Tafuta

BURUNDI: Maaskofu wanahamasisha kutumia fursa ya uchaguzi wa Mei 2020 kubadili safu ya uongozi wa kisiasa. BURUNDI: Maaskofu wanahamasisha kutumia fursa ya uchaguzi wa Mei 2020 kubadili safu ya uongozi wa kisiasa.  

Baraza la Maaskofu Katoliki Burundi waongelea uchaguzi

Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Burundi wamewataka wananchi kutumia vyema haki yao ya kupiga kura ili kurejeza amani nchini humo. Lengo ni kuwaelimisha wananchi juu ya haki yao ya kimsingi ya kupiga kura ili kuleta mabadiliko kwa njia za haki na amani. Mwaliko huo umetolewa wakati nchi ya Burundi ikielekea kwenye uchaguzi wa kitaifa utakaofanyika tarehe 20 Mei, 2020.

Na Padre Angelo Shikombe, - Vatican.

Baraza la Maaskofu Katoliki Burundi wamewataka wananchi nchini Burundi kutumia vyema haki yao ya kupiga kura ili kurejeza tena amani nchini humo. Ujumbe huo wa Baraza la Maaskofu nchini Burundi unalenga kuwaelimisha wananchi juu ya haki yao ya kimsingi ya kufanya mabadiliko ya uongozi kwa njia za haki na amani. Uamuzi huo umefikiwa na Baraza la Maaskofu wakati nchi ya Burundi ikielekea kwenye uchaguzi wa kitaifa unaotarajiwa kufanyika tarehe 20 Mei, 2020. Ujumbe huo uliotolewa katika mkutano wa mwaka wa Maaskofu uliofanyika kuanzia tarehe 11 hadi 13 Septemba 2019 na kusomwa katika makanisa yote ya kikatoliki nchini Burundi.

 Ujumbe huo unaelekeza kutumia vema fursa ya kupiga kura kwa sababu ndiyo nafasi pekee inayoweza kutumika kwa ajili ya kufanya mabadiliko ya kiutawala.Baraza la Maaskofu nchini Burundi limeyasema hayo kufutia migawanyiko ya kibabe na kandamizi inayoendelea nchini Burundi ambayo inakiuka mwongozo wa kikatiba na makubaliano yaliyofikiwa huko Arusha mnamo mwaka 2000. Maaskofu katika ujumbe wao wanakazia umuhimu wa kujadiliana kama njia ya kupambana na migogoro. Ikumbukwe kuwa, Burundi imekuwa ikiishi katika kipeo cha kisiasa, kiuchumi, kitaasisi na kijamii kilichosababisha maelfu ya wanaburundi kukimbilia nchi za jirani baada ya Rais Pierre Nkurunziza kushika hatamu kwa awamu ya tatu mnamo mwaka 2015. Maaskofu wanapongeza jitihada zilizochukuliwa na vyama vya kisiasa vya upinzani za kugombea kinyang’anyiro hicho na kuwaandaa wapiga kura.

Baraza la Maaskofu halingependa kufumbia macho baadhi ya matukio ya kinyama yaliyopelekea watu kuikimbia inchi yao kutokana na vurugu za kisiasa. Aidha wamekumbuka matukio ya kudai mfumo wa vyama vingi utambuliwe kikatiba. Pamoja na hayo, hawakusita kutaja matukio ya kiuharifu ya kisiasa yanayokumbatia mauaji ya halaiki ambayo sehemu kubwa ni watu waliokuwa na hoja zilizo kinyume cha Serikali iliyoko madarakani.  Kutokana na hali hiyo Maaskofu wameamua kuwakumbusha wananchi kutumia vyema haki yao ya kupiga kura na kujenga amani itakayowasaidia kujipatia uhuru, maendeleo na amani.

02 October 2019, 09:47