Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya 30 ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa: Kiburi ni kaburi la utu na heshima ya binadamu: Sala inasimikwa katika imani, toba na wongofu wa ndani! Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya 30 ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa: Kiburi ni kaburi la utu na heshima ya binadamu: Sala inasimikwa katika imani, toba na wongofu wa ndani! 

Tafakari Jumapili 30 Mwaka C: Kiburi ni kaburi la utu wa mtu!

Huruma ya Mungu ni zawadi, hatuwezi kuinunua wala kuidai. Huruma ya Mungu tunaipata na kuipokea kwa sharti tu la kujinyenyekesha na kukiri ukosefu wetu mbele ya Mungu katika sakramenti ya kitubio kama mtoza ushuru aliyesimama mbali kwa haya bila kuthubutu hata kuinua macho yake mbinguni, bali alijipiga-piga kifua akisema, Ee Mungu, uniwie radhi mimi mwenye dhambi. SALA!

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Karibu ndugu msikilizaji wa Radio Vatican katika tafakari ya liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 30 ya mwaka C wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Ujumbe wa injili unatoa angalizo kwa wale ambao wamejikinai na kujiona wenye haki, na kuwadharau wengine. Tukumbuke kuwa, “Bwana ndiye mhukumu mwenye haki wala hakijali cheo cha mtu,” YbS 35:12. Somo la kwanza kutoka kitabu cha Yoshua bin Sira latuonya kwamba Mungu hapokei sadaka watoazo matajiri kutokana na sehemu ya mali waliojipatia kwa kuwanyonya na kuwaonea maskini na wanyonge ili kumridhisha, kwani Mungu daima ni mwenye haki, anatetea haki za wanyonge na maskini, anasikiliza sala zao waliodhulumiwa, hayadharau kamwe malalamiko ya yatima, wala ya mjane amwelezapo habari zake. Yoshua bin Sira anasisitiza kwamba malalamiko yake aliyeonewa yatapata kukubaliwa, na dua yake itafika hima mbinguni, kwani sala yake mtu mnyenyekevu hupenya mawingu, wala haitatulia hata itakapowasili, wala haitaondoka hata aliye juu atakapoiangalia, akaamua kwa adili, kutekeleza hukumu. Ndiyo maana mzaburi katika kiitikio cha wimbo wa katikati anakazia kusema, maskini huyu aliita Bwana akasikia.

Katika somo la pili Paulo anahitimisha barua yake ya pili kwa Timotheo kwa maagizo na salamu za mwisho akisema kuwa karibu “atamiminwa” na kwa ajili ya Yesu atakufa. Anasadiki amefanya kazi yake ya kitume vizuri kwa hiyo Mungu atampa tuzo akisema: Nimevipiga vita vilivyo vizuri, mwendo nimeumaliza, Imani nimeilinda, baada ya hayo nimewekewa taji ya haki, ambayo Bwana, mhukumu mwenye haki, atanipa. Paulo yuko mahakamani Roma, haogopi adhabu ya kifo iliyo mbele yake, maana ameweka tumaini lake lote kwa Mungu akisema; Bwana ataniokoa na kila neno baya, na kunihifadhi hata nifike ufalme wake wa mbinguni. Paulo, kisha kusema hayo anawaombea msamaha kwa Mungu wakristo walioiongopea imani na kumuacha peke yake, akisema, wote waliniacha; naomba wasihesabiwe hatia kwa jambo hilo. Katika Injili ilivyoandikwa na Luka, Yesu anakosoa na kusahihisha mtazama wa mafarisayo waliojikinai ya kuwa ni wenye haki, wakiwadharau watu wengine na kufikiri kwamba uhusiano kati ya Mungu na watu ni kama wa kibiashara, kwamba kutimiza tu amri jinsi zilivyo, Mungu atakulipa mbinguni.

Ndiyo maana Farisayo alisali na kuomba moyoni mwake huku amesimama kwa kiburi akisema, Ee Mungu, nakushukuru kwa kuwa mimi si kama watu wengine, wanyang’anyi, wadhalimu, wazinzi, walevi wala kama huyu mtoza ushuru. Mimi nafunga mara mbili kwa juma; hutoa zaka katika mapato yangu yote. Huku ni kujikinai na kujiona mwenye haki mbele za Mungu. Yesu anatufundisha kuwa Huruma ya Mungu ni zawadi, hatuwezi kuinunua wala kuidai. Huruma ya Mungu tunaipata na kuipokea kwa sharti tu la kujinyenyekesha na kukiri ukosefu wetu waziwazi mbele ya Mungu katika sakramenti ya kitubio kama mtoza ushuru aliyesimama mbali kwa haya bila kuthubutu hata kuinua macho yake mbinguni, bali alijipiga-piga kifua akisema, Ee Mungu, uniwie radhi mimi mwenye dhambi. Yesu anasema huyu alishuka kwenda nyumbani kwake amehesabiwa haki kuliko Farisayo kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliywe atakwezwa.

Farisayo hakutazama makosa yake mwenyewe, hakuona udhaifu wake bali mazuri yake tu, tena yawezekana hakufurahia uwepo wa mtoza ushuru, mtu mwenye dhambi hekaluni ndiyo maana anasema wala yeye si kama huyo mtoza ushuru. Tabia ya namna hii ya kuwahukumu wengine inaweza kutupata sisi au tayari tunacho, yaani tunapowaona baadhi ya watu kanisani tunashawishika kudhani kwa matendo yao tunayofahamu fika hawakupaswa hata kufika mazingira ya kanisa. Tukumbuke kuwa, Yesu alikufa Msalabani kwa ajiri ya ukombozi wetu sote. Tena matunda ya dhambi zetu ndiyo sababu ya kuteswa kwake hata kufa Msalabani. Kila binadamu ni mdhambi kwa kiwango chake hivyo hatuna haki ya kukasirikiane kanisani, wala kuwa na kinyongo cha kumpangia Mungu katika kutoa neema na baraka zake. Kumbe tusioneane wivu katika mambo yanayomhusu Mungu. Tunapokuwa katika Sakramenti ya Kitubio Padre mhudumu wa Sakramenti hii katika nafsi ya Kristo anayemwakilisha Mungu, hana haja ya kusikia historia ya mema yetu tufanyayo kwani huo ni ufarisayo.

Ndugu msikilizaji, wala hatupaswi kusimulia mabaya ya watu wengine, isipokuwa tu kwa moyo wa unyenyekevu na majuto kusema wazi bila kuficha wala bila kigugumizi makosa yetu tu. Katika Sakramenti ya kitubio hatufanyi malinganisho ya dhambi, wala uhalalishaji wa dhambi, ila makosa yetu tuliyoyafanya kwa kujua au kutokujua. Mtoza ushuru alijiachia mbele ya Mungu kama alivyo na kama alivyoyatenda makosa yake akiomba huruma na msamaha huku amejawa na hofu ya Mungu kiasi kwamba hakuthubutu hata kuinua macho yake mbinguni, bali alijipiga-piga kifuani mwake akisema, “Ee Mungu, uniwie radhi mimi mwenye dhambi,” Lk 18:13. Hii ndiyo toba ya kweli na aibu juu ya dhambi, lakini sio aibu ya kuziungama. Kutokutaja dhambi unazozikumbuka kwa sababu ya aibu na kuamua kuziweka kwenye kundi la zile ulizozisahau ni kufuru ya Sakramenti ni kumkufuru Roho Mtakatifu na dhambi hii haisameheki kwani Yesu mwenyewe anasema, aliyemkufuru Roho Mtakatifu hatasamehewa,” Lk 12:10. Tukumbuke kuwa Mungu ajua yote, hadanganywi wala hadanganyiki. Tuziungame dhambi zote bila aibu. Tukitambua kuwa hakuna dhambi kubwa mbele ya Mungu ambayo atashindwa kuisamehe, na hakuna dhambi ndogo mbele ya Mungu ambayo hataichukulia maanani.

Daima na bila kiburi tutegemee msaada wa Mwenyezi Mungu. Sala na Kiburi haviendani. Tunaposali tuepuke kiburi. Sala ya Mfarisayo iliambatana na kiburi. Alisali kwa majivuno ya kutafuta sifa hivyo sio mfano wa kuigwa. Tusitegemee Mungu kutukirimia lolote katika kuwaona ndugu zetu hawafai mbele zake, tukumbuke ni Mungu mwenyewe alimtoa mwanaye kufa msalabani kwa ajiri ya dhambi zetu. Tunaposali tuepuke vizingiti vya sala kama ya farisayo vinavyoweza kutufanya tusisali vizuri. Mtume Paulo alifikia hatua ya kutokutishika na jambo lolote ili kuilinda imani aliyoipokea. Ni hatua ya kuishinda hofu na kuukumbatia uzima wa milele ingawa tunajua wote lazima tutakufa. Ni kujiachia katika mikono ya Kristo, na kuacha yeye atende kadiri apendavyo. Ni kutokuwa na shaka lolote juu ya sababu ya kuja kwake Yesu Kristo kwetu, kuteseka kwake, kusulubiwa kwake, kifo chake na ufufuko wake. Mtume Paulo analiweka fumbo hili kwa maneno haya: “Bwana ataniokoa na kila neno baya, na kunihifadhi hata nifike ufalme wake wa mbinguni. Utukufu una Yeye hata milele na milele. Amina,” 2Tim 4:18. Swali la kujiuliza, Je, ninaweza kuyatamka maneno haya bila hofu yoyote ninapokabiliwa na mateso sababu ya imani yangu? Tumsifu Yesu Kristo. 

J30 ya Mwaka C
24 October 2019, 16:16