Tafuta

Vatican News
Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili 29 ya Mwaka C wa Kanisa: Sala inasimikwa katika imani, matumaini na mapendo yanayomwilishwa katika fadhila ya unyenyekevu. Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili 29 ya Mwaka C wa Kanisa: Sala inasimikwa katika imani, matumaini na mapendo yanayomwilishwa katika fadhila ya unyenyekevu. 

Tafakari Jumapili 29 Mwaka C: Sala inamwilishwa katika haki!

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya 29 ya Mwaka C wa Kanisa ni mwaliko kwa waamini kusali bila kuchoka pamoja na kuhakikisha kwamba, wanaimwilisha sala yao katika matumaini kwa Mungu anayeganga, anayeponya na kuwaokoa wale wote waliokimbilia ulinzi na tunza yake ya kibaba. Waamini wajenge utamaduni wa kujiaminisha kwa Mungu katika maisha yao ya kila siku.

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

UTANGULIZI: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News karibu katika tafakari ya Neno la Mungu. Tunatafakari leo masomo ya dominika ya 29 ya Mwaka C wa Kanisa, dominika ambayo pia Kanisa linaadhimisha Siku ya Kimisionari ulimwengu katika mwezi huu ambao ni mwezi wa pekee wa kuhamasisha ari, mwamko na utume wa kimisionari. Maadhimisho haya yanaongozwa na kauli mbiu “Kubatizwa na Kutumwa Kutangaza Injili: Kanisa la Kristo katika Umisionari Duniani. Somo la kwanza (Kut 17:8-13 ) ni kutoka katika kitabu cha Kutoka. Somo hili linatupeleka katika mazingira ambapo Waisraeli wapo safarini kutoka Misri kuelekea nchi yao ya ahadi. Safari hii haikuwa rahisi kwani njiani walikumbana na magumu ya kila aina. Leo wanapita katika mipaka ya taifa la Waameleki. Waameleki hawa wanawazuia kupita na hivi Waisraeli wanalazimika kupigana nao vita wapite na kuendelea na safari yao. Lakini vita hii inaonekana kuwa sio vita ya kawaida kwa sababu ushindi wake unategemea na kuinuliwa juu kwa mikono na fimbo ya Musa. Musa alipoinua mkono wake Israeli ilishinda, alipoushusha Ameleki alishinda.

Sasa ili kuhakikisha mkono wa Musa unabaki umeinuliwa, Haruni na Huri wakamketisha Musa na wao wenyewe wakaishika na kuiinua juu mikono ya Musa hadi vita ilipoisha. Somo hili linaonesha kuwa ni nguvu ya Mungu iliyowatoa Waisraeli utumwani Misri, ikawavusha katika bahari ya Sham na ni nguvu hiyo hiyo ya Mungu inayowaokoa katika magumu mbalimbali wanayokutana nayo katika safari yao ya maisha. Nguvu hii inaoneshwa kwa alama ya fimbo ya Musa. Ni fimbo hii hii ilitumika katika hatua zote hizo. Kitendo cha Musa kuketi na kuinua mikono yake kunaliwakilisha taifa zima la Israeli katika mashusiano yake na Mungu. Pale Israeli anapomwinulia Mungu mikono, yaani kumtegemea, ni hapo ambapo juhudi zake zitampatia mafaniko. Pale anapochoka, yaani anapokengeuka juhudi zake zote ni kazi bure. Ni katika imani hii waliimba Zaburi 124 na kukiri kuwa “kama si Bwana aliyekuwa pamoja na sisi, Israeli na aseme sasa… (adui zetu) wangalitumeza hai hasira ao ilipowaka juu yetu” (rej. Zab 124:1-4).

Somo la pili (2 Tim 3:14- 4:2) ni kutoka katika Waraka wa pili wa Mtume Paulo kwa Timotheo. Paulo katika kifungu cha somo hili la leo anamsisitiza Timotheo kuyashikilia yale aliyofundishwa na yale anayoyaamini. Na anamuagiza ayasimamie hayo bila kutetereka na tena ayafundishe daima iwe ni wakati unaomfaa au ule usiomfaa. Awe pia tayari kukaripia, kukemea na kuonya kila inapolazimu. Timotheo ni mwanafunzi wa Paulo na ni Paulo aliyemsimika kuwa Askofu wa Efeso. Paulo katika uzoefu na mang’amuzi yake ya kichungaji anatambua kuwa wakati mchungaji anaweza kuiagalia jamii yake na akadhani kuwa yale anayoyafundisha hayana uhalisia tena katika jamii hasa kama jamii inazidi kupiga hatua kimaendeleo. Hapa Paulo anamuonya Timotheo asifikiri hivyo. Anamhakikishia kuwa kile alichofundishwa ni kitu sahihi: “maana unajua ni akina nani ambao ulijifunza kwao” na tena anamuonesha kuwa msingi wa mafundisho na mapokeo yote aliyopewa ni Neno la Mungu, “Andiko lenye pumzi ya Mungu ambalo linafaa kwa mafundisho yote”. Kwa maneno mengine Mtume Paulo anamwambia Timotheo ashikilie hapo hapo kwa maana Neno la Mungu halipotezi kamwe umaana wake hata kama jamii inabadilika.

Injili (Lk 18:1-8) Katika Injili ya dominika ya leo ambayo ni kutoka kwa Mwinjili Luka, Yesu anatoa mfano unaomhusu kadhi /hakimu na mwanamke aliyemwendea akiwa na shida. Kazi ya kadhi ilikuwa ni kutatua migogoro kati ya watu na kuhakikisha kuwa kila mtu anapata haki yake. Alipaswa kuwa ni mtu anayewasikiliza watu na kuwa karibu na watu. Mfano tu unapoanza, kadhi huyu anatambulishwa kama mtu asiyekuwa na sifa ya kuwa kadhi kwa maana alikuwa “hamchi Mungu wala hajali watu”. Mjane ambaye hana mtetezi na ambaye tumaini lake pekee la kupata haki lipo kwa kadhi hapewi nafasi ya kusikilizwa. Injili haielezi kama alitaka rushwa au nini lakini hii inathibisha pia kuwa huyu hakuwa kadhi mwema. Lakini baada ya muda kadhi akajitafakari na kuamua kumpa mjane haki yake ili tu asiendelee kumsumbua kwa kumjia mara nyingi.

Ufunguo wa kutafsiri maana ya mfano huu wa Yesu tuaupata katika maneno ya mwanzo na ya mwisho katika Injili hii. Mwanzoni injili inasema “akawaambia mfano ya kwamba imewapasa kumwomba Mungu sikuzote wala wasikate tamaa”. Kwa maneno haya ya utangulizi, anayesikiliza mfano anaalikwa kuusikiliza akijua kuwa unahusu kumwomba Mungu bila kukata tamaa. Mwishoni Yesu anasema “walakini atakapokuja Mwana wa Adamu ataiona imani duniani?” Hili ni hitimisho linalompa changamoto aliyesikiliza mfano huu, kwanza kuona uhusiano uliopo kati ya sala na imani na pia kujiangalia katika wahusika wa mfano aliousikiliza na kutoka na mang’amuzi yatakayomsaidia kuikuza na kuilinda imani yake.

Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News kila mwaka ifikapo mwezi Oktoba, Kanisa huadhimisha mwezi wa umisionari. Ni mwezi ambapo kama kanisa tunajikumbusha kwa namna ya pekee juu ya wajibu wetu wa kuwa wamisionari, yaani wajibu wa kutoka na kwenda kuhubiri Habari Njema ambao ni wajibu wa kuwa wainjilishaji. Siku yenyewe ya maadhimisho huwa ni dominika inayotangulia dominika ya mwisho ya mwezi wa kumi. Kwa mwaka huu, mwezi huu wa umiosionari umekuwa ni mwezi wa pekee kwa sababu ni mwaka wa 100 tangu Papa Benedikto XV alipotoa fundisho kuu la umisonari katika barua yake ya kitume “Maximum illud” mwaka 1919. Hivyo tunalenga kujitafakari tupo wapi katika kuyaishi mafundisho hayo ya kinabii yaliyotolewa miaka 100 iliyopita.

Kauli mbiu ya mwaka huu ni kuwa “Tumebatizwa na Kutumwa: Kanisa la Kristo katika Umisionari Duniani”. Katika kauli mbiu hii Baba Mtakatifu Francisko anatualika kujitafakari upya na kuchochea moyo wa umisionari katika kanisa kama wajibu tuliopewa kwa ubatizo wetu kwa ajili ya wokovu wetu na wa dunia nzima. Maadhimisho haya yanalenga kutupa nafasi ya kujiuliza, katika mazingira yetu ya leo tunaweza kutekeleza vipi utume wetu huu wa umisionari? Katika mazingira yetu tunawaona wachungaji na waamini wa madhebu mbali mbali ya Kikristo wakitembea nyumba kwa nyumba kutafuta wafuasi, wakiaandaa mikutano, wakisambaza vipeperushi na kadhalika kwa ajili ya kuwaalika watu wajiunge na imani. Huu kwao ni umisionari. Umisionari wetu wakatoliki katika mazingira ya leo ukoje? Ni swali hili la msingi ambalo siku ya leo inatupa nafasi ya kulitafakari ili kwa pamoja tuutwae upya wajibu wetu msingi wa kuwa wainjilishaji ndani na nje ya Kanisa katika mahali ha hali mbalimbali tunazoishi ndani yake. Tufanye hizi kwa maneno, lakini zaidi kwa njia ya ushuhuda wa maisha yetu!

Liturujia J29
19 October 2019, 14:27