Vatican News
Chama cha Huduma ya Uamsho wa Kikatoliki nchini Italia, RnS ni chombo cha Huduma ya Uinjilishaji unaofumbatwa katika ushuhuda! Chama cha Huduma ya Uamsho wa Kikatoliki nchini Italia, RnS ni chombo cha Huduma ya Uinjilishaji unaofumbatwa katika ushuhuda! 

Chama cha Huduma ya Uamsho wa Kikatoliki: Chombo cha huduma!

Pentekoste endelevu katika maisha na utume wa Kanisa iwasaidie wanachama wa Chama cha Uamsho wa Kikatoliki nchini Italia, RnS., kukuza na kudumisha: tunu msingi za maisha ya ndoa na familia; mawasiliano yanayowajibisha. Wawe ni chachu inayochachusha malimwengu kwa njia ya utakatifu maisha; na hatimaye, chumvi inayoganga na kuponya madonda ya watu wa Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Chama cha Uamsho wa Kikatoliki nchini Italia, RnS., kuanzia tarehe 31 Oktoba hadi tarehe 3 Novemba 2019 kinakutana huko mjini Rimini, Italia, ili kuadhimisha mkutano wake wa 43 unaosindikizwa na kauli mbiu “Watu wote watawatambua ya kuwa ninyi mmekuwa wanafunzi wangu, mkiwa na upendo ninyi kwa ninyi” (Yoh. 13:35): Kuinjilisha na kupendana”. Kardinali Gualtiero Bassetti, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI, katika ujumbe wake kwa ajili ya maadhimisho haya anasema, hiki ni kipindi maalum cha kupyaisha utekelezaji wa sera na mikakati ya shughuli za kichungaji kuanzia mwaka 2019 hadi mwaka 2022. Hiki ni kipindi cha kuendelea kujizatiti katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji mpya. Huduma hii inakwenda sanjari na utume wa kusikiliza, kulitafakari na hatimaye, kumwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha, daima wakijitahidi kufuata maongozi ya Roho Mtakatifu.

Karama na mapaji ya Roho Mtakatifu ni kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Injili ya upendo kwa watu wa Mataifa. Ikumbukwe kwamba, matunda ya Roho Mtakatifu ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wote wa Mungu. Kardinali Gualtiero Bassetti, anakaza kusema, Pentekoste endelevu katika maisha na utume wa Kanisa iwasaidie wanachama wa Chama cha Uamsho wa Kikatoliki nchini Italia, RnS., kujielekeza zaidi katika kukuza na kudumisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia; changamoto, matatizo na fursa za mawasiliano ya jamii, ili kweli waweze kuwa ni chachu inayochachusha malimwengu kwa njia ya utakatifu maisha; waamini wawe ni chumvi inayoganga na kuponya madonda ya watu wa Mungu, ili hatimaye, waweze kuonja furaha ya Injili katika uhalisia wa maisha na hivyo kuondokana na ndoto za mchana. Hii ni fursa ya kusali na kutafakari kuhusu: Sheria, Huruma ya Mungu, Utume wa Kanisa, Huduma ya Injili ya Upendo, Ukuaji wa kiutu na maisha ya kiroho, ili yote haya yaweze kuelekezwa kwa walengwa.

Wanachama wanakumbushwa kwamba, Roho Mtakatifu “huvuma apendako”, ili kuwakirimia watu maisha mapya yanayosimikwa katika tunu msingi za maisha ya Kiinjili kama ilivyokuwa kwa Nikodemo, kwani kuna haja ya kuzaliwa upya kwa “Maji na Roho Mtakatifu”. Waamini wajiaminishe kwa Roho Mtakatifu, ili waweze kuwa huru zaidi. Kuinjilisha na kupenda ni chanda na pete, kwani ni mambo yanayopaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha na vipaumbele vya watu. Kama waamini wanaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa. Wawe tayari kupokea na kuambata mafanikio makubwa, lakini pia wasisahau kwamba, wanaweza kukumbana na mateso na madhulumu katika ushuhuda wao. Kwa njia ya karama na mapaji ya Roho Mtakatifu, wanachama wa Chama cha Uamsho wa Kikatoliki nchini Italia, RnS, wawe tayari pia kukabiliana na changamoto na matatizo mbali mbali; ili wanapoyavuka kwa ari na moyo mkuu waweze kuwa ni mashuhuda na vyombo vya Injili ya upendo.

Kwa upande wake Dr. Salvatore Martinez, Rais wa Chama cha Huduma ya Uamsho wa Kikatoliki nchini Italia, RnS., anasema, wale wote walioitikia kuwa wafuasi wa Kristo kwa kipindi cha miaka minne yaani kuanzia mwaka 2019- 2022, wawe tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa Mungu na jirani zao. Mkutano huu unahitimisha maadhimisho Mwezi Oktoba 2019, ambao ulikuwa umetengwa maalum na Mama Kanisa kwa ajili ya kuhamasisha ari na mwamko wa kimisionari duniani, kwa mwaka huu 2019, Kanisa linapo endelea kuadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu Papa Benedikto XV alipochapisha Waraka wa Kitume "Maximum Illud" yaani “Kuhusu Shughuli za Kimisionari. Dr. Salvatore Martinez ametoa ushuhuda wa jinsi ambavyo Roho Mtakatifu anavyoendelea kutenda kazi katika maisha na utume wa Kanisa sehemu mbali mbali za dunia, licha ya uwepo wa changamoto za kimisionari. Huu ni muda wa kuinjilisha, kupendana na kuhudumia kwa upendo thabiti.

Historia ya Chama cha Huduma ya Uamsho wa Kikatoliki nchini Italia, inapambwa kwa tunu msingi za Kiinjili. Licha ya mapungufu katika maisha na utume wake, lakini bado Chama hiki kimekuwa ni muujiza wa upendo wa Mungu kwa waja wake. Upendo wa Mungu unawawajibisha kupendana wao kwa wao, kielelezo na ushuhuda wa utakatifu unaopata chimbuko lake kutoka kwa Roho Mtakatifu.

Uaamsho wa Kikatoliki
01 November 2019, 13:54