Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili 30 ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa: Sala inamwilishwa katika toba, wongofu wa ndani na unyenyekevu wa moyo! Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili 30 ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa: Sala inamwilishwa katika toba, wongofu wa ndani na unyenyekevu wa moyo! 

Tafakari Jumapili 30 Mwaka C: Sala! Toba na Wongofu wa ndani!

Sala ya kweli inamwilishwa katika imani, matumaini na mapendo. Hii ni hija ya toba, wongofu wa ndani na unyenyekevu wa moyo kama njia ya kuweza kukutana na Mwenyezi Mungu kutoka katika undani wa maisha ya mtu! Sala inapaswa kujenga na kuimarisha mahusiano mema na Mwenyezi Mungu, kwa kumpatia kipaumbele cha kwanza; kwa kuwajali na kuwaheshimu pia jirani!

Na Padre Alcuin Maurus Nyirenda, OSB. – Roma.

Taifa letu limeanza kujenga utamaduni wa kusali kabla ya mikutano ya hadhara ya kiongozi wa Taifa letu. Tumshukuru Roho Mtakatifu aliyevuvia wazo hilo. Aidha shukrani kwa Rais John Josefu Pombe Magufuli anayewaalika viongozi wa dini Waislamu na Wakristu kuongoza sala kabla ya kuhutubia wananchi. Yeye mwenyewe anasikika daima akisali hadharani: “Ndugu zangu napenda kumshukuru Mungu mwenye rehema kwa kutuwezesha kukutana hapa tukiwa wenye afya njema.” Pahala pengine alisema: “Tusali tumwombe mwenyezi Mungu ili sote tutubu.” Inabidi viongozi wa dini hasa wakristo kumshukuru Rais kwa kusaidia kufundisha katekesi ya kusali daima. Kadhalika watawa hasa wamonaki wanaofuata Kanuni ya Mtakatifu Benedikto wanawiwa na Rais huyu kwa kutusaidia kuiishi kauli mbiu ya “Ora et Labora” yaani “Sala na Kazi”, pale anapowaapisha viongozi mbalimbali anawaagiza: “Nendeni mkachape kazi. Mkamtangulize Mungu katika kazi zenu.” Kanuni hii ya sala na kazi ndiyo iliyoleta maendeleo Ulaya hadi Benedikto anaitwa: “Mlinzi na Baba wa mchakato wa maendeleo fungamani Barani Ulaya.”

Injili ya Jumapili ya 30 ya Mwaka C wa Kanisa inahusu watu wawili Mfarisayo na Mtoza Ushuru wanaopanda kwenda Hekaluni kusali. Hekaluni ni pahala pa kusali, yaani pahala pa kumsifu Mungu, pa kumwomba, kusujudu na kumshukuru. Endapo tumemkosea Mungu basi hekaluni ni pahala pia pa kutubu na kujuta makosa yetu. Sanasana ni pahala pa kukutana na Mungu na kuongea naye. Kama anavyosema Mzaburi: “Lini nitauona uso wa Mungu?” (Zab 42). Kimaadili Wafarisayo walikuwa wakereketwa, wanaharakati, watu wa uamsho, watu wema, wenye haki, watu wa sala, wa kufunga na kutoa sadaka. Kwa mfano Mfarisyo Nikodemus aliyeenda kwa Yesu usiku. Hata Mtume Paulo alijisema kuwa yeye ni Mfarisayo aliyefundishwa na Gamalieli. Wafarisayo walionekana watakatifu machoni pa watu wote. Kasoro yao tunayoweza kuivumilia ni ile kujigamba na ya kudharau wengine. Kumbe, Watoza ushuru walikuwa mafisadi wakubwa na wahujumu uchumi. Mathalani Zakayo alikuwa fisadi wa kutupwa. Tungetegemea Yesu angemtumbua mtoza ushuru kwa kumung’unya fedha ya umma, kumbe, anamshukia Mfarisayo aliyejimwambafai kuwa ni mtu wa haki! Yaani hadi sipati picha!

Ndugu zangu kigezo anachotumia Yesu cha kuwahukumu watu hawa siyo cha maadili. Bali anatumia kigezo cha sala. Kwa vyovyote Yesu anao wafuasi wengi: watakatifu, wazuri, wema, wakereketwa wa dini, hodari na wanayo nia njema ya kumfuata Mungu. Lakini anayo mashaka na wasiwasi mkubwa sana juu ya sala wanazozifanya. Yesu anataka kuwaangalisha wasije wakatumbukia katika dimbwi kama aliloangukia Mfarisayo aliyejimwambafai kama wanavyosema waswahili! Watu hawa wawili walipoingia hekaluni yasemwa kwamba: “Yule Farisayo akasimama akiomba.” Huko kusimama hakuna maana ya majivuno, kwa sababu hata mtoza ushuru naye “alisimama kwa mbali.” Kwa sababu desturi ya Wayahudi ni kusali wima. Kasoro kubwa katika sala inaanza Yesu anaposema “Yule Mfarisayo alisimama akiomba moyoni mwake.” Huku kuomba moyoni, hakumaanishi kusali kimoyo-moyo au kimya kimya. La hasha, kwa sababu kadiri ya desturi Myahudi ni kusali kwa sauti ya juu inayosikika. Neno la lugha ya Kigiriki la kusali moyoni mwake ni “pros heauton”. Maana yake ni kusali kwa kujiamini na kwa kujielekeza sala kwa wewe mwenyewe.

Hapa yaonekana Mfarisayo huyu anasali kwa “kamungu” au mungu mdogo aliye ndani yake. Kamungu hako kanaona wivu, kanachukia, kanadharau kama anavyofanya yeye mwenyewe. Mfarisayo ametumia mwanya huo kutaka kujikuza na kujituliza mwenyewe. Mfarisayo anaendelea kujianika zaidi mbele ya Mungu: “Ee Mungu nakushukuru kwa kuwa mimi si kama watu wengine, wanyang’anyi, wadhalimu, wazinzi, wala kama huyu mtoza ushuru.” Lugha kama hii inatumika pia mbele ya viongozi wa serikali ili kuwaumbua mafisadi. Hata Yesu haoneshi kumpinga huyu Mfarisayo anachosema, kwani anasema ukweli mtupu na ukweli daima utawaweka watu huru! Kisha Mfarisayo anaendelea kuorodhesha matendo ya maadili ya dini anayofanya: “Mimi nafunga mara mbili kwa juma; hutoa zaka katika mapato yangu yote.” Hata hapa hakuna ubaya, kwani ukweli wa mambo kimaadili na kidini Mfarisayo huyu yuko vizuri sana. Kwa hiyo siyo vibaya kuorodhesha mafanikio ya maendeleo yaliyofikiwa na viongozi wetu wa serikali tunaposali, ikiwa kama alama ya kumsifu na kumshukuru Mungu.

Kama nchi yetu ingekuwa na watu wengi wenye maadili kama ya Mfarisayo huyu, hata kama ni wanatafuta kiki, tungekuwa pahala pazuri sana kimaadili na kiuchumi. Kumbe, hapo ndipo anapotushtukia Yesu. Kuhusu Mtoza Ushuru Yesu anasema: “Lakini yule mtoza ushuru alisimama mbali, wala hakuthubutu hata kuinua macho yake mbinguni, bali alijipiga-piga kifua akisema, Ee Mungu, uniwie radhi mimi mwenye dhambi.” Mtoza ushuru anasimama mbali na madhabahuni na yule Mfarisayo. Hata macho yake hayainui mbinguni bali anajipiga-piga tu kifua chake. Lakini kimaadili mtu huyu ni fisadi tena ni ufisadi uliohalalishwa hata na serikali, kwa sababu mtoza ushuru alipewa fursa ya kuongeza gharama ya mapato, kusudi kinachozidi kinaingia mfukoni mwake. Hivi watoza ushuru walisanya pesa nyingi na waliishi maisha ya raha sana, yaani wao walikuwa wanakula “bata kwa kwenda mbele”. Sasa anaingia Hekaluni kujuta. Lakini hata majuto yenyewe anafanya kijumla jumla bila kuorodhesha kinaganaga dhambi za uhujumu.

Kumbe, Yesu anatoa hukumu kinyume cha mategemeo ya wengi. “Nawaambia, huyu (mtoza ushuru) alishuka kwenda nyumbani kwake amehesabiwa haki kuliko yule (Faraisayo). Yesu hasemi kwamba mwenendo wa Mtoza ushuru ni sawa, au mwenendo wa Mfarisayo ni mzuri. La hasha, bali anataka kuzungumzia juu ya sala. Yaani sala ilielekezwa kwa Mungu gani? Kumbe, yaonekana sala ya Mtoza ushuru ilimwelekea Mungu wa kweli na ya Mfarisayo ilimwelekea mwenyewe. Kuhusu nani tunayemwelekezea sala zetu, tunaweza wengi kutumbukia kwenye hatari ya kukosa kumpa Mungu sifa bali tukajielekezea sisi wenyewe. Rais anatuonesha mifano mizuri ya namna ya kusali. Mara moja alimgombeza Diwani mmoja aliyetaka kumpigia magoti ya kumshukuru. “Simama! Mungu peke yake tunampigia Magoti. Mimi ni kiumbe mdogo sana mbele yake.” Aidha daima Rais anasema: “Tumshukuru Mungu na kumtolea sifa kwa maendeleo yote yaliyofikiwa.”

Mwisho, Yesu alisema juu ya yule Mtoza ushuru: “Huyu alishuka kwenda nyumbani kwake amehesabiwa haki.” Neno la kigiriki “dedikaiomenos” yaani kuhesabiwa haki, maana yake halisi ni kuwekwa huru, kuwekwa sawa, kurekebishwa, kuneemeka. Mtoza ushuru ameelekeza sala zake kwa Mungu naye ameingia ndani mwake na kumweka huru. Yaani Mungu ameweza kupata mwanya wa kuingia ndani ya Mtoza ushuru na kubadilisha maisha yake. Kumbe, kinyume chake Mfarisayo huyu amerudi nyumbani kama alivyokuwa mwanzo, yaani mtu safi, mtu bora na mkereketwa wa dini. Mungu hakufanikiwa kumwingia na kumgeuza. Mfarisayo ameshindwa kutambua kuwa Mungu hahesabu matendo yetu bali anaonesha njia ya maisha. Kumbe, inabidi sala itugeuze. Kwa sababu sala nzuri ni ile inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya mtu! Mfano wa sala inayomgeuza na kumwongoa mtu ni kama ile ya mchungaji wa Mkoa wa Njombe, iliyombadilisha Rais hadi akatangua hukumu aliyoitoa kwa OCD aliyeacha kufuatilia mauaji ya watoto wa Njombe. “Mwambie nimemsamehe kutokana na maombi haya.” Baada ya kuutoa msamaha huu Rais alisali mbele ya kadamnasi kama mtoza ushuru wa Injili ya leo.

“Ndugu zangu tumesamehewa na Mwenyezi Mungu. Tumshangilie Mungu kwa msamaha aliotupa". Asitokee mtu mwingine tena wa kufanya mabaya kwa sababu Mungu tumemkosea lakini ametusamehe. Sasa kila mmoja (Mwananjombe) akachape kazi yake, akamtegemee Mungu katika kazi yake na katika utajiri wake wala asimtegemee Shetani, Ibilisi. Tukamtegemee yeye katika siku zote za kazi zetu na za maisha yetu. Njombe ikaneemeke ikawe Njombe mpya. Tukapate mazao mazuri. Tukazae watoto wengi wenye afya njema. Ikiwezekana wale mapacha wakazaliwe sabini mara sabini. Na wale wazazi waliopotelewa na watoto wao. Haya machungu waliyo nayo yakaondolewe kwa nguvu za Mwenyezi Mungu. Wakafarijike na wakabarikiwe tena.”

 

24 October 2019, 16:58