Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya 31 ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa inasimikwa katika: Toba, wongofu wa ndani na malipizi ya dhambi kama anavyoonesha Zakayo Mtoza ushuru. Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya 31 ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa inasimikwa katika: Toba, wongofu wa ndani na malipizi ya dhambi kama anavyoonesha Zakayo Mtoza ushuru. 

Tafakari Jumapili 31 Mwaka: Toba, wongofu na malipizi ya dhambi

Zakayo Mtoza ushukuru anatubu na kumwongokea Mungu na macho yake yanafunguliwa, na hivyo kuona dhambi zilizokuwa zinampekenya na akawa tayari kutimiza malipizi kwa kuwasaidia maskini na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii. Waamini wanahamasishwa kumtafuta Mungu na kuwahudumia jirani zao, kama kielelezo cha ushuhuda wa imani tendaji.

Na Padre Paschal Ighondo - Vatican.

Karibu ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, katika tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 31 ya mwaka C wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Ujumbe wa leo ni wokovu umefika kwako usiogope. Somo la kwanza la kitabu cha Hekima ya Sulemani linatupatia jibu la kwanini Mungu anawaacha wadhambi na watu waovu wanaendelea kuishi na tena wakishamiri na wema wakiteseka. Mungu ameviumba na anavidumisha viumbe vyote kwa sababu ya mapendo yake makuu. Kwa sababu ya mapendo hayo anawavumilia wakosefu ili wakitubu dhambi zao awasamehe akisema kuwa, wale wanaokengeuka kutoka katika njia njema Mungu awaonya, akiwakumbusha kwa mambo yale yale wanayokosa, ili waokoke katika ubaya wao, na kumuamini yeye. Lakini wasipotubu mwisho wao ni kuangamia milele.

Somo la Pili, linalotoka katika Waraka wa pili wa Mtume Paulo kwa Wathesalonike, Waraka aliouandika miezi michache tu baada ya ule wa kwanza kwani Wathesalonike walifadhaishwa na madhulumu, mateso na mafundisho ya uongo kuhusu kuja kwa Yesu mara ya pili. Paulo anawakumbusha wathesalonike yale aliyokuwa ametangulia kuwafundisha akiwahakikishia kuwa Kristo atarudi kuwafariji wamwaminio na kuwaadhibu wale wanaowatesa wao. Anawaambia kwamba siku ya Bwana, yaani, siku ya hukumu, haitawafikia mara moja, bali itatanguliwa na matukio mbalimbali ndiyo maana anasisitiza kufanya kazi katika waraka huu akisema asiyefanyakazi na asile kwasababu baadhi yao waliacha kufanya kazi kwa kuamini kwamba Kristo angerudi upesi kuwachukua. Hali hii hata nyakati zetu haijatuacha salama, kila kukicha wanaibuka watabiri wa siku za mwisho hata wengine kuuza tiketi za kwenda mbinguni. Tunaonywa tuchukue tahadhari juu ya mafundisho haya ya uongo.

Injili kama ilivyoandikwa na Luka inakaza kwamba Yesu ni Mkombozi na rafiki wa wakosefu na waliodharauliwa, tena wana wa kweli wa Ibrahimu ni wale wanaotubu kweli dhambi zao na kumsadiki Mungu. Jumapili iliyopita tulitafakari sala ya majuto ya mtoza ushuru ambaye jina lake halikutajwa, lakini alitubu kwa unyenyekevu na kusamehewa makosa yake kinyume na farisayo aliyejikinai, mwenye majivuno na kiburi. Leo tunakutana na mtoza ushuru mwingine maarufu kwa jina la Zakayo. Huyu Zakayo ni Myahudi tajiri, mfupi kwa kimo na mkuu wa watoza ushuru. Kwa kawaida watoza ushuru walikuwa wala rushwa wakubwa kwani walitoza ushuru zaidi ya kiasi kilichowekwa ndiyo maana walipomuuliza Yohane Mbatizaji na sisi tufanyeje? Yohane aliwajibu msitoze zaidi ya kiasi kilichowekwa (Lk.3:12-13). Kwa mtazamo huu Wafarisayo na Waandishi walimtazama Zakayo kama mdhambi mkuu. Halafu kwa Wayahudi, mtu mfupi kama Zakayo alionekana kuwa amelaaniwa na Mungu na hafai kwa kazi yoyote na hawezi kuwa jirani na Mungu.

Myahudi halisi asiye na hila lazima awe mrefu mwenye sura nzuri ya kuvutia kwa sababu hizi ndio maana hawakushughulika kumsaidia Zakayo kumwona Bwana. Kwa mshangao Zakayo anafanya tendo ambalo kwa mtu tajiri na mkuu kama yeye si la kawaida, anaamua kupanda juu ya mkuyu, mti unaoteleza mno, tena kwa haraka ili amuone Yesu. Bwana anatambua nia na kusudi la Zakayo anafika na kumwambia “Zakayo shuka upesi, kwa kuwa leo imenipasa kushinda nyumbani mwako”. Yesu anamtaja kwa jina Zakayo hata kama hajawahi kumwona kabla, pana nini zaidi, hakika alitambua mahangaiko, nia na moyo wa Zakayo ulikua juu Yake. Kwa nini Zakayo alitaka kumwona Yesu? Kwanza Zakayo alisikia habari za Yesu kuwa ni masiha waliyekuwa wakimtamani na kumngoja kwa hamu, pili ni mwokozi, tatu ni mponyaji, nne ni mtenda miujiza, tano umati wa watu uliokusanyika kumsikiliza ulimvuta na kumsukuma kumwona Yesu yupoje na zaidi sana neema ya Mungu iliyokuwa ikimsukuma toka ndani kumwona ili afanye toba ndiyo maana alifurahi mno Yesu alipomwambia ashuke juu ya mkuyu kwani imempasa aingie kwake.

Zakayo mtoza ushuru hakutegemea hata siku moja kumkaribisha nyumbani kwake Masiha, Mtenda miujiza, Mwokozi, Mponyaji na Mhubiri mashuhuri. Tendo hili lilimshangaza lakini alitiwa nguvu na heshima aliyopewa na Yesu Kristo. Manung’uniko ya Waandishi na Mafarisayo hayakumkatisha tamaa bali kumtia nguvu na shauku ya kuchukua hatua kuwaonyesha yeye ni mtu mpya, kwa sababu amempata rafiki mpya mwenye kubadili maisha yake, na ili kuthibitisha hilo anatangaza rasmi nusu ya mali yake anawapa masikini na wahitaji; na yeyote aliyemnyang’anya na kumdhulumu atamlipa mara nne zaidi, tendo hili la kulipa mara nne zaidi ni zaidi ya toba kwani yeyote aliyefanya hivyo alitakiwa kulipa mara mbili zaidi (Kut. 22:4) na kama aliungama wazi alirudisha kile alichoiba na thamani ya moja ya tano ya hicho kitu kilichoibiwa (Wal 6.5, Hes 5:7). Hivi alionyesha kwa vitendo kuwa yeye amekuwa kiumbe kipya. Yaani kuwa mwana wa Abrahamu sio tu kwa rangi na kabila bali mwana halisi wa Abrahamu mwenye toba.

Simulizi hili la kuongoka kwa Zakayo linaletwa kwetu leo sio kama simulizi la kihistoria kwamba lilikuwa bali ni tukio hai kiroho linalotualika sote kumtafuta Bwana. Ikumbukwe kwamba, Kristo Yesu ni ufunuo wa Uso wa huruma na upendo wa Mungu. Yesu anamtaja Zakayo kwa jina sio kwa mapungufu au dhambi zake. Tumeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu naye Mungu amesimika ndani mwetu dhamiri inayotukumbusha uovu wetu pale tunapomkosea kwa dhambi zetu. Mungu hutuonya akitumia mambo ya kawaida kabisa maishani mwetu kwa kuzigusa dhamiri hai zichukie ubaya na kutamani wema wa Mungu. Hivyo ndivyo mtoza ushuru Zakayo alivyoguswa na mafundisho yake Bwana wetu Yesu Kristo akitamaani kuacha ubaya kwa kumwamini Mungu akitenda mema yanayoendana na malipizi ya ubaya wa dhambi kwa Mungu na jirani. Tuige mfano wa Zakayo tulipodhulumu turudishe mara nne na tuwe na moyo wa kuwasaidia maskini kwa mali alizotujalia Mungu. Tumsifu Yesu Kristo.

JP 31 ya Mwaka C
30 October 2019, 15:30