Jumuiya ya watu wa Mungu kutoka DRC inasherehekea Jubilei ya Miaka 25 ya umoja na mshikamano wa kiimani Jimbo kuu la Roma. Jumuiya ya watu wa Mungu kutoka DRC inasherehekea Jubilei ya Miaka 25 ya umoja na mshikamano wa kiimani Jimbo kuu la Roma. 

Jumuiya ya watu wa Mungu kutoka DRC: Jubilei ya Miaka 25 ya Umoja

Ibada hii ya Misa Takatifu ni kumbu kumbu ya Jubilei ya Miaka 25 tangu Jimbo Kuu la Roma lilipowakabidhi watu wa Mungu kutoka DRC, Kanisa la “Natività” ili kuweza kukutanika ili kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa. Hii ilikuwa ni mwaka 1994. Papa Francisko anapenda kuwatia shime katika imani, matumaini na mapendo, ili kweli waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa unjilishaji.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko kwa kuguswa na mateso pamoja na mahangaiko ya watu wa Mungu nchini Jahuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Congo, DRC, Jumapili ya kwanza ya Kipindi cha Majilio, yaani tarehe 1 Desemba 2019, majira ya saa 4: 00 kwa saa za Ulaya ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya watu wa Mungu nchini DRC, kama sehemu ya hija ya faraja na matumaini kwa Mungu nchini DRC ambao kwa miaka ya hivi karibuni wamepitia vipindi vigumu vya vita, kinzani, migogoro, majanga pamoja na milipuko ya mbali mbali ya magonjwa. Baba Mtakatifu anapenda kusali ili kuwatia shime watu wa Mungu kutokukata tamaa, bali waendelee kujiaminisha chini ya ulinzi na tunza ya Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo! Ibada hii ya Misa Takatifu ni kumbu kumbu ya Jubilei ya Miaka 25 tangu Jimbo Kuu la Roma lilipowakabidhi watu wa Mungu kutoka DRC, Kanisa la “Natività” ili kuweza kukutanika ili kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa. Hii ilikuwa ni mwaka 1994 na tangu wakati huo, viongozi kadhaa wameitembelea na kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu.

Familia ya Mungu kutoka DRC imekuwa ni kielelezo makini cha mchakato wa uinjilishaji wa tamaduni na utamadunisho wa Injili hata nje ya DRC. Watu wengi wanavutwa kushiriki Ibada ya Misa Takatifu kwa sababu ni chemchemi ya furaha, imani, matumaini na mapendo yanayobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Adhimisho la  Fumbo la Ekaristi Takatifu chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa ni kiini cha Parokia. Kimsingi, Fumbo la Ekaristi Takatifu linaadhimishwa siku ya Bwana; Jumuiya ya waamini inapopata nafasi ya kusikiliza, kutafakari Neno la Mungu na hatimaye, kutumwa kutangaza na kushuhudia matendo makuu ya Mungu katika uhalisia wa maisha yao, kama kielelezo cha imani ntendaji! Neno Parokia, linapata asili yake kutoka katika lugha ya Kigiriki yaani “παρоικια” maana yake “Ujirani”. Baba Mtakatifu anakaza kusema, Parokia ni kitovu cha maisha na utume wa Kanisa, mahali pa kuinjilisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu, tayari kutoka kifua mbele kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili; huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. 

Baba Mtakatifu Francisko anawataka waamini kuwa daima tayari kujisadaka kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia tunu msingi za  Kiinjili; huku wakikesha na kusali, ili Bwana wa mavuno atakapokuja awakute wakiendelea na kazi na hapo wataweza kuona matunda ya jasho lao. Ni katika muktadha huu kwamba, historia ya vikundi vya uinjilishaji parokiani inaweza kueleweka kwani hadi wakati huu, vimeenea sehemu mbali mbali za dunia, huku vikijitahidi kufuata mwongozo na dira ya Kristo Mfufuka bila ya woga wala makunyanzi licha ya matatizo na changamoto wanazokumbana nazo katika mchakato mzima wa uinjilishaji. Pale wanapojisikia kuwa ni mitume wamisionari, hapo wanapata ari na mwamko mpya, kwani wanafarijiwa na kutiwa nguvu na Roho Mtakatifu, ili kamwe wasitindikiwe katika shida na mahangaiko yao ya ndani. Jumuiya ya waamini kutoka Congo DRC, imekuwa pia mstari wa mbele kutafuta na kuombea amani; kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za Kanisa Katoliki DRC katika mchakato wa kutafuta: haki, amani, maridhiano, ustawi na maendeleo ya wengi.

Mkataba wa Amani wa San Silvestro uliotiwa sahihi kunako tarehe 31 Desemba 2016 ulipaswa kuheshimiwa na pande zote zinazohusika. Itakumbukwa kwamba, Mkataba huu ulipania kurejesha tena demokrasia na utawala wa sheria baada ya Rais Joseph Kabila kung’ang’ania madarakani hata baada ya muda wake kisheria kuwa umekwisha! Kulikuwa kuna haja kwa Serikali pamoja na wadau mbali mbali kuhakikisha kwamba, wanaunda mazingira ambayo yangepelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2018 kuwa huru, haki na wa amani, ili kuwawezesha wananchi wa DRC kutekeleza haki yao ya kikatiba kwa kushiriki kikamilifu katika mchakato mzima wa uchaguzi uliopaswa kuleta mageuzi makubwa katika mfumo mzima wa demokrasia nchini humo! Kamati Maalum ya Waamini Walei nchini DRC, CLC, iliitaka familia ya Mungu nchini humo, kusimama kidete, bila kusinzia, ili haki iweze kutendeka na demokrasia kushika mkondo wake, bila wajanja wachache kutaka kuvuruga amani kwa kuiba kura.

Hii ni changamoto inayotolewa na Kamati hii wakati ambao zoezi zima la kuhesabu kura za uchaguzi mkuu uliofanyika nchini humo, tarehe 30 Desemba 2018 likiwa linaendelea. Kamati Maalum ya Waamini Walei Nchini DRC katika kipindi cha mwaka 2018 iliandaa maandamano makubwa ili kumshinikiza Rais Joseph Kabila kuondoka madarakani baada ya kukosa sifa ya kuongoza nchi kikatiba. Hatimaye, Rais Joseph Kabila akang’atuka  kutoka madarakani baada ya kuiongoza DRC kwa kipindi cha miaka 17. DRC ikaanza kipindi cha  mwaka 2019 kwa mapinduzi ya kidemokrasia kwa kubadilishana madaraka kwa njia ya kidemokrasia, tukio la kihistoria, kutendeka tangu mwaka 1960 DRC ilipojipatia uhuru wake kutoka kwa Ubelgiji!

Papa: Misa DRC
30 November 2019, 09:43