Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya 32 ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa: Tafakari juu ya fumbo la kifo, ufufuko wa wafu, maisha na uzima wa milele! Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya 32 ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa: Tafakari juu ya fumbo la kifo, ufufuko wa wafu, maisha na uzima wa milele! 

Tafakari Jumapili 32: Fumbo la Kifo katika maisha ya mwanadamu!

Nasadiki kwa Ufufuko wa mwili: Kanisa lina amini na kutumaini kwa uthabiti kabisa kama vile Kristo Yesu alivyofufuka kweli kutoka wafu na anaishi daima, vivyo hivyo wenye haki baada ya kifo chao, wataishi daima na Kristo Yesu Mfufuka, naye atawafufua siku ya mwisho. Ufufuko wa waamini ni kazi ya Fumbo la Utatu Mtakatifu. Neno mwili, linamwelezea mtu katika hali yake ya udhaifu! KIFO!

Na Padre Alcuin Maurus Nyirenda, OSB. – Roma.

Katika tamaduni za mataifa mengi hapa duniani zikiwemo za makabila ya Waafrika, kuna hadithi na simulizi ziitwazo “Ngano” au kwa Kiingereza Myths. Mathalani Wabantu wanazo Ngano kuhusu joka kubwa sana lenye vichwa vya kutisha, au Mnyama mkali mwenye pembe nyingi, au mti mkubwa liposimama jini au wanapokusanyika wachawi. Kuna pia Ngano zinazowahusu watu wadogo na wanyonge wanaoibukia kufanya mambo ya kishujaa, kama vile ngano za akina Chaupele, Kalikalangi, Ngulyeki nk. Ngano hizi zinasimulia jinsi mtu huyo mdogo maskini na mnyonge anavyoweza kupambana na mnyama wa hatari, lakini anafaulu kupambana naye na kumwua kiurahini na kunusuru maisha ya wengine. Ngano nyingine zilichorwa kwenye mawe au kuchongwa vinyago vilivyoakisi fikra ya binadamu kuhusu kifo na hatima yake. Kwa bahati mbaya Ngano hizo zinapuuzwa, kisha michoro na sanamu zinaishia kuitwa vinyago badala ya kuzifanyia tafakari ya maisha na kifo.

Uhalisia huu wa uwepo wa Ngano na sanamu (vinyago) katika tamaduni za mataifa mbalimbali ni ushahidi tosha wa lugha moja ya ulimwengu kuhusu maisha na hatima yake. Sambamba na Ngano na michoro kuna pia lugha nyingine zinazoakisi maana ya maisha na kifo. Mathalani Kilio ni lugha inayozungumzwa na kueleweka na wote wakati wa ajali na kifo. Binadamu anasononeka sana na kujiuliza, kwa nini maisha yanakoma. Namna mbalimbali za kutafuta ufumbuzi wa fumbo la kifo unajieleza katika Ngano, katika sanaa hata katika ngoma za makabila yetu. Ngano na sanaa mbalimbali zinafumba siri kuu ya uzima na tamati ya binadamu yaani kifo. Ngano na hadithi nyingi za Waafrika zinahusiana na kifo na maisha baadaye. Ngano hizo zinapata uzito zaidi katika imani kwa mahoka na Mulungu (Mungu). Lakini Mungu huyo anajulikana kwa Sifa zake tu kama vile Mulungu au Muwulunga yaani muumbaji au mtengenezaji. Wengine wanamwita Chapanga (mpangaji), Wengine Mwene (Mwenyewe au Mwenyezi).

Kutokana na imani hiyo kwa Mungu na Mahoka, Mbantu anatambua kwamba tunapokufa tunarudi nyumbani kujiunga na Muumbaji wetu pamoja na mahoka waliotutangulia. Jibu hili nalo lina udhaifu mkubwa kwa vile hatujui huko nyumbani ni wapi na kupoje. Wamisri walijaribu kulipatia utatuzi suala la kifo kwa kuyahifadhi maiti isioze. Wakayaita Mumiani. Lengo lao kuu ni kukisimanga kifo. Kwamba hata kama kimemchukua mpendwa wao, lakini wao wanaweza bado kumhifadhi na kuendelea kukaa na mfu wao (maiti). Kwa hiyo kifo kimekula kwake! Lakini wasijue kwa kufanya hivyo ndiyo kwanza walikuwa wanakienzi kifo kwa kukijengea makumbusho au sanamu. Wasumeri na Wamesopotamia wao walikuwa na Ngano (myths) walizosimuliana ili kujaribu kujua  kinatokea nini baada ya kifo. Wao waliamini kwamba mtu akifa na kuiacha dunia hii anaenda katika ulimwengu ambao hawezi tena kurudi duniani. Lakini hawakujua anaenda wapi na ulimwengu huo hawakujua uko wapi.

Wabudha wanaamini kuwa kifo ni mzunguko wa maisha, yaani kufa na kuzaliwa tena. Lakini kuhusu mahali na namna ya kuzaliwa inategemea unavyoishi sasa kama vizuri au vibaya. Fikra hizi ni sawa na Ngano za kukitania kifo. Hakuna anayeweza kuzishuhuda kwa maisha halisi. Ngano (myth) za Wagiriki zinasimulia juu ya mtu wa ajabu aitwaye Orfeo. Huyo Orfeo alikuwa mwanamuziki mahili. Aliweza kupiga kinubi na kuvuta milima, mawe, miti, wanyama, ndege hata wadudu kufika kumsikiliza na kucheza muziki wake. Lakini Orfeo mwenyewe baadaye alikufa akashindwa kabisa kukitawala kifo. Fasihi yake ni kwamba binadamu anaweza kutumia ufundi wake wote kuvuta na kutawala akili na kukonga vionjo vya watu na viumbe vyote vikavutika kwake, lakini hawezi kamwe kukitawala kifo. Kadhalika Wanafalsafa wa Kigiriki kama vile Sokrates, Aristotle walishindwa kulijibu swali hili, bali walijua hatima yao ni kaburi.

Wayahudi (Israeli) walijua kwamba baada ya kufa watu wanashuka kuzimu Sheol au Shaal maana yake kuita. Sheol kuna mizimu na maisha yake hayana maana kwani huko huwezi kumsifu Mungu. Wayahudi wanamwabudu Mungu kusudi awaongoze na kuwapa furaha hapahapa ulimwenguni. Fikra hii inatufundisha jinsi gani inatubidi kuyapatia umuhimu maisha ya ulimwengu huu. Kwa mara ya kwanza wazo la Ufufuko kwa Wayahudi linaibuka katika Kitabu cha Danieli (170 KK) walipoanza kuzungumza juu ya hatima ya mashahidi na watu wenye haki yaani walioshika Tora kiaminifu na hatima ya waovu atakapofika Masiha. Jibu likawa kwamba wenye haki watafufuka kutoka sheol na kushiriki furaha ya ufalme wa Mungu lakini katika maisha haya haya. Waovu wataachwa wasote huko huko sheol. Ndivyo alivyofahamu Mafarisayo hata Marta alipomjibu Yesu: “Mimi ninajua kwamba kaka yangu Lazaro atafufuka siku ya mwisho.”

Wazaburi walilijibu swali la hatima ya binadamu kwa tenzi za kumsifu Mungu. Hapana mwanadamu hana tena ujanja! Katika sala walijisikia kuwa wao ni hasid yaani wapendwa wa Mungu. Kwa hiyo waliamini kuwa wapendanao hawaachani kamwe: “Maana hutaacha roho yangu kuzimu, wala hutamwonesha uharibifu anayekuaminia. Utanionesha njia ya uzima, utanipa shibe na furaha, kuume kwako nitastarehe milele.” (Zab 16:10-11). Hata hivyo, fikra hizo za mzaburi zilikuwa za kuungana na Mungu katika maisha haya haya baada ya kifo. Kadhalika Masadukayo tunaowasikia leo katika Injili, wao hawakusadiki kabisa juu ya ufufuko. Wasadukayo ni makuhani waliojisikia kuwa ni washenga kati ya Mungu na watu. Sala na sadaka walizotoa zilikuwa kwa ajili ya kumwomba Mungu awabariki waendelee kuwa matajiri na kuishi vizuri hapa hapa duniani kwani walijua baada ya kifo wataenda Sheol. Kwa hiyo mahusiano yao na Mungu yaliishia “mtukula” yaani kiuchumi ili mkono uende kinywani. Wengine wakasema, eti ponda mali kufa kwaja! Taabu kweli kweli!

Katika kipengele hiki inapoingia fikra za ulimwengu wetu wa sanaa, wa michezo na sherehe. Baada ya yote hayo unaitwa “kufabasi., wengine wanachombeza eti "kufa kunoga".  Kwa hiyo, inabidi kutoa heshima kwa mfu kwa kumjengea kaburi zuri kwani hapo ndiyo umefika. Leo Masadukayo hao wanamwendea Yesu na kumwuliza swali juu ya kifo na ufufuko kama wanavyojua Waisraeli wote. Wakaibua Ngano (simulizi) ya ndoa ya Sara Tobia kuhusu mwanamke aliyeolewa na wanaume saba. Yaani, endapo ufufuko maana yake ni kurudi tena katika maisha haya ya kuoana, basi siku ya ufufuo hapatakalika. Yesu akawajibu: “Wana wa ulimwengu huu huoa na kuolewa, lakini wale wanaoingia katika ufalme wa Mungu ujayo, hao wako katika ufufuko wa wafu, hao ni kama malaika, hawaoi wala kuolewa.” Wasadukayo hao walishindwa kuelewa kwamba maisha yajayo ni tofauti kabisa na maisha ya hapa duniani. Katika ufufuko Yesu harudi tena kukaa duniani na mwili wa utukufu wa kibinadamu, bali anaenda Sheol na mwili wa utukufu ili kuwahamisha wafu wote na kupitiliza kwenda nao kwenye ulimwengu wa Mungu.

Ndiyo maana siku ya ufufuko wa Yesu wanawake wanapofika kaburini walikutana na kijana, anayewaambia: “Yesu aliyesulibiwa hayuko hapa, na siyo Yeye tu, bali hakuna kilichobaki hapa, kwani yeye na waliokuwa hapa wameenda maisha mengine. Wameingia katika ulimwengu wa milele wa Mungu.” Hapa Yesu kwanza anatupatia maana ya maisha haya, halafu anatoa hatima ya maisha haya kuwa ni maandalizi ya maisha ya milele ambayo tutayaishi katika ulimwengu wa Mungu. Pili, Yesu anabainisha ukweli huo kwa kurejea kwenye ulimwengu wa kibiblia (Kutoka 3) ambapo wako wengi walioishafufuka na kuingia katika ulimwengu wa Mungu. Anamtaja Mungu wa Ibrahimu, Mungu wa Isaaki na Mungu wa Yakobo. Huyo siyo kamungu fulani ka pahala fulani. La hasha, bali ni Mungu wa watu hai wasiokufa. Kama watu hao wanakufa basi hata Mungu wao ni wa maiti.

Lakini kama ni Mungu wa wazima basi huyo hawezi kuwaacha marafiki (Mahasid) na waswahibu wake waozee kaburini. Kwa hiyo “Kama Mungu yuko basi sitakufa.” Kumbe Kristo amekuja kubatiza imani yetu kwa Mungu na kwa Mahoka. Jibu la uhakika la hatima ya binadamu limedhihirika katika ufufuko wa Yesu. Katika Kristu, uzima wa kweli na wa milele umeingia katika mwili huu unaokufa. Tumsifu Yesu Kristo!

07 November 2019, 16:36