Tafuta

Askofu mkuu Nkwande asema: Kwa sasa vipaumbele ni wongofu wa kichungaji, kimisionari na malezi makini kwa waseminari na mapadre. Askofu mkuu Nkwande asema: Kwa sasa vipaumbele ni wongofu wa kichungaji, kimisionari na malezi makini kwa waseminari na mapadre. 

Askofu mkuu Nkwande: Wongofu wa kichungaji, kimisionari na malezi

Askofu mkuu Renatus Leonard Nkwande amezindua rasmi Mwaka wa masomo 2019 – 2020 kwa Seminari Kuu ya Mtakatifu Karoli Lwanga, Segerea, ikiwa na jumla ya Majandokasisi 177 na walezi wao 12 ; Amebariki na kuzindua nyumba ya Mapadre iliyofanyiwa ukarabati mkubwa pamoja na kutoa madaraja madogo madogo kwa Mafrateri Seminarini hapo. Wamempongeza kwa Daraja!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Wakati umefika wa kupyaisha ari, mwamko wa utume na shughuli za kimisionari na kichungaji katika maisha ya kiroho, kijamii na kikanisa. Mwongozo wa Malezi ya Kipadre “Ratio Fundamentalisi Institutionis Sacerdotalis” yaani “Zawadi ya wito wa Kipadre” unafafanua mambo msingi yanayopaswa kuzingatiwa na Makanisa mahalia katika mchakato wa malezi na majiundo ya kipadre. Ni mwongozo makini unaotoa sheria, kanuni na taratibu zinazopaswa kutekelezwa katika safari ya malezi ya awali kwa majandokasisi na majiundo endelevu kwa wakleri. Mkazo umewekwa katika majiundo ya maisha ya kiroho kwa kujikita katika ujenzi wa utamaduni wa kusoma, kutafakari na kumwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha. Mababa wa Kanisa wanakazia umuhimu wa maisha ya Kisakramenti; Mafundisho Tanzu ya Kanisa bila kusahau malezi  na majiundo ya kiakili, kiutu na kichungaji. Yote haya yakitekelezwa kwa umakini mkubwa, wakleri, watawa na waamini walei wataweza kutekeleza dhamana na wajibu wao katika umoja, upendo na mshikamano unaowawezesha kufanya kazi kama kikosi cha ushindi kinachofumbatwa katika wongofu wa shughuli za kichungaji na kimisionari.

Hivi karibuni, Baba Mtakatifu Francisko aliwataka wakleri na watawa wawe na ujasiri wa kupambana na changamoto mamboleo, zinazoibuliwa kutokana na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano ya jamii. Wawe ni watu wenye matumizi sahihi na yanayowawajibisha katika matumizi ya vyombo vya mawasiliano. Vyombo hivi wakati mwingine, vinaweza kuharibu utu na heshima ya watu; kwa kuchafua maisha ya kiroho pamoja na kujeruhi maisha ya utu na kidugu katika jumuiya. Wakleri na watawa wajitahidi kujifunza kutumia vyombo vya mawasiliano ya jamii kwa ubunifu mkubwa ili kusaidia mchakato wa uinjilishaji. Ni katika muktadha huu, Askofu mkuu Renatus Leonard Nkwande wa Jimbo kuu la Mwanza, Tanzania, hivi karibuni amezindua rasmi Mwaka wa masomo 2019 – 2020 kwa Seminari Kuu ya Mtakatifu Karoli Lwanga, Segerea, iliyoko Jimbo kuu la Dar es Salaam, ikiwa na jumla ya Majandokasisi 177 na walezi wao 12 wanaoendelea kujisadaka ili kuwafunda mafrateri hawa barabara!

Takwimu zinaonesha kwamba, idadi ya mafrateri kwa mwaka 2019-2020 ni kubwa kuwahi kutokea Segerea tangu kuanzishwa kwake na Kardinali Polycarp Pengo, kunako mwaka 1979. Askofu mkuu Nkwande ametumia nafasi hii hadhimu kubariki na kuzindua nyumba ya mapadre iliyofanyiwa ukarabati mkubwa baada ya ajali ya moto iliyotokea hapo tarehe 16 Januari 2019 na kusababisha uharibifu mkubwa wa majengo na mali za mapadre walezi Seminarini hapo. Hii imekuwa pia ni nafasi kwa Jumuiya ya Seminari Kuu ya Segerea kumpongeza Askofu mkuu Nkwande aliyeteuliwa na hatimaye kusimikwa kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Mwanza. Askofu mkuu Renatus Leonard Nkwande amewataka wakleri na watawa kujikita katika wongofu wa shughuli za kichungaji unaotoa kipaumbele cha kwanza katika maisha na utume wa Kanisa, ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mungu nchini Tanzania.

Huu ni mwaliko wa kuondokana na mazoea ya kutoa huduma kwa “kujifungia ndani ya Parokia”. Umefika sasa wakati kwa Mapadre kutoka huko Sakristia wanakojichimbia na kuanza kuchakarika kwa ajili ya kuwatangazia watu Injili ya furaha, inayosimikwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Wongofu wa kichungaji unajielekeza zaidi katika kuwahudumia watu wa Mungu katika familia zao, mahali pao pa kazi, bila kusahau mateso na mahangaiko ya watu wao kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu katika maisha na utume wake. Huko ndiko wanakopaswa kwenda kuzima kiu ya uwepo endelevu wa Kristo Yesu kwa waja wake. Inasikitisha kuona wakleri wakiwa wamebweteka Parokiani kwa kusoma magazeti, kuangalia luninga pamoja na matumizi mengine ya mitandao ya kijamii. Maendeleo haya ya teknolojia yasaidie mchakato wa uinjilishaji mpya, ili Neno la Mungu liwafikie na kuwagusa huko huko kwenye “vijiwe na maskani yao”.

Kwa ufupi huu ndio wongofu wa shughuli za kichungaji na kimisionari unaopewa kipaumbele cha pekee kwa wakati huu, ili kuliwezesha Kanisa kuendelea kusoma alama za nyakati! Roho Mtakatifu ni Nafsi ya tatu katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, Mungu mmoja. Ni jina halisi la yule ambaye Kanisa linamwabudu na kumtukuza pamoja na Baba na Mwana. Kanisa limempokea Roho Mtakatifu kutoka kwa Kristo Yesu na lina muungama katika ubatizo wa watoto wake wapya wanaozaliwa kwa maji na Roho Mtakatifu.  Roho Mtakatifu ni mfariji, msaidizi na ni mtakasaji. Ni Roho wa Bwana, kidole cha Mungu na Roho wa Mungu. Roho Mtakatifu yupo tangu hata kabla ya nyakati akitenda kazi katika umoja na Baba na Mwana. Roho Mtakatifu ni mhimili mkuu wa mchakato wa uinjilishaji. Askofu mkuu Renatus Leonard Nkwande ni tunda kutoka Seminari kuu ya Segerea. Ametumia fursa hii kuwataka walezi kuhakikisha kwamba, wanatoa nafasi ya pekee kwa Roho Mtakatifu, ili Kanisa la Mungu liweze kuongezeka kwa idadi na ubora kama ilivyokuwa kwenye Kanisa la Mwanzo.

Kanisa litaendelea kuombea miito, lakini pia walelewa na walezi wanapaswa kuacha nafasi kwa Roho Mtakatifu ili aweze kuwaunda na kuwafunda majandokasisi kadiri ya mahitaji ya Kanisa mahalia kwa wakati huu. Ili kutekeleza dhamana na utume huu, wanapaswa kuwa wanyenyekevu, vinginevyo watajikuta wanatumia nguvu kubwa na akili nyingi, lakini matokeo yake ni “kiduchu”. Uwepo wa Askofu mkuu Nkwande umechochea matumaini mapya kwa majandokasisi kwamba, inawezekana kufikia “utimilifu” wa Daraja Takatifu ya Upadre, ikiwa kama watajiaminisha chini ya ulinzi na maongozi ya Roho Mtakatifu. Baba Mtakatifu Francisko katika barua binafsi “Motu Proprio” “Aperuit Illis” anasema, “Dominika ya Neno la Mungu” inapata chimbuko lake kutoka katika Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu, chimbuko la toba na wongofu wa ndani unaowakirimia waamini upendo, huruma na msamaha wa dhambi zao.

Kwa njia ya Roho Mtakatifu, Mitume walipewa uwezo wa kutangaza na kushuhudia Fumbo la Wokovu. Utambulisho wa Wakristo unafumbatwa kwa namna ya pekee, katika mahusiano ya dhati kati ya: Kristo Mfufuka, Maandiko Matakatifu na Jumuiya ya waamini. Ndiyo maana Mtakatifu Jerome anasema “Kutojua Maandiko Matakatifu ni kutomfahamu Kristo”. Baba Mtakatifu anasema, wazo la kuanzisha “Domenika ya Neno la Mungu” lilimwijia mara baada ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya Huruma ya Mungu, ili kuendeleza majadiliano kati ya Mwenyezi Mungu na waja wake; mwaliko wa kuendelea kulipyaisha Kanisa kwa amana na utajiri unaobubujika kutoka katika Maandiko Matakatifu. Barua hii ni jibu ya kilio cha watu wa Mungu kutoka sehemu mbali mbali za dunia, waliotaka kujenga na kudumisha umoja unaobubujika kutoka katika Maandiko Matakatifu. Ni mwaliko wa kulisoma, kulitafakari na hatimaye, kulimwilisha na kulishuhudia katika uhalisia wa maisha yao.

Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican katika hati yao “Dei Verbum” yaani “Neno la Mungu wanagusia kuhusu “Ufunuo; Urithishaji wa ufunuo wa Kimungu; Uvuvio wa Kimungu na ufafanuzi wa Maandiko Matakatifu; Agano la Kale pamoja na Agano Jipya wanatilia mkazo umuhimu wa Neno la Mungu katika maisha na utume wa Kanisa. Umoja wa Wakristo upate chimbuko lake kwa kusikiliza Neno la Mungu, linalofafanuliwa na wachungaji, kiasi kwamba, hata Mahubiri yanachukuliwa kuwa kama “Kisakramenti” muda muafaka wa kufafanua uzuri wa Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha ya waamini. Makatekisita, wafundwe kikamilifu, ili wawasaidie waamini kukua katika imani kama ilivyokuwa kwa wale wafuasi wa Emmau, waliobahatika kufafanuliwa Maandiko Mtakatifu na Kristo Yesu alipokuwa anatembea pamoja nao njiani.

Askofu mkuu Renatus Leonard Nkwande, amewataka Majandokasisi waliopewa Madaraja mbali mbali katika huduma ya Kanisa na hasa Daraja la Usomaji kuendelea kukuza na kudumisha kipaji cha ubunifu sanjari na kusoma alama za nyakati. Amesema, huko mbeleni kumenoga! Ni wakati wa kujichimbia katika ari na wongofu wa kimisionari, kwa kuwa tayari kuwa wamisionari ndani na nje ya Tanzania. Wawe tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kulinda, kutetea na kudumisha imani, maadili na utu wema. Wawe tayari kujenga na kudumisha dhamiri safi, ili kutoa tafsiri sahihi ya mapenzi ya Mungu na kuyatekeleza. Askofu mkuu Nkwande ameipongeza Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania, WAWATA, kwa sadaka na majitoleo yao kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa na hasa zaidi katika kulitegemeza Kanisa. Askofu mkuu Nkwande, amewataka WAWATA kujifunga kibwebwe kwa ajili ya malezi na makuzi ya watoto wao, ili waweze kuwarithisha pia mambo matakatifu.

Naye Padre Thobias Ndabhatinya, Gambera wa Seminari Kuu ya Segerea, kwa niaba ya Jumuiya ya Segerea amempongeza Askofu mkuu Renatus Nkwande na kumtakia utume mwema kwa familia ya Mungu nchini Tanzania. Amewashukuru watu wa Mungu nchini Tanzania pamoja na wafadhili wote waliochangia kwa hali na mali hadi kufanikisha ukarabati wa nyumba ya mapadre Segerea bila kuwasahau wale wote wanaoendelea kuchangia katika malezi na makuzi ya majandokasisi seminarini hapo!

Askofu Mkuu Nkwande
02 November 2019, 15:27