumwa kwa jinsi wanavyopoteza vichwa na utashi wao katika maamuzi yao. Ni kujivua utu wao yaani akili na utashi. Sasa tuangalie na ile anwani iliyoandikwa na kuwekwa juu ya Msalaba wake Yesu.

Mwinjili Luka kama alivyokuwa na nia ya kuwaalika Wakristo wa jumuiya yake bali hata nasi leo kuutafakari ufalme wa Yesu akiwa pale juu Msalabani. Akiwa pale juu msalabani, Yesu anatuonesha kuwa aina gani ya ufalme wake, ni yeye anayekubali kujishusha kiasi cha kudharirika, anayejua kuwa njia pekee ya kumpa Mungu utukufu ni katika kuchagua nafasi ya mwisho na kumtumikia aliye mdogo kwa upendo. Pia kulikuwa na wale wezi au awatenda maovu wawili walioteswa pamoja naye pale juu Msalabani mmoja mkono wa kulia na mwingine wa kushoto. Kama makutano, kama wakuu, kama maaskari, mmoja wa hawa wezi wawili haelewi mpango wa wokovu wa Mungu, anakosa kuelewa sura ya Mungu katika sura ya Yesu anayeteseka pale juu Msalabani. Naya kama wakuu anamtarajia Masiha anayekimbia mateso na msalaba na hapo kuonesha uwezo wake ili kushuka pale juu msalabani, kwake Yesu ni mtenda miujiza tu, hivyo kinyume chake anakosa maana na nafasi katika maisha yake.

Ni yule muovu mwingine ndiye anayeona sura ya Mungu katika sura ya Yesu, anaona wokovu na msamaha katika sura ya Yesu. Anasali na kuomba Yesu amkumbuke katika ufalme wake.  Anamuita na kumtambua Yesu kwa jina na zaidi sana nafasi ya Yesu kama Masiha, kama Kristo. Na Yesu anamuhakikishia kuwa pamoja naye Paradiso, ndio maisha ya umilele katika muunganiko na Mungu mwenyewe. Anaomba msamaha na wokovu n asio muujiza wa kushuka pale juu msalabani, anatambua maana na umuhimu wa kushiriki katika historia ya wokovu. Nawatakia tafakari na Dominika njema na Sherehe njema ya Kristo Mfalme.

25 November 2019, 16:59