Tafuta

Vatican News
Sr. Mariana Nyakunga Mdemu wa Shirika la Wafranciskani wa Bwana amefariki dunia mjini Roma, nchini Italia, tarehe 14 Oktoba 2019. Sr. Mariana Nyakunga Mdemu wa Shirika la Wafranciskani wa Bwana amefariki dunia mjini Roma, nchini Italia, tarehe 14 Oktoba 2019.  (AFP or licensors)

Sr. Mariana Nyakunga Mdemu afariki dunia akiwa Roma, Italia!

Sr. Mariana Nyakunga Mdemu aliyefariki dunia tarehe 14 Oktoba 2019 mjini Roma; Alhamisi tarehe 16 Oktoba 2019 kunaadhimishwa Ibada ya Misa Takatifu mjini Roma kuanzia saa 10: 30 Jioni ili kutoa nafasi kwa familia ya Mungu kusali na kutoa heshima zake za mwisho. Mara baada ya Misa, mwili wa Sr. Mariana utapelekwa Sicilia kwa Ibada na mazishi, Ijumaa tarehe 18 Oktoba 2019.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mababa wa Kanisa wanasema, Fumbo la maisha ya mwanadamu limening’inizwa katika udhaifu wake, kiasi kwamba, kifo kinawakumba watu wote pasi na ubaguzi. Jambo la msingi kwa kila mwamini ni kuhakikisha kwamba, kila siku ya maisha yake, anajiandaa kikamilifu ili kuweza kukabiliana na fumbo la kifo, ili hatimaye, kukutana na Kristo Yesu, rafiki mwema, Mkombozi wa ulimwengu, ndugu na mfano bora wa kuigwa katika sadaka na majitoleo kwa ajili ya ukombozi wa dunia! Shirika la Masista Wafranciskani wa Bwana linasikitika kutangaza kifo cha Sr. Mariana Nyakunga Mdemu, kilichotokea tarehe 14 Oktoba 2019 mjini Roma, nchini Italia, baada ya kuugua kwa muda mfupi! Sr. Mariana Nyakunga Mdemu tarehe 13 Oktoba 2019 alijisikia vibaya na kukimbizwa Hospitali ya Policlinico Umberto Primo iliyoko mjini Roma. Madaktari wakagundua kwamba, mishipa ya damu kichwani ilikuwa imepasuka na hivyo wakalazimika kumfanyia operesheni ya haraka ili kuokoa maisha yake, lakini tarehe 14 Oktoba 2019 majira ya asubuhi, akaitupa mkono dunia.

Sasa Mwenyezi Mungu amemwita kwenye makao ya uzima wa milele kwani yote yamekamilika, “Consummatum est”. Sr. Mariana Nyakunga Mdemu alizaliwa tarehe 20 Februari 1973 huko Jimboni Iringa na baadaye, wazazi wake wakahamia Jimbo kuu la Tabora na kujenga makazi yao kwenye Parokia ya Ipuli, Jimbo kuu la Tabora. Katika maisha yake, alitamani sana kumtumikia Mungu na jirani zake na hamu hii, ikatimia kunako mwaka 2002 alipokwenda Roma, Italia kuanza malezi na majiundo yake ya kitawa ndani ya Shirika la Wafranciskani wa Bwana. Itakumbukwa kwamba, Watawa hawa wanatekeleza utume wao Jimbo kuu la Arusha nchini Tanzania. Tarehe 13 Oktoba 2010, miaka tisa iliyopita akaweka nadhiri zake za daima kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Kati ya waombolezaji kutoka Jumuiya ya Watanzania wanaoishi na kusoma mjini Roma ameandika hivi: “Nadhiri ya ufukara, usafi wa moyo na utii, hukamilika pale mtawa anapoungana na muasisi wake, yaani Mwenyezi Mungu”.

Fumbo la kifo, liwe ni changamoto kwa ajili ya kutafakari, kukesha na kutekeleza dhamana na nyajibu mbali mbali kwa uaminifu na ukamilifu kwa kutambua kwamba, wameteuliwa ili kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa Mungu na jirani. Fumbo la kifo ni fursa ya kufakari kwa kina na mapana Injili ya uhai. Mpango wa mazishi unaendelea kufanyika Shirikani kwa matumaini kwamba, walau mwakilishi kutoka katika Familia ya Sr. Mariana Nyakunga Mdemu ataweza kuhudhuria kwani Mama yake mzazi ni mzee hawezi kumudu kishindo hiki cha majonzi ya kuondokewa na binti yake, aliyemsindikiza hatua kwa hatua katika maisha ya kitawa kwa ajili ya Mungu na jirani zake. Kwa watanzania waliobahatika kukutana na Sr. Mariana Nyakunga Mdemu wanashuhudia kwamba, kwa hakika alikuwa ni mtawa ambaye alisimika maisha yake katika sala. Hata ukiangalia vitabu vyake vya sala, vimechakaa sana, dalili kwamba, alijitahidi kuboresha maisha yake kwa Sala na Sakramenti za Kanisa.

Wanasema, haya ni mambo yaliyomsaidia kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa jirani zake. Alikuwa ni mtawa mcheshi, kielelezo cha furaha ya Injili; alikuwa ni mvumilivu, mpole na mwenye upendo kwa wote bila ubaguzi. Watawa wenzake, wanamkumbuka kwa busara na ushauri aliowapatia katika safari ya maisha yao, wakiwa huku ughaibuni au Tanzania. Alijisadaka sana kwa ajili ya huduma kwa watawa wenzake mpaka dakika ya mwisho! Kwa machozi na uchungu mkubwa, watanzania wanaoishi na kusoma mjini Roma, wanajiandaa kumsindika katika safari yake ya mwisho, kwenye makao ya uzima wa milele huko Sicilia, Kusini mwa Italia mipango yote itakapokamilika. Wanaendelea kumwombea Mama yake mzazi ili aweze kuupokea msiba huu kwa imani na matumaini; kwa watawa wenzake na watu wa Mungu kutoka Tanzania, wajitahidi kuiga yale mema yaliyotendwa na Marehemu Sr. Sr. Mariana Nyakunga Mdemu. Sasa Pumzika kwa Amani. Amina!

Sr. Mariana Nyankunga
15 October 2019, 10:55