Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya 29 ya Mwaka C wa Kanisa. Mama Kanisa anawaalika waamini kusali kwa imani na matumaini, kwani Mungu anasikiliza na kujibu sala zao kwa wakati wake. Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya 29 ya Mwaka C wa Kanisa. Mama Kanisa anawaalika waamini kusali kwa imani na matumaini, kwani Mungu anasikiliza na kujibu sala zao kwa wakati wake. 

Tafakari Jumapili 29 Mwaka C: Salini kwa imani na matumaini!

Si kwamba Mungu asikilizi sala zetu bali tunaalikwa kusali daima na kubaki wenye imani na matumaini. Sala ye kweli inaambatana na imani ya kweli. Ni shabaha ya Yesu leo kutualika kuwa watu wa sala daima bila kuchoka na tukiwa wenye imani ya kweli kwa Mungu. Hii ni changamoto pia kumwilisha sala katika matendo kwa kutambua kwamba, sala inahitaji udumifu, vinginevyo ni hatari!

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.

Amani na Salama! Kusali au sala sio kumshawishi Mungu atende kadiri ya matakwa yetu bali kumuomba neema zake za msaada ili tuweze kupokea mapenzi yake katika maisha yetu. Kama ndivyo kwa nini basi leo tunaalikwa kusali daima bila kukoma? Nini hasa maana ya sala? Sehemu ya Injili ya leo, Yesu anatuonesha nini maana ya sala kwa kutumia mfano wa hakimu au kadhi dhalimu pamoja na mjane aliyekuwa analilia haki yake. Wakati wahusika wakuu katika Injili ya leo ni wawili, kwanza ni kadhi au hakimu dhalimu, asiyekuwa na hofu ya Mungu, mtu mwenye moyo mgumu na labda kwa lugha ya siku hizi mmoja anayejimwambafai kwa kila hali na upande wa pili ni mjane mnyonge, asiyekuwa na mtetezi. Katika Maandiko Matakatifu tunaona yatima na wajane kuwa ni ishara ya watu wanyonge na wasio na watetezi isipokuwa Mungu pekee. Huyu mjane leo hakujali unyonge wake au kukosa kwake fedha za kuweka wakili, bali aliona silaha pekee ni kutokukoma kudai na kuomba haki yake dhidi ya maadui na maasimu wake mbele ya kadhi yule dhalimu.

Baada ya kuona wahusika hawa wakuu wawili tunaona Injili inaendelea kwa mazungumzo ya moyoni kwa yule kadhi dhalimu. Hakimu dhalimu anakiri kuwa yeye ni mtu asiye na hofu ya Mungu wala kujali watu bali anaona ni heri ampatie haki mjane yule kwani alikuwa hakomi kumfuata na kumsumbua ili apate haki yake. Kadhi anachoshwa na hivyo kwa vile hakutaka tena usumbufu ule anaona ni heri nimtendee haki mjane yule. Ili kupata ujumbe wa sehemu ya Injili ya leo tunajiuliza pia, ni nani anamwakilisha hakimu dhalimu? Hata kama tumeona tabia za kadhi dhalimu si nzuri kwani hakuwa na hofu ya Mungu bali kwa hakika anamwakilisha Mungu. Si nia wala shabaha ya Yesu kumuonesha Mungu aliye mgumu na mkatili na asiyeguswa na shida na kilio cha wanyonge wanaomlilia bali ni kutualika kuwa na matumaini bila kukoma kama yule mjane aliyekuwa anasaka haki yake kwa hakimu dhalimu. Si kwamba Mungu asikilizi sala zetu bali tunaalikwa kusali daima na kubaki wenye imani na matumaini. Sala ye kweli inaambatana na imani ya kweli. Ni shabaha ya Yesu leo kutualika kuwa watu wa sala daima bila kuchoka na tukiwa wenye imani ya kweli kwa Mungu.

Kama ilivyokuwa katika nyakati za Yesu hata nyakati zetu pia tunaona ukosefu wa haki katika maeneo mbali mbali iwe kati ya uwanda wa siasa na serikali zetu, uwanda wa kimahakama, kijamii na hata kidini. Sisi kama waamini tunaalikwa daima kuwa watu wa haki na kumuomba Mungu ili haki iweze kutawala duniani. Mwinjili Luka anaandika wakati ambapo wakristo wale wa mwanzo walikuwa wakipitia madhulumu na mateso mengi na kuwaalika basi kubaki katika sala na imani. Ni mwaliko hata kwetu leo tunaposhuhudia ukosefu wa haki katika jamii zetu hatuna budi kubaki katika sala yenye matumaini na imani kubwa. Kama nilivyotangulia kusema kuwa kusali sio kumshawishi Mungu atende kadiri ya matwako yetu bali kuweza kupokea mpango na mapenzi yake katika maisha yetu. Ni kuinua mioyo yetu mbele yake ni njia pekee inayodumisha mahusiano yetu ya upendo na Mungu wetu. Hatusali kwa kuwa tuna shida na mahangaiko tu hivyo tunataka Mungu asikie kilio na shida zetu bali ni kuonesha upendo na imani yetu kwake.

Ni Yeye aliye kweli Mungu na Bwana wetu, ni Yeye aliye kimbilio letu katika kila hali za maisha yetu. Iwe ni nyakati nzuri au zile ngumu daima tunaalikwa kubaki katika mahusiano naye bila kukata tamaa au kupoteza imani.  Tunaporejea katika Maandiko Matakatifu tunaona kusali daima ni kubaki katika mahusiano na Mungu bila kujali nyakati na hali zetu. Ni njia ya kuonesha imani yetu kwake bila kujali magumu au mepesi tunayopitia. Mtume Paolo katika waraka wake kwa Warumi 15:30 anatualika kupambana naye katika sala. Kusali ni kupambana kadiri ya Mtume Paolo. Yakobo alikesha katika kupambana na Mungu ndio kusema alikesha katika sala. Mwanzo 32:23-33. Mwinjili Luka anatuhakikishia leo kuwa hakika sala zetu zinamfikia Mwenyezi Mungu aliye asili na chanzo cha wema wote. Kama hakimu dhalimu aliweza kumpatia haki mjane yule, je si zaidi Mungu Baba yetu aliye mwema na mwenye huruma. Luka 11:13 Kama sisi tulio waovu tunaweza kuwapatia mambo mema watoto wetu Je, si zaidi kwa Mungu Baba yetu wa mbinguni? Hivyo msingi wa sala ni imani kwa Mungu.

Tunabaki katika sala daima kwani tuna imani katika wema na huruma na upendo wa Mungu kwetu. Kusali ni kukua katika imani kwa Mungu, hivyo tunaalikwa kusali tukiwa wenye imani na matumaini kwa Mungu, hatuna sababu ya kuwa na mashaka kwani Mungu wetu ni wema wenyewe na mapenzi yake kwetu daima ni mema. Kanisa lile la mwanzo linawakilishwa na huyu mjane kwani halikuwa na mtetezi bali silaha pekee ni kudumu katika sala. Hata nasi leo kama Kanisa au kama muumini mmoja mmoja tunaalikwa kubaki na silaha moja tu nayo ni sala na kusali kwa imani. Kubaki usiku na mchana yaani bila kukoma katika sala. Mungu wetu ni mwaminifu hivyo mwinjili Luka anatuonesha kuwa Mungu ataleta haki duniani. Katika unyonge na udogo wetu tunahakikishiwa kuwa ni Mungu pakee aliye mtetezi wetu na ni Baba yetu Mwema. Mungu daima ni mwaminifu na ndio Injili leo inahitimishwa na swali, Je, Mwana wa Adamu atakapokuja duniani ataikuta imani? Imani ndio nguzo yetu pekee tunapobaki katika sala. Hatuwezi kusema tunasali kweli kama tunakosa imani.

Imani kama tulivyotafakari Dominika chache nyuma tuliona kuwa ni zawadi, hivyo hatuna budi kama Mitume kusali bila kukoma ili tukue katika imani na hapo tunaweza kubaki bila kukoma katika sala. Injili ya leo inatualika nasi kutafakari kuwa Mwenyezi Mungu anasikiliza sala zetu na ni mwaminifu daima kwani kwa muda wa kufaa au saa ile ya neema anajibu kila sala yetu. Kuna nyakati tunashawishika kuona kuwa Mwenyezi Mungu hasikii maombi na sala zetu bali leo mwinjili anatuonesha kuwa Mungu daima ni mwaminifu na mwema kwetu sote. Mwenyezi Mungu daima anajibu sala na maombi yetu. Nawatakia Dominika na tafakari njema.

19 October 2019, 13:45