Vatican News
Makatekista ni vyombo muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa Barani Afrika, lakini wanapaswa kuwezeshwa zaidi! Makatekista ni vyombo muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa Barani Afrika, lakini wanapaswa kuwezeshwa zaidi!  (AFP or licensors)

Nafasi ya Makatekista katika maisha na utume wa Kanisa Afrika!

Makatekista wameonesha umuhimu wa pekee katika kuzisimamia na kuziongoza Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo, shule ya Neno la Mungu, ukarimu na upendo kwa familia ya Mungu. Kwa njia ya mifano bora ya Makatekista kutoka sehemu mbali mbali Barani Afrika, Kanisa Barani Afrika limeweza kuzamisha mizizi katika maisha na vipaumbele vya watu. Makatekista wawezeshwe zaidi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Makatekista ni wadau wakuu katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima Barani Afrika. Wao wamekuwa mstari wa mbele katika Uinjilishaji wa awali Barani Afrika na wanaendelea kuwa mstari wa mbele katika kuwatayarisha wakatekumeni ili kupokea Sakramenti za Kanisa. Makatekista wameonesha umuhimu wa pekee katika kuzisimamia na kuziongoza Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo, shule ya Neno la Mungu, ukarimu na upendo kwa familia ya Mungu. Kwa njia ya mifano bora ya Makatekista kutoka sehemu mbali mbali Barani Afrika, Kanisa Barani Afrika limeweza kuzamisha mizizi katika maisha na vipaumbele vya watu Mchango wa Makatekista bado ni muhimu na endelevu anasema Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI katika Waraka wake wa Kitume Dhamana ya Afrika, Africae Munus. Maaskofu mahalia wanapaswa kuhakikisha kwamba Makatekista wanapewa majiundo awali na endelevu: kiakili, kimafundisho, kimaadili na kichungaji, ili waweze kutekeleza vyema dhamana na wajibu wao katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Kanisa mahalia pia linapaswa kuhakikisha kwamba, Makatekista wanapata mahitaji yao msingi ili kuziwezesha familia zao kusonga mbele kimaendeleo. Makatekista waoneshe upendo na ukarimu; uaminifu na udumifu katika maisha na utume wao. Wawe ni vyombo na mashuhuda wa Neno la Mungu na Mafundisho ya Kanisa na kwa njia hii wataweza kutoa katekesi safi na kuongoza vyema vikundi vya sala na tafakari ya Neno la Mungu. Ikiwa kama Makatekista watakuwa waaminifu kwa utume wao, watasaidia kuchangia utakatifu wao binafsi pamoja na kusaidia kujenga Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Askofu Selesius Mugambi, Mwenyekiti wa Utume wa Familia, Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya hivi karibuni katika semina maalum kwa Makatekista kutoka kwenye familia ya Mungu nchini Kenya na waratibu wa utume wa familia amewataka kutekeleza dhamana na wajibu wao kikamilifu ili kuhakikisha kwamba wanasaidia mchakato wa umwilishaji wa wosia wa Baba Mtakatifu Francisko “Furaha ya upendo ndani ya familia” ili kuziwezesha familia kupendana, kushikamana na kudumu katika kifungo cha upendo, tayari kujenga na kudumisha familia kama Kanisa dogo la nyumbani, shule ya utakatifu, haki, amani, upendo, ukarimu, msamaha na upatanisho.

Ni katika msingi bora wa familia, hapo watoto wataweza kupata malezi na majiundo makini, ili kupenda na kushikamana na watoto wenzao ndani ya jamii. Kanisa Barani Afrika linapenda kuwekeza kwa namna ya pekee kwa familia ili kweli familia za Kikristo ziweze kuwa ni mfano bora wa Injili ya familia inayoyotangazwa na kushuhudiwa kwa watu! Askofu Mugambi anakaza kusema dhamana na nafasi ya Makatekista ndani ya Kanisa Katoliki ni muhimu sana, kwani wanawawezesha wazazi na walezi kurithisha, kukuza na kustawisha imani miongoni mwa watoto wao na kama familia moja! Makatekista wanapaswa kunolewa vyema ili mafundisho yao yaweze kujikita zaidi katika Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa na Mafundisho Jamii ya Kanisa, ili kuwasaidia wanafamilia halisi wanaoishi katika mazingira yanayofahamika. Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ilikua ni fursa kwa familia kukutana na kuadhimisha matendo makuu ya Mungu katika maisha yao, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kuwashirikisha jirani zao huruma na upendo wa Mungu katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Familia ziwe ni kitovu cha upendo, huruma, msamaha na upatanisho wa kweli!

Askofu Mugambi amewakumbusha Makatekista kwamba, familia ya Kikristo kadiri ya mpango wa Mungu inafumbatwa katika upendo kati ya mwanaume na mwanamke na kwamba, familia ya Mungu nchini Kenya inahamasishwa kukuza na kudumisha ukuu, utakatifu na udumifu wa maisha ya ndoa na familia msingi wa utamaduni, upendo, mshikamano na mafungamano ya kijamii, tayari kutangaza na kushuhudia Injili ya uhai inayofumbatwa katika Injili ya familia dhidi ya utamaduni wa kifo. Familia ni shule ya ubinadamu, mahali pa kujifunza kupenda na kupendwa; kusamehe na kusamehewa; kuwajibika pamoja na kuonesha mshikamano wa umoja, udugu na upendo. Wazazi na walezi wanapaswa kuhakikisha kwamba, wanasimama kidete kutoa malezi na majiundo makini kwa watoto wao, kwani hii ni dhamana ambayo kamwe haiwezi kutekelezwa na taasisi nyingine iwayo yote. Wazazi na walezi wawajibike kwa kuwa waaminifu kwa maisha na utume wao ndani ya familia; waaminifu na wakweli katika maagano yao ya ndoa na kwamba, Makatekista kama watendaji wa karibu sana na familia wanao mchango mkubwa katika maisha na utume wa familia.

Papa: Makatekista
24 October 2019, 14:44