Kardinali Lorenzo Baldisseri katika hotuba yake ya utangulizi amefafanua kuhusu umuhimu wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia kwa maisha na utume wa Kanisa. Kardinali Lorenzo Baldisseri katika hotuba yake ya utangulizi amefafanua kuhusu umuhimu wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia kwa maisha na utume wa Kanisa. 

Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia: Umuhimu wake kwa Kanisa

Kardinali Lorenzo Baldisseri katika hotuba yake elekezi amekazia zaidi: Umuhimu wa sinodi katika maisha na utume wa Kanisa Ukanda wa Amazonia; Muundo mpya wa maadhimisho ya Sinodi hii; Washiriki; Maandalizi yalivyokwenda; Taratibu za maadhimisho ya Sinodi; Mawasiliano na hatimaye, ni umuhimu wa Sinodi ya ekolojia fungamani. Sinodi ni muhimu katika utume wa Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia kuanzia tarehe 6-27 Oktoba, 2019 yanaongozwa na Kauli mbiu: “Amazonia: njia mpya ya Kanisa na kwa ajili ekolojia fungamani”. Kardinali Lorenzo Baldisseri, Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu katika hotuba yake elekezi wakati wa kikao cha kwanza cha Sinodi, Jumatatu, tarehe 7 Oktoba 2019, amekazia umuhimu wa sinodi katika maisha na utume wa Kanisa Ukanda wa Amazonia; Muundo mpya wa maadhimisho ya Sinodi hii; Washiriki; Maandalizi yalivyokwenda; Mbinu na taratibu za maadhimisho ya Sinodi; Mawasiliano na hatimaye, ni umuhimu wa Sinodi ya ekolojia fungamani. Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia yanafumbata rasilimali na utajiri mkubwa; unaowazunguka watu mahalia kutoka sehemu mbali mbali za dunia; lakini kwa sasa mazingira ya Ukanda wa Amazonia yako hatarini, kumbe, kuna wajibu wa kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote.

Hii ni changamoto kubwa katika maisha na utume wa Kanisa, kumbe, Kanisa linawajibika kuziinjilisha tamaduni ili kuitamadunisha Injili; kwa kusimama kidete ili kukazia ekolojia fungamani. Lengo la Sinodi hii ni kubainisha njia mpya za uinjilishaji Ukanda wa Amazonia, kwa kusikiliza kilio cha Dunia Mama na kilio cha maskini; kwa kupembua matatizo, changamoto na fursa zilizopo ili kutoa mapendekezo yatakayofanyiwa kazi na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Muundo mpya wa maadhimisho ya Sinodi hii unafuata Katiba ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko “Episcopalis Communio” yaani “kuhusu Sinodi za Maaskofu” inayobainisha kwamba, Sinodi ni chombo cha uinjilishaji kinachofumbatwa katika ujenzi wa utamaduni wa kusikiliza, kuadhimisha na kutekeleza kwa umoja. Hatua zote muhimu zimetekelezwa ili kuhakikisha kwamba, kunakuwepo na ushiriki mkamilifu wakati wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia.

Maaskofu wote kutoka Ukanda wa Amazonia wanashiriki kama kielelezo cha dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa. Kuna ushiriki mpana wa Kanisa la Kiulimwengu kwa sababu kiungo kimoja kikiumia, viungo vyote huumia nacho, na kiungo kimoja kikitukuzwa, viungo vyote hufurahi pamoja nacho. Haya ni maadhimisho ya imani ya Kanisa yanayosindikizwa kwa sala za Kanisa zima chini ya uongozi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Hii ndiyo maana ya maandamano ya Mababa wa Sinodi kuanzia kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro hadi kwenye Ukumbi wa Sinodi za Maaskofu. Washiriki wa Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia ni 185; kati yao 137 wanashiriki kutokana na nyadhifa zao; 113 wanawakilisha Majimbo Makuu ya Ukanda wa Amazonia; 13 ni Wakuu wa Mabaraza ya Kipapa pamoja na wajumbe wote wa Baraza la Maandalizi ya Sinodi. Kuna watawa 13 walioteuliwa na Shirikisho la Mabaraza ya Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume Kimataifa na wajumbe 33 ni wale ambao wameteuliwa rasmi na Baba Mtakatifu Francisko.

Kuna wawakilishi wa Makanisa na Jumuiya za Kikristo, ili kuweza kufanya kazi kwa pamoja, kielelezo cha umoja wa Kanisa, ili kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo Yesu, Ukanda wa Amazonia. Kuna wataalam 25 na wasikilizaji 55 pamoja na wawakilishi 16 wa wananchi mahalia. Shughuli zote hizi zinaratibiwa na Askofu Fabio Fabene, Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu. Mchakato wa Maandalizi ya Sinodi Ukanda wa Amazonia: Tarehe 15 Oktoba 2017 Baba Mtakatifu Francisko akatangaza rasmi maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia. Tarehe 19 Januari 2018 Sekretarieti Kuu ya Sinodi za Maaskofu ikakutana kwa mara ya kwanza na “Mtandao wa Kanisa Amerika ya Kusini”, (Pan-Amazon Ecclesial Network of the Latin American Church, REPAM. Tarehe 9 Machi 2018, Baba Mtakatifu akaunda Kamati maalum iliyoandaa “Hati ya Maandalizi ya Sinodi na hatimaye, Hati ya Kutendea Kazi ya Sinodi, “Instrumentum Laboris”. Kuna umati mkubwa wa watu wa Mungu walioshiriki katika mchakato wa maandalizi haya kwa kutambua kwamba, Sinodi hii inagusa pia masuala ya: kisiasa, kijamii, kiuchumi na kitamaduni.

Utamaduni wa kusikiliza ni kipaumbele cha kwanza katika maadhimisho ya Sinodi hii mintarafu mwanga wa Wosia wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko: “Evangelii gaudium” yaani “Furaha ya Injili” na Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Mambo makuu yaliyochambuliwa ni: ekolojia ya mazingira; utamaduni; ekolojia ya kisiasa, kiuchumi; elimu pamoja na tasaufi ya kiekolojia. Tema zote hizi zimesaidia kutengeneza “Instrumentum Laboris” yaani “Hati ya Kutendea Kazi”. Mkutano uliofanyika George Town tarehe 19 - 21 ulitoa mchango mkubwa katika maandalizi ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia. Mbinu na taratibu za maadhimisho ya Sinodi ni kuwawezesha Mababa wa Sinodi kuchapisha Hati ya Sinodi. “Instrumentum Laboris” inatoa mwongozo na vipaumbele vinavyopaswa kuzingatiwa.

Mababa wa Sinodi wanayo fursa ya kuchangia mawazo na mang’amuzi yao katika mkutano mkuu na kwenye mikutano ya vikundi “Circuli minori”. Kutafuatia mchakato wa kuandika Hati ya Mwisho ya Sinodi itakayopigiwa kura, kipengele baada ya kipengele. Mwishoni, Mababa wa Sinodi watawachagua Wajumbe wa Baraza Maalum la Sinodi, watakaokuwa na dhamana ya kumshauri Baba Mtakatifu katika maandalizi ya Wosia wa Kitume, baada ya Maadhimisho ya Sinodi. Baraza la Kipapa la Mawasiliano ndilo lililopewa dhamana ya kusambaza na kutangaza yale yote yanayojiri katika maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia. Hii ni Sinodi ya ekolojia fungamani, tema ambayo imepewa kipuembele cha pekee, ili kusaidia mchakato wa kudhibiti uchafuzi mkubwa wa mazingira kwa kulinda na kudumisha utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Mawasiliano ya nyaraka muhimu yanafanyika kwa njia ya mtandao, ili kuokoa gharama za uchapishaji. Hii ni sehemu ya mchakato wa wongofu wa kiekolojia unaotekelezwa kwa vitendo.

Hotuba Elekezi
07 October 2019, 16:02