Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya 30 ya Mwaka C wa Kanisa: Sala ya kweli inamtukuza Mwenyezi Mungu na kumpatia nafasi mwamini kutambua udhaifu wake wa ndani! Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya 30 ya Mwaka C wa Kanisa: Sala ya kweli inamtukuza Mwenyezi Mungu na kumpatia nafasi mwamini kutambua udhaifu wake wa ndani! 

Tafakari Jumapili 30 ya Mwaka: Sala ya Farisayo na Mtoza Ushuru?

Mzizi wa kila dhambi ni majivuno na “kujimwambafai kiroho”. Tunaalikwa kuwa wanyenyekevu ili Mungu atukuzwe katika maisha yetu. Hatuna budi kuepuka kishawishi cha kujimwambafai kiroho na hata katika maisha yetu ya kila siku ili kuweza kupata matunda ya wokovu. Roho ya kifarisayo si tu ilikuwa nyakati zile za Yesu, bali Mwinjili Luka anawalenga waamini wa jumuiya yake na yetu leo.

Don Gaston George Mkude, - Roma.

Amani na Salama. Dominika iliyopita tuliona mfano wa mjane asiyekoma kwenda kwa kadhi dhalimu mpaka pale alipomtatia haki yake, ni mfano wa mmoja anayebaki katika sala kwa imani bila kukoma. Na Dominika ya leo pia dhana hiyo ya sala inazidi kutolea mfano mwingine na Bwana wetu Yesu Kristo kwa mfano wa Farisayo na Mtoza ushuru.  Katika Injili ya Dominika ya leo ni vema kutafakari kwa makini ili kupata ujumbe kusudiwa. Na hasa kuna kishawishi cha kukosa kujitambua nafasi yetu sisi wenyewe mintarafu wahusika hawa wakuu yaani Farisayo na Mtoza ushuru.  Kwa haraka haraka labda hata tunashawishika kuona hakuna la kujifunza kutoka kwa mfarisayo bali tu kwa mtoza ushuru. Hebu tumtafakari mfarisayo anayekwenda kusali hekaluni bila majivuno na kujiinua na kujiabudu mwenyewe kwa maisha yake ya fadhila na badala yake aende akisali na moyo wa udogo na wenye kuhitaji huruma ya Mungu pale hekaluni.

Farisayo anafika kusali ila kwa kweli sala ya kweli ni ile inayomtukuza Mungu na si kujitukuza sisi wenyewe. Ndio kusema Farisayo anakosa kujua maana ya sala na kusali. Kusali daima ni kuzungumza na Mungu, ni kumwinulia mioyo yetu Mwenyezi Mungu ili Mungu atukuzwe katika maisha yetu na si kujinyanyua sisi. Farisayo badala ya kusali kumwelekea Mungu alibaki kujielekea yeye mwenyewe, ni mmoja kwa lugha ya mtaani tungelisema alikuwa anajifukizia ubani mwenyewe badala ya kumfukizia Mwenyezi Mungu. Farisayo walijulikana kuwa watu wenye maisha ya kiroho ya hali ya juu na hata ya kiutu pia kati ya wayahudi. Sheria iliwataka kufunga mara moja ila wao walifunga mara mbili kwa wiki yaani Jumanne na Alhamisi kwa ajili ya toba ya dhambi za wengine ili nao wapate baraka za Mungu.  Mambo ya Walawi 16:29. Na hata walitoa kiaminifu tofauti na makundi ya watu wengine ile moja ya kumi ya mapato yao au zaka kama tunavyozoea leo. Rejea Kumbukumbu la Torati 14:22-27.

Hivyo Yesu si kwamba yupo kinyume au anamkaripia kwa kushika imani na amri za Mungu vema bali ile hali yake ya kujihesabia haki mwenyewe na kukosa kusali sala ya kweli. Mhusika wa pili ni Mtoza ushuru anayebaki nyuma au sehemu ile yenye giza ya Hekalu, ni watu waliochukiwa na hata kuonekana kuwa mbali na Mungu kwani walishirikiana na watawala wageni wa Kirumi katika kuwanyonya Wayahudi. Hapo ni wazi Yesu anawagusa na kuwastua sana wasikilizaji wake, kwani anachagua kama mfano wa kuigwa sio mtu mwema bali wale waliojulikana kuwa waovu na wadhambi na waliochukiwa na watu katika ulimwengu ule.  Si lengo wala nia ya Yesu Kristo kuwa nasi hatuna budi kuiga tabia za yule mtoza ushuru kwa kuibia na kuwadhulumu watu au kuacha kushika sheria na maagizo ya imani yetu kwa kuhofia kuitwa au kulingwanishwa na Mafarisayo. Na ndio maana tangu mwanzo nimewaalika kutafakari vema ili kupata ujumbe kusudiwa wa Yesu Kristo.

Wahusika hawa wawili wa leo tunaona utofauti wao na hapo ndipo kuna ujumbe wa leo wanapofika kusali pale hekaluni. Farisayo narudia tena kusema anataja na kujiinua mwenyewe kwa matendo mema na fadhila anayoishi na hata kujitofautisha na wengine walio wadhambi. Ndio kusema anasali kwa kujielekea yeye mwenyewe na siyo kwa Mwenyezi Mungu. Sio sala ya kweli kwani si sala inayomwelekea Mungu bali anajielekea yeye mwenyewe na kujitukuza na kujipa haki. Kila mara hatuna budi kukumbuka kuwa wokovu wetu unategemea kwa nafasi ya kwanza si kwa matendo yetu mema kama vile tunaupata kwa mastahili hapana, daima ni zawadi ya Mungu kwetu na hivyo nasi hatuna budi kuupokea kwa unyenyekevu. Kamwe tusiingie katika kishawishi kuwa sala zetu au matendo yetu mema ni malipo yetu kwa wokovu utokao kwa Mungu.

Mtoza ushuru anajipiga kifua na kuomba huruma na rehema za Mungu, anasali kwa kutambua udogo na uduni wake mbele ya Mungu, anakiri na kuungama dhambi na makosa yake mbele ya Mungu na kumuomba Mungu msamaha. Sala yake inaonesha kuwa wokovu ni zawadi kutoka kwa Mungu na si mastahili kutokana na matendo yetu mema, kwa hakika pamoja na uovu na dhambi zake kuna japo machache alikuwa anayatenda katika maisha yake, ila haoni hayo na wala kuyakumbuka na kuyataja mbele ya Mungu, badala yake anakiri udogo wake na kuomba huruma ya Mungu. Mtoza ushuru sio mfano mzuri wa mtu anayeshika imani au dini yake bali anabaki kuwa mfano wa mmoja anayetegemea katika huruma na wema wa Mungu kwa wokovu wake. Ni mmoja anayetambua kuwa wokovu sio kwa mastahili yetu hata kama tuna nafasi yetu bali daima mwanadamu hana budi kuona ni zawadi ya Mungu hivyo tunaalikwa kuupokea kwa moyo wa unyenyekevu na udogo.

Wakati Farisayo anasali kujielekea yeye mwenyewe au anajifukizia ubani mwenyewe, anazungumza na nafsi yake, upande wa pili mtoza ushuru anakuwa ni kielelezo cha sala ya kweli. Sala ya kweli ni ya moyo unaopondeka, moyo wa toba, unyenyekevu wa ndani, mazungumzo na Mungu anayejua yote na ndiye asili ya wokovu wetu. Sala ya mnyonge ndio ina nguvu ya kupenya mawinguni na kumfikia Mungu kadiri ya Kitabu cha Hekima ya Yoshua Bin Sira. Imani yetu inaonekana kwa jinsi tunavyosali. (Lex Orandi, Lex Credendi). Sala inaakisi imani na maisha yetu na hasa mahusiano yetu na Mungu, jinsi ile mmoja anasali inaonesha mahusiano yetu ya ndani na Muumba wetu. Hivyo ni katika sala tunaungama na kukiri ukuu na wema wa Mungu kwetu wanadamu ambao tunabaki daima maskini sio kwa kukosa pesa bali tunaotegemea wema na wokovu wake.

Mzizi wa kila dhambi ni majivuno na “kujimwambafai kiroho”. Hivyo leo tunaalikwa daima mbele ya Mungu kwenda na moyo wa udogo na uduni, ili Mungu atukuzwe katika maisha yetu na si kinyume chake. Hatuna budi kuepuka kishawishi cha kujimwambafai kiroho na hata katika maisha yetu ya kila siku ili kuweza kupata matunda ya wokovu.  Roho ile ya kifarisayo si tu ilikuwa nyakati zile za Yesu, bali Mwinjili Luka anawalenga waamini wa jumuiya yake na yetu leo. Kwani hata kati yetu bado kuna nyakati tunakuwa na kishawishi cha kushindwa kuwa na sura halisi ya Mungu. Ni mara kadhaa tunashawishika kuona kuwa wokovu ni kwa mastahili ya matendo yetu mema na kusahau kuwa kwa nafasi ya kwanza ni kwa upendo na wema wa Mungu.  Kishawishi cha kujimwambafai kiroho na kujihesabia haki na kuwadharau wengine na kuona wapo mbali na Mungu na hivyo sala yetu inakuwa si sala ya kweli kwani ni kujinyanyua na kujikweza na kujitukuza sisi wenyewe. Nawatakia tafakari na Dominika njema.

26 October 2019, 15:00