Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili 31 ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa. Jengeni utamaduni wa kukutana na Kristo Yesu, chachu ya toba, wongofu na malipizi ya dhambi Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili 31 ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa. Jengeni utamaduni wa kukutana na Kristo Yesu, chachu ya toba, wongofu na malipizi ya dhambi 

Tafakari Jumapili 31 Mwaka: Zakayo mtoza ushuru na fisadi atubu!

Kipofu na Zakayo wana kiu ya kumwona Yesu na hasa kuuona Uso wake: Ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa mwanadamu. Yesu pamoja na kufuatana na umati mkubwa, lakini wengi wao bado hawajauona uso wa Yesu na kumtambua kuwa ndiye: Mkombozi, wengi walimwona Yesu kama mtenda miujiza tu! Mtu mwenye uwezo wa pekee wa kuponya na kutenda miujiza.

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.

Amani na Salama! Yesu mara tu alipoingia katika mji wa Yeriko akiwa anafuatana na umati mkubwa wa watu pamoja na wanafunzi wake, anakutana na kipofu anayemlilia na kumuomba ili apate kuona tena na Yesu anamponya kipofu yule. Luka 18:35-43. Ni katika muktadha huo pia Yesu anakutana na Zakayo mkuu wa watoza ushuru. Kuwa kipofu kwa Wayahudi ilionekana ni laana na adhabu kutoka kwa Mungu kwa ajili ya madhambi na hata watoza ushuru kama tulivyoona katika Injili ya Dominika iliyopita, nao walikuwa ni watu walioonekana kuwa ni wadhambi na hivyo mbali na Mungu. Kipofu na mtoza ushuru ni watu wadhambi, waliotengwa na kuonekana wapo mbali na Mungu. Hivyo wote wawili kipofu na Zakayo tunaona wana kiu ya kumwona Yesu na hasa kuuona Uso wake Yesu, ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa mwanadamu. Yesu pamoja na kufuatana na umati mkubwa tunaona wengi wao bado hawajauona uso wa Yesu kwa maana kumtambua Yesu kama Kristo, kama Mkombozi anayekuja ili kututoa katika hali duni ya dhambi, wengi walibaki kumuona Yesu kama mtenda miujiza tu na si zaidi ya hapo, ni mtu kama watu wengine ila mwenye uwezo wa pekee wa kuponya na kutenda miujiza.

Anayekutana na Yesu lazima mwishoni awe mtu mpya, kubadili si tu kichwa bali namna ya kuishi, kukutana na Yesu ni kukutana na Wokovu na ukombozi wetu. Pamoja na umati mkubwa ule lakini mwinjili Luka anatuonesha alikuwa ni huyu mkuu wa watoza ushuru Zakayo ndiye aliyekuwa na hamu na shauku ya kukutana na uso wa Yesu, ndio kusema kukutana na wokovu na si kumuona Yesu kwa mshangao wa kawaida kama mtenda miujiza. Hakika wengi walibaki kumshangaa Yesu kama mwalimu mwenye mvuto au uwezo wa pekee na kamwe si kama Kristo wa Mungu, mkombozi wa mwanadamu. Jina Zakayo kutoka jina la Kiyahudi “Zakkai” (2 Makabayo 10:10) likiwa na maana ya “Mwenye haki na aliye msafi”. Inatushangaza kwani Zakayo kama tujuavyo alikuwa mtoza ushuru na zaidi sana ni mkuu wa watoza ushuru, watu waliotengwa na kusetwa na jamii hasa ya kidini kwani walionekana kuwa ni wadhambi kwa jinsi walivyonufaika na wizi na madhulumu ya kodi na kwa kuungana na utawala wa kigeni wa warumi kuwanyonya na kuwagandamiza wanyonge.

Mwinjili Luka anamtaja kwa jina si kwa ajali bali kuna ujumbe hasa kwa jinsi alivyokuwa na njaa na kiu ya kukutana na uso wa Yesu na pia Yesu anamuita kwa jina alipomuona pale juu ya mkuyu. Mwinjili Luka si tu anatutajia jina lake kuwa ni Zakayo ila anakwenda mbali hata kutuambia kuwa alikuwa mfupi kwa kimo. Kuwa mfupi ndio kusema jinsi alivyoonekana na jamii inayomzunguka, ni kama doa jeusi katika nguo nyeupe, ndio kusema Zakayo kama mdhambi alikuwa kama doa katika jamii ya watu walio wasafi na watu wa haki, hivyo alitengwa kwa kuwa ni mdhambi, fisadi na mla rushwa wa kutupwa! Zakayo alitambua hali yake ya kuwa mfupi na hivyo kutokujihesabia haki yeyote, ni kama mtoza ushuru aliyefika kusali hekaluni katika Dominika iliyopita naye alitambua uduni na udogo wake na hivyo kusimama kwa mbali na kujipigapiga kifua akiomba toba na msamaha wa madhambi na makosa yake. Zakeo naye leo alitambua uduni na udogo wake na ndio tunaona anajiongeza kwa kupanda mkuyu.

Mwinjili Luka anazidi kumtambulisha pia kuwa Zakayo alikuwa tajiri, ila pamoja na utajiri wake anatuonesha kuwa bado alikuwa na njaa na kiu ya kutaka kukutana na nafsi ya Yesu. Pamoja na kuwa na kila kitu katika maisha yake lakini bado anajiona anapungukiwa na jambo moja lenye kuweza kumaliza njaa na kiu yake kwa daima. Zakayo mtoza ushuru anatambua kuwa ni kwa kukutana na kuuona uso wa Yesu hapo ndipo kiu na njaa yake ya ndani itaweza kumalizika. Ni kiu na njaa sio ya chakula na kinywaji cha kawaida bali ni ile ya ndani inayomfanya kukosa amani na furaha ya kweli. Ni njaa na kiu ya ndani kabisa katika nafsi yake ambayo haiwezi kumalizika au kukidhiwa kwa mali za ulimwengu huu. Hivyo anapanda juu ya mkuyu ili apate naye kuuona uso wa Yesu. Anafanikiwa kuupanda mkuyu ili naye aliye mdhambi aweze kumuona Yesu ili ile njaa na kiu yake iweze kumalizika. Zakayo kutokana na ufupi wake wa kimo hakuweza kumuona Yesu isipokuwa kwa kupanda mkuyu ule.

Ndio kusema, jamii au watu wanatuzunguka mara nyingi wanakuwa ni kikwazo pia kwa sisi kukutana na uso wa Yesu, ni mtazamo wa jamii uliomseta tayari Zakayo aliyekuwa mkuu wa watoza ushuru kuwa ni mdhambi mkubwa na hivyo hana nafasi ya kukutana na uso wa Mungu mwenye huruma. Zakayo anafanya jitihada binafsi, anajiongeza kwa lugha ya leo na hii inasukumwa na ile njaa na kiu aliyo nayo ndani mwake ya kutindikiwa na huruma ya Mungu. Kama iliìvyokuwa kwa kipofu wa Yeriko badala ya makutano kuwa msaada kwake ili akutane na Yesu walikuwa ni kikwazo kwake, naye anazidi kupaaza sauti yake akimlilia Yesu ili apate kuona tena. Ndivyo nasi kila mara tunapotaka kukutana na uso wa Yesu tunakutana na vizuizi vingi na hasa kupitia watu wanaotuzunguka. Jumuiya zetu mara nyingi tumekuwa sababu ya makwazo badala ya kuwapeleka watu kwa Yesu tumekuwa sababu ya kuwaweka mbali na wokovu.

Namna zetu mara nyingi ni kama zile za Farisayo katika Injili ya Dominika ya 30 ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa, kuona wengine walio wadhambi na wakosefu basi hao hawana nafasi katika ufalme wa Mungu, hawana nafasi katika jumuiya zetu za wenye haki na watakatifu. Injili ya leo inatualika kubadili vichwa vyetu, mitazamo yetu hasa katika kuwasaidia wengine ili waweze kukutana na uso wa Yesu. Makutano hawakuishia kuwaona kipofu na Zakayo kuwa ni wadhambi bali hata walishangaa na kukwazika kumuona Yesu akila na kunywa pamoja na wale walioonekana kuwa ni wadhambi na wakosefu. Na hata walikwazika na kulalamika baada ya kumuona Yesu akila na kunywa au kutembea pamoja na wadhambi. Yesu anashiriki na wadhambi ndio kusema kwao Yesu ni mdhambi na mkosefu kwa kuwa alikuwa anashiriki na watu najisi. Yesu leo si tu anamwalika Zakayo ashuke haraka bali anaingia nyumbani kwa mdhambi, kwa Zakayo.

Uso na macho ya Yesu ni tofauti na uso na macho ya makutano, kwani Yesu anapofika chini ya mkuyu ule anaangalia juu na kumuona Zakayo. Si tu anamuona Zakayo bali anakuwa wa kwanza kumuita kwa jina Zakayo na kumwalika kushuka kwa haraka. Zakayo alipanda juu ili yeye aweze kumuona Yesu ila ni Yesu kutoka chini anakuwa wa kwanza kumuona Zakayo mdhambi au mkuu wa wadhambi! Kila mara Yesu anakuwa wa kwanza kumuona mdhambi, kumtambua na kumuita kwa jina. Yesu daima anatuona kwa nafasi ya kwanza na anatutambua kwa majina yetu ndio kusema anajua uduni na udogo wetu, anatujua kila mmoja wetu. Yesu anatuonesha upendo na huruma yake ya milele, jinsi anavyompenda mwanadamu hata anatuona sio kutokea juu mbinguni bali kutoka chini anatuangalia sisi tunapokuwa juu tunapokuwa na hamu na shauku ya kumuona. Upendo wa Mungu kwa mwanadamu! Wafilipi 2:7-8 Kenosis, Yohana 8:10

Yesu anamwambia Zakayo kuwa leo lazima nibaki nyumbani mwako, nyumbani mwa yule aliyetengwa na kusetwa na jamii inayomzunguka kwa kuwa ni mdhambi ndimo Yesu anataka kubaki na kula na kunywa. Inanipasa ndio kusema njaa na kiu ya Mungu ni Upendo kwa mwanadamu aliye mnyonge na mdhambi. Ni njaa na kiu ya Mungu kila mmoja wetu kufikia wokovu. Na ndio unapaswa kuwa wito wetu kama Kanisa la kimisionari kuona kila roho haipotei bali inaonja wema na wokovu wa Mungu. Injili ya leo inamalizikia kwa kalamu nyumbani kwa Zakayo. Tungetegemea Yesu awe kalamuni pamoja na watu wema na wenye haki ila badala yake alishiriki pamoja na wadhambi.  Wenye haki walibaki nje wakilalamika, ndio kusema kulalamika ni kukosa upendo na huruma na ndio kitu kinachotutenga kushiriki katika kalamu ile ya Kimungu au maisha ya wokovu. Kila mara wapendwa hatuna budi kuwa tunaalikwa kuwa wamisionari ndio kusema kuwa wapelekaji wa uso wa Yesu, wajumbe wa huruma na upendo wa Mungu kwa watu wake.

Yesu anatukumbusha kuwa amekuja kwa ajili ya wadhambi na wakosefu, walio wagonjwa, wanaomuhitaji Mungu, kwa ajili ya wale wanaohitaji wokovu. Na ndio tunaona Zakayo ameonja upendo wa Mungu naye anajibu mara moja kwa upendo si tu kwa kumkaribisha Yesu nyumbani mwake bali hata kuwakumbuka maskini.  Zakayo anawapa nusu ya utajiri wake kwa maskini na kwa wale aliowadhulumu atawarejeshea mara nne ya kile alichowapora. Wokovu umefika kwa nyumba hii ndio kusema Zakayo hakubaki kama awali bali anabadili maisha yake. Haitoshi kuambatana na Yesu kama makutano wakati hatupo tayari: kutubu, kuongoka na kutimiza malipizi kwa kubadili maisha yetu, hatupo tayari kukutana na uso wa Yesu bali tunabaki kumuona Yesu kama mtenda miujiza, kama bwana mazingaombwe. Tumfuate Yesu ili tukutane na wokovu, tukutane na mkombozi. Matunda ya kukutana na uso wa Yesu hakika ni kuwa na maisha mapya, ni kuwa na maisha yanayoakisi uso wa upendo na huruma yake Yesu mwenyewe kwa wengine. Nawatakia Dominika na tafakari njema.

02 November 2019, 12:05